SERIKALI imeshauriwa
‘kuwatumbua’ watumishi waliosababisha halmashauri za mkoa wa Mwanza kuendelea
kupata hati zenye mashaka baada ya kutozingatia viwango vya kimataifa vya
uandaaji wa hesabu (IPSAS).
Changamoto hiyo
ilitolewa na baadhi ya wajumbe wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) wa
Mwanza kilichofanyika jijini hapa wiki iliyopita, ambapo taarifa ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2014/2015 ilionesha
kuwa halmashauri sita kati ya saba zinazounda mkoa huo zilipata hati zenye
mashaka.
Halmashauri zilizopata
hati zenye mashaka kutokana na ukaguzi huo wa CAG ni Jiji la Mwanza na wilaya
za Kwimba, Magu, Misungwi, Sengerema na Ukerewe, huku Ilemela ikiwa ndiyo
wilaya pekee iliyopata hati safi/inayoridhisha.
Taarifa
hiyo ya CAG inataja makosa yaliyosababisha halmashauri hizo kupata hati zenye
mashaka kuwa ni pamoja na watumishi husika kutozingatia viwango vya kimataifa
vya uandaaji wa hesabu ambapo hazikuonesha thamani ya ardhi na viwanja
vinavyomilikiwa katika hesabu za mwisho zinazoishia Juni 2015.
Sababu
nyingine ni kufanya malipo ya fedha yenye nyaraka pungufu, kutowasilisha vitabu
vya kukusanya mapato, kutopeleka fedha benki, kutoingiza madeni yanayodaiwa katika
hesabu za mwisho na kutowasilishahati za malipo ya fedha.
Baadhi
ya wajumbewa kikao hicho walielezea kukerwa kwao na makosa hayo ya kihesabu
wakionesha wasiwasi kwamba huenda ni mpango wa makusudi uliosukwa na watumishi
wachache kwa ajili ya kujinufaisha kiharamu na fedha za umma.
“Hali hii inatupa
wasiwasi kwamba huenda ni namna ya watu fulani waliojipanga kuhujumu na kula
fedha za umma kwa sababu haiwezekani halmashauri hizo sita kupata hati zenye
mashaka kutokana na makosa yanayofanana.
“Inawezekana
halmashauri hizo hazina wataalamu wa masuala ya usimamizi wa fedha na huenda
serikali imeajiri vilaza wasiyo na taaluma inayotakiwa,” alilalamika mjumbe wa
kikao hicho, Edward Mboje aliyejitambulisha kuwa ni Katibu wa UDP Mkoa wa
Mwanza.
Hata hivyo, licha ya
kauli hiyo ya Mboje kuungwa mkono na wajumbe wengine kadhaa, hakuna majibu wala
ufafanuzi uliotolewa katika kikao hicho kilichoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa
Mwanza, John Mongella
CHANZO: RAIA MWEMA