Saturday, February 3, 2018

ZIARA YA MH. MANSOOR JIMBONI













TAREHE 01.02.2018

MBUNGE wa Jimbo la Kwimba mkoani Mwanza, Shanif Mansoor, amesema asilimia 80 ya vijiji jimboni hapa vipo mbioni kupata umeme.

Amesema miradi hiyo ya umeme wa Rea Vijijini, itapatikana kwa kipindi cha kuanzia sasa hadi kufikia mwaka 2020, ili kuwasaidia wananchi kupata maendeleo.

Mansoor aliyasema hayo juzi katika ziara yake ya kikazi jimboni hapa, na kwamba anahitaji kuwasaidia wananchi kupata maendeleo ya kisekta.

"Napenda kusema kazi tumeshaanza. Mwaka huu kuna mradi mkubwa sana wa umeme wa Rea Vijijini. Baadhi ya maeneo umeme haujafika....lakini tutapata umeme hadi Mwakilyambiti.

"Kwa hiyo anapambana kuhakikisha asilimia 80 ya vijiji vya Jimbo la Kwimba vinapata umeme wa Rea, ifikapo mwaka 2020," alisema Mbunge huyo wa Jimbo la Kwimba na kuongeza:

“Naomba sana ushirikiano wenu wananchi, ili tuijenge Kwimba na taifa kwa ujumla katika maendeleo ya kweli.”

Katika hatua nyingine, Mansoor aligawa majembe ya kilimo 18,000 yenye thamani ya zaidi ya sh. Milioni 200, ambapo karibu kila kaya itanufaika na vifaa hivyo.

Alisema lengo la kuwawezesha wananchi vifaa hivyo vya kilimo, ni kuwawezesha kuzalisha mazao ya chakula na biashara.

Alisema kuwa, licha ya kuahidi kutoa vifaa hivyo kwa wananchi lakini pia amelenga kuinua uchumi wa kila mwananchi kupitia kilimo, ndani ya
Jimbo la Kwimba.

"Sitaki mpate tabu wakati mbunge wenu nipo. Halmashauri yetu ya wilaya nayo nimeipatia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara, katika Shule ya Sekondari Bujiku Sakila.”

Aliipongeza pia Serikali kwa kujenga mradi wa maji jimboni Kwimba, unaogharimu zaidi ya sh. Milioni 576.

Kwa mujibu wa mh.Mansoor, mradi huo tayari umeshakamilika kwa kiwango cha
asilimia 80, ambapo umelenga kupunguza kama si kuondoa kabisa adha ya maji katika jimbo la kwimba.

“Mimi mwenyewe nataka kila kijiji kiwe na mradi wa maji safi na salama ya kunywa kutoka ziwa victoria,umeme na miundombinu rafiki pamoja na kutengeneza barabara za mitaa ya miji inayoendelea katika jimbo la kwimba.

“Nimechimba mabwawa na visima zaidi ya 35 vya maji kwa nguvu zangu. Lengo langu ni kuwasaidia wananchi walioniamini na kunipa kura za kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa 2015,” alisema Mansoor.

Wakati huo huo, Mansoor amewakatia bima za afya viongozi wote wa Halmashauri za Kata wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Kwimba.

Alisema kuwakatia kwake bima viongozi hao ni lengo la kutaka kuwasaidia, katika changamoto za masuala ya afya, hivyo anahitaji kuona jamii inatekeleza vema majukumu yake.

SOURCE: GSENGO BLOG

Previous Page Next Page Home