Taasisi hizo zimepania kushirikiana kwa hali na
mali katika kuyakomboa makundi hayo ya jamii kiuchumi, kiafya na kiusalama kwa
dhana ya kuyafungulia ukurasa mpya wa maisha bora.
Katika juhudi hizo, Tasaf III imeyaidhinisha makundi hayo kwenye mpango
maalumu wa kutambuliwa, kuthaminiwa na kuwezeshwa kupata mahitaji ya msingi ya
chakula, malazi, mavazi, matibabu na elimu.
Wazee wanapewa kipaumbele cha ziada cha kuimarishiwa ulinzi dhidi ya vitendo vya uonevu, dhuluma, kujeruhiwa na kuuawa kutokana na imani potofu za kichawi zinazochochewa na waganga wa jadi, hususan wapiga ramli chonganishi.
Mkuu wa Wilaya (DC), Karen Yunus na
Mbunge wa Magu, Bonaventura Kiswaga, wameahidi kuzipatia taasisi hizo
ushirikiano wa dhati katika kuyaondolea makundi hayo ya jamii hali ya unyonge
na vikwazo vya kufurahia maisha yao duniani.
Tasaf na kaya masikini
Tasaf na kaya masikini
Mratibu wa Tasaf Wilaya ya Magu, Philip Msangi, amelieleza Raia Mwema wiki hii kwamba kaya 5,937 zimeingizwa kwenye mpango wa kuwezeshwa kujikimu katika mahitaji ya msingi ya chakula, mavazi na malazi. Pia mahitaji ya sare na vifaa vya shule kwa wanafunzi ambao wazazi wao ni walengwa wa mpango huo wa kunusuru kaya masikini.
Walengwa hao pia watawezeshwa kupata matibabu, kiingilio katika Bima ya Afya ya Jamii (CHF), kuweka akiba na kuwekeza katika miradi midogo ya uzalishaji mali kuongeza kipato cha familia na kujenga mazingira endelevu hata baada ya kuondolewa kwenye mpango huo.
Msangi anasema mpango huo umetengewa Sh bilioni 4.879 kutoka serikalini kwa kipindi cha miaka mitatu na kwamba matumizi yake yanahusisha malipo taslimu kwa walengwa na gharama za uendeshaji katika ngazi ya wilaya, kata na vijiji.
“Hadi sasa Tasaf III Wilaya ya Magu tumeshapokea shilingi 1,355,517,000 kati ya shilingi 4,879,861,200 zilizotengwa kwa ajili ya walengwa 5,937,” anabainisha mratibu huyo.
Malipo kwa walengwa hufanywa kila baada ya miezi miwili kwa ratiba maalumu ya kitaifa inayojulikana kama Dirisha la Malipo. Fedha hupelekwa vijijini chini ya ulinzi wa askari polisi na viongozi wote ngazi ya kijiji hushirikishwa kusimamia kazi ya ulipaji.
Mratibu huyo wa Tasaf anafafanua kwamba kuna ruzuku za aina mbili; ile isiyo na masharti wanayopatiwa walengwa wote 5,937 na ya masharti wanayopatiwa walengwa wenye watoto wenye mahitaji ya shule na matibabu.
“Utaratibu umeweka wa kufanya ufuatiliaji katika shule za msingi, sekondari, zahanati, vituo vya afya na hospitali kuratibu mahudhurio na maendeleo ya watoto wanaopata ruzuku ya masharti,” anasema.
Mmoja wa walengwa hao, Asha Shibugulu (61) mkazi wa Itumbili, Magu anasema “Ninapokea shilingi 40,000 kutoka Tasaf kila baada ya miezi miwili, ambazo zimenisaidia kuanzisha biashara ya karanga inayoniwezesha kujikimu katika chakula, mavazi na kulipa kodi ya nyumba.”
Tasaf inavyowatambua wazee
Msangi anasema ingawa wazee si walengwa wa moja kwa moja, mpango wa kunusuru kaya masikini unaotekelezwa na Tasaf III unawanufaisha baadhi yao kulingana na vigezo vya umasikini na nafasi zao za uwajibikaji katika familia.
Kati ya kaya 5,937 zinazopokea ruzuku ya fedha kutoka Tasaf, 2,652 sawa na asilimia 44.6 ni za wazee, ambapo kaya za wazee wanawake ni 2,219 (83.6%) na za wanaume ni 433 sawa na 16.4% ya wazee wote wanaolengwa na mpango huo wilayani Magu.
Changamoto zilizoonekana katika utekelezaji wa mpango huo ni pamoja na wazee wengi kutokujua kusoma na kuandika, hivyo kushindwa kuendesha miradi yao kikamilifu na baadhi ya wanajamii kutokutambua umuhimu wa wazee, hivyo kuwanyima fursa zinazopatikana katika jamii.
Changamoto nyingine ni baadhi ya wazee, hasa wanaume kuwanyanyasa wazee wenzao wanawake kwa kuwanyang’anya fedha walizolipwa na Tasaf na baadhi yao kuzitumia visivyo kama vile kununua pombe.
“Lakini pia, baadhi ya wazee wamekuwa na wategemezi wengi, hivyo kufanya fedha wanazolipwa kutotosha kugharimia mahitaji ya familia zao,” anaongeza mratibu huyo wa Tasaf.
Hata hivyo, anasema Tasaf III inaendelea kuhamasisha jamii kuwathamini wazee na kutoa elimu ya ujasiliamali, uwekaji wa akiba na uwekezaji kwa walengwa wote wa mfuko huo. Pia kuhimiza ushiriki wa wazee katika shughuli za maendeleo na uzalishaji mali, kuunda vikundi vyao waweze kutambulika na kupata fursa za kufadhiliwa na wahisani.
Maperece inavyowatetea wazee
Mratibu na Mweka Hazina wa Shirika la Maperece, Julius Mwengela, anaamini kwamba masuala ya wazee yatapata ufumbuzi iwapo serikali na wadau wengine zikiwamo taasisi za kiraia zitayaingiza kwenye mipango yao ya maendeleo.
Mwengela anasema Shirika la Maperece linalotambuliwa kama kinga ya wazee linakusudia kuwafanyia wazee mambo mazuri zaidi kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano.
“Tuwaone wazee kama ni rasilimali katika jamii yetu. Sisi Maperece ni wadau wa kusukuma masuala ya wazee, tunaomba madiwani, mbunge na viongozi wa Serikali kwa jumla mtuunge mkono ili pia tuweze kutokomeza mauaji dhidi ya wazee wetu,” anasema.
Shirika la Maperece lilianzishwa mwaka 1993 na kupata usajili kamili mwaka 1994 kwa ajili ya kutetea haki za wazee chini ya ufadhili wa Shirika la HelpAge International.
Kauli ya DC, Mbunge Magu
Mkuu wa Wilaya ya Magu, Yunus, anakiri kuwa Shirika la Maperece limepanda mbegu nzuri inayozaa matunda ya kuwanasua wazee kutoka kwenye matatizo yanayowaandama katika jamii.
“Watu wengi kutoka wilaya na mikoa mbalimbali na hata nje ya nchi wanakuja Magu kujifunza namna ya kushughulikia masuala ya wazee kwa ufanisi. Maperece imeifanya Magu kuwa mfano mzuri wa kuigwa,” anasema na kuongeza: “Wazee ni suluhu ya jamii, tusiwasahau kwenye bajeti zetu kwani wana mchango mkubwa katika jamii ikiwa ni pamoja na kulea wajukuu. Tukiwatambua wazee na mahitaji yao wataishi kwa faraja.”
Kwa upande mwingine, wazee wamekuwa wakiomba kuimarishiwa ulinzi wasiendelee kuuawa kutokana na imani za kishirikina, lakini pia Sera ya Taifa ya Wazee ya Mwaka 2003 itungiwe sheria itakayowapa nguvu ya kudai haki zao.
Mbunge wa Magu (CCM), Kiswaga, anaunga mkono msukumo huo akisema; “Sheria ya wazee inatakiwa kutungwa haraka ili matakwa yao yatimizwe ikiwa ni pamoja na kulipwa pensheni jamii. Mimi hili nitalibeba, nitalipeleka bungeni ili kuwasaidia wazee wasiendelee kuishi katika mazingira magumu.”
Hoja ya kwamba baadhi ya wazee wamekuwa wakibebeshwa mzigo wa kulea wajukuu imethibitishwa na Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Magu, Coletha Sanga, akisema juhudi za kupiga vita kasumba hiyo zinaendelea. “Tunapiga vita kasumba ya watu kuwapeleka watoto wao kulelewa na babu na bibi zao vijijini, kisha wao kurudi mijini kuendelea kutafuta watoto wengine,” anasisitiza.
Juhudi za Jeshi la Polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Justus Kamugisha, anasema jeshi hilo linaendelea kukazania suala la kuishawishi jamii kuondokana na imani potofu za kuwahusisha wazee na matukio mabaya yanatokea katika jamii.
Anasema jitihada hizo zitahusisha ushirikiano wa karibu na wadau wengine zikiwemo asasi za kiraia na madhehebu ya dini ili pia kuwahimiza wanajamii kuepuka kasumba ya kujichukulia sheria mkononi.
“Tutaendelea kuimarisha vikosi kazi vyetu ili viweze kufanya kazi kwa weledi na ufanisi mkubwa katika kuwalinda wazee dhidi ya vitendo vya kushambuliwa na kuuawa,” anasema.
Mganga wa jadi azungumza
Mwenyekiti wa waganga wa tiba asilia wilayani Magu, Makoye Kanyerere, ameahidi kusimamia kwa dhati maazimio ya kuwafichua wapiga ramli ili washughulikiwe kisheria, lakini akiomba usiwepo unyanyasaji unaofanywa na askari polisi dhidi ya waganga wa jadi wasiyo na hatia.
“Niko tayari, nitashirikiana na polisi kupambana na wauaji wa wazee na albino, tutadhibiti upigaji ramli miongoni mwetu, lakini polisi nao wafanye kazi kwa haki, wasionee na kunyanyasa waganga wa tiba asilia wasiyo na tatizo,” anasema Kanyerere.
Mapendekezo ya HelpAge International
Shirika la HelAge International linaamini kwamba kukosekana kwa mipango thabiti, fedha na nguvu ya pamoja baina ya wizara na mashirika husika kunadhoofisha mapambano dhidi ya mauaji ya wazee nchini.
“Mauaji ya wazee yanachukuliwa kwa sura ya imani za uchawi, hivyo kujenga dhana kuwa haiwezekani kuyathibitisha mahakamani kama ilivyo kwa kesi nyingine,” anasema Mratibu wa HelpAge International nchini, Joseph Mbasha.
Anaendelea; “Mara nyingi viongozi wa serikali, wanasiasa na asasi za kiraia hukaa kimya wakati makosa makubwa dhidi ya binadamu kama haya (mauaji ya wazee) yanapofanyika. Lakini pia, Sera ya Taifa ya Wazee ya Mwaka 2003 imecheleweshwa kutungiwa sheria kwa miaka 13 sasa.”
Shirika hilo linapendekeza kwamba wadau muhimu wakiwamo Jeshi la Polisi, Mahakama, Usalama wa Taifa na watetezi wa haki za binadamu kuhakikisha wanakuwa na mpango maalum unaopimika wa kupambana na mauaji ya wazee.
“Mahakama zifikirie namna ya kuwa na utaratibu maalumu wa kuharakisha kesi za mauaji ya wazee na agenda ya mauaji hayo iwe ya kudumu katika vikao na mikutano, hasa maeneo yanayoathirika zaidi,” anaongeza Mbasha.
Hata hivyo, mapambano dhidi ya mauaji ya wazee yamekuwa yakikabiliwa na vikwazo mbalimbali ikiwa ni pamoja na waathirika wa matukio hayo kutokuwa tayari kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kuwabaini wahalifu husika kutokana na baadhi ya mauaji kupangwa na wanandugu/wanafamilia.
Pia kumekuwepo na vitisho vya kuuawa kwa wahanga wanaojaribu kufichua taarifa za kuwezesha kuwakamata watuhumiwa, lakini pia baadhi ya viongozi wa kijamii wamekuwa sehemu ya tatizo kutokana na wao kuamini masuala ya ushirikina.
Aidha, katika baadhi ya maeneo, hususan vijijini kumekuwepo na kikwazo cha miundombinu mibovu isiyopitika kwa urahisi, hivyo kusababisha upelelezi wa mauaji ya wazee na uhalifu mwingine kuchukua muda mrefu na kuwakatisha tamaa waathirika.
Lakini pia, kumekuwepo na kikwazo cha uelewa mdogo miongoni mwa jamii husika na wengi wao hawana imani ya dini na hofu ya Mungu. Vikwazo hivyo vinahitaji nguvu ya pamoja kuvipatia ufumbuzi wa haraka ili kunusuru maisha ya wazee katika jamii.
Chanzo: RAIA MWEMA
No comments:
Post a Comment