(Chanzo: gazeti la mwananchi, jan 2014)
Kwa Watanzania wenye umri mkubwa waliopata kusoma historia
au kusikia hadithi za makabila, hasa ya Wasukuma na Wanyamwezi, hawakukosa
kusikia habari ya Ng’wanamalundi.
Mtu huyo aliyewahi kuutingisha utawala wa Wajerumani,
alizaliwa katika ukoo wa kawaida akiwa mcheza ngoma mashuhuri, mwaka wa
kuzaliwa kwake haufahamiki ila alifariki dunia mwaka 1936, akiwa tayari mtu
mzima.
Watu wengi wamekuwa wakimjadili kwa maoni tofauti, wengine
wakimsifu kama shujaa huku wengine wakihusisha uwezo wake na nguvu za giza.
Katika makala hii usahihi wa historia yake unaelezwa na
mjukuu wake wa pili, Kishosha Sitta (80) mkazi wa Kijiji cha Mwalugulu wilayani
Kahama mkoani Shinyanga, anayesimulia alivyomfahamu babu yake huyo.
Sitta anaanza kueleza kuwa jina halisi la babu yake halikuwa
Ng’wanamalundi bali lilikuwa Igulu Bugomola, ambaye alizaliwa katika Kijiji cha Mwakubunga Nera wilayani Kwimba mkoani Mwanza.
Ng’wanamalundi alikuwa mtoto pekee wa kiume na wa mwisho
kati ya wanne, kwa baba yake Bugomola na mama yake, Ngolo Igulu.
Sitta anasema Igulu (Ng’wanamalundi), alikuwa na tabia ya
uzururaji tangu utotoni na mara nyingi haikuwa rahisi kumkuta nyumbani. Alikuwa
mashuhuri kutokana na umahiri wake wa kucheza ngoma na mara nyingi alipokuwa
akitembea mitaani alifuatwa na kundi kubwa la watoto.
“Hali hiyo iliwachukiza wazazi wengi wenye watoto waliokuwa
wakiambatana naye, kiasi cha kumchukia hata Ng’wanamalundi mwenyewe, kutokana
na watoto wengi hasa waliokuwa wakitoka familia za wafugaji kutoweka na hiki
kilikuwa chanzo cha mifugo mingi kupotea baada ya kutelekezwa na watoto hao,”
anasema Sitta.
Hali ya kuchukiwa kwa Ng’wanamalundi ilienea pale kijijini
kiasi cha kuanza kumkebehi, hasa kutokana na umbo lake refu na miguu yake
myembamba kuanzia magotini hadi kwenye makanyagio, ikiwa mirefu kuliko kawaida.
Sitta anasema hali hiyo ilisababisha kumdhihaki na
kumwongezea chuki zaidi kwa wanakijiji wa eneo hilo waliodiriki kumtukana kwa
lugha ya Kisukuma; “Mamirundi galyo lilihumbura bana bise” ikiwa na maana
‘mamiguu yake marefu linarubuni watoto wetu”.
Hapo ndipo ukawa mwanzo wa kufutika kwa jina la Igulu na
kuwa Ng’wanamalundi, jina ambalo lilitokana na urefu wa miguu yake na kila kona
walimuita hivyo.
Kadiri siku zilivyosonga mbele Ng’wanamalundi alizidi
kujiimarisha katika kikundi chake cha ngoma ambayo ilivuta vijana wengi, pia
baadaye ilitumika kama jeshi la kukodiwa na Watemi inapotokea vita.
Pamoja na wazazi kumchukia sana, lakini vijana walimpenda na
kikundi chake kikubwa cha ngoma kilipendwa na kutumika katika sherehe
mbalimbali kwenye familia za Kitemi za wakati huo.
Mwanzo wa miujiza
Sitta anasema Ng’wanamalundi na wenzake wawili walikwenda
kwa bibi kizee mmoja kutafuta dawa itakayowasaidia katika shughuli zao za
kucheza ngoma, ambapo bibi kizee huyo alikubali kuwasaidia.
“Tujagi lolo ngh’wiporu bana bane akiwa na maana kwamba
twendeni sasa porini watoto wangu. Mwanamalundi aliongozana na wenzake pamoja
na kizee huyo mpaka porini.
“Walipofika porini bibi Kizee huyo alikamata vinyonga watatu
na kuwaekea vichwani, kwa kila mmoja na kuendelea kusonga mbele porini, baada
ya kufika katikati ya pori nene, kizee aliwaambia wote wasimame,” anasimulia
Sitta.
Anasema baada ya kusimama aliamuru kila mmoja achimbe shimo
lenye urefu hadi kiunoni, na baada ya kukamilika kwa mashimo hayo aliwaambia
wakusanye kuni na kuzitumbukiza.
Baada ya kazi hiyo kukamilika Sitta anasema walipekecha moto
na kuziwasha zile kuni na moto uliposhika kasi aliwachukua wale vinyonga watatu
na kuwawekea dawa mdomoni na kisha aliwatupia ndani ya moto huo, wakateketea
wote.
“Ng’wanamalundi na wenzake wakiwa bado wanashangaa vinyonga
hao kuungua, ghafla alitokea kifaru kwenye moto huo na kuanza kuwakimbiza hovyo
na wote wakasambaritika na bibi kizee wao,” anasema na kuongeza;
Ngw’anamalundi alikimbia akapanda juu ya mti, kifaru alifika
kwenye shina la mti na kuanza kuliparua kwa hasira na baadaye aliondoka kabla
hajafika mbali alimuona yule bibi kizee akikutana na faru huyo.”
Anasema Ng’wanamalundi alishuhudia kifaru akimrarua rarua
bibi kizee mpaka akafa, kisha kifaru alitoweka kusikojulikana huku akimuacha
Ng’wanamalundi asijue la kufanya juu ya mti.
Sitta anasema: “Ng’wanamalundi baada ya muda alishuka juu ya
mti na kwenda kwenye maiti ya yule bibi kizee, akaamua aibebe mgongoni
airejeshe nyumbani, lakini kabla hajafika mbali alisikia sauti ikisema, “Igulu
bajahe abiyo akiwa na maana Igulu wenzako wamekwenda wapi”.
Sauti hiyo ilimshtua Ng’wanamalundi ambaye alimshusha bibi
kizee mgongoni mwake na akashangaa kumuona akiwa hai asiyekuwa na jeraha
lolote, kama alivyokuwa baada ya kushambuliwa na faru.
“Igulu tujage ahante ugo waliwalinaga, akiwa na maana Igulu
twende kwenye mti uliokuwa umepanda, Ng’wanamalundi aliongozana na bibi kizee
huyo mpaka kwenye ule mti aliyachukua magamba ya mti yaliyokuwa yameparuliwa na
faru,” anasema Sitta.
Baada ya zoezi hilo kukamilika bibi kizee huyo
alimtengenezea dawa aliyokuwa akihitaji, na kisha Mwanamalundi alirejea kwao
kuendelea na shughuli zake za ngoma aina ya Kahena, ambayo mpaka leo inaendelea
kwa jina lingine la Wigashe.
Anakutana na Mtemi Chlya
Sitta anaongeza kuwa, Ng’wanamalundi akiwa katika harakati
zake za kujiimarisha katika masuala ya dawa zake za ngoma, alienda kuchimba
kwenye pori la Mwandutu huko wilayani Maswa sasa ni Wilaya ya Kishapu, ambalo
lilikuwa katika miliki ya Mtemi Chalya.
Imeelezwa kuwa baada ya kufika katika pori hilo akiwa na
wafuasi wake wakiendelea kuchimba dawa, ghafla alitokea Mtemi Chalya na
kumuuliza; “Ubebe nani wakuwilaga kwiza ngh’wiporu lyane” akiwa na maana; “Wewe
nani amekuambia kuja kwenye pori langu?”
Mwanamalundi alimjibu; “ Ubebe ulintemi wa banhu pye nu nene
nding’wenekele wa maporu pyee.” Akiwa na maana “Wewe ni Mtemi wa watu wote na
mimi ni mmiliki wa mapori yote”. Kauli hiyo ilimuudhi Mtemi Chalya.
Anasema, kufuatia kauli hiyo Mtemi Chalya aliita jeshi lake
kwa lengo la kuja kumkamata, lakini walishangaa baada ya kufika katika eneo
waliloelezwa na Mtemi wao kuwa Ng’wanamalundi anatakiwa kukamatwa na kuuawa,
lakini walishindwa baada ya kukuta simba wengi sana.
Jeshi hilo na Mtemi ilibidi kukimbia kujiokoa kwani simba
hao walianza kuwashambulia, wengine walitawanyika ovyo na baadhi yao wachache
tu ndiyo walionusurika.
Lakini cha kushangaza walipofika walimkuta Ng’wanamalundi na
wafuasi wake wakimalizia kula chakula nyumbani kwa Mtemi Chalya, ambaye hata
yeye alichanganyikiwa na kushindwa kuongea lolote.
Sitta anasema, Ng’wanamalundi baada ya kumaliza kula chakula
kwa Mtemi Chalya aliondoka na wafuasi wake na akapitia kwenye lile pori
akachimba dawa zake na kuondoka kwenda kuendelea na maisha yake.
“Katika ngoma zake; Ng’wanamalundi alikuwa na tabia ya
kuwatahadharisha mashabiki wake kuacha kwenda wakiwa wamejipaka dawa yoyote
ile, anasema. Aliwaambia: “Bing’we akwiziza munho wibilaga bugota bosebose ulu
kutora akotora henaha,ulo nsabo akupandika heneha.”
Kauli hiyo ilikuwa na maana nyie asije mtu amejipaka dawa
yoyote hapa kama ni kuoa, ataoa hapahapa kama ni mali atapata hapahapa, hata
hivyo kuna wale walipuuza kauli hiyo kwa kuja wamejipaka dawa kwa lengo la
kujipima uwezo wa dawa zao. Lakini hawakufanikiwa na badala yake walikufa.
inaendelea sehemu ya pili.....
inaendelea sehemu ya pili.....
No comments:
Post a Comment