Saturday, June 18, 2016

UWAJIBIKAJI WA VIONGOZI KWA USTAWI BORA WA MWANANCHI.


BY NGUDU NYUMBANI BLOG
18/06/2016

Katika jitihada za kuona jamii yetu inapiga hatua moja zaidi mbele, na pengine kutoka hali iliyopo sasa kuna haja ya uwajibikaji mkubwa kwa viongozi na wananchi kwa ujumla.

Nilikuwa najaribu kupitia ripori ya mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali(CAG) ya mwaka 2015, Kuhusu ukaguzi wa taarifa za fedha za miradi ya mendeleo kwenye halmashauri zetu.
Hasa nikiangalia kwenye jamii yetu ya Kwimba, ripoti ni nzuri kidogo tofauti na ya miaka kadhaa iliyopita ambapo wilaya haikuwa na hati ya kuridhisha kwa maana ya kuwa na kasoro na mapungufu mengi katika kutekelza miradi ya maendeleo.

Katika miradi mitano ya maendeleo iliyokaguliwa na kutolewa ripoti, walau miradi minne imefanya vizuri kasoro mmoja ambao haujafanya vizuri. Programu ya maendeleo ya kilimo(ASDP), mfuko wa afya(HBF), mfuko wa barabara(RF) na Programu ya maendeleo ya sekta ya maji(WSDP) ndiyo iliyopata hati inayoridhisha, huku mfuko wa maendeleo ya jamii(TASAF) ukipata hati isiyoridhisha.

Pamoja na  baadhi ya miradi hiyo kufanya vizuri lakini ripori imetaja changamoto na mapungufu mbalimbali ambayo serikali inapaswa kutilia mkazo ili kuboresha miradi hiyo na mingine mingi inayofanyika katika jamii zetu.
Mfano mpango wa maendeleo wa kilimo wa wilaya(DADP), unashughulikia vipi changamoto anazokumbana nazo mkulima wa pamba, alizeti na mazao mengine anayolima mkulima wa Kwimba?. Vipi kuhusu kilimo cha umwagiliaji kwa baadhi ya maeneo kinapewa msisitizo gani katika kumkomboa mwananchi wa kawaida anayetegemea kilimo kujikimu na hali ya maisha.

Katika taarifa mbalimbali za serikali, Halmashauri zote nchini zimeshauriwa kutekeleza maazimio 12 yaliyoazimiwa na wakuu wa mikoa, mkoani Dodoma mwaka 2014 ili kuainisha changamoto za ukosefu wa ajira kwa vijana na utatuzi wake.

 Katika hili ushirikishwaji wa mwananchi ni muhimu sana ili halmashauri ziweze kubaini changamoto haswa zinazowakabili vijana wengi kwenye suala la ajira na namna bora ya kushughulika nazo, ikiwa ni pamoja na Mipango mathubuti ya kuwasaidia. Niliwahi kuandika huko nyuma nikimshauri diwani wangu kwa niaba ya madiwani wenngine suala la fursa za ujasiliamali.
Pia katika kusomasoma habari mbalimbali niliona habari ya halmashauri moja ambapo baraza la madiwani walipitisha mpango wa bima ya afya ulioboreshwa .unaotolewa na mfuko wa hifadhi za jamii CHF kwa kuwa umepanua wigo wa matibabu kwa wananchi wengi waishio vijijini na kurekebisha masharti ya kujiunga. 
Sina hakika kama kwetu tumefikia huku, kama na kwetu hali ipo hivi basi ni vizuri. Ila kama bado kuna haja ya viongozi tuliowachagua kuangalia uwezekano wa kupendekeza masuala ya muhimu kama haya kama njia mojawapo ya kuboresha ustawi wa wananchi wao.
Suala la watumishi hewa na mishahara hewa kwenye taasisi nyingi za serikali mathalan halmashauri kufikia sasa limefanyiwa kazi kwa ustadi mkubwa kiasi cha kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zinatumiwa na watu wachache. Kia halmashauri ya wilaya ilikwa inawajibika kubaini watumishi hewa kupitia idara zote zilizo chini ya halmashauri hizo.

Zoezi hili linapaswa kuwa endelevu kwa maana ya kudhibiti ufujaji wa mali za umma. Na pia wahusika wote walioiingizia serikali hasara kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria.

Kuanzia april na  mwezi may mwaka huu(2016) kuna mradi wa uimarishaji mifuko ya sekta za umma(PS3) ambapo katika mkoa wa mwanza umeanza na wilaya mbili za KWIMBA na SENGEREMA ambapo mradi huo utatekelezwa kwa miaka mitano katika awamu ya kwanza. mradi unafadhiliwa na shirika la maendeleo la kimataifa la marekani(USAID).
kwa kila mkoa zimetengwa wilaya mbili zenye mahitaji makubwa ya uboreshaji mifumo yake ya sekta za umma.
Matarajio makubwa ya mradi huu utaimarishwa katika ngazi ya kitaifa na katika halmashauri, ili kutumia rasilimali kwa uwazi, kwa kuwezesha ushirikishwaji wa wananchi katika kupanga na kufuatilia na kutoa matokeo ya ufanisi wa kazi kwa kila sekta.
maeneo ya utekelezaji wa mradi huo ni Utawala Bora na Ushirikishwaji wa Raia, Rasilimali Watu, Rasilimali Fedha, Mifumo ya Mawasiliano na Utafiti Tendaji (Operational Research).

Katika hatua nyingine inashauliwa kwamba, kila hamashauri inapaswa kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajiri ya kuviwezesha vikundi mbalimbali vya ujasiriamali mathalan vinavyowahusu vijana na wanawake.  
Hili limekuwa likilalamikiwa kutofanyika kama inavyopaswa, ama kwa wakurugenzi au watendaji wa halmashauri kadhaa kutotenga kiwango hicho cha asilimia kwa kuviwezesha vikundi na kuvisimamia viweze kukidhi matakwa na mahitaji yao na ya jamii nzima kwa ujumla.

Aidha, halmashauri inapaswa kupanga bajeti yake ya miradi ya maendeleo inayopaswa kutekelezwa kabla ya bajeti ya serikali kupitia bajeti za wizara hazijapitishwa na bunge. Hilo limekwisha fanyika kwa halmashauri zote mpaka sasa, na baadhi kuweka wazi Mipango ya mabaraza yao ya madiwani kuhusu utekelezaji wa miradi yao waliyoiainisha katika bajeti zao. 
Sina hakika kama na kwetu wana utamaduni huo wa kuwafanya wananchi wao kujua nini kinapaswa kufanywa na kwa muda gani.

Nilijaribu kupitia mifumo ya bajeti za halmashauri na kuona mpangilio wa vyanzo vya mapato ya upangaji na uendeshaji wa bajeti hizo ambapo ni pamoja na;  Ruzuku kutoka Serikali Kuu; masharti, jumla & sawia; Mapato ya Ndani ya H/M; Fedha za Wahisani; Mikopo toka taasisi za kifedha, ikiwemo LGLB, Municipal Bounds; Michango ya wananchi,taasisi za hiari pamoja na nguvu kazi ya wananchi.

Kufanya kilicho sahihi kunahitaji zaidi muongozo wa maadili sahihi, ni imani viongozi tuliowachagua wakishirikiana na viongozi wandamizi wa serikali kufuata utaratibu sahihi wa kufanya kilich sahihi pia.
Katika kufanikisha hilo kuna mambo kadhaa ya kuzingatia. Moja, kuzingatia taaluma katika kutoa huduma bora na stahiki, pia kufanya kazi kwa bidii, kutokuwa na upendeleo na  kuwa na matumizi sahii ya taarifa za uendeshaji Mipango.

Pili, ni viongozi kuwa waaminifu kwa maana ya kufuata maadili ya kazi wanazozifanya. Na mwisho ni kutimiza wajibu wao. Katika kutimiza wajibu kunahitaji mambo kama utii kwa serikali, Kuwajibika kwa umma, pamoja na Kuheshimu na kutii sheria.

Bila kuzingatia mambo ya msingi kama hayo, ni dhahiri mambo yatakuwa sege mnege kwa sababu kila mtu anaweza kufanya awezalo ilimradi aonekane amefanya jambo.  Siku zote utekelezaji wa Mipango kwa kadri ilivyopaswa ni tiba mujarabu katika kuboresha maisha ya wananchi. uwajibikaji wa viongozi huchochea ustawi bora wa maendeleo ya mwananchi!

Tafakari!
NGUDU NYUMBANI BLOG
nguduone@gmail.com.



No comments:

Post a Comment

Previous Page Next Page Home