Mkuu wa mkoa wa Mwanza Magesa Mulongo
ametoa muda wa siku tano kwa wakazi wa kijiji cha Ndami na jeshi la jadi
Sungusungu wilayani kwimba, kuhakikisha wanampata mtoto mwenye ulemavu wa ngozi
– Alibinism, Pendo Emanuel akiwa hai au amekufa ikiwa ni pamoja na wahusika wa
tukio hilo kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya dola.
Agizo hili la mkuu wa mkoa wa Mwanza Magesa Mulongo,
linakuja kufuatia watu wasiojulikana kumuiba mtoto Pendo Emanuel mwenye ulemavu
wa ngozi majira ya saa 4 usiku Desemba 27 mwaka jana nyumbani kwao katika
kijiji cha Ndami na kutoweka naye kusikojulikana, mkasa ambao umeilazimu kamati
ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Mwanza kuapa kuwa serikali haitalala usingizi
mpaka mtoto huy mwenye umri wa miaka minne apatikane.
Mwenyekiti wa chama cha watu wenye ulemavu wa ngozi
mkoa wa Mwanza Alfred Kapole amesema kuwa miongoni mwa kesi 72 zilizokuwa
mahakamani zikihusu mauaji ya walemavu wa ngozi, ni kesi tatu ndizo
zilizotolewa hukumu mpaka sasa, huku akiilaumu ofisi ya mkemia mkuu wa serikali
pamoja na mahakama kwa kuchelewesha kesi hizo.
Mama mzazi wa mtoto Pendo, Bi. Sophia
Juma pamoja na mkurugenzi wa shirika lisilokuwa la kiserikali la Chiriko Bi.
Specioza Kasoli wamesema kila mtu ana haki ya kuishi na kulindwa na kuongeza
kwamba mtoto huyo ni kati ya watu 74 wenye ulemavu wa ngozi wilayani kwimba na
alikuwa ni mtu wa 9 kwa kupatiwa ulinzi.
Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza
Valentino Mlowola amesema tayari askari polisi wamepiga kambi katika kijiji
hicho kwa kazi moja tu ya kuhakikisha mtoto huyo anapatikana, lakini pia
watuhumiwa wanasakwa kwa udi na uvumba ili wafikishwe mahakamani kwa kosa la
jinai.
No comments:
Post a Comment