Jeshi la polisi mkoani
mwanza linawashikilia watu wanne, akiwemo baba mzazi, Emmanuel shirinde(28) wa
mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, pendo emmanuel ambaye aliporwa na watu
wasiojulikana waliovamia nyumbani kwao
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Valentino
Mlowola, tukio la uporwaji wa mtoto huyo lilitokea Desemba 27, mwaka huu saa
4.30 usiku katika kijiji cha Ndami tarafa ya Mwamashimba wilayani Kwimba mkoani
hapa.
Akifafanua, Kamanda Mlowola alisema siku ya tukio saa 4.30 usiku
Shirinde akiwa amelala nyumbani kwake na familia yake, akiwemo Pendo,
walivamiwa na watu wawili wasiojulikana.
Alisema watu hao walivunja mlango kwa kutumia jiwe kubwa,
maarufu kama ‘fatuma’, ambapo waliingia ndani na kumchukua mtoto huyo huku
wakimzuia baba mtu kupiga kelele.
Kamanda Mlowola alisema baba wa mtoto, alisema baada ya mtoto
wake kuporwa, alisikia mlio wa pikipiki ikiondoka nyuma ya nyumba yake na ndipo
alipotoa taarifa Polisi, ambao walifika eneo la tukio saa 7 usiku.
Alisema kwa kuwa kijiji wanachoishi kipo mpakani mwa wilaya ya
Misungwi na Kwimba, polisi wa wilaya hizo walishirikiana kuwasaka bila
mafanikio.
Hata hivyo, alisema timu ya Polisi kutoka makao makuu, imewasili
ili kusaidiana na polisi wa mkoani hapa kumsaka mtoto huyo ili apatikane akiwa
hai.
“Tunamshikilia baba mzazi ili aweze kutusaidia, mazingira ya
kijiji sio rahisi watu kutoka mbali wakafahamu kama nyumba fulani ina mtu
mwenye ulemavu wa ngozi, lazima waliongozwa na mwanakijiji,” alisema Kamanda.
Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi limeahidi kutoa zawadi
ya Sh milioni tatu kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazowezesha kupatikana
kwa mtoto huyo.
Hili ni tukio la kwanza la kuporwa kwa mtu mwenye ulemavu wa
ngozi mkoani hapa, kuripotiwa tangu mwaka huu uanze na kwamba ni tukio la nne
nchini.
Kamanda Mlowola alitoa rai kwa wananchi wa mkoa wa Mwanza, wenye
taarifa juu mtoto huyo washirikiane na Jeshi la Polisi ili kuokoa maisha ya
mtoto huyo.
Takwimu zilizotolewa na Chama cha Albino Tanzania (TAS) wakati
wa maadhimisho ya Siku ya Amani Kimataifa, zinaonesha kuwa kutoka mwaka 2006
hadi Septemba 2014, albino 74 wameshauawa kikatili, huku 56 wakinusurika kifo
na 11 kati yao wameongezewa ulemavu mwingine wa kudumu.
No comments:
Post a Comment