Utangulizi
Ndugu
zangu;
Watanzania
Wenzangu;
Kama ilivyo ada imefikia
siku ya kuuaga mwaka mmoja na kuukaribisha mwaka mwingine. Leo tunauaga mwaka
2014 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2015. Tunamshukuru Muumba wetu mwingi wa
rehema kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kuifikia siku ya leo. Kwa ndugu na
jamaa zetu ambao hawakujaliwa kuiona siku ya leo tuzidi kuwaombea mapumziko
mema. Nasi tumuombe Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema atujaalie umri
mrefu, afya njema na mafanikio tele kwa kila tuliombalo katika mwaka 2015 na
miaka ijayo.
Ndugu
wananchi;
Hizi ni salamu zangu za mwisho za mwaka mpya kutoa nikiwa Rais wa nchi yetu.
Mwakani salamu kama hizi zitatolewa na Rais wetu mpya. Mimi wakati huo
nitakuwa raia wa kawaida kijijini kwangu Msoga nikifuatilia kwenye TV na radio
hotuba ya Rais wa Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi yetu akitoa salamu zake za
kwanza za mwaka mpya, itakuwa siku ya furaha na faraja kubwa kwangu.
Hali ya Usalama
Ndugu
Wananchi;
Tunaumaliza mwaka 2014 kwa
salama na amani. Mipaka yetu iko salama na hakuna tishio lolote la
kiusalama kutoka ndani au nje ya nchi yetu. Uhusiano wetu na nchi jirani na
nyinginezo duniani ni mzuri. Hakuna nchi iliyo adui au tunayoitilia shaka
kuwa na njama za kuhatarisha usalama wa Tanzania. Nawapongeza
wanadiplomasia wetu pamoja na viongozi na watendaji wa vyombo vya ulinzi na
usalama kwa kuendelea kuifanya nchi yetu kuwa salama.
Uhalifu
Unapungua
Ndugu
Wananchi;
Taarifa za Polisi zinaonyesha kuwa, mwaka 2014 vitendo vya uhalifu vimepungua
ikilinganishwa na mwaka 2013. Mwaka huu, matukio ya uhalifu yaliyoripotiwa Polisi yalikuwa 64,088 ikilinganishwa na matukio 66,906 katika mwaka 2013. Haya ni
matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi wakishirikiana na vyombo
vingine vya usalama pamoja na raia wema. Naomba ushirikiano huu uendelee
mwaka ujao na miaka ijayo ili tuweze kupata mafanikio makubwa zaidi.
Ajali
za Barabarani
Ndugu
Wananchi;
Nimefarijika kusikia pia
kuwa matukio ya ajali za barabarani nchini nayo yanaendelea kupungua. Mwaka huu
kumetokea ajali 14,048zilizosababisha vifo vya
watu 3,534 na wengine 16,166 kujeruhiwa. Mwaka 2013 kulitokea ajali 22,383 zilizosababisha vifo 3,746 na majeruhi19,433. Hivyo mwaka huu
kulikuwa na ajali 8,335, vifo 212 na majeruhi 3,267 pungufu kuliko mwaka jana. Huu ni mwelekeo mzuri na wa kutia moyo
ingawa bado ni nyingi mno. Naomba yale tuliyoyafanya yaliyotuwezesha kupata
unafuu huu mwaka huu yaendelezwe maradufu mwaka 2015 na miaka ijayo.
Ugaidi
Ndugu
Wananchi;
Mwaka huu tumefanikiwa kutambua mtandao wa viongozi na washirika wao
wanaotuhumiwa kupanga na kufanya mashambulizi ya kigaidi kwa kutumia mabomu na
kumwagia watu tindikali Tanzania Bara na Zanzibar. Watu 112 wanaotuhumiwa kujihusisha
na vitendo vya ugaidi wametiwa nguvuni. Tayari watuhumiwa 87 kati yao wameshafikishwa
mahakamani na waliosalia watafikishwa wakati wo wote. Uchunguzi
unaendelea ili kuwatambua wahusika wengine ambao hawajakamatwa.
Ndugu
wananchi;
Kwa niaba ya Watanzania wenzangu wote, natoa pongezi nyingi kwa vyombo vyetu
vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri waliyofanya ya kutambua mtandao wa ugaidi
nchini na kuchukua hatua thabiti za kuudhibiti. Hali kadhalika
nawashukuru raia wema waliotoa taarifa zilizowezesha haya kufanyika.
Hatupaswi kubweteka wala kudhani kuwa mambo yamekwisha. Lazima
tuendelee kuchukua tahadhari muda wote kwani hatujui adui anapanga kufanya
hujuma gani, lini na wapi.
Dawa za Kulevya
Ndugu Wananchi;
Tumeendelea
kupata mafanikio ya kutia moyo katika vita dhidi ya biashara na matumizi ya
dawa za kulevya nchini. Mwaka huu watuhumiwa 935 wakiwemo vigogo wa
biashara hii haramu duniani wamekamatwa. Jumla ya kesi 19 zimefunguliwa
Mahakamani. Aidha, kiasi cha kilo 400 za heroine, kilo 45 za cocaine na kilo 81,318 za bangi
zimekamatwa. Narudia kutoa pongezi nyingi kwa Kikosi Kazi Maalum cha
Kukabiliana na dawa za kulevya nchini kwa mafanikio yanayoendelea kupatikana.
Matunda ya kazi yao tunayaona. Naomba juhudi ziongezwe maradufu mwaka
ujao na miaka ijayo. Serikali itaendelea kuwaunga mkono.
Ndugu wananchi;
Kama
nilivyoahidi mwaka jana, Muswada wa Sheria ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za
Kulevya umeshasomwa kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa Novemba, 2014 wa Bunge
letu tukufu. Pamoja na kupendekeza kuongeza adhabu kwa makosa ya kujihusisha na
dawa za kulevya, Muswada huo pia unapendekeza kuanzisha chombo kipya chenye
nguvu cha kuzuia na kupambana na dawa za kulevya. Muswada huu ukipitishwa
na kuwa Sheria tutakuwa tumeongeza nguvu ya mapambano dhidi ya biashara na
matumizi ya dawa za kulevya nchini.
Ujangili
wa Wanyamapori
Ndugu
Wananchi;
Katika mwaka tunaomaliza
leo mapambano dhidi ya ujangili na biashara
haramu ya bidhaa zinazotokana na wanyama pori yameimarishwa. Kwa ujumla kasi ya
ujangili imeendelea kupungua. Katika mwaka 2014 ndovu 114 waliuawa ikilinganishwa na
ndovu 219waliouawa mwaka 2013 au
ndovu 473 mwaka 2012.
Aidha,
majangili 1,354 wamekamatwa na pembe za ndovu 542 na silaha mbalimbali 184 nazo zilikamatwa. Naamini uamuzi wa kuifanya Idara ya Wanyamapori
katika Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa Wakala yaaniTanzania Wildlife Agency (TAWA) kutaongeza nguvu ya kuhifadhi wanyama pori na mapambano
dhidi ya ujangili.
Natoa pongezi nyingi kwa askari wa wanyamapori, Jeshi la Polisi na vyombo
vingine vya Serikali na raia wema kwa kazi nzuri wanayoendelea kufanya na
mafanikio yanayoendelea kupatikana. Juhudi za kupambana na ujangili na
biashara haramu ya bidhaa zinazotokana na wanyama pori zitaendelezwa kwa nguvu
zaidi mwaka ujao 2015 na miaka inayofuatia. Napenda kutumia fursa hii
kuwashukuru kwa dhati marafiki zetu wa maendeleo wanaotuunga mkono kwa hali na
mali katika mapambano haya. Naomba waendelee kutusaidia.
Hali
ya Uchumi Jumla
Ndugu
wananchi;
Mwaka 2014 ulikuwa mzuri kwa uchumi wa taifa. Uzalishaji katika sekta nyingi
ulikuwa ni mzuri. Ndiyo maana tunategemea kuwa tutafikia au hata kuvuka lengo
tulilojiwekea la pato la taifa kukua kwa asilimia 7.4 mwaka huu. Mwaka 2013 pato la taifa lilikua kwa asilimia 7.3. Mfumuko wa bei uliendelea kushuka na kufikia asilimia 5.8 Novemba, 2014
ukilinganisha na Januari 2014 ulipokuwa asilimia 6.0. Hali nzuri ya
upatikanaji wa chakula nchini imesaidia sana kufanya mfumuko wa bei kuendelea
kushuka. Ni matumaini yangu kuwa mfumuko wa bei utaendelea kushuka
na kufikia asilimia 5 ifikapo Juni, 2015.
Mauzo
Nje
Ndugu
Wananchi;
Mauzo
nje yameendelea kuongezeka. Katika kipindi kilichoishia Oktoba 31, 2014,
Tanzania iliuza nje bidhaa na huduma zenye thamani ya dola za Marekani milioni 8,503.9 ukilinganisha na mauzo ya dola milioni 8,332.5 katika kipindi kama hicho
mwaka 2013. Mapato yetu yangekuwa makubwa zaidi kama bei za kahawa, chai,
korosho na pamba zisingeanguka au bei ya dhahabu nayo isingepada.
Akiba
ya Fedha za Kigeni
Ndugu
Wananchi;
Akiba
yetu ya fedha za kigeni ilikuwa Dola za Marekani milioni 4,251.8 kwa kipindi kilichoishia Novemba 30, 2014.
Kiasi hicho kinatuwezesha kuagiza bidhaa toka nje kwa miezi 4.1. Hii ni chini ya lengo letu
la kuwa na akiba ya fedha za kigeni ya kuagiza bidhaa kwa miezi minne na nusu. Hata hivyo, sina wasiwasi kabisa
kwamba tofauti hii ndogo tutaweza kuiziba mwaka 2015.
Mapato
ya Serikali
Ndugu
Wananchi;
Makusanyo
ya mapato ya Serikali kwa mwezi, kati ya Julai hadi Novemba, 2014 yaliongezeka
kutoka shilingi bilioni 3,555.5 kipindi kama hicho mwaka 2013 hadi shilingi bilioni 3,924.1 mwaka huu. Hata hivyo, makusanyo hayo yalikuwa asilimia 90 ya lengo tulilojiwekea la kukusanya shilingi bilioni 4,459.7. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato, zipo sababu mbalimbali
zilizosababisha lengo lisifikiwe katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa
2014/2015. Hatua zipasazo zinaendelea kuchukuliwa kurekebisha mambo hayo
ili katika nusu ya pili ya mwaka huu wa fedha makusanyo yafikie lengo na
ikiwezekana yazidi ili kufidia pengo la nusu ya kwanza.
Takwimu
Mpya za Pato la Taifa
Ndugu
wananchi,
Ni utaratibu wa kawaida wa
nchi zote duniani kuwa na mwaka unaotumika kuwa kizio (base year) cha kukokotoa
takwimu za Pato la Taifa. Ni utaratibu wa kawaida pia kwa kila
baada ya muda fulani mwaka wa kizio hubadilishwa. Lengo ni kuboresha
takwimu husika. Katika marekebisho hayo pia huingizwa thamani ya bidhaa na
huduma mpya katika pato la taifa na kuziondoa zilizotoweka ili kutoa picha
halisi ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Katika miaka ya hivi
karibuni nchi za Ghana (mwaka 2010), Nigeria (mwaka 2013) na Kenya (mwaka
2014) wamefanya marekebisho ya takwimu zao za pato la taifa. Na sisi Tanzania
tumefanya hivyo mwaka huu (2014). Hii ni mara ya tano kwa nchi yetu
kurekebisha takwimu za pato la taifa. Mara nne zilizopita ilikuwa mwaka
1966, 1976, 1992 na 2001.
Ndugu
wananchi;
Ofisi
ya Taifa ya Takwimu imekamilisha marekebisho ya takwimu za pato la taifa
na kukokotoa takwimu mpya kwa kutumia mwaka 2007 kama mwaka wa kizio.
Kutokana na marekebisho yaliyofanyika, pato la taifa kwa mwaka 2013 ni shilingi trilioni 70 kwa kutumia bei za mwaka
2007. Ukitumia bei za mwaka 2001, pato la taifa kwa mwaka 2013 ni shilingi trilioni 53.17. Kuongezeka kwa pato
la taifa kumeongeza pia pato la wastani la kila Mtanzania kutoka shilingi 1,186,200 (sawa na US$ 742) kwa bei za mwaka
2001 hadi shilingi 1,560,050 (sawa na US$ 977) kwa bei za mwaka 2007.
Kilimo
na Chakula
Ndugu
Wananchi;
Mwaka
2014 ulikuwa mzuri sana kwa uzalishaji wa mazao ya chakula nchini. Uzalishaji
ulikuwa tani milioni 16.02 ukilinganisha na uzalishaji wa tani milioni 14.38 mwaka wa jana 2013. Hili ni ongezeko la tani milioni 1.64. Kwa mujibu wa mahitaji yetu ya chakula nchini kuna ziada yatani milioni 3.25. Katika ziada hiyo, mahindi
yanachangia tani milioni
1.55, mchele tani 794,000 na kiasi kinachobakia
kinachangiwa na mazao mengine ya chakula.
Ndugu
wananchi;
Kuna
jambo moja muhimu kuhusu ununuzi wa nafaka ambalo ningependa
kulifafanua. Naomba ieleweke kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula
(NFRA) sio mnunuzi wa mahindi yote, mpunga wote na mtama wote
unaozalishwa na wakulima nchini. Wakala hununua sehemu ndogo tu ya
nafaka ya ziada iliyozalishwa na hununua kwa ajili ya kuweka akiba ya taifa ya
chakula cha kutumika wakati wa dharura ya watu kupata tatizo la njaa.
Aidha, Wakala hununua kiasi kinacholingana na uwezo wa maghala yake
kuhifadhi. Kwa sasa uwezo wa maghala yetu ni kuhifadhi tani 246,000 ingawaje tunaendelea
kujenga maghala mengine mpaka tufikie uwezo wa kuhifadhi tani 400,000 ifikapo 2015. Hivyo basi kwa Wakala kununua tani
292,415.41 mwaka huu ina maana kwamba
kiasi cha karibu tani 50,000 zinahifadhiwa nje ya maghala kwa kutumia maturubai. Huu siyo
utaratibu mzuri na haifai kuendelea nao kwani kuna hatari ya nafaka hiyo
kuharibika na kuzua mgogoro mkubwa siku moja.
Ndugu
wananchi;
Baada
ya NFRA kununua tani 292,415.41 kuna takribani tani milioni 2.96 za nafaka ya ziada ambayo
iliyobaki mikononi mwa wakulima. Mategemeo yetu ni kuwa wafanyabiashara wetu
watanunua nafaka hiyo kwa ajili ya kuuza mijini na kwingineko inakohitajika.
Bahati mbaya mwaka huu kama ilivyokuwa mwaka wa jana,
wafanyabiashara wetu hawakuweza kununua nafaka yote ya ziada ambayo Serikali
haikuweza kununua kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Hali hii
imezua tatizo ambalo Serikali kwa kushirikiana na wafanyabiashara nchini hatuna
budi kulitafutia majawabu. Tunalazimika kutafuta masoko mengine ndani na
hata nje ya nchi ya kuuza mahindi, mpunga na mtama wa ziada. Nimeagiza
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na Wizara ya Viwanda na Biashara kukaa
chini na kushirikiana na wafanyabiashara kulitafutia ufumbuzi suala hili lenye
maslahi makubwa kwa wakulima na nchi yetu kwa jumla.
Ndugu
Wananchi;
Katika
mazingira haya, ninapopata taarifa ya kuwepo watu wanaotaka kuuza mahindi
nje ya nchi lakini wanawekewa vikwazo na maafisa wa Serikali
inanishangaza na kunisikitisha. Nawataka wale wote wanaofanya hivyo
waache mara moja na badala yake wawasaidie wafanyabiashara hao
kufanikisha azma yao. Hali kadhalika, tuwashawishi watu wengine nao wajitokeze
kufanya biashara hiyo. Jambo muhimu ninalopenda kulisisitiza ni
kwamba pawepo na utaratibu mzuri ili biashara hiyo ifanywe kwa kutumia njia
halali na zilizo wazi. Kutumia njia za panya hakukubaliki na wala hakuna
sababu ya kufanya hivyo.
Miradi
ya Kimkakati
Ndugu
wananchi;
Katika mwaka 2014
utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa
Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16) umeendelea vizuri. Tunayo matumaini makubwa
kwamba katika mwaka 2015 miradi mingi itakamilika.
Tuanze
na Mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara na Songosongo hadi Dar es
Salaam. Mradi huu unategemewa kukamilika Januari, 2015. Utakapokamilika
utatuwezesha kutimiza lengo letu la kuzalisha MW 2,780 za umeme ifikapo 2016.
Mipango ya kupata ardhi ya ujenzi wa mitambo ya kuchakata gesi asili kuwa
ya kumiminika (LNG) ili iweze kusafirishwa kwenda kwenye masoko, inakwenda
vizuri.
Ndugu
Wananchi;
Utekelezaji
wa mradi mkubwa wa kimkakati wa kusambaza umeme vijijini umeendelea vizuri na
tumepata mafanikio makubwa yasiyokuwa na mfano wake katika historia ya
nchi yetu. Hadi kufikia Novemba, 2014, jumla ya vijiji 3,836 vimepatiwa umeme na
vingine 1,500 vinategemewa kupatiwa umeme ifikapo Juni, 2015. Hivyo basi,
vijiji 5,336 kati ya vijiji 12,423 vya Tanzania Bara vitakuwa vimepatiwa umeme. Hii ni sawa naasilimia 43 ya vijiji vyote nchini vitavyokuwa vimepata umeme. Hivi sasa
wananchi milioni 17.3 nchi nzima sawa asilimia 36 wamefikiwa na huduma
ya umeme ikilinganishwa na watu milioni 8.1 sawa na asilimia 18.4 waliokuwa wamefikiwa na huduma hiyo mwaka 2012. Mwaka 2015
tunatarajia watu milioni 18.2 sawa na asilimia 38 watafikiwa na umeme. Kwa upande wa vijijini mwaka 2012 watu milioni 2.3 sawa naasilimia 7 walikuwa na umeme. Ifikapo Juni 2015, idadi hiyo itaongezeka
na kuwa milioni 7.4 sawa na asilimia 21. Haya ni mafanikio
makubwa kwa wananchi wengi vijijini na mijini kupata umeme katika kipindi
kifupi kiasi hiki. Ni mageuzi ya aina yake yatokayotoa mchango muhimu
katika kuinua hali za maisha ya Watanzania.
Ndugu
Wananchi;
Tunaanza kuiona nuru ya
matumaini kwamba siku si nyingi kutoka sasa, makaa ya mawe ya Mchuchuma na
madini ya chuma ya Liganga yataweza kutumika kwa maendeleo ya nchi yetu na watu
wa Ludewa. Maandalizi yote muhimu yamekamilika kwa ajili ya Januari, 2015
kuanza ujenzi wa mgodi wa makaa ya mawe kule Mchuchuma, mtambo wa kufua umeme,
ujenzi wa mgodi wa chuma kisichoyeyushwa pale Liganga na ujenzi wa kiwanda cha
kuyeyusha chuma.
Natoa
pongezi maalum kwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na wabia wenzao, Kampuni
ya Sichuan Hongda ya China kwa hatua iliyofikiwa. Inakadiriwa kuwa miradi
hii ikikamilika itatoa ajira 33,000 za moja kwa moja na
zisizokuwa za moja kwa moja.
Ndugu
Wananchi;
Mradi
mwingine mkubwa wa kimkakati ni ule wa kujenga Eneo Maalumu la Kiuchumi
(Special Economic Zone) la Mbegani, Bagamoyo. Kwa mujibu wa mpango kazi
wa wabia wa mradi huo yaani Mamlaka ya Kuendeleza Maeneo huru ya Uwekezaji
(EPZA), Kampuni ya China Merchants Holdings
International na Mfuko wa Uhifadhi wa
Akiba ya Mali za Serikali ya Oman (Oman State General Reserve Fund), ujenzi wa
bandari na miundombinu mingine itakayowezesha viwanda kujengwa imepangwa kuanza
Julai 2015.
Miundombinu
ya Usafiri na Uchukuzi
Ndugu
Wananchi;
Katika
mwaka huu wa 2014 kazi ya kujenga barabara za lami na kuimarisha barabara za
udongo ili ziweze kupitika wakati wote ziliendelea kote nchini. Huu nao
ni mradi mkubwa wa kimkakati. Barabara za lami 19 zenye urefu wa kilometa 1,459 zimekamilika kujengwa mwaka huu katika Mikoa ya Ruvuma, Mbeya,
Rukwa, Kagera, Dar es Salaam, Dodoma, Tanga, Morogoro, Arusha, Tabora na
Shinyanga. Ujenzi unaendelea kwa barabara nyingine 24 katika mikoa ya Dodoma,
Iringa, Mbeya, Kilimanjaro, Rukwa, Simiyu, Katavi, Tabora, Mwanza, Dar es
Salaam, Kagera na Pwani ambazo wakati wo wote mwaka 2015
zitakamilika. Maandalizi ya kuanza ujenzi wa barabara nyingine naneyanaendelea vizuri sehemu mbalimbali nchini.
Kwa
kutumia fedha za Mfuko wa Barabara, tumeendelea kufanya kazi ya ujenzi na ukarabati
wa barabara za udongo kote nchini. Mwaka huu Mfuko huo umetengewa shilingi bilioni 751.7 ukilinganisha na shilingi bilioni 504.4 mwaka jana. Aidha, mwaka huu tumeweka jiwe la msingi la ujenzi wa
Daraja la Mto Kilombero. Matumini yetu ni kuwa ujenzi wa daraja hilo na Daraja
la Kigamboni utakamilika mwaka 2015. Ujenzi wa Daraja la Malagarasi
ulishakamilika mwaka jana, kinachosubiriwa ni sherehe ya uzinduzi.
Kwa upande wa jiji la Dar es Salaam, tunategemea kukamilisha ujenzi wa Awamu ya
Kwanza ya barabara za mabasi yaendayo kasi. Ni matarajio yetu pia kwamba mabasi
yataanza kusafirisha abiria katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka
2015. Halikadhalika, tunategemea katika mwaka 2015 ujenzi utaanza wa
barabara zinazozunguka jiji la Dar es Salaam (ring roads), barabara ya Mwenge -
Morocco na ile ipitayo juu ya nyingine (flyovers) eneo la TAZARA. Vile vile,
daraja jipya la Salenda litaanza kujengwa. Aidha, kivuko cha abiria 300 cha MV Dar es Salaam
kitaanza kusafirisha abiria kati ya Dar es Salaam Kaskazini na Ferry mapema
mwakani. Hatua zote hizi zinalenga kupunguza msongamano wa magari katika
jiji la Dar es Salaam.
Usafiri
wa Anga na Reli
Ndugu
wananchi;
Jitihada za kuboresha huduma ya usafiri katika Reli ya Kati zimeendelea kwa
mafanikio. Mwaka huu vichwa vinane vya treni vimekarabatiwa, mabehewa mapya 22 ya abiria na mabehewa 274 ya mzigo yamenunuliwa.
Mabehewa hayo yameanza kuwasili nchini kati ya Novemba na Desemba mwaka
huu. Kati ya Januari na Mei, 2015 tunatarajia kupokea vichwa vipya vya
treni 13. Uboreshaji huu wa huduma
za treni unakwenda sambamba na ukarabati wa reli yenyewe, ujenzi wa madaraja na
kuimarisha maeneo yaliyo korofi katika reli hiyo.
Kuhusu ujenzi wa reli
iliyo pana zaidi (standard guage), yenye uwezo wa kubeba mabehewa mengi
na kuwezesha treni kwenda kwa mwendo wa kasi zaidi, juhudi za kutafuta fedha za
ujenzi au wabia wa kushirikiana nasi kujenga zinaendelea. Wakati huo huo,
tunaendelea na juhudi za kutafuta ufumbuzi kwa matatizo ya reli ya TAZARA ili
mambo yaende vizuri. Tutashirikiana kwa karibu na wabia wenzetu wa
Zambia. Bahati nzuri Serikali ya China iko tayari kuunga mkono
juhudi zetu za kufufua reli ya TAZARA.
Usafiri
wa Anga
Ndugu
Wananchi;
Sekta ya usafiri wa anga imeendelea kukua katika mwaka 2014. Idadi ya abiria
wanaowasili na kutoka katika viwanja vyetu vya ndege nchini imeongezeka kutoka
abiria milioni 2.5 mwaka 2013 hadi abiria milioni 3.5 kufikia Septemba, 2014.
Safari za ndege kati ya Tanzania na nchi za nje zimeongezeka kutoka 274 Januari, 2013 hadi 295 kufikia Septemba,
2014. Hili ni ongezeko la asilimia 8. Safari za ndege ndani ya
nchi nazo zimeongezeka kutoka safari 230,458 mwaka 2013 hadi safari 241,922 mwaka 2014. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 39. Maongezeko haya ni kielelezo na ushahidi kuwa shughuli za utalii
na biashara nchini zimeendelea kukua.
Ndugu
Wananchi;
Ujenzi wa Jengo la 3 (Terminal 3) la Abiria katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere unaendelea vizuri. Jengo hilo
litakapokamilika mwakani, litakuwa na uwezo wa kuhudumia wastani wa abiria milioni 8 kwa mwaka. Aidha,
ukarabati wa Jengo la 2 (Terminal2) utafanyika ili liweze
kutoa huduma iliyo bora zaidi. Sambamba na ujenzi huo, Wakala wa Viwanja vya
Ndege wameendelea kukarabati na kuboresha viwanja vya ndege vya KIA, Mwanza, Songwe, Bukoba, Tabora na Kigoma. Tunatarajia
ukarabati wa viwanja vya ndege vyaShinyanga na Sumbawanga kuanza mapema mwaka 2015.
Elimu
Ndugu
wananchi;
Tumeendelea kupiga hatua za kuridhisha katika kuboresha elimu nchini.
Tumefanikiwa kupunguza tatizo la upungufu wa maabara, vitabu na walimu wa shule
za msingi na sekondari. Mwaka huu tumeajiri walimu 36,339 kati ya 81,562 wanaohitajika. Tumebakiwa
na upungufu wa walimu 45,223 yaani 26,946 wa shule za msingi na 18,277 wa shule za sekondari hususan wa
masomo ya sayansi. Hivi sasa hatuna
tatizo la walimu wa masomo ya sanaa katika shule za sekondari.
Mwaka huu tumeanza mpango maalumu wa kutoa mafunzo ya Diploma ya Ualimu kwa
masomo ya sayansi na hisabati katika Chuo Kikuu cha Dodoma ambapo jumla ya
wanafunzi 5,602 wa masomo hayo wamedahiliwa. Mpango huu utatuwezesha kupunguza
pengo kubwa tulilonalo la walimu wa sayansi katika muda mfupi zaidi.
Ujenzi
wa Maabara
Ndugu
wananchi;
Ujenzi
wa maabara za Fizikia, Kemia na Baiolojia katika shule za sekondari za
Kata 3,463 umekwenda vizuri kiasi. Kwa idadi hiyo ya shule inatakiwa
zijengwe maabara 10,389 ilipofika Novemba, 2014. Taarifa kutoka TAMISEMI zinaonyesha
kuwa hadi kufikia Desemba 29, 2014, maabara 4,207 sawa na asilimia 40.5 zilikuwa zimekamilika, maabara 5,688 sawa na asilimia 54.8 zilikuwa katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji, na maabara 494 sawa na asilimia 4. zilikuwa katika hatua za
awali za ujenzi.
Ndugu
Wananchi;
Natoa
pongezi nyingi kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti na Wakurugenzi
Watendaji wa Halmashauri za Wilaya na Miji nchini pamoja na wananchi, kwa
jitihada kubwa iliyofanyika. Kwa kutambua jitihada hizo, nimeongeza miezi sita zaidi kwa wale ambao
hawajakamilisha ujenzi wa maabara hizo wafanye hivyo. Sikusudii kuongeza tena
muda baada ya hapo. Naomba watumie kipindi hicho kitumike kutafuta vifaa
vya maabara. Serikali itasaidia upatikanaji wa watunza maabara (laboratory technicians) ambao tumeanza programu
kubwa ya mafunzo yao na mahitaji mengine ya maabara.
Ununuzi
wa Vitabu
Ndugu
Wananchi;
Tumeendelea kupunguza tatizo la uhaba wa vitabu na
vifaa vya kufundishia katika shule za msingi na sekondari. Tumekuwa
tunanunua vitabu kwa kutumia Bajeti ya Serikali na misaada kutoka kwa marafiki
zetu wa maendeleo. Kwa mfano, Serikali ya Marekani imetupatia vitabumilioni 2.5 vya masomo ya sayansi na hisabati kwa shule za sekondari.
Ongezeko hili la vitabu linashusha uwiano uliopo sasa wa kitabu kimoja kwa wanafunzi wanne na kufikia kitabu kimoja kwa wanafunzi wawili. Lengo letu ni kila mtoto kuwa na kitabu chake kwa kila somo
ifikapo mwaka 2016.
Sera
Mpya ya Elimu na Mafunzo
Ndugu
wananchi;
Mafanikio mengine
tuliyopata mwaka huu ni kukamilika kwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014.
Hii ni hatua muhimu sana katika maendeleo ya elimu nchini hakuna badala yake.
Sera mpya inalenga kuinua ubora wa elimu na mafunzo na kuweka mifumo na
taratibu zitakazowezesha Watanzania wengi zaidi kupata fursa za elimu iliyo
bora na inayolinga na wakati tulionao. Jambo jipya sana na la kihistoria
katika Sera mpya ya Elimu ni dhamira ya Serikali ya kuondoa ada katika elimu ya
sekondari kuanzia mwaka 2016. Mpaka sasa hatuna ada kwenye shule za
msingi, sasa wakati umefika kufanya hivyo pia kwa elimu ya sekondari. Kwa
mujibu wa maelezo hayo ya Sera, nimekwishatoa maagizo kwa Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya
Fedha na Tume ya Mipango kuanza kutafakari namna jambo hilo litakavyotekelezwa.
Afya
Ndugu
Wananchi;
Katika
mwaka 2014 jitihada za kuboresha huduma ya afya kwa Watanzania
ziliendelea. Tulipambana kwa mafanikio na mlipuko wa homa ya dengue
iliyowapata watu 1,039 na kusababisha vifo vya watu 3 kati yao. Kwa upande wa
maradhi ya ebola tumejiandaa vya kutosha kutambua watu wenye maradhi hayo
wanapoingia nchini kupitia viwanja vya ndege vya kimataifa na vituo vyote vya
mpakani. Aidha, tumejipanga vyema kuwahudumia wagonjwa wa maradhi hayo
iwapo watatokea.
Mwaka
huu pia, Madaktari wetu watano wamekwenda Liberia kusaidiana na ndugu zetu wa huko katika
kukabiliana na ugonjwa wa ebola. Madaktari wetu hao wako salama na
wanaendelea vizuri kutoa huduma. Madaktari hao watakaporejea nchini watakuwa
hazina kubwa ya taifa katika kupanga mipango ya kukabiliana na ugonjwa huu
hatari. Hali kadhalika, watakuwa viongozi wa wengine katika kutibu
wagonjwa wa maradhi ya ebola iwapo watatokea nchini.
Ndugu
Wananchi;
Katika kipindi cha Januari
hadi Desemba, 2014, tumeweza kuajiri watumishi wa sekta ya afya 8,345 ambao kati yao kuna
madaktari 244, madaktari bingwa 75, wauguzi 2,555 na wataalamu wa kada nyingine za afya 5,471. Mwaka huu pia tumefanikiwa kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka
wanafunzi 7,956 katika mwaka 2012/2013 hadi wanafunzi 9,730. Kwa ongezeko hilo, sasa tumefikia asilimia 97 ya lengo letu la kudahili wanafunzi 10,000 ifikapo mwaka 2017.
Jitihada
zetu za kuongeza fursa za mafunzo kwa Madaktari, Wauguzi na wataalamu wengine
wa afya zina muelekeo mzuri. Ujenzi wa hospitali ya kufundishia pale Mloganzila
unaendelea vizuri na hospitali ya kufundishia ya Chuo Kikuu cha Dodoma
umekamilika. Ni matarajio yangu kuwa wakati wo wote mwakani ujenzi wa
kampasi mpya ya Chuo Kikuu cha Muhimbili pale Mloganzila utaanza. Ujenzi huo
ukikamilika Chuo kikuu cha Muhimbili kitaweza kudahili wanafunzi 12,000 kutoka wanafunzi 2,500 wa sasa jambo ambalo
litafanya upungufu wa Madaktari, Wauguzi na Wataalamu wa Afya kupata jawabu la
uhakika. Tumeendelea kufanya mambo mengine ikiwemo ujenzi wa jengo la tiba za
ubongo na mishipa ambalo limekamilika pale Muhimbili, sasa tunahangaikia kupata
vifaa.
Maji
Ndugu
Wananchi;
Katika mwaka huu wa 2014
tumeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kuwapatia wananchi maji safi na
salama mijini na vijijini. Kwa ajili hiyo miradi 498 ya maji vijijini
imekamilika na miradi 740 ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Miradi mingine 378 ipo katika maandalizi ya
ujenzi kuanza. Ni matarajio yetu kwamba katika mwaka ujao wa 2015, miradi
mingine 731 itatekelezwa na vituo 25,790 vya kuchota maji vitajengwa. Miradi hii ikikamilika tutaweza
kuwafikia asilimia 71 ya wananchi wanaopata maji
safi na salama vijijini kutoka asilimia 58 ya sasa. Kwa ajili hiyo, tutakuwa tumevuka lengo tulilojiwekea la
kuwapatia watu maji asilimia 65 ya Watanzania waishio vijijini ifikapo 2015. Ombi langu kwa ndugu
zetu wa Hazina waiangalie sekta hii ya maji kwa ukaribu zaidi na wawapatie
fedha kwa wakati.
Ndugu
Wananchi;
Utekelezaji wa mradi wa kuipatia maji miji ya Mwanga – Same – Mkomazi pamoja na miji na vijiji
vyote vya njiani, utaanza Februari, 2015. Fedha zimekwishapatikana na
Mkandarasi wa Awamu ya Kwanza ameshapatikana. Makandarasi wa Awamu ya
Pili na Tatu watapatikana muda si mrefu kutoka sasa. Hii pia itahusu
kupata Mkandarasi wa mradi wa maji wa mji wa Orkesment.
Ndugu
Wananchi;
Mwaka huu miradi ya
kuipatia maji miji kadhaa nchini ilikamilika na tatizo la upungufu wa maji
litakuwa limepatiwa ufumbuzi. Ipo miji kadhaa ambayo miradi imefikia
hatua ya juu na kwamba wakati wowote mwakani itakamilika. Jiji la
Dar es Salaam lipo katika kundi hili. Kazi ya upanuzi wa miradi ya maji
ya Ruvu Juu na Ruvu Chini kwa msaada wa Serikali ya Marekani na mkopo kutoka
Serikali ya India imefikia hatua nzuri. Inatarajiwa kukamilika katika
nusu ya kwanza ya mwaka 2015. Mwaka ujao pia visima virefu
vya Kimbiji na Kipera vitachimbwa na Bwawa la Kidunda litaanza kujengwa.
Serikali
ya India pia imekubali kutupatia mkopo wa Dola za Marekani milioni 268.2 kwa ajili ya kugharamia mradi wa kuipatia maji miji ya Tabora,
Nzega na Igunga kutoka Ziwa Victoria. Uwezekano wa kujumuisha miji
ya Sikonge na Urambo katika mradi huo utaangaliwa.
Bunge
na Mahakama
Ndugu
Wananchi;
Katika mwaka 2014,
mihimili ya Bunge na Mahakama iliendelea kutekeleza vyema majukumu yao.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeweza kuendesha shughuli zake kama
ilivyopangwa pamoja na kulazimika kugawana Ukumbi ule wa Bunge na Bunge Maalum
la Katiba. Bunge limefanya mikutano mitatu, Miswada 17 ya Sheria ilisomwa kwa mara ya kwanza, Sheria tano na maazimio saba yalipitishwa. Maswali ya
msingi 569 na ya nyongeza 1,541yaliulizwa na kujibiwa.
Aidha, sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow nalo lilijadiliwa na kutolewa
maazimio. Tumeshaanza kuchukua hatua kuhusu maazimio hayo na bado
tunaendelea.
Napenda kuitumia nafasi
hii kutoa pongezi nyingi kwa Wabunge wetu kwa kutekeleza vizuri wajibu wao wa
Kutunga Sheria na kusimamia Serikali. Nawasihi waendelee na msimamo huo
mwema na chanya kwa maslahi ya nchi yetu na watu wake.
Ndugu
Wananchi;
Kwa upande wa Mahakama napenda kutambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa ya
kupunguza mrundikano wa mashauri katika Mahakama za ngazi zote. Wahenga
wamesema “mcheza kwao hutunzwa”. Hatuna budi kutoa
pongezi maalum kwa Jaji Mkuu, Mheshimiwa Mohamed Chande Othman kwa uongozi wake
mahiri. Chini ya uongozi wake Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa
Mahakama Kuu na Mahakimu Wakazi na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo wamejiwekea
malengo ya kusikiliza na kutoa hukumu kwa mashauri yasiyopungua200 kwa mwaka kila mmoja wao.
Habari njema na ya kuleta faraja ni kwamba utekelezaji unaendelea vizuri.
Mashauri 870 yalisikilizwa na kuamuliwa
kwenye Mahakama ya Rufani, mashauri 11,334 kwenye Mahakama Kuu, mashauri 8,715 kwenye Mahakama ya Mahakimu Wakazi na Mashauri 25,683 katika Mahakama za
Wilaya. Aidha, mkakati wa kupeleka timu ya Majaji wa Mahakama Kuu
kwa wakati mmoja kwenye maeneo yenye mashauri mengi kama ilivyofanyika Kigoma,
Shinyanga na Tabora umesaidia sana kupunguza mrundikano wa mashauri ya siku nyingi.
Haijawahi kutokea mashauri mengi kiasi hicho kusikilizwa na kumalizwa katika
historia ya Mahakama nchini.
Ndugu
Wananchi;
Mkakati huu mpya umeleta
matumaini mapya kwamba tatizo la kuchelewesha kwa mashauri ambalo
lilidhaniwa kuwa ni tatizo sugu sasa limeanza kupatiwa ufumbuzi. Kwa
niaba ya Watanzania wenzangu wote natoa shukrani na pongezi nyingi kwa Jaji
Mkuu, Majaji wa Rufani, Jaji Kiongozi, Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakimu wa
ngazi zote kwa kazi nzuri waifanyayo.
Hali kadhalika, nampongeza
Mtendaji Mkuu wa Mahakama na watendaji wote wa Mahakama kwa kazi nzuri
waifanyayo ya kuwawezesha Majaji na Mahakimu kutimiza ipasavyo majukumu
yao. Hakika utendaji Mahakamani umebadilika na kuwa bora zaidi. Mimi
naahidi kuendelea kusaidia Mahakama kwa kuwahimiza ndugu zetu wa Hazina kutoa
kwa wakati pesa zilizotengwa katika bajeti.
Mapambano
Dhidi ya Rushwa
Ndugu
Wananchi;
Mapambano dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka yameendelea bila ya
ajizi. Katika mwaka huu wa 2014 TAKUKURU wamepokea taarifa 237 na wamekamilisha uchunguzi
wa mashauri 545. Watuhumiwa
waliofikishwa Mahakamani ni 428. Mashauri
yaliyomalizika ni 205, kati ya hayo 125 watuhumiwa waliachiliwa na 80 walipatikana na hatia na
kuhukumiwa. Mwaka huu wa 2014 mali na fedha taslimu zenye thamani ya shilingi bilioni 38.96 zimeokolewa. Katika kuimarisha Taasisi hiyo kiutendaji,
maafisa wapya 394 wameajiriwa.
Sherehe
za Miaka 50 ya Muungano
Ndugu
Wananchi;
Mwaka huu wa 2014
tuliadhimisha miaka 50 ya Muungano wa nchi zetu mbili yaani Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika kwa heshima inayostahili. Maadhimisho
yalifikia kilele tarehe 26 Aprili, 2014 na zilifanyika sherehe nchini kote
na sherehe hizo zilifana sana. Ni ukweli usiopingika kuwa kwa Muungano
wetu kuweza kudumu kwa nusu karne ukiwa bado imara na unazidi kustawi ni
mafanikio makubwa. Matumaini kwa siku za usoni ni mazuri. Naamini
Muungano wetu utaimarika zaidi iwapo Katiba Inayopendekezwa itapitishwa kwani
yale mambo yenye kuleta matatizo hivi sasa yatakuwa yamepatiwa ufumbuzi.
Miaka
50 ya JWTZ
Ndugu
Wananchi;
Wakati nchi inasherehekea
miaka 50 ya Muungano, baadhi ya vyombo na taasisi muhimu kitaifa zilifanya
hivyo hivyo. Miongoni mwa walioadhimisha nusu karne ya kuundwa kwake ni
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kama mjuavyo JWTZ ilizaliwa tarehe 1
Septemba, 1964. Jeshi letu liliadhimisha siku yao hiyo kwa kufanya zoezi kubwa
la kivita lililoanza Kibaha mkoani Pwani na kumalizikia Monduli Mkoani
Arusha.
Nilibahatika kushuhudia
siku ya mwisho ya zoezi hilo. Nilifurahishwa sana na kiwango cha utayari
kivita cha Jeshi letu. Wanajeshi wetu walionesha weledi wa hali ya juu, umahiri
mkubwa, ujasiri, ukakamavu na uvumilivu wa aina yake wakati wa kutekeleza
majukumu yao katika mazingira magumu ya uwanja wa medani za vita. Niliwapongeza
siku ile na narudia tena leo kuwapongeza. Niliyoyaona yamenihakikishia mimi na
Watanzania wote kuwa Jeshi letu la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania liko imara
kulinda mipaka ya nchi yetu na kuhakikisha usalama wa taifa letu na watu wake.
Jeshi letu bado ni lile tunalolijua sisi sote, lakini limezidi lile
lililomng’oa mvamizi Dikteta Iddi Amin wa Uganda, tena limezidi kwa mbali.
Mchakato
wa Katiba Mpya
Ndugu
Wananchi;
Mwaka huu pia tumeshuhudia
kukamilika kwa zoezi muhimu la kuandika Katiba Inayopendekezwa. Kama tujuavyo
sote, mchakato uliozaa Katiba Inayopendekezwa ulikuwa na changamoto nyingi
ndani na nje ya Bunge Maalum la Katiba. Pamoja na hayo, Bunge hilo
lilikamilisha kazi yake kwa salama siku mbili kabla ya tarehe 4 Oktoba, 2014
ambayo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho. Mimi na Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa
Dkt. Ali Mohamed Shein tulikabidhiwa nakala za Katiba Inayopendekezwa tarehe 8
Oktoba, 2014. Nimeshatimiza wajibu wangu wa kuchapisha katika Gazeti la
Serikali na kutangaza siku ya kupiga kura ya maoni kuwa tarehe 30 Aprili, 2015.
Nimeshatoa maagizo kwa Tume ya Uchaguzi kufanya matayarisho husika ya
kuwezesha Kura ya Maoni kufanyika.
Ndugu
Wananchi;
Moja ya mambo muhimu
ambayo Tume ya Uchaguzi inafanya kwa sasa ni kuandikisha wapiga kura katika
Daftari la Mpiga Kura. Tume imeamua kutumia mfumo mpya wa Biometric
Voters Register. Uandikishaji wa majaribio umefanyika katika baadhi ya
Kata katika Majimbo ya Mlele, Kawe na Kilombero. Matatizo yaliyojitokeza
yatasaidia kuboresha mfumo huo kabla ya uandikishaji wa watu wote wenye sifa
stahiki kuanza.
Ndugu
Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kuwafahamisha Watanzania wenzangu wote kuwa mfumo
mpya unatengeneza Daftari Jipya la Mpiga Kura ingawaje lugha inayotumika ni
uboreshaji wa Daftari la sasa. Uboreshaji huu wa Daftari la Mpiga Kura ni
tofauti na ule tuliouzoea ambapo walikuwa wanaandikishwa wapiga kura wapya na
wale waliopoteza vitambulisho vyao. Safari hii wanaandikishwa wote wapya
na wa zamani na wote watapata vitambulisho vipya. Hivyo basi, sisi wenye
vitambulisho vya kupiga kura vya zamani tusifanye ajizi, tujitokeze
kujiandikisha wakati ukifika.
Jambo la pili ni kwamba,
Daftari la Mpiga Kura linalotayarishwa siyo kwa ajili ya Kura ya Maoni ya
Katiba Inayopendekezwa peke yake, daftari hilo hilo litatumika pia kwenye
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015. Hivyo basi, kujiandikisha ni jambo muhimu
sana. Usipofanya hivyo siyo tu utajinyima fursa ya kushiriki kuamua
kuhusu Katiba Inayopendekezwa bali pia utakosa fursa ya kuchagua Rais wako,
Mbunge wako na Diwani wako. Katu usikubali yakukose hayo.
Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa
Ndugu
Wananchi;
Kama mjuavyo tarehe 14 Desemba, 2014 na 20 Desemba, 2014 ulifanyika Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa kuchagua viongozi wa vitongoji, vijiji na mitaa. Uchaguzi
umekwisha na viongozi wamekwishapatikana. Sasa ni wajibu wa viongozi hao
kufanya kazi waliyoiomba. Kwa walioendesha uchaguzi ni wakati mzuri wa
kufanya tathmini ili wapate mafunzo yatokanayo na uchaguzi huo. Kwa
TAMISEMI na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri, lengo liwe ni kuona namna ya
kuimarisha mazuri na kusahihisha makosa na matatizo yaliyojitokeza. Kwa
walinzi wa amani watambue matatizo ya kiusalama yaliyotokea na kuona namna ya
kutengeneza mikakati ya kuzuia matatizo ya namna hiyo yasijitokeze tena. Hatma
ya yote, shabaha yetu ni kutaka kufanya vizuri zaidi katika chaguzi zijazo za
Serikali za Mitaa na kufanya vizuri zaidi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Jumuiya
ya Afrika Mashariki
Ndugu
Wananchi;
Mwaka huu Tanzania
imechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ni zamu yetu
kwa mujibu wa mzunguko wa uongozi wa Jumuiya yetu kati ya nchi wanachama. Ni
dhamana kubwa na kwamba wenzetu wa Afrika Mashariki wanatutegemea tuwaongoze
katika kutekeleza malengo na madhumuni ya Jumuiya kama yalivyoainishwa katika
Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hali kadhalika,
tunategemewa kuongoza katika utekelezaji wa maamuzi mbalimbali ya vikao vya
Jumuiya. Hii inahusu maamuzi yaliyokwishafanywa kabla yetu ambayo
utekelezaji wake unaendelea na uamuzi mpya utakaofanywa katika kipindi cha
uongozi wetu.
Kwa niaba ya Watanzania
wote napenda kuwashukuru ndugu zetu wa Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda kwa
kutuamini. Napenda kuahidi kuwa hatutawaangusha. Sisi Watanzania
tutafanya kila tuwezalo kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa manufaa ya
Jumuiya yenyewe, nchi zetu na wananchi wa Afrika Mashariki. Tutajitahidi
kuwa wabunifu kwa nia ya kuona utangamano unakua na kustawi kwa kasi na kuzaa
matunda ya maendeleo tunayoyatarajia sote. Matunda tuliyoyatarajia
tulipoamua kuanzisha Jumuiya hii na matunda tuliyoyapata tulipoamua kwa hiari
yetu kujiunga nayo kuwa wanachama.
SADC,
AU NA UN
Ndugu
Wananchi;
Kuhusu Jumuiya ya
Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa,
tunaahidi kuendelea kuwa wanachama waaminifu na kushiriki kwa ukamilifu katika
utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mashirika haya ya kikanda na kimataifa.
Kwa upande wa SADC tutaendelea kushiriki katika utekelezaji wa mikakati na
mipango ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na ile ya kisiasa na kiusalama kama
ilivyoainishwa katika RISDP (Regional Indicative Strategic Development Plan) na
SIPO (SADC Strategic Indicative Plan for the Organ). Kwa ajili hiyo Tanzania,
itaendelea kutoa mchango wake katika kukuza utangamano wa kiuchumi katika SADC
na kusaidia kuimarisha uhusiano mwema na usalama miongoni mwa nchi wanachama wa
SADC. Hii ni pamoja na kusaidia katika kutatua migogoro ya kisiasa na kusalama
kati ya nchi wanachama.
Kwa upande wa Umoja wa
Afrika tutaendelea kutekeleza maamuzi ya vikao na taasisi mbalimbali za Umoja
huo. Daima tutakuwa wanachama waaminifu wa Umoja wa Afrika na kuchangia
katika uimarishaji wake. Kuhusu Umoja wa Mataifa tutaendelea kutimiza
wajibu wetu kama wanachama wa Umoja huo wa kimataifa ulio adhimu na muhimu
kwetu na dunia nzima. Tutaendelea kushiriki katika shughuli za ulinzi wa
amani chini ya Umoja wa Mataifa. Hivi sasa tunao wanajeshi wetu katika
majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi
ya Kongo, Sudan na Lebanon. Tuko tayari wakati wote kuchangia zaidi iwapo Umoja
wa Mataifa watatutaka tufanye hivyo.
Hitimisho
Ndugu
Wananchi;
Namaliza hotuba yangu hii
ndefu kwa kuwashukuru Watanzania wote kwa kuiunga mkono Serikali yetu na kwa
mchango wenu uliowezesha nchi yetu kupata mafanikio haya makubwa tunayojivunia
katika mwaka 2014. Tumeweza kuvuka mitihani na nyakati zenye majaribu mengi.
Umoja wetu na mshikamano wetu ndivyo vilivyotuwezesha kufika hapa. Tunauanza
mwaka 2015 kwa matumaini makubwa. Mwaka 2015 unatupa fursa kubwa ya kuendelea
kuliimarisha zaidi taifa letu. Mwaka ujao ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu, hivyo
huenda ukawa na changamoto na majaribu magumu zaidi kuliko mwaka huu.
Uelewa wetu, umoja wetu, mshikamano wetu na moyo wetu wa uzalendo ndivyo
vitakavyotuvusha kama ilivyokuwa kwa miaka ya nyuma. Mimi nina imani
kubwa kwa uwezo na utayari wa Watanzania wenzangu kuidumisha sifa nzuri ya nchi
yetu ya umoja na mshikamano wa watu wake uliozaa amani na utulivu.
Tumeweza mwaka huu na miaka ya nyuma, tutaweza tena mwakani na miaka ijayo.
Inawezekana, Timiza Wajibu Wako! Nawatakia heri ya mwaka mpya.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment