DIWANI wa Kata ya Ngula wilayani Kwimba, Palu Mashagu (CUF),
anashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa tuhuma
za kuomba na kupokea rushwa ya Sh 150,000.
Taarifa kutoka Kwimba na kuthibitishwa jana na Kamanda wa
Takukuru, Faustine Maijo, ilisema Mashagu alikamatwa Mei 6, mwaka huu mchana
katika ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Ngula akidaiwa kuomba na kupokea Sh 150,000
kutoka kwa mtumishi wa Halmashauri ya Kwimba, Nyabugumba Jonathan.
Mashagu ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF wilaya ya Kwimba
anadaiwa kuomba na kupokea kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kumsaidia
mtumishi huyo pamoja na wenzake wanne waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma za
ubadhirifu wa Sh milioni 72 za mradi wa usafi na mazingira.
Kutokana na tuhuma hizo kufika katika vikao vya Halmashauri ya
Kwimba, kikao cha Baraza la Madiwani kiliazimia kufanya uchunguzi wa tuhuma
hizo na kuunda kamati ya madiwani watano chini ya uenyekiti wa Diwani wa
Nkalalo, Enos Ntwale, kuchunguza wizi wa fedha hizo kabla ya hatua nyingine
dhidi ya wahusika kuchukuliwa.
Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Shija Malando (Kata ya
Hungumalwa), Peter Msalaba (Kata ya Nyambiti), Tabu Samson (Viti Maalumu) na
Mashagu.
Akizungumzia taarifa za diwani wake kutiwa mbaroni kwa kosa la
rushwa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kwimba, Zephania Masangu, alisema amepokea
taarifa hizo lakini hajui undani wake na kubainisha alikuwa miongoni mwa
wajumbe wa kamati yake aliyounda Aprili 29, mwaka huu.
“Kamati niliyounda ilishakamilisha kazi yake na taarifa
kukabidhiwa sasa maelezo zaidi nadhani wanajua waliomkamata mngewauliza wao,”alisema Masangu.
Akizungumzia suala hilo mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo
aliyekataa jina lake kuandikwa alidai taarifa walizopokea katika kamati
yao zimedai Mashagu aliomba rushwa ya Sh 500,000 kwa Ofisa Afya Msaidizi
aliyetoa taarifa Takukuru ndipo ukawekwa mtego na kumnasa akipokea Sh 150,000.
Chanzo:
mpekuzihuru
No comments:
Post a Comment