TAASISI ya Kupambana na Kudhibiti Rushwa nchini (TAKUKURU)
imewaburuza mahakamani vigogo watatu wa Serikali kwa makosa mawili
ya matumizi mabaya ya madaraka na kutumia nyaraka mbalimbali
kumtapeli mwajiri wao.
Vigogo hao ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala
Mkoa wa Shinyanga, Patrick Karangwa (45), Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya
ya Magu Mkoa wa Mwanza, Ntinika Paul (51) na Mhasibu Mkuu wa Wilaya ya Magu,
Mathayo Masuka.
Walifikishwa wiki iliyopita katika Mahakama ya Wilaya ya
Nyamagana Mkoa wa Mwanza, mbele ya Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama hiyo,
Janeth Masesa.
Ilidaiwa kuwa watuhumiwa hao walitenda makosa hayo mwaka 2009
wakati wakiwa wafanyakazi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Ilielezwa kuwa wakati wakitenda makosa hayo, Karangwa alikuwa
Mchumi Mkuu Jiji la Mwanza, Paul alikuwa mweka hazina mkuu wa
jiji hilo wakati Masuka alikuwa mkaguzi wa ndani wa jiji la Mwanza.
Watuhumiwa hao walikana mashtaka hayo na wapo nje kwa dhamana na
kesi hiyo inatarajiwa kutajwa tena Juni 11 mwaka huu.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Kasomambuto Mbengwa,
alithibitisha taasisi hiyo kuwakifikisha vigogo hao mahakamni.
No comments:
Post a Comment