Chanzo :ikulu
Mheshimiwa
Spika;
Tunayo kila sababu ya
kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kutujalia uzima na kutuwezesha
kuishuhudia siku hii adhimu katika historia ya Bunge letu na nchi yetu.
Hatimaye siku ya kuvunja Bunge la Kumi imewadia ili kuwezesha hatua husika za
mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ziweze kutekelezwa.
Nakushukuru sana
Mheshimiwa Spika kwa kunipatia nafasi hii ya kulihutubia Bunge lako tukufu ili
niweze kutimiza wajibu wangu huo wa msingi Kikatiba. Lakini, shukrani
zangu kubwa ni kwa uongozi wako mahiri na shupavu. Umeliongoza Bunge
vizuri. Najua haikuwa kazi rahisi. Penye wengi pana mengi. Lakini kwa
uhodari mkubwa umeweza kulifikisha jahazi bandarini salama salmini.
Hakika wewe ni nahodha makini na jemedari hodari, uliyethibitisha uhodari na
umakini wako katika uwanja wa medani. Wewe ndiwe mwanamke wa kwanza
kushika wadhifa huu wa juu kabisa katika mhimili huu wa kutunga sheria na
umeidhihirishia dunia kuwa wanawake wakipewa nafasi wanaweza.
Mheshimiwa
Spika;
Niruhusu pia nitoe
shukrani na pongezi zangu za dhati kwa Waheshimiwa Wabunge kwa kazi kubwa na
nzuri mliyoifanya. Mmetimiza ipasavyo wajibu wao wa Kikatiba wa Kutunga Sheria
na kusimamia Serikali. Nawashukuru kwa ushirikiano wenu na msaada wenu.
Ni ukweli ulio wazi kuwa bila ya ninyi Wabunge wetu na Bunge hili, tusingeweza
kupata mafaniko na maendeleo tuliyoyapata. Mmejijengea, nyinyi wenyewe na Bunge
letu heshima kubwa mbele ya wananchi. Mmeitendea haki demokrasia ya
Tanzania na kuliletea heshima kubwa Bunge letu nchini, kikanda na kimataifa.
Mheshimiwa
Spika;
Tarehe 30 Desemba 2005
nilipozindua Bunge la Tisa nilielezea mtazamo wangu kuhusu nchi yetu na kutaja
majukumu ya msingi na vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Nne. Nilisema
tutatekeleza wajibu wetu na vipaumbele hivyo kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi
mpya. Tarehe 16 Julai, 2010 wakati wa kuvunja Bunge hilo nilielezea mafanikio
tuliyopata na changamoto zilizotukabili katika kipindi hicho. Tarehe 28
Novemba, 2010 wakati wa kuzindua Bunge hili la Kumi niliainisha vipaumbele vya
Serikali ya Chama cha Mapinduzi katika kipindi changu cha pili cha uongozi wa
nchi yetu na kuahidi kuvitekeleza kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi.
Kama ilivyo ada, leo tunafikia mwisho wa uhai wa Bunge la Kumi, naomba kutumia
fursa hii kutoa mrejesho wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali na yale mambo
ambayo tuliahidi na kupanga kufanya.
Umoja,
Amani na Usalama
Mheshimiwa
Spika;
Niliahidi kuwa katika
kipindi cha uongozi wangu nitafanya kila niwezalo kuhakikisha kuwa Tanzania
inaendelea kuwa nchi moja na watu wake wanaendelea kuwa wamoja, wanaopendana na
kushirikiana licha ya tofauti zao za rangi, dini, makabila, mahali watokako, na
ufuasi wa vyama vya siasa. Pia, kwamba nchi yetu itaendelea kuwa yenye amani,
usalama na utulivu.
Leo tunapoagana, ninyi
na mimi, ni mashuhuda kuwa Tanzania na Watanzania tumebakia kuwa wamoja.
Hata hivyo, katika kipindi hiki kumekuwepo na matukio ya hapa na pale madogo na
makubwa, yaliyotishia umoja wa nchi yetu na watu wake. Yapo mambo
yaliyopandikizwa kuleta chuki baina ya Tanzania Bara na Zanzibar, baina ya
Wakristo na Waislamu na baina ya maeneo fulani ya nchi na wengine.
Bahati nzuri, msimamo
thabiti wa viongozi wakuu wa Serikali zetu mbili wakisaidiwa na viongozi
wengine pamoja na ushirikiano na viongozi wa dini na wa jamii na uelewa wa
wananchi, vimeliwezesha taifa letu kushinda changamoto hizo na matishio yote
hayo. Changamoto hizi zimethibitisha ubora wa mazungumzo. Ni kweli
kabisa kwamba wanaozungumza hawagombani na wanaozungumza humaliza tofauti zao
bila kugombana.
Mheshimiwa
Spika;
Niruhusuni, nitumie
nafasi hii kuwashukuru kwa mara nyingine viongozi wakuu wenzangu, Makamu wa
Rais, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Waziri Mkuu, Makamu wa Kwanza wa
Rais Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, viongozi wa dini, viongozi wa
jamii na wananchi wote kwa ushindi tulioupata katika kudumisha umoja
wetu. Hata hivyo, tahadhari kubwa lazima iendelee kuchukuliwa kwani watu
wenye nia mbaya kwa nchi yetu au na umoja wetu hawajaisha na hawajafurahi
kwamba hawajafaulu. Huenda wakajaribu tena. Tunachotakiwa kufanya ni kuendelea
kushikamana ili hata wakijaribu tena washindwe.
Muungano
Wetu Umeimarika Zaidi
Mheshimiwa
Spika;
Nafurahi kwamba namaliza
kipindi changu cha uongozi tukiwa tumeweza kudumisha na kuuimarisha Muungano wetu
adhimu na adimu Barani Afrika. Mtakumbuka kuwa katika hotuba yangu ya
kufungua Bunge la Tisa nilisisitiza umuhimu wa viongozi wa pande zetu mbili
kukutana mara kwa mara kuzungumzia ustawi wa Muungano wetu. Nafurahi
kwamba jambo hili limefanyika chini ya uenyekiti wa Makamu wa Rais, akisaidiwa
na Waziri Mkuu kwa upande wa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar, Waziri
Kiongozi katika awamu yangu ya kwanza na Makamu wa Pili wa Rais katika
awamu hii.
Mafanikio yaliyopatikana
ni makubwa. Masuala mbalimbali ya zamani na mapya yamezungumzwa,
yameshughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi. Kwa mfano, hadi mwaka 2005
zilikuwa zimebakia kero 13 za Muungano zilizoainishwa na Tume
ya Shelukindo, hivi sasa zimebaki kero nne. Tayari ufumbuzi wa kero moja
unakamilishwa kiutawala na tatu zimeshughulikiwa kwa ukamilifu katika Katiba
Inayopendekezwa. Kama kura ya maoni ingekuwa imefanyika na Katiba hiyo
kupitishwa kungekuwa hakuna kiporo cha kero za Tume ya Shelukindo. Lakini
kwa vile kura ya maoni haijafanyika ndiyo maana tunaendelea kuzitaja. Hata
hivyo, Serikali zetu mbili zimezungumza na kukubaliana tutafute njia ya
kumaliza suala la rasilimali ya mafuta na gesi. Ndiyo maana katika
Muswada wa Petroli hoja ya Zanzibar kuwa na mamlaka kamili ya kusimamia
uchimbaji wa mafuta na kumiliki mapato yake ilijumuishwa. Natoa shukrani nyingi
kwa Bunge lako tukufu kwa kupitisha Muswada huo. Moja ya kero kubwa katika
Muungano tumeimaliza.
Mpasuko
wa Kisiasa Zanzibar
Mheshimiwa
Spika;
Mtakumbuka kuwa
nilizungumzia kusononeshwa kwangu na mpasuko wa kisiasa uliokuwepo Zanzibar
wakati ule na kuelezea utayari wangu wa kusaidia kuuondoa. Kama mjuavyo
mazungumzo yalifanyika ndani ya CCM na CUF na baina ya vyama hivyo na muafaka
ukapatikana. Serikali ya Umoja wa Kitaifa ikaundwa na mpasuko wa kisiasa ukawa
umepatiwa tiba. Matokeo ya yote hayo ni kuwa mazingira ya kisiasa na
kijamii yamekuwa bora zaidi siku hizi kuliko ilivyokuwa kabla ya hapo.
Ni matumaini yangu kuwa
ndugu zetu wa Zanzibar watayadumisha mafanikio haya ili waendelee kuishi kwa
amani, upendo na udugu. Natambua kuwepo kwa changamoto za hapa na pale katika
uendeshaji wa Serikali hiyo. Jambo linalonipa faraja ni kuwa matatizo
yenyewe hayahusu muundo wa Serikali bali yanaletwa na watu kupishana kauli au
kutofautiana katika uendeshaji wa baadhi ya mambo. Mimi naamini hayo ni mambo
yanayoweza kumalizwa kwa wadau kukaa kitako na kuzungumza kama ilivyokuwa kabla
ya muafaka.
Amani
na Usalama
Mheshimiwa
Spika;
Nchi yetu iko salama,
mipaka iko salama kwa sababu Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania
limeendelea kutimiza ipasavyo jukumu lake la kulinda uhuru na mipaka ya nchi
yetu. Katika kipindi hiki tumewekeza sana katika kuliimarisha Jeshi letu kwa
vifaa na zana za kisasa za kivita na mafunzo. Tumeimarisha Kamandi za Nchi
Kavu, Anga na Majini. Utayari kivita wa jeshi letu ni mzuri tena wa hali ya
juu. Weledi na nidhamu ya Wanajeshi wetu ni ya hali ya juu. Tumeboresha
maslahi na makazi ya wanajeshi kwa kujenga nyumba mpya za kuishi. Utekelezaji
wa mpango wa kuwajengea nyumba 10,000 unaendelea vizuri. Hadi
hivi sasa nyumba 6,064 zinaendelea kujengwa nchi nzima na kati
yake nyumba 3,096 zimekamilika. Namaliza kipindi changu cha
kuwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama kwa kujiamini
kwamba “Tupo vizuri”. Pamoja na hayo kazi ya utekelezaji wa Mpango wa
Miaka 15 wa kuimarisha JWTZ lazima iendelezwe ili kulifikisha Jeshi letu pale
tulipopakusudia.
Mheshimiwa
Spika;
Katika miaka 10 hii
tumefanya jitihada kubwa ya kupambana na uhalifu ili kulinda usalama wa maisha
na mali za watu waishio Tanzania. Mtakumbuka kuwa mwaka 2005 na mwanzoni
mwa 2006 kulikuwa na matukio mengi ya ujambazi. Niliahidi wakati wa
kampeni na katika hotuba yangu Bungeni kwamba hatutawaacha majambazi waendelee
kutamba. Hali ile imedhibitiwa. Ingawaje matukio ya ujambazi hayajaisha, lakini
hayako kama ilivyokuwa wakati ule.
Hali kadhalika, matukio
ya uhalifu wa kuwania mali yamepungua kutoka 53,268 mwaka 2005
hadi 43,808 mwaka 2014. Natoa pongezi nyingi kwa Jeshi la
Polisi kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya na wanayoendelea kufanya. Jambo
ambalo bado hatujafanikiwa vya kutosha ni ajali za barabarani. Lazima tuendelee
kuzitafutia muarobaini wake. Niruhusuni niwatambue na kuwashukuru Inspekta
Jenerali (mstaafu) Omari Mahita, Inspekta Jenerali (mstaafu) Said Mwema na
Inspekta Jenerali Ernest Mangu aliyepo sasa kwa uongozi wao mzuri.
Mafanikio haya ni
matokeo ya uwekezaji wa Serikali katika utakelezaji wa mpango wa maboresho ya
Jeshi la Polisi uliobuniwa wakati wa uongozi wa Ndugu Saidi Mwema, IGP mstaafu.
Jeshi la Polisi linaendelea kuwezeshwa kwa zana, vifaa na mafunzo.
Taratibu zimekamilika za kulipatia Jeshi hilo magari ya kutosha ili kuongeza
ufanisi.
Pia, tumeendelea
kuboresha maslahi na mazingira ya kuishi Maafisa na Askari. Kwa ajili
hiyo tumekarabati baadhi ya nyumba zilizopo, tumejenga nyumba kadhaa mpya za
ghorofa, za kawaida na mabweni. Mipango imekamilika ya kuwezesha ujenzi
wa nyumba 10,000 ambazo zitapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo
la uhaba wa nyumba za kuishi katika Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa
Spika;
Jeshi letu la Magereza
nalo limeendelea kutekeleza vizuri majukumu yake ya kulinda wafungwa na
kurekebisha tabia zao. Aidha, huduma za malazi, mavazi, chakula na usafiri kwa
wafungwa zimeendelea kuboreshwa. Changamoto kubwa ni msongamano wa wafungwa
Magerezani. Naamini mipango ya kujenga magereza mapya na kupanua yaliyopo
ikitekelezwa tatizo litaisha. Aidha, mpango wa maboresho ya Jeshi la
Magereza ukikamilika na kutekelezwa, utaboresha mazingira ya kufanyia kazi
na kuishi maafisa na askari, hivyo kupandisha morali wao na kuongeza
ufanisi.
Jeshi
la Kujenga Taifa
Mheshimiwa
Spika;
Ahadi yangu ya kuanzisha
upya utaratibu wa kuchukua vijana wa mujibu wa Sheria katika Jeshi la Kujenga
Taifa imetimia. Mpaka hivi sasa vijana 38,200 wamekwisha
hitimu mafunzo hayo wakiwemo Waheshimiwa Wabunge. Nawapongeza sana
Waheshimiwa Wabunge walioshiriki kwa kuongoza kwa mfano. Imesaidia sana
utaratibu huo kuanza upya bila vipingamizi. Ni matumaini yangu kuwa
Wizara ya Fedha, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa watakaa pamoja
kujadili namna ya kutafuta ufumbuzi kwa changamoto zilizopo. Naamini zinaweza
kumalizwa, vijana wetu wakashiriki mafunzo bila matatizo yoyote.
Utawala
Bora
Mheshimiwa
Spika;
Katika kipindi cha miaka
kumi hii tumetekeleza dhamira yetu ya kujenga na kuimarisha utawala bora kwa
sera, sheria, mifumo, taasisi na kwa rasilimali watu. Tumefanya hivyo katika
maeneo yote muhimu yakiwemo yale yahusuyo haki za binadamu, demokrasia,
mapambano dhidi ya rushwa, maadili ya viongozi, ukusanyaji wa mapato na nidhamu
ya matumizi ya fedha za umma na mgawano wa madaraka hati ya mihimili.
Bunge
la Jamhuri ya Muungano
Mheshimiwa
Spika;
Serikali imetimiza
ipasavyo wajibu wake kwa mhimili mkuu wa dola wa Kutunga Sheria. Tulianzisha
Mfuko wa Bunge na kuongeza fedha katika bajeti ya Bunge toka shilingi
bilioni 30.58 mwaka 2005/06 hadi shilingi bilioni 173.76 mwaka
2015/16. Pia tumeanzisha Mfuko wa Jimbo ili kuwawezesheni Wabunge kuchangia
katika kutatua changamoto za maendeleo zinazowakabili wananchi wa majimbo yao.
Bunge letu limetekeleza ipasavyo majukumu yake kupitia Kamati zake za kudumu na
pale ilipolazimu Kamati teule zilizoundwa.
Katika kipindi hiki
miswada 163 imepitishwa, maswali ya msingi 7,544 na
ya nyongeza 22,632 yameulizwa na kujibiwa. Kamati teule 2ziliundwa.
Haya ni mafanikio makubwa kwa Bunge letu. Bunge hili limefanya kazi kubwa
na kazi ya kutukuka. Michango na ushauri wake umekuwa chachu ya baadhi ya
hatua na mabadiliko ya kisera, kisheria na kiutendaji yaliyofanywa na Serikali.
Kwa kweli mnastahili pongezi nyingi. Huwezi kutaja mafanikio ya Serikali
ya Awamu ya Nne bila kutambua mchango wa Bunge hili.
Mchakato
wa Katiba
Mheshimiwa
Spika;
Kama sote tujuavyo,
kupitia Sheria iliyotungwa na Bunge hili, mwaka 2013 tulianzisha mchakato wa
Mabadiliko ya Katiba kwa lengo la kuipatia nchi yetu Katiba mpya iliyo bora
zaidi kuliko iliyopo sasa. Nafurahi kwamba mchakato huo ulituwezesha kupata
Katiba Inayopendekezwa ambayo imekidhi matarajio hayo. Narudia kutoa pongezi za
dhati kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Bunge Maalum la Katiba kwa kazi kubwa
na nzuri waliyofanya. Hatua iliyobaki ni Kura ya Maoni ambapo sote tunasubiri
maelekezo ya Tume ya Uchaguzi. Mimi naamini iwapo itapitishwa, Katiba
Inayopendekezwa itaimarisha zaidi taifa letu.
Vyama
vya Siasa
Mheshimiwa
Spika;
Katika kipindi hiki
tumeshuhudia vyama vya siasa vikiendelea kuimarika na kujijenga nchini. Idadi
ya vyama vya siasa imeongezeka kutoka 18hadi 24.
Vyama vya siasa vimefanya shughuli zake kwa uhuru. Viongozi na wanachama wao
wamefanya mikutano mingi na hata maandamano kote nchini. Baraza la Vyama vya
Siasa na TCD vimekuwa vyombo muhimu vilivyofanya kazi nzuri ya kujenga
ushirikiano miongoni mwa vyama vya siasa. Yamekuwa majukwaa muhimu ya
mashauriano baina ya vyama vya siasa kwa masuala mbalimbali. Matatizo na
changamoto nyingi zimeweza kupatiwa ufumbuzi. Ni matumaini yangu kuwa
vyombo hivi viwili vitaendelezwa na kuimarishwa miaka ijayo.
Huu ni mwaka wa
Uchaguzi, na vyama vya siasa ndiyo wahusika wakuu. Ni matumaini yangu kuwa
vyama vya siasa vitaheshimu na kuzingatia maadili ya uchaguzi. Hii
itasaidia kuwepo kwa utulivu na amani katika mchakato wa uchaguzi.
Uchaguzi
Mkuu
Mheshimiwa
Spika;
Habari kubwa hapa nchini sasa ni uchaguzi
mkuu. Tayari Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) na ile ya Zanzibar (ZEC)
zimekwisha tangaza tarehe 25 Oktoba, 2015 kuwa ni siku ya kufanyika uchaguzi
mkuu. Maandalizi ya uchaguzi huo yanaendelea vizuri. Tume ya Taifa ya
Uchaguzi inaendelea na zoezi la uandikishaji wa wapiga kura kwa mfumo mpya wa teknolojia
ya Biometric Voters Register (BVR). Hadi sasa zoezi la
uandikishaji limekamilika katika mikoa 13 na linaendelea
katika mikoa 11 na katika mkoa wa Dar es Salaam na Zanzibar
uandikishaji unategemea kuanza mwezi huu. Kwa taarifa za Tume ya Uchaguzi,
tayari wamekwisha andikisha hadi sasa wapiga kura milioni 11 kati
ya lengo la kuandikisha wapiga kura kati ya milioni 21 hadi 23.
Sisi katika Serikali
tutaendelea kutimiza wajibu wetu wa kuiwezesha Tume kutimiza wajibu wake.
Napenda kuwahakikishia kuwa kila Mtanzania mwenye haki ya kupiga kura atapata
fursa ya kuandikishwa. Shime tuhimize watu wajitokeze kujiandikisha ili
wasikose haki yao hiyo.
Uhuru
wa Habari
Mheshimiwa
Spika;
Mtakubaliana nami kuwa
katika kipindi hiki uhuru wa habari na uhuru wa watu kutoa maoni yao umepanuka
sana. Tanzania kuna magazeti ya kila siku 16 na kati ya hayo
ya Serikali ni 2 (Daily News, Habari Leo). Pia magazeti
ya kila wiki yapo 62. Aidha, kuna vituo vya redio 115 na
vya televisheni 29. Serikali haifanyi uhakiki wa habari kabla
ya kuchapishwa au kuandikwa. Tumeamua hivyo kwa imani yangu kwamba ustawi
wa demokrasia hutegemea sana uhuru wa vyombo vya habari. Pili, kwa vile
tunatambua manufaa ya vyombo vya habari kuelimisha jamii, kupambana na maovu na
kuhimiza uwajibikaji.
Pamoja na hayo,
hatukusita wala kuchelea kuchukua hatua pale uhuru huo ulipotumiwa vibaya na
kutishia kuvuruga amani, umoja na usalama wa jamii au taifa. Au, pale
ambapo Sheria za nchi zimekiukwa. Huo ni wajibu wetu wa kikatiba ambao mimi na
wenzangu tuliapa kuutimiza.
Mheshimiwa
Spika;
Katika kuongeza uwazi na
mawasiliano na wananchi mwaka 2007 tulianzisha tovuti ya wananchi. Tovuti hiyo
imeshapokea hoja 117,243 na kati ya hizo zilizohusu Serikali
zilikuwa 78,258 na zote zimeshughulikiwa.
Katika kuboresha mfumo
wa mawasiliano, Tanzania imeshahama kutoka mfumo wa analogia na kuingia kwenye
mfumo wa digitali. Hii ni hatua kubwa muhimu kwa maendeleo ya tasnia ya
habari nchini. Jambo ambalo nasikitika kuwa hatukuweza kulikamilisha ni
utungaji wa Sheria ya Haki ya Upatikanaji wa Habari na Sheria ya Vyombo vya
Habari. Miswada imekamilika na kusomwa mara ya kwanza hapa Bungeni lakini
mchakato wake haukuweza kufika mwisho. Tunawaachia wenzetu wajao washughulike
nayo katika Bunge la 11.
Vita
dhidi ya Rushwa
Mheshimiwa
Spika;
Vita dhidi ya rushwa ni
eneo jingine ambalo tulilivalia njuga katika Awamu ya Nne. Tumepata mafanikio
ya kutia moyo katika mapambano dhidi ya rushwa ingawaje kazi bado ni kubwa.
Tumefanya mambo matatu. Kwanza, tumetunga Sheria Na. 11 ya mwaka 2007 ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa ambayo imeongeza nguvu ya mapambano dhidi ya uovu huu.
Idadi ya makosa ya rushwa iliongezwa kutoka 4 mpaka24 na
wigo wa wakosaji pia, kwa kuhusisha watu katika sekta binafsi. Mifumo ya
upelelezi na uendeshaji mashitaka nayo imeimarishwa.
Tumeunda chombo kipya
TAKUKURU badala ya TAKURU ambacho kimepewa majukumu ya kuzuia na kupambana na
rushwa badala ya kuzuia peke yake. TAKUKURU imepewa mamlaka zaidi katika
kuongoza mapambano haya. Taasisi imeendelea kuimarishwa kwa kuipatia zana na
vifaa vya kufanyia kazi pamoja na rasilimali watu na mahitaji mengine.
Tumeiwezesha TAKUKURU kufungua ofisi katika Mikoa na Wilaya zote.
Mheshimiwa
Spika;
Maboresho haya
yamewezesha idadi ya kesi za tuhuma za rushwa zinazofikishwa mahakamani
kuongezeka kutoka kesi 50 mwaka 2005 hadi1,900 mwaka
2014. Jumla ya shilingi bilioni 87.8 ziliokolewa. Watumishi wa
Serikali 97 wameachishwa kazi kwa tuhuma za rushwa na matumizi
mabaya ya ofisi zao baada ya ushahidi wa kijinai kukosekana. Kwa upande wa
kupambana na rushwa kwenye shughuli za uchaguzi, tumetunga Sheria ya Kudhibiti
Gharama za Uchaguzi Na. 6 ya mwaka 2010 ili kutoa majibu ya kilio cha siku
nyingi dhidi ya watu wanaotumia fedha kununua kura.
Mapato
na Matumizi ya Fedha na Mali za Serikali
Mheshimiwa
Spika;
Nilieleza katika hotuba yangu ya Kuzindua Bunge la Tisa tarehe 30 Desemba, 2005
kuwa tutatoa kipaumbele cha juu kwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali na nidhamu
ya matumizi ya Serikali. Leo miaka kumi baadae ninaona fahari tumepata
mafanikio makubwa. Mapato ya Serikali yameongezeka kutoka shilingi
bilioni 177.1 mwaka 2005 kwa mwezi hadi takriban shilingi
bilioni 850. Hii imewezesha bajeti ya Serikali kukua kutoka trilioni
4.13 mwaka 2005/2006 hadi trilioni 22.49 mwaka
2015/2016. Isitoshe imetuwezesha kupunguza misaada na mikopo ya washirika wa
maendeleo kutoka asilimia 42 ya Bajeti ya Serikali mwaka
2005 hadi asilimia 15 mwaka 2014/2015 na tumejipa lengo
la kushusha zaidi hadi asilimia 8 mwaka huu wa fedha wa
2015/2016.
Mheshimiwa
Spika;
Mafanikio haya
yametokana hasa na kazi kubwa tuliyoifanya ya kuimarisha Mamlaka ya Mapato
ambao wanastahili pongezi zetu nyingi. Bado naamini tunaweza kufanya vizuri
zaidi ya hivi, kama tukiongeza udhibiti kwa mianya ya kupoteza mapato na kuimarisha
zaidi TRA na mamlaka nyingine za ukusanyaji mapato ya Serikali. Bado ukusanyaji
wa mapato yasiyokuwa ya kodi katika Halmashauri za Wilaya na Miji na katika
Wizara, Idara zinazojitegemea na Wakala wa Serikali uko chini ya lengo.
Huku kuendelee kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa
Spika;
Kwa upande wa nidhamu ya matumizi ya fedha na mali za Serikali tulielekeza
nguvu zetu katika kuimarisha utaratibu wa manunuzi Serikalini na ukaguzi wa
hesabu za Serikali. Kwa upande wa ununuzi wa bidhaa na huduma, tumeendelea
kuimarisha Sheria na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma ili iweze kuhakikisha kuwa kuna
usimamizi thabiti wa sheria hiyo na kanuni zake. Kama mjuavyo sehemu, kubwa ya
fedha za Serikali hutumiwa katika ununuzi wa bidhaa na huduma, hivyo kuwepo
usimamizi mzuri ni jambo jema. Ukikosekana, wizi na rushwa hutawala.
Mheshimiwa
Spika;
Kwa upande wa ukaguzi wa
hesabu za Serikali, tumechukua hatua za makusudi za kuimarisha Ofisi ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Tumetunga Sheria mpya inayoipa
nguvu na uhuru zaidi Ofisi hiyo. Aidha, tumewaongezea bajeti, vitendea kazi na
rasilimali watu. Ofisi 8 za Mikoa zimejengwa na 2 zinaendelea
kujengwa.
Nafurahi kwamba maagizo
yangu kwa viongozi na watendaji katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kuhusu
Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kupewa uzito
linazingatiwa. Taarifa hizo sasa zinasomwa, zinajadiliwa na hatua kuchukuliwa
kwa kasoro zilizoonekana. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali imefanya kazi
nzuri. Wezi na wabadhirifu wanaobainika kuchukuliwa hatua za kisheria
mara makosa yanapogundulika. Kitaifa taarifa hiyo hujadiliwa Bungeni kwa
muda wa kutosha.
Mheshimiwa
Spika;
Niliamua pia kuanzisha
Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali na kuwaweka Wakaguzi wa Ndani wote
wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa chini ya Mamlaka yake na kuwajibika kwake.
Ofisi hii imesaidia kuhakikisha sheria na kanuni za matumizi ya fedha na mali
ya umma zinaheshimiwa. Pia, katika ufuatiliaji na utekelezaji wa mapendekezo ya
CAG. Uimarishaji wa ukaguzi wa ndani na ule wa CAG umesaidia
kuboresha hesabu za Serikali kuwa nzuri zaidi siku hizi. Hati safi zimeongezeka
na hati chafu zinazidi kupungua Serikalini. Kwa mfano katika Halmashauri za
Wilaya na Miji, hati safi zimeongezeka kutoka 56 mwaka 2006 hadi 150 mwaka
2014. Hati zenye mashaka ni 13 na hakuna Hati
isiyoridhisha. Kazi ya kuimarisha ukaguzi na nidhamu ya matumizi lazima
iendelezwe.
Maadili
ya Viongozi wa Umma
Mheshimiwa
Spika;
Katika miaka 10 hii
tumeimarisha mfumo wa kusimamia maadili ya viongozi. Tumefanya hivyo kwa
kutambua kuwa maadili mema ni sifa ya msingi ya kiongozi na huiletea heshima
Serikali. Tumeendeleza Kamati ya Maadili na kuunda Baraza la Maadili kwa mujibu
wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya 1995. Tumepanua
wigo na kwamba sasa mali za viongozi na familia zao hutolewa taarifa na
kiongozi katika Tamko la Mali la kila mwaka. Hii inasaidia kuondoa
uwezekano wa kiongozi kuficha mali kwa mgongo wa mwenza wake au mtoto.
Mheshimiwa
Spika;
Kamati ya Maadili sasa
si tu inapokea fomu na kuzihifadhi, bali inafanya ukaguzi wa mali za viongozi
na kuzifuatilia. Kikwazo chao ni kupata rasilimali fedha. Hili litazamwe zaidi.
Pale inapoonekana kuna makosa ya kimaadili wahusika hufikishwa kwenye Baraza la
Maadili. Sote tumeshuhudia kazi nzuri iliyofanywa na Baraza hilo wakati wa
sakata la Escrow. Bado kazi ya kuimarisha Kamati ya Maadili kwa
rasilimali fedha, vitendea kazi, majengo ya ofisi na rasilimali watu haina budi
kuendelezwa.
Muhimili
wa Mahakama
Mheshimiwa
Spika;
Katika kipindi cha
miaka 10 hii tumefanya jitihada kubwa za kuimarisha mhimili wa
Mahakama. Miongoni mwa mambo mengine, tumefanya mambo muhimu kwa madhumuni ya
kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa jukumu lake la msingi la utoaji haki.
Kwanza, tumetenganisha shughuli za kutoa haki na
za utawala. Tumeunda Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya kushughulikia mambo
ya fedha na utawala. Hivyo basi, Wasajili wa Mahakama wanabaki na jukumu
la kutoa haki. Mpaka sasa mabadiliko haya yamekuwa ya manufaa makubwa kwa
Mahakama kwani yameboresha utekelezaji wa majukumu katika Mahakama. Pili, tumeanzisha
Mfuko wa Mahakama ambao unaipa Mahakama uhuru katika kuendesha shughuli
zake. Sambamba na hilo tumeongeza bajeti ya Mahakama kutoka shilingi
bilioni 36.6mwaka 2006/07 hadi shilingi bilioni 87.6 mwaka
2014/15. Jambo linalohitaji kuboreshwa ni Hazina kutoa fedha kwa wakati ili
shughuli zifanyike kama ilivyopangwa.
Mheshimiwa
Spika;
Jambo la tatu, ni
kwamba tumeongeza idadi ya Majaji wa Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu, Mahakimu
Wakazi na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo. Lengo letu ni kuongeza
nguvukazi ya kusikiliza na kuamua mashauri. Kwa upande wa Mahakimu wa Mahakama
za Mwanzo wameanza kuteuliwa watu wenye Shahada ya Sheria. Hivi sasa
itawawezesha watu wenye mashauri katika Mahakama hizo kupata utetezi wa
Mawakili. Kati ya mwaka 2005 na 2015 tumeongeza Majaji wa Rufani kutoka 8 mwaka
2005 hadi 16, na Majaji wa Mahakama Kuu kutoka 37hadi 81 katika
kipindi hicho. Hali kadhalika, tumeongeza idadi ya Majaji wanawake. Katika Mahakama
ya Rufani wapo 5 na katika Mahakama Kuu wapo 32 na
kufanya jumla yao kuwa 37. Hivi sasa tunao jumla ya Mahakimu
Wakazi 1,266 katika ngazi zote za Mahakama. Kati ya hao534 sawa
na asilimia 35 ni wanawake. Idadi ya Majaji na Mahakimu
wanawake hivi sasa ni kubwa kuliko wakati wowote uliopita.
Mheshimiwa
Spika;
Kutokana na mipango
mizuri iliyowekwa na Jaji Mkuu Mohamed Chande Othman Mahakama zimepiga hatua
kubwa katika kupunguza mlundikano wa kesi Mahakamani. Majaji wamejiwekea
malengo kwa kila Jaji asikilize na kuamua mashauri yasiyopungua 220 kwa
mwaka na kila Hakimu Mkazi mashauri 250 na wale wa Mahakama ya
Mwanzo mashauri 260 kwa mwaka. Kwa sababu hiyo, kuanzia Julai,
2014 hadi kufikia mwezi Machi mwaka 2015 yalifunguliwa mashauri 177,586 na
Mahakama ilisikiliza na kuamua mashauri 179,962. Maana yake ni
kuwa zimesikilizwa zote na nyingine zilizobakia miaka ya nyuma. Bila shaka kwa
kasi hii sasa mrundikano wa kesi utabakia kuwa historia katika kipindi kifupi
kijacho. Nawapongeza sana Majaji na Mahakimu kwa kazi nzuri waifanyayo.
Kwa upande wa ujenzi wa
majengo ya Mahakama Kuu, wamekamilisha ujenzi wa jengo la Mahakama Kuu za
Divisheni ya Kazi pamoja na majengo ya Mahakama Kuu Mikoa ya Shinyanga na
Kagera. Aidha, majengo mawili ya Mahakama za Wilaya na 12 ya
Mahakama za Mwanzo nayo yamekamilika. Hivi sasa, ujenzi unaendelea wa majengo
ya Mahakama Kuu 9 za mikoa iliyosalia, Mahakama za Wilaya 9 na
za mwanzo25.
Maboresho
ya Mfumo wa Utoaji Haki
Mheshimiwa
Spika;
Jambo lingine ambalo
tumefanya katika nia ya kuongeza uwajibikaji, ufanisi, na kupunguza malalamiko
ya wananchi na ucheleweshaji wa mashauri ni kutenganisha kazi ya upelelezi wa
makosa ya jinai na uendeshaji wa mashtaka hayo Mahakamani. Polisi waliokuwa
wanafanya yote sasa watashughulikia upelelezi na ofisi ya Mkurugenzi wa
Mashtaka ndiyo inayoendesha mashauri. Tayari Ofisi za Mkurugenzi wa Mashtaka
zimekwishafunguliwa katika kila Mkoa na sasa tunaenda wilayani. Aidha,
tumeboresha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa rasilimali watu, vitendea
kazi na fedha ili kuongeza ufanisi katika utendaji wa ofisi hiyo muhimu
sana. Kuna haja ya kuendelea kuongezea rasilimali fedha na vitendea kazi
ili ufanisi uongezeke zaidi.
Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
Mheshimiwa
Spika;
Katika kipindi hiki,
tumeimarisha Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kuiwezesha kwa
nyenzo, rasilimali fedha na watu. Tume sasa inafanya kazi katika eneo lote la
Jamhuri ya Muungano. Aidha, kutokana na utumiaji wa mfumo wa elektroniki
malalamiko ya wananchi mengi zaidi yanafikishwa kwenye Tume na mengi yanapatiwa
ufumbuzi. Kwa mfano, idadi ya malalamiko yaliyowasilishwa Tume yameongezeka
kutoka 9,455 mwaka 2006 hadi 25,921 mwaka
2014 na uwezo wa Tume kushughulikia malalamiko kwa mwaka umeongezeka kutoka
malalamiko 3,021 mwaka 2005 hadi malalamiko 18,501 mwaka
2014.
Utendaji
Serikalini
Maeneo
ya Utawala
Mheshimiwa
Spika;
Kwa nia ya kusogeza
huduma, mwaka 2010 tulianzisha mikoa mipya 4 ya Geita, Simiyu, Njombe
na Katavi na wilaya mpya 19. Pia, tulianzishaHalmashauri 45, kata 1,432, vijiji 1,949,
Mitaa 1,379 na vitongoji 8,777. Nimeamua kuanzisha
mkoa mpya wa Songwe kutoka mkoa wa Mbeya na Wilaya sita kama
ifuatavyo: Tanganyika mkoani Katavi, Kigamboni na Ubungo mkoani Dar es Salaam,
Songwe mkoani Mbeya, Kibiti mkoani Pwani na Malinyi mkoani Morogoro. Najua
tulikuwa na maombi mengi lakini kwa sasa tufanye haya.
Maslahi
ya Wafanyakazi
Mheshimiwa
Spika;
Serikali ya Awamu ya Nne
imelipa umuhimu wa juu suala la kuboresha maslahi ya watumishi wa Serikali.
Karibu kila mwaka tumekuwa tunaongeza kima cha chini cha mshahara. Kwa sababu
hiyo, kima cha chini cha mshahara kimeongezeka kutoka shilingi 65,000 mwaka
2005 hadi shilingi 265,000 mwaka wa jana. Mwaka huu
tumefikia shilingi 300,000. Najua bado hakikidhi mahitaji lakini ukilinganisha
na tulikokuwa kipindi hiki tumeongeza sana mishahara ya wafanyakazi. Vile vile,
tumeendelea kupunguza kodi ya mapato kwa mfululizo kutoka asilimia 18mwaka
2005 hadi asilimia 11 mwaka huu. Dhamira yetu ni kutaka kutoa
nafuu zaidi kwa wafanyakazi. Vile vile, tumewapandisha vyeo
watumishi 233,876 na kulipa malimbikizo ya watumishi 422,348 ya
kiasi cha shilingi bilioni 384.8.
Mheshimiwa
Spika;
Tumetekeleza sera ya
ugatuaji wa madaraka kwa wilaya jambo ambalo limelazimu kuongeza rasilimali
fedha na watu kwa Halmashauri za Wilaya na Miji. Kwa ajili hiyo ruzuku kwa
Halmashauri zetu imeongezeka kutoka shilingi bilioni 780 mwaka
2005/2006 hadi shillingi trilioni 4.69mwaka 2015/2016. Aidha,
tumeimarisha utumishi katika Halmashauri kwa kuajiri watumishi wengi wa kada
mbalimbali.
Usawa
wa kijinsia
Mheshimiwa
Spika;
Mwaka 2005 niliahidi
wakati wa kampeni na wakati wa kuzindua Bunge la Tisa, kuwa tutaongeza ushiriki
wa wanawake katika shughuli na nyanja mbalimbali za maisha ya watu wa nchi yetu
ikiwemo nafasi za maamuzi. Ninyi na mimi ni mashahidi kwamba tumetimiza ahadi
hiyo. Idadi ya Wabunge wanawake imeongezeka kutoka 62 mwaka
2005 hadi 127. Hivi sasa hamsini kwa hamsini ni rasmi katika
Katiba Inayopendekezwa. Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu na
Bunge letu tumepata Spika mwanamke Mheshimiwa Anne Semamba Makinda.
Wanawake wameongezeka
katika ngazi zote kuu za uamuzi. Kwa mfano, tunao Mawaziri wanawake 10, Naibu
Mawaziri wanawake 5, Majaji wanawake 37 na Wakuu
wa Wilaya wanawake wako 53. Kwa upande wa Makatibu Wakuu,
Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi Watendaji n.k. pia
wameongezeka. Katika elimu nako tuna usawa wa kijinsia kwa upande wa idadi ya
wanafunzi wa kike na wa kiume katika shule za msingi na sekondari. Katika
vyuo vya elimu ya juu, idadi ya wanafunzi wa kike imeongezeka kwa kasi
kutoka 10,039mwaka 2005 hadi 78,800 mwaka 2014.
Hali
ya Uchumi
Mheshimiwa
Spika;
Wakati ninaingia
madarakani mwaka 2005 niliwaahidi Watanzania wenzangu kuwa tutafanya kila
tuwezalo kujenga uchumi ulio imara na shirikishi. Hususan, nilisema
nitaendeleza sera za mageuzi ya kiuchumi na kuweka misingi madhubuti ya kukuza
uchumi, kuongeza ajira, kuongeza Pato la Taifa na kupunguza umaskini. Katika
miaka kumi iliyopita tumeendelea kusimamia kwa kiwango kizuri sera za uchumi
jumla na sera za uchumi katika ngazi ya chini zinazogusa wananchi wa kawaida.
Jitihada zetu hizo
zimezaa matunda ya kutia moyo. Katika kipindi hiki, Pato la Taifa lilikua kwa
wastani wa takriban asilimia 7. Nchi
yetu ni miongoni mwa mataifa 10 ya Afrika na 20 duniani
ambayo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa. Pato ghafi la Taifa limeongezeka
zaidi ya mara tatu kutoka shilingi trilioni 14.1 mwaka 2005
hadi kufikia trilioni 79.4 mwaka 2014. Hivyo basi, pato la
wastani la Mtanzania nalo limeongezeka kutoka shilingi 441,030 mwaka
2005 hadi shilingi 1,724,416 mwaka 2014.
Mheshimiwa
Spika;
Mauzo yetu ya nje
yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.67 mwaka
2005 hadi Dola za Marekani bilioni 8.76 mwaka 2014[A1] na kutunisha akiba yetu ya fedha za
kigeni na kutuwezesha kuagiza bidhaa na mahitaji ya nchi kutoka nje kwa kipindi
cha miezi 4.1 kama tulivyopanga. Mfumuko wa bei ni asilimia 6.1.
Mheshimiwa
Spika;
Kama mjuavyo, mwaka 2000
nchi yetu ilijiwekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya hadi mwaka 2025. Mwaka 2010
tulitengeneza Mpango wa Muda Mrefu (Long Term Perspective Plan) wa (2010 –
2025) wa kuongoza utekelezaji wa Dira kwa miaka 15 iliyobaki. Tuligawa
utekelezaji wake katika Mipango mitatu ya Maendeleo ya Miaka Mitano kila mmoja.
Tuko katika hatua za mwisho za utekelezaji wa Mpango wa Kwanza, (2011/12 –
2015/16) na kuandaa mpango wa pili (2016/17 – 2021/22).
Mpango
wa Matokeo Makubwa Sasa
Mheshimiwa
Spika;
Kwa madhumuni ya kuboresha utendaji wa Serikali nilianzisha Mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN). Huu ni mfumo mpya wa kupanga, kufuatilia na kusimamia
utekelezaji wa malengo na shughuli za Serikali kwa nia ya kuhakikisha kuwa
kilichokusudiwa kinafanyika, tena kwa wakati. Tuliamua kuanza na sekta sita
za Elimu, Nishati, Kilimo, Uchukuzi, Maji na Mapato ya Serikali.
Baadae sekta ya afya na uboreshaji mazingira ya uwekezaji ziliongezwa.
Katika kipindi hiki
kifupi Mpango umethibitisha kuwa wenye manufaa. Mambo katika sekta
zilizojumuishwa katika BRN yameanza kwenda vizuri. Changamoto yetu kubwa
imekuwa ni upatikanaji wa fedha zinazohitajika kwa wakati kutoka Hazina. Kama
changamoto hiyo isingekuwepo mambo yangekuwa mazuri zaidi.
Uboreshaji
wa Mazingira ya Biashara na Uwekezaji
Mheshimiwa
Spika;
Kwa kutambua umuhimu wa uwekezaji katika kukuza uchumi, kuzalisha ajira,
kuongeza mapato na kupunguza umaskini, Serikali yetu imekuwa inachukua hatua
thabiti za kutengeneza mazingira mazuri ya kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje
kuchagua Tanzania kuwa nchi inayofaa kuwekeza.
Mwaka 2010 tumetengeneza Sera na kutunga Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma
na Sekta Binafsi (Public Private Partnership—PPP). Lengo letu ni kuweka
mazingira mazuri kwa sekta binafsi kuvutika kushirikiana na Serikali katika
shughuli za kiuchumi na maendeleo. Faida kubwa ya utaratibu huu ni
kuipunguzia Serikali mzigo wa kuwekeza katika baadhi ya shughuli ambazo sekta
binafsi inaweza kubeba sehemu ya gharama. Hii siyo tu inaongeza kasi ya
maendeleo, bali kuiwezesha Serikali kuokoa fedha ambazo inaweza kuzitumia kwa
shughuli nyingine.
Juhudi zetu za kuboresha mazingira ya uwekezaji zinaendelea kuzaa matunda mema.
Kati ya 2005 na 2014, Kituo chetu cha Uwekezaji (TIC) kimesajili miradi 7,159 yenye
thamani ya Dola za Marekani bilioni 154.274. Kati ya miradi
hiyo asilimia 49.38 ni ya wawekezaji wa ndani,asilimia
23.41 ni wawekezaji wa kutoka nje na asilimia 27.18 ni
miradi ya ubia baina ya Watanzania na wawekezaji wa kigeni. Ajira 16,000zilipatikana.
Ukuaji huu wa uwekezaji umeongeza mapato ya Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa ya
uwekezaji iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Viwanda na Biashara
Duniani (UNCTAD) ya mwaka 2015, Tanzania inaongoza Afrika Mashariki kwa kuvutia
uwekezaji. Ilipata Dola za Marekani bilioni 2.142 sawa
na asilimia 31.5 ya uwekezaji wote katika Jumuiya yetu.
Sekta
za Uzalishaji
Sekta
ya Kilimo
Mheshimiwa
Spika;
Kuendeleza kilimo
ilikuwa ni moja ya mambo tuliyoyapa kipaumbele cha juu. Shabaha yetu kuu ni
kutaka kuongeza tija ili uzalishaji uongezeke, wakulima wapate mavuno mengi,
masoko ya uhakika yawepo na bei iwe nzuri ili mapato yao yaongezeke na umasikini
uwapungukie. Vile vile wao na taifa lijitosheleze kwa chakula.
Kwa ajili hiyo mwaka
2006 tuliasisi Programu ya miaka 7 ya Maendeleo ya Sekta ya
Kilimo (Agricultural Sector Development Programme—ASDP). Katika Programu hiyo,
matatizo yanayofanya tija na uzalishaji katika kilimo kuwa mdogo yalitambuliwa
na kutengenezewa mpango wa kuyatatua. Serikali pia ilianzisha mikakati,
programu na mipango mingine ya kuongeza msukumo katika kuleta mageuzi ya
kilimo. Miongoni mwa hiyo ni mkakati wa Kilimo Kwanza, Mpango wa
Kuendeleza Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Mpango wa
Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo (TAFSIP), Sera ya Umwagiliaji
tuliyoitunga mwaka 2010 na Programu ya Mageuzi na Modenaizesheni ya Ushirika.
Mheshimiwa
Spika;
Pamoja na hayo, tumeongeza
pia bajeti ya sekta ya kilimo kutoka shilingi bilioni 233.3 mwaka
2005/06 hadi shilingi bilioni 1,084.7 mwaka 2014/15. Kuongezwa
kwa bajeti kumewezesha fedha za ruzuku ya mbolea na pembejeo kuongezeka
kutoka shilingi bilioni 7.5 mwaka 2005/06 hadi shilingi
bilioni 299.3 mwaka 2013/14. Matrekta makubwa na madogo yameongezeka
kutoka 7,491 mwaka 2005 hadi 16,412 mwaka
2014. Kwa sababu hiyo matumizi ya jembe la mkono yamepungua kutoka asilimia
70 hadi asilimia 62. Tumeongeza maafisa ugani kutoka 3,379mwaka
2005 hadi 7,974 mwaka 2014.
Vituo vya utafiti wa
kilimo tumeviongezea rasilimali fedha, watu na vitendea kazi. Aidha, tumeanza
safari ya kufufua mashamba ya mbegu ya Serikali na kuhusisha sekta binafsi,
Jeshi la Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa katika kuzalisha mbegu.
Aidha, tumeimarisha Wakala wa Mbegu (Agricultural Seed Agency – ASA) na
kuongeza uzalishaji wa mbegu bora kutoka tani 10,477.17 mwaka
2005 hadi tani 32,340 mwaka 2014.
Mheshimiwa
Spika;
Juhudi za Serikali
kuendeleza kilimo zimezaa matunda mazuri. Tija katika uzalishaji wa mazao ya
biashara na chakula imeongezeka. Kwa upande wa mazao ya chakula uzalishaji
umeongezeka kutoka tani milioni 9.66 mwaka 2005 hadi
tani milioni 16.01 mwaka 2014. Ongezeko hili limeliwezesha
taifa letu kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 125 mwaka
2014 ikilinganishwa na asilimia 95 mwaka 2005.
Uzalishaji wa mazao ya asili ya biashara umeongezeka toka tani 427,738 mwaka
2005 hadi tani 569,054 mwaka 2014 na uzalishaji wa mbegu za
mafuta umeongezeka karibu ya mara 4 toka tani 1,389.9 mwaka
2005 hadi tani 5,545.6 mwaka 2014. Aidha, uzalishaji wa
matunda nao umeongezeka toka tani milioni 1.2 mwaka 2005 hadi
tani milioni 4.4 mwaka 2014 na maua toka tani 5,862 hadi
tani 10,790.
Mheshimiwa
Spika;
Upatikanaji wa masoko ya
uhakika na bei nzuri kwa mazao ya wakulima bado ni changamoto. Pia kuna tatizo
la upungufu wa maghala ya kuhifadhi mazao. Jitihada zinaendelea kupata mkopo au
wabia wa kujenga maghala ya kisasa nchi nzima. Programu ya Mageuzi na
Modenaizesheni ya Ushiriki ilianzishwa ili kutatua tatizo la masoko. Aidha,
tumeanza maandalizi ya kuanzisha soko la bidhaa (Commodity Market Exchange) kwa
nia hiyo hiyo. Naamini misingi mizuri tuliyoijenga pamoja na kuenea kwa SACCOS
na kuanza kwa Benki ya Kilimo ikiendelezwa itatoa mchango mkubwa katika
kuongeza kasi ya mapinduzi ya kilimo.
Mifugo
Mheshimiwa
Spika;
Kwa upande wa mifugo, dhamira yetu ilikuwa kuanza safari ya kuleta mageuzi
katika sekta hii. Safari hiyo tumeianza kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya
Mifugo. Changamoto zinazochangia maendeleo duni ya sekta hii zimeainishwa na
kutengenezewa mkakati wa utekelezaji. Katika kipindi hiki malambo 1,008,
majosho 2,364 na maabara 104 za
mifugo zimejengwa. Visima virefu 101 vimechimbwa, malambo 370 na
majosho 499 yamekarabatiwa katika kipindi hiki cha miaka 10.
Ukarabati na ujenzi wa
majosho umeongeza idadi kutoka 2,177 mwaka 2006 hadi 3,637 mwaka
2015. Tumeongeza Maofisa Ugani kutoka2,270 mwaka 2005 hadi 6,041 mwaka
2014. Kuhusu uhamilishaji, tumeongeza vituo kutoka kituo 1 mwaka
2005 hadi vituo 8 mwaka 2015 na kuwezesha ng’ombe 955,360 kuhamilishwa
katika miaka 10 hii.
Mheshimiwa
Spika;
Mazingira mazuri ya uwekezaji kwa sekta binafsi tuliyoyajenga yamewezesha
viwanda vya kusindika nyama, maziwa na vyakula vya mifugo kuongezeka. Viwanda
vya kusindika maziwa vimeongezeka kutoka 22 mwaka 2005
hadi 74 mwaka 2015. Viwanda vya kuzalisha vyakula vya mifugo
vimeongezeka kutoka viwanda 6 mwaka 2005 hadi 80 mwaka
2015 vikiwa na uwezo wa kusindika tani milioni 1.4 za vyakula
hivyo kwa mwaka. Aidha viwanda na machinjio ya kisasa 9 vimejengwa
katika kipindi hiki. Usindikaji wa ngozi pia umeongezeka kutoka vipande 790,000 mwaka
2005 hadi vipande milioni 3.78 mwaka 2014. Hivi sasa kwa
mfano, uzalishaji wa malisho ya mifugo (hei) umefikia marobota 957,860 ikilinganishwa
na marobota 178,100 mwaka 2005.
Safari yetu ya kuanza
kuondoka kwenye uchungaji kwenda kwenye ufugaji imeanza. Vijiji vingi vimeandaa
mipango ya matumizi bora ya ardhi na hivyo vimetenga maeneo ya kilimo na ya
ufugaji. Tuendelee kuhimiza vijiji vyetu kutekeleza mipango hiyo ili wafugaji
wapate maeneo ya malisho mbali na mazao ya wakulima. Pia, tuhimize uhamilishaji
kama mlango wa kuingilia kwenye kuboresha kosafu za mifugo yetu.
Uvuvi
Mheshimiwa
Spika;
Wakati nazindua Bunge la Tisa tarehe 30 Desemba 2005 nilisema kuwa Serikali ya
Awamu ya Nne itatoa kipaumbele kwenye kuendeleza sekta ya uvuvi. Katika
kutekeleza hayo tumefanya yafuatayo. Kwanza, nimeunda Wizara mpya
ya Mifugo na Uvuvi. Pili, tulifuta kodi ya zana za uvuvi ili
kuwawezesha wavuvi kupata zana bora na za kisasa kwa bei nafuu zaidi. Tatu, tumeimarisha
vyuo vya uvuvi na hivi sasa vina uwezo wa kudahili wanafunzi 1,215 ikilinganishwa
na wanafunzi 127 mwaka 2005. Hii imetuwezesha kuongeza wagani
wa uvuvi kutoka 103 mwaka 2005 hadi 540 mwaka
2014. Nne, tumeongeza sana juhudi za kupambana na uvuvi haramu
ili kutunza mazingira, mazalia ya samaki na kuzuia kuvuliwa au kuuawa kwa
samaki wadogo.
Tumeimarisha maabara ya
Taifa ya Samaki pale Nyegezi kwa vifaa vya kisasa na wataalamu ili iende na
wakati. Tano, tumeongeza msukumo wa kuhimiza ufugaji wa samaki na
kuwezesha mashamba ya samaki kuongezeka kutoka 13, 011 mwaka
2005 hadi 20, 325 mwaka 2014.
Uvuvi haramu unapungua.
Mapato ya sekta ya uvuvi yameongezeka kutoka shilingi bilioni
351.6 mwaka 2005 hadi shilingi trilioni 1.8 mwaka
2013. Bado tuna kazi kubwa ya kufanya katika sekta hii ili kuongeza
tija na mapato ya wavuvi na taifa.
Utalii
Mheshimiwa
Spika;
Kwa upande wa utalii, tumeendelea na jitihada za kuiendeleza sekta hii muhimu.
Tumeongeza kutangaza vivutio vya utalii vya nchi yetu katika masoko makubwa
duniani. Sekta ya utalii imekua kwa wastani wa asilimia 7.1 na
imechangia asilimia 25 ya mapato ya fedha za kigeni. Idadi ya
watalii imeongezeka kutoka watalii 612, 754 mwaka 2005 hadi
watalii 1,140,156 mwaka 2014. Idadi ya vitanda katika mahoteli
imeongezeka kutoka 15,828 hadi 21,929. Mapato pia
yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 823.05 mwaka 2005
hadi Dola za Marekani bilioni 2 mwaka 2014. Ajira za moja kwa
moja zimeongezeka kutoka 32,673 hadi 686,130 na
zisizokuwa za moja kwa moja kutoka165,883 hadi 1,318,109.
Haya ni mafanikio makubwa na ya kujivunia.
Mheshimiwa
Spika;
Katika kipindi hiki
tumekabiliana na tukio kubwa la ujangili wa wanyamapori hasa wa ndovu kutokana
na kushamiri kwa biashara ya meno ya ndovu na bei kuwa kubwa katika nchi za
Mashariki ya Mbali. Vuguvugu la ujangili lilifikia kiwango cha kutishia
kumaliza ndovu nchini na dunia nzima. Tukaamua kuchukua hatua za kuidhibiti
hali hiyo. Tumefanya operesheni tatu kukabiliana na tishio hili. Ya kwanza,
iliendeshwa na Idara ya Wanyamapori na Misitu wakishirikiana na TANAPA na
Ngorongoro Conservation Area. Hii hasa ilihusu kupambana na ujangili
katika hifadhi na mapori ya Kaskazini mwa Tanzania. Mafanikio makubwa
yalipatikana.
Mheshimiwa
Spika;
Operesheni ya pili ni
ile iliyohusisha Jeshi la Polisi katika hifadhi na sehemu nyingine za Tanzania.
Operesheni Kipepeo kama ilivyoitwa nayo ilipata mafanikio. Na ya tatu,
Operesheni Tokomeza iliyohusisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama. Pamoja na
changamoto zake operesheni hizi zimesaidia sana kupunguza kasi ya ujangili
nchini. Matokeo yake katika sensa ya ndovu iliyofanyika mara ya mwisho, ukiacha
Ruaha, hali katika hifadhi na mapori mengine ina muelekeo mzuri.
Kuundwa kwa Mamlaka ya
Wanyamapori (TAWA) yenye mamlaka makubwa zaidi ya kusimamia sekta ya
wanyamapori nako kutaimarisha uhifadhi na mapambano ya ujangili. Kwa mipango na
program zilizopo Wizarani, naamini mambo yatakuwa mazuri zaidi muda si mrefu.
Viwanda
Mheshimiwa
Spika;
Katika miaka kumi hii, sekta ya viwanda imeendelea kukua kwa kasi nzuri ya
kutia moyo. Viwanda vikubwa, vya kati na vidogo vimeongezeka kutoka 11,
544 mwaka 2005 hadi viwanda 51,224 mwaka 2015. Kati
ya mwaka 2005 na 2014 na miradi 751 imepewa leseni za kudumu
na BRELA ya kuanzisha viwanda. Mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa
umefikia asilimia 7.3 mwaka 2014 kutokaasilimia
6.8 mwaka 2005. Mchango wa viwanda kwenye mauzo ya nje umeongezeka
kutoka asilimia 9.3 mwaka 2005 hadi asilimia 23.3 mwaka
2014.
Tunategemea ukuaji
mkubwa wa viwanda katika Mpango wa Pili wa maendeleo wa miaka 5 kutokana
na misingi imara tuliyoijenga katika Mpango wa Kwanza. Ujenzi wa kiwanda cha
chuma kule Liganga na makaa ya mawe cha Mchuchuma, unatarajiwa kuanza mwaka huu
na kiwanda cha kuchakata gesi pale Lindi unatarajiwa kuanza baada ya taratibu
za kuwapatia ardhi zitakapokamilika. Hivi ni viwanda vya msingi na mama
ambavyo vitachochea kasi ya ukuaji wa viwanda nchini na uchumi kwa jumla.
Madini
Mheshimiwa
Spika;
Sekta ya Madini ndiyo ya pili baada ya utalii kwa kuingiza fedha nyingi za
kigeni. Kama nilivyoahidi, tulipitia upya sera, sheria na mikataba ya madini
iliyokuwepo na kutengeneza sera na sheria mpya. Halikadhalika,
tulianzisha mazungumzo na baadhi ya makampuni ambayo hatimaye yalizaa
marekebisho ya mikataba yao na hivyo kuboresha maslahi ya taifa.
Kufuatia marekebisho
hayo, makampuni husika ya madini yanalipa kodi ya mapato. Bila ya hivyo huenda
mpaka leo yangekuwa hayajaanza kulipa kodi. Kutumika kwa Sheria mpya ya Madini,
viwango vipya vya mrahaba na kupunguzwa kwa misamaha ya kodi vimeongeza mapato
ya Serikali. Aidha, tuliunda Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) ambao
umewezesha kukagua mahesabu ya migodi kuhusu uwekezaji na mauzo ya madini na
kuwawezesha TRA kutoza kodi stahiki kutoka kwa makampuni hayo.
Mheshimiwa
Spika;
Mabadiliko haya pamoja
na kuongezeka kwa uwekezaji katika sekta hii yamewezesha mchango wa sekta ya
madini katika Pato la Taifa kuongezeka kutoka asilimia 2.9 mwaka
2005 hadi kufikia asilimia 3.5 mwaka 2014. Thamani ya mauzo ya
madini nje ya nchi pia imeongezeka kutoka Dola za Marekani milioni
655.5 mwaka 2005 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni
1.794 mwezi Desemba 2014. Mambo yangekuwa mazuri zaidi kama bei ya
dhahabu isingeshuka katika kipindi hiki.
Mheshimiwa
Spika;
Serikali ilifanya uamuzi wa kulifufua na kuliwezesha Shirika letu la Madini
(STAMICO) kuanza tena kazi ya utafutaji na uchimbaji wa madini kupitia kampuni
zake tanzu. STAMICO kwa kupitia kampuni yake ya STAMIGOLD imeanza kuzalisha
dhahabu na kuuza nje. Vilevile, tumejiunga na Mpango wa Uwazi wa Uvunaji wa
Maliasili (EITI) ambao umesaidia sana katika kuongeza uwazi katika biashara ya
madini na kusaidia katika ukusanyaji wa mapato kutoka kwenye makampuni ya
madini.
Katika kipindi hiki, migodi mitatu mipya ilianzishwa nayo ni Migodi ya dhahabu
wa Buzwagi (Shinyanga) na New Luika (Mbeya) na mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka
(Ruvuma). Aidha, miradi mikubwa mingine 8 imeendelezwa
na kufikia hatua ya kuanzisha mgodi ukiwemo Mradi wa Urani wa Mkuju (Ruvuma),
Mradi wa Chuma Liganga na Mradi wa Makaa ya Mawe wa Mchuchuma (Njombe). Pia,
ajira rasmi kwenye migodi mikubwa nchini imeongezeka kutoka waajiriwa 3,517 mwaka
2005 hadi waajiriwa 15,000 mwaka 2014. Hali kadhalika,
makampuni ya madini yameongeza unununzi wa bidhaa na huduma hapa nchini (local
procurement) kutoka Dola za Marekani milioni 230.41 mwaka 2005
hadi Dola za Marekani milioni 536.56 mwaka 2014.
Mheshimiwa
Spika;
Katika kipindi hiki pia,
tumetenga maeneo 8 kwa ajili ya wachimbaji wadogowadogo.
Maeneo haya yamewezesha wachimbaji wadogo kuchimba madini bila bughudha. Aidha,
Wizara imenunua mitambo miwili kwa ajili ya uchorongaji wa miamba kusaidia
utafiti wa madini kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Tumeanzisha mfuko wa
kuwakopesha wachimbaji wadogo pale Wizarani ili kutoa fursa kwa wachimbaji
wadogo kupata mikopo ya kuendeleza shughuli zao.
Nishati
Mheshimiwa
Spika;
Wakati naanza kazi ya
uongozi wa nchi yetu, Tanzania ilikuwa inakabiliwa na ukame mkubwa
uliosababisha upungufu mkubwa wa chakula. Pia kulikuwa na upungufu mkubwa wa
umeme kwa sababu ya mabwawa ya kuzalisha umeme kukosa maji ya kutosha.
Serikali ililazimika kulisha watu zaidi ya milioni 3,776,000 na
kukodisha mitambo ya kuzalisha umeme. Kwa siku za usoni tuliamua kuchukua hatua
thabiti ya kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi asilia na vyanzo
vingine kama vile makaa ya mawe, mionzi ya jua na upepo.
Ujenzi umekamilika wa
bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara na Songo Songo litakaloongeza kiasi cha
gesi kuja Dar es Salaam na kuwezesha uzalishaji wa megawati 3000 za
umeme. Wakati huo huo kazi ya kujenga vituo vya kufua umeme inaendelea pale Kinyerezi,
Dar es Salaam. Umeme huo utakidhi mahitaji ya umeme sasa na miaka kadhaa
ijayo.
Mheshimiwa
Spika;
Katika kipindi
hiki tuliunda Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ambao wamefanya kazi kubwa na
nzuri ya kusambaza umeme kwa vijiji 5,336 kati ya vijiji 12,423 nchini.
Kazi kubwa iliyofanyika vijijini inapochanganywa na ile ya mijini imeongeza
idadi ya Watanzania wanaopata umeme kutoka asilimia 10 hadi asilimia
40 mwaka 2015. Uamuzi uliofanywa katika Bajeti ya mwaka huu wa
kukusanya fedha kwa ajili ya umeme vijijini kupitia mafuta ya petroli,
utasaidia sana kuongeza kasi ya kusambaza umeme vijijini.
Gesi
Asilia
Mheshimiwa
Spika;
Tumepata mafanikio
katika utafutaji wa mafuta na gesi asilia. Kuanzia mwaka 2010 nchi yetu imepata
bahati ya ugunduzi wa kiasi kikubwa cha gesi bahari kuu. Mpaka sasa
zimegundulika futi za ujazo trilioni 47.08. Ukijumlisha na futi
za ujazo trilioni 8 zilizogunduliwa takriban miaka 40
iliyopita kule Songo Songo na Msimbati jumla ya rasilimali ya gesi asilia
nchini ni futi za ujazo trilioni 55.08. Kazi ya utafutaji
inaendelea na wataalamu wanasema kuwa Tanzania inaweza kuwa na akiba ya futi za
ujazo trilioni 200. Kiasi cha gesi kilichogunduliwa mpaka
sasa ni kikubwa na kufanya Tanzania kuwa mahala papya pa kuipatia dunia nishati
hii.
Gesi asilia tuliyonayo
ikisimamiwa na kutumiwa vizuri itaiwezesha nchi yetu na watu wake kupata
maendeleo makubwa na kuondokana na umaskini. Ni fursa ya aina yake ya
kuipatia Serikali mapato makubwa na kuiwezesha kutimiza kwa uhakika majukumu
yake na mipango yake. Lakini, ili hayo yaweze kufanyika hapana budi pawepo
usimamizi mzuri wa hatua zote muhimu za mnyororo wa thamani: yaani utafutaji,
uchimbaji, usafirishaji, uuzaji wa gesi asilia na matumizi yake nchini kama
nishati na mali ghafi ya viwanda upande mmoja. Upande mwingine inategemea
sana matumizi mazuri ya mapato yatokanayo na rasilimali hiyo.
Mheshimiwa
Spika;
Ni kutokana na kutaka
kuhakikisha kwamba mambo yanakuwa hivyo ndiyo maana tumetunga Sera ya Gesi
Asilia na kuwasilisha katika Bunge hili ile Miswada miwili yaani wa Sheria ya
Petroli na ule wa Matumizi ya Mapato ya Mafuta na Gesi. Nawashukuru
Waheshimiwa Wabunge kwa kuipitisha Miswada hii nami nitaitia saini mara
nitakapoletewa.
Usafirishaji
na Uchukuzi
Barabara
Mheshimiwa
Spika;
Serikali ya Awamu ya
Nne, imetoa kipaumbele cha juu kwa uendelezaji wa miundombinu ya usafirishaji
na uchukuzi nchini. Hii ni pamoja na barabara, reli, bandari, usafiri wa majini
na usafiri wa angani. Tumeendeleza kazi ya kuongeza mtandao wa barabara
za lami nchini kwa mafanikio makubwa. Karibu barabara kuu zote nchini na
zile zinazounganisha mikoa zimekamilika kujengwa au kazi ya ujenzi inaendelea.
Kwa sababu hiyo hivi leo kutokea po pote nchini kwenda Dar es salaam unafika
siku hiyo hiyo, tofauti na ilivyokuwa zamani watu walichukua zaidi ya siku
moja. Adha ya kupita Kenya na Uganda kwa watu wa Mikoa ya Ziwa
tumeimaliza.
Katika mkakati wetu wa
kupanua mtandao wa barabara za lami nchini, tulitambua barabara za urefu
wa kilomita 11,474 za kujengwa kwa kiwango cha lami.
Baadae tuliongeza barabara nyingine na kufikisha kilomita 17,742 katika
mpango huo. Utekelezaji wake upo katika hatua mbalimbali. Tayari
ujenzi wa kilomita 5,568 kwa upande wa barabara kuu na kilomita 535 kwa
barabara za mijini umekamilika. Ujenzi wakilomita 3,873 unaendelea.
Upembuzi yakinifu na usanifu umekamilika kwa barabara za urefu wa kilometa
4,965 kinachosubiriwa ni kupatikana fedha ujenzi uanze. Baadhi
ya barabara hizo zimo katika bajeti ya mwaka huu wa fedha. Barabara za urefu
wa kilometa 3,336zinafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.
Mheshimiwa
Spika;
Katika kipindi hiki pia, madaraja madogo 7,200 na
makubwa 12 yamejengwa na mengine 16 yapo
katika hatua mbalimbali za ujenzi. Miongoni mwa madaraja makubwa
yaliyokamilika ni daraja la Mto Malagalasi na yanayojengwa ni daraja la
Kigamboni na lile la Mto Kilombero. Madaraja haya yalikuwa miongoni mwa
matano yaliyopangwa kujengwa katika Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka
Mitano mara baada ya uhuru. Madaraja mawili yaani la Kirumi lilijengwa mwaka
1985 na la Rufiji mwaka 2003. Kwa upande wa vivuko, tumeongeza vipya 15 na
kufikisha idadi ya 28 kote nchini mwaka 2014.
Mheshimiwa
Spika;
Tumeongeza sana fedha katika mfuko wa barabara kutoka shilingi bilioni 73.08 mwaka
2005/06 hadi shilingi bilioni 866.63 mwaka 2015/16. Hii
itasaidia katika matengenezo ya barabara za lami tulizojenga na kujenga
nyingine mijini. Hali kadhalika itatumika kuimarisha barabara za udongo na
changarawe wilayani na vijijini ziweze kupitika wakati wote. Katika
kipindi hiki barabara za changarawe zimeongezeka kutoka kilometa
9,424 hadi kilometa 22,089.
Mheshimiwa
Spika;
Katika miaka kumi hii idadi ya vyombo vya moto yaani magari, bajaji na pikipiki
imeongezeka kutoka 1,696,088 mwaka 2005 hadi3,313,254 hivi
sasa. Ongezeko hili linalotokana na hali ya kiuchumi ya watu wengi kuwa
nzuri limezua tatizo la msongamano.
No comments:
Post a Comment