Sunday, November 29, 2015

TAARIFA KWA UMMA JUU YA KILIMO MKOA WA MWANZA.



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA

OFISI YA MKUU WA MKOA WA MWANZA TAARIFA KWA UMMA TAREHE 18/11/2015

Ndugu Wanahabari.
Mkoa wa Mwanza kwa kawaida hupata misimu miwili ya mvua kwa mwaka. Misimu hiyo ni ya mvua za vuli na masika ambapo mvua za vuli huanza kunyesha mwezi Septema/Oktoba hadi kufikia mwezi Januari; na msimu wa mvua za masika hunyesha Kuanzia mwezi Machi hadi Mei ya kila mwaka. Wastani wa mvua ni mm 720 hadi mm 1200 kwa mwaka ambazo hutawanyika kati ya mm 570 mm kwa mwaka hadi mm 1800 kwa mwaka.

Ndugu Wanahabari.
 Mkoa wa Mwanza unatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani kwa maana ya mvua za juu ya wastani wa mm 1300 katika kipindi hicho cha Oktoba – Desemba, 2015. Hii ni kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Kwa kuzingatia utabiri huo wa hali ya hewa, tunawashauri wakulima na wananchi katika Mkoa wa Mwanza kufanya yafuatayo:-
Kulima mazao ya chakula aina ya wanga yanayohitaji au kustahimili mvua za wastani hadi mvua za juu ya wastani na pia kukomaa kwa muda mfupi kiasi cha kuweza kukomaa kufikia mwezi Desemba, 2015/Januari, 2016. Mkazo zaidi utiliwe kwenye mazao ya:-
Viazi vitamu hasa mbegu (Variety) zisizolikishwa (Non-Orange Fortified) aina ya Polista na Ukerewe, “Kishiga Mdege” na matembele; pamoja na mbegu zilizolikishwa (Orange Fortified) kama Ejumla, Karotoda na Kabode.
Mazao mengine ni mahindi hasa katika ukanda wa mazao (agro-ecological zone) unaopata mvua za wastani wa mm 1100 hadi 1200 kwa mwaka au Zaidi ukanda ambao unajumuisha Tarafa za Ukara na Ilangala katika Wilaya ya Ukerewe na Tarafa za Kahunda na Buchosa katika Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa. Aina ya mbegu (variety) za mahindi zinazopendekezwa ni:-
(i) Aina ya mbegu ya mahindi chotara (hybrid) ni pamoja na SeedCo yenye alama ya pundamilia (SC 513), Pannar inayokomaa kwa muda mfupi (PAN 4M-19) na kati PAN 15), Delkab (DKC 8053).
 (ii) Aina ya mbegu ya mahindi isiyochotara/ya chavua huria (OPV) ni pamoja na Kilima, Stuka, TAN 600H, Kitale na TMV 1. Mpunga hususan mbegu aina ya SARO 5 (TXD 306) na Supa inayolimwa mabondeni (low land rice); na NERICA 2 na 4 zinazolimwa nchi kavu.

Ndugu Wanahabari.
Tunawashauri wananchi wetu kutenga fedha na kununua pembejeo za kilimo hasa mbegu, mbolea na dawa za kilimo mapema kwa kuzingatia kuwa matumizi ya pembejeo yanaweza kuongezeka kutokana na mvua hizo ambazo zinaweza kusababisha kuoshwa ama dawa za kudhibiti wadudu waharibifu na magonjwa au mfumuko wa magonjwa hasa ya ukungu kutokana na mazingira ya unyevunyevu mwingi katika ardhi na hewani. Aidha, pembejeo zinaweza kupanda bei na kuwa adimu kutokana na kutopatikana kwa wingi na kwa urahisi kwa sababu ya mvua kuharibu miundombinu ya barabara hasa katika maeneo ya vijijini na kuathiri usafirishaji mazao. Ili kupunguza gharama za uzalishaji kutokana na mvua, wakulima wanaweza kugawanya kiasi cha mbolea kinanchohitajika kwa eneo na kuweka kwa awamu lakini pia tunawashauriwa kuwatumia Maafisa Ugani katika Wilaya.

Vilevile tunawashauri wakulima kulima kwa kukinga au kuzuia mmomonyoko wa udongo kutokana na mvua hasa katika maeneo yenye miinuko na vilima. Mmomonyoko wa udongo unaweza kukingwa au kuzuiliwa kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulima kilimo cha matuta kwa kukinga/kukata mteremko, kulima na kuacha mistari (strip) ya nyasi au kufanya kilimo hifadhi. Zaidi, wakulima katika maeneo yanayo hifadhi unyevu kwa wingi au kutwaamisha maji (mabonde) wanaweza kulima kwa kufuata uelekeo wa maji kwa kuacha mistari ya nyasi kuzuia mmomonyoko wa udongo au kulima kilimo hifadhi kinachopunguza ukwatuaji wa udongo.

Ndugu wanahabari.
Tunawashauri wananchi kujiwekea akiba ya chakula hasa cha aina ya wanga kutokana na sababu kwamba mvua zinazotarajiwa katika kipindi hicho cha Oktoba na Desemba, 2015 zinaweza kuharibu miundombinu ya barabara na kusababisha ugumu wa usafirishaji wa vyakula hivyo kuleta uhaba wa vyakula katika masoko. Msisitizo wa kujiwekea akiba ya chakula unatolewa Zaidi kwa kuzingatia ukweli kwamba, Mkoa wa Mwanza wenye wakazi 2,772,509 huhitaji jumla ya Tani 708,376 za chakula aina ya wanga kwa mwaka mzima, ambapo, katika msimu wa kilimo wa 2014/2015 Mkoa ulizalisha Tani 495,863.2 za chakula aina ya wanga hivyo kuuwezesha kujitosheleza kwa 70% tu kwa chakula aina ya wanga.
Aidha, tunahimiza wafanyabishara kuleta chakula kutoka kwenye maeneo yenye ziada ya chakula aina ya wanga , lakini pia wananchi kutumia chakula kwa umakini na kuuza sehemu ya mazao ya biashara na mifugo ili kuweza kununua chakula. Aidha, Mkoa unasisitiza kuwa wafanyabiashara walioidhinishwa kununua na kuuza chakula kutoka katika maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Sumbawanga kufanya hivyo kwani mkoa umeutengewa jumla ya Tani 5,400 za mahindi kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa nafaka katika masoko ya Mkoa wa Mwanza hii nikutokana na tathmini iliyofanywa na wadau.

Ndugu wanahabari
 Kupitia kwenu tunawaomba wananchi kujiwekea akiba ya chakula aina ya wanga katika ngazi ya kaya, kwa kuzingatia kuwa wastani wa watu katika kaya ya watu 6 katika mkoa wetu, tunawashauri kuhifadhi magunia 3 ya mahindi yenye uzito wa kilo 100 lakini pia magunia 5 ya muhogo mkavu yenye uzito wa kilo 60 kila moja sawa na kilo 314.64 katika kipindi cha Novemba 2015 na Januari 2016 endapo kaya hiyo itatumia mahindi au muhogo kama chakula cha wanga katika kipindi hicho.

 Kwa upande wa wakulima wanaotumia miundombinu ya umwagiliaji katika Skimu ya Umwagiliaji Mahiga kwenye Wilaya ya Kwimba tunawashauri kuchukua tahadhari kwani mabwawa yanaweza kukatika kutokana na mvua zinazotarajiwa na inaweza kusababisha mmomonyoko wa udongo, kusombwa mazao shambani, kukosa maji ya kumwagilia, kuongezeka kwa gharama za ukarabati wa mabwawa na hata kupoteza maisha ya watu na mali zao.

 Mwisho wakulima na wananchi kwa ujumla tunawashauri kuchukua tahadhari dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mvua zinazotarajiwa na kuzitumia vizuri mvua hizo katika kuzalisha mazao yanayopendekezwa ili Mkoa uzalishe chakula cha kuutosheleza katika msimu wa 2016/2017. Mara baada yakusema hayo niwashukuru sana kwakuja lakini zaidi sana kuweza kuchukua taarifa hii na kutufikishia kwa umma wa watanzania kupitia vyombo vyenu vya habari.

 Mungu Awabariki Sana , Ahsanteni kwa Kunisikiliza!


Chanzo:HAPA

No comments:

Post a Comment

Previous Page Next Page Home