Friday 20th November 2015
Chanzo :ikulu
Mheshimiwa
Spika;
Niko hapa leo kutimiza matakwa ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 91 Ibara ndogo ya kwanza
inayonitaka kulihutubia na kulifungua rasmi Bunge hili. Naomba nimshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya njema, na kutuwezesha kuwepo hapa
siku ya leo. Aidha nitumie fursa hii kuwakumbuka wenzetu ambao, kwa namna na
nafasi mbalimbali, walishiriki katika mchakato wa uchaguzi huu na kwa bahati
mbaya walipoteza maisha yao kabla ya mchakato haujakamilika. Kwa hao wote
waliotangulia mbele za haki ninamuomba Mwenyezi Mungu azirehemu roho zao na
awape pumziko la amani. Nitumie nafasi hii kuwapa pole ndugu na jamaa ambao
ndugu zao walifariki na wengine kupata ulemavu wakati wa mchakato wa uchaguzi
huu.
Pia natoa pongezi kwako wewe
Mheshimiwa Spika, Job Ndugai na Mheshimiwa Naibu Spika, Dkt. Ackson Tulia kwa
kuchaguliwa kwenu kuongoza Bunge letu la 11. Waheshimiwa Wabunge wamewapa imani
yao, na mimi kwa nafasi yangu nawahakikishia imani na matumaini yangu makubwa
kwenu. Sina shaka Mheshimiwa Spika, chini ya uongozi wako Bunge letu limepata
kiongozi mahiri, makini na mweledi.
Aidha, niwapongeze Wabunge wote kwa
kuchaguliwa kuwa wabunge wa Bunge hili la 11. Aidha, nitumie nafasi hii
kuwapongeza wale wote waliochaguliwa katika nafasi za udiwani katika kata
mbalimbali kote nchini. Natoa pongezi hizi kwa dhati kabisa kabisa kwa sababu
kuu mbili:
o Kwanza, ni kwa
sababu ushindani katika uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa ni mkubwa sana kuanzia
ndani ya vyama vyetu na baadae katika Uchaguzi Mkuu uliohusisha na
kushindanisha wagombea toka vyama tofauti.
o Pili,
nawapongeza kwa sababu wananchi wamewapa imani na ridhaa ya kuwawakilisha
katika kipindi ambacho matarajio yao kwa Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi yetu
ni makubwa sana. Watatupima kwa namna tutakavyokidhi kiu na matarajio yao. Sote
tuliahidi kuwatumikia wananchi, na kutokana na utumishi wetu kwao tuweze
kutatua matatizo yao mbalimbali, na kuongoza mabadiliko makubwa ya kiutendaji,
usimamizi wa matumizi ya mali za umma na rasilimali za taifa, na ugawaji wa
rasilimali hizo kwa haki. Mimi na Mheshimiwa Samia Suluhu, Makamu wa Rais
tuliwaahidi wananchi kuwa tutawatumikia na tutahakikisha kuwa katika utumishi
wetu tutawajali wananchi wote, lakini zaidi wananchi wa kawaida. Naamini
wenzangu pia ndicho mlichoahidi na daima tukumbuke kuwa kazi zetu na mipango
yetu yote tutakayoipanga na kuisimamia italenga katika kuwanufaisha watu wetu.
Mheshimiwa
Spika;
Niwahakikishie tu wananchi kuwa
mambo tuliyowaahidi tutayatekeleza. Sikusudii kurejea mambo yote niliyoahidi
katika hotuba yangu hii ya leo, lakini nataka niwatoe wasiwasi kabisa kwamba
tuliyoahidi tumeahidi na ahadi ni deni. Nataka Wananchi mniamini kuwa sikutoa
ahadi ili tu mnipigie kura, niliahidi kuwatumikia na kuwafanyia kazi, na hicho
ndicho nitakachofanya. Ni imani yangu kwamba Waheshimiwa Wabunge na Madiwani
pia watafanya hivyo hivyo kama tutakavyofanya sisi.
Napenda pia kutoa
shukrani zangu za dhati kabisa kwa Watanzania wote. Tulijiandikisha kwa wingi
sana kwa ajili ya kupiga kura, tulishiriki na kufuatilia kwa karibu sana
kampeni za uchaguzi, na tukajitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura. Kinyume na
ilivyotabiriwa na wasio tutakia mema hakuna siku iliyokuwa na utulivu mkubwa na
amani kama siku ya tarehe 25 Oktoba tulivyokwenda kupiga kura. Hata baada ya
matokeo kuanza kutangazwa tulionyesha utulivu mkubwa, na hata pale ambapo
matokeo yalipotangazwa na yakawa sivyo baadhi yetu walivyoyatarajia bado
tuliyapokea kwa hali ya utulivu na uungwana mkubwa.
Wale waliotarajia kuwa tutafarakana
wameondoka wakiwa wamefadhaika sana huku wakijiuliza hivi hawa Watanzania ni
Waafrika wa namna gani. Ndugu zangu Watanzania, kwa mara nyingine tena
tumedhihirisha, kwetu sisi wenyewe, kwa Afrika na dunia, kwamba sisi ni kisiwa
cha Amani katika bahari iliyochafuka. Tunayo haja ya kujipongeza na kujiwekea
nadhiri kuwa tuaendelea kuidumisha hali hii na kuilinda amani ya nchi yetu.
Ombi langu kwa vyama vya siasa, wanasiasa wa vyama vyote na viongozi wa dini ni
kutimiza wajibu wetu wa kuilea amani ya nchi yetu.
Aidha, napenda niungane na ninyi
pamoja na Watanzania wote kuvipongeza vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama (Jeshi
la Wananchi Tanzania (JWTZ), Polisi, Magereza, Uhamiaji na Usalama wa Taifa
pamoja na mgambo) kwa jinsi walivyoshiriki katika kuhakikisha nchi yetu
inaendelea kuwa salama katika kipindi chote cha uchaguzi.
Nawapongeza pia Tume ya Taifa ya
Uchaguzi kwa namna walivyosimamia zoezi zima la uchaguzi toka hatua za awali za
kujiandikisha hadi siku ya kupiga kura na kutangaza matokeo. Mmetimiza wajibu
wenu kwa weledi na umahiri mkubwa katika mazingira magumu na yenye changamoto
nyingi. Hongereni, hongereni sana!
Mheshimiwa
Spika;
Naomba kwa namna ya pekee, niwashukuru viongozi wakuu wa nchi yetu
walionitangulia kwa kazi kubwa na nzuri walioifanyia nchi yetu. Natambua
mchango wa Waasisi wa taifa letu, Mwalimu Nyerere na Mzee Karume kwa kujenga
misingi imara wa umoja, mshikamano na amani ya nchi yetu. Mzee Mwinyi (Mzee
Ruksa) kwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa na kuijenga misingi yake.
Mzee Mkapa (Mzee wa Ukweli na Uwazi) kwa kupanua na kuimarisha misingi ya
uchumi na siasa ya nchi yetu. Mzee Kikwete (Mzee wa Maisha Bora) kwa kuendeleza
misingi hiyo na kupanua fursa mbalimbali kwa wananchi kujiletea maendeleo yao.
Wamefanya kazi kubwa. Nawashukuru sana na ninawatakia uzee mwema na maisha
marefu ili tuzidi kuchuma busara zao.
Mhishimiwa
Spika;
Tumeingia kwenye uchaguzi wamoja,
tumeshindana katika kampeni tukiwa wamoja, na tumemaliza uchaguzi wetu tukiwa wamoja.
Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla kwamba
Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kulinda kwa nguvu na uwezo wote Tunu hizi
za Umoja na Amani. Hatutakuwa na simile kwa mtu au kikundi chochote ambacho
kitataka kuvuruga umoja na amani yetu kwa misingi ya udini, rangi, ukabila,
vyama au ukanda.
Mheshimiwa
Spika;
Wakati wa kampeni, yako maeneo yaliyojitokeza kwa kulalamikiwa sana na
wananchi. Ningependa niyataje baadhi ya maeneo yaliyolalamikiwa, maeneo hayo ni
pamoja na:
o Rushwa -
Suala la rushwa limelalamikiwa sana takriban katika maeneo yote yanayogusa
wananchi.
o TAMISEMI -
Upotevu wa mapato, kushindwa kukusanya kodi, ubadhirifu, matumizi mabaya ya
fedha na utekelezaji wa baadhi ya miradi chini ya viwango, wizi, uzembe, n.k.;
o Ardhi –
Migogoro ya wakulima na wafugaji, viwanja, kuhodhi maeneo bila kuyaendeleza,
mipango miji, kujenga maeneo ya wazi, n.k.;
o Bandari -
Rushwa, wizi, ubadhirifu na urasimu;
o Maji –
Kiwango cha chini cha upatikanaji wa maji safi na salama, huduma ya maji
kupatikana mbali na makazi, n.k.;
o TRA -
Ukwepaji kodi, rushwa, ubadhirifu, urasimu na upotevu wa mapato kwa kushindwa
kukusanya kodi hasa kodi zinazotakiwa kulipwa na wafanyabishara wakubwa;
o TANESCO -
Kukatika kwa umeme mara kwa mara na uwepo wa umeme wa mgao;
o Maliasili na Utalii -
Ujangili ambao lazima Idara husika inashiriki, Migogoro ya mipaka kati ya
vijiji na Hifadhi, Upotevu wa mapato, n.k.;
o Huduma za Afya (Hospitali) -
Huduma kuwa mbali na wahitaji, Ukosefu wa madawa, hujuma kwenye vifaa vya
vipimo, msongamano wa wagonjwa na tozo zisizostahili, lugha mbaya za watumishi
kwa wagonjwa, uhaba wa majengo, vitendea kazi, rasilimali watu na fedha,
kushindwa kukusanya mapato yanayowahusu, n.k.;
o Uhamiaji na Ajira -
Kutoa hovyo hati za uraia, Vibali vya kuishi nchini kwa wageni, Kushindwa
kusimamia ajira za wageni hususan kwa kazi zinazoweza kufanywa na wazawa, n.k.;
o Elimu -
Uhaba wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia, michango mingi isiyo ya lazima,
malalamiko ya walimu yasiyoisha, mazingira ya kusomea ikiwa ni pamoja na
majengo, Madawati, Ukosefu wa nyumba za walimu, n.k.;
o Polisi -
Malalamiko ya wananchi kubambikiwa kesi, upendeleo, Madai ya askari, Ukosefu wa
nyumba za askari, Ukosefu wa vitendea kazi vya kisasa, n.k.;
o Zimamoto –
Kuchelewa kufika kwenye matukio, kufika kwenye matukio bila vitendea kazi kama
maji, n.k.;
o Mizani –
kucheleweshwa kwa magari yanayosafiri;
o Mahakama -
Natambua jitihada za Mahakama katika kushughulikia swala la mrundikano wa kesi.
Hata hivyo, bado kumekuwa na malalamiko mengi juu ya ucheleweshaji wa kesi.
o Madini –
Wenyeji kutofaidika, Vilio vya wachimbaji wadogowadogo kutengewa maeneo ya
uchimbaji na kupatiwa mikopo, kutolipa kodi stahiki, usumbufu kulipa fidia,
n.k;
o Kilimo na Mifugo –
Uhaba wa pembejeo za mifugo na kilimo, Tatizo la masoko, Kukopwa mazao ya
wakulima, Ukosefu wa Wataalamu wa Ugani, Upungufu wa Maghala, Mabwawa, Malambo,
Majosho, n.k.;
o Uvuvi –
Vifaa duni na masoko, Uvuvi haramu, Uwekezaji mdogo katika Sekta ya Uvuvi
hususan viwanda vya mazao ya uvuvi n.k., na hasa katika ukanda wetu wa bahari;
o Reli –
Uchakavu wa miundombinu ya nchi, Kutokuwepo kwa usafiri wa uhakika wa reli,
upungufu wa bandari kavu, Mizigo mingi kusafirishwa kwa barabara, n.k.;
o ATC –
Shirika la Ndege lipo, Wafanyakazi wapo zaidi ya 200, na wanalipwa
mishahara ila ndege ni moja (1);
o Makundi Maalum –
Haki za wazee, Walemavu, Wanawake na watoto zimekuwa zikikiukwa;
o Wafanyakazi, Wasanii na Wanamichezo – Mzigo wa kodi kwa wafanyakazi, Haki na maslahi yao, n.k.;
Kero hizi tutazishughulikia kwa
nguvu zetu zote. Wizara, Ofisi na Taasisi husika zijipange ipasavyo kutatua
kero hizi. Nimetaja baadhi ya kero hizi ili nanyi Waheshimiwa Wabunge mzitambue
na mshirikiane na Serikali na wadau wengine tuzitatue haraka.
Pamoja na kero hizo tutashughulikia
pia mambo yafuatayo.
Kuimarisha
Muungano
Mheshimiwa
Spika;
Nilipoapa kuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, niliapa kuulinda Muungano wa nchi yetu. Hata bila kiapo,
mimi ni muumini wa dhati wa Muungano wetu wa kipekee, uliounganisha nchi mbili
zilizokuwa huru za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, tena
kwa hiari na kwa wino wa kalamu, na si mtutu kama miungano mingine duniani.
Naamini kwa dhati ya moyo wangu kuwa Muungano wetu ndio umoja wetu, amani yetu
na salama yetu. Ninayo kila sababu ya kuulinda na kuuenzi Muungano wetu adhimu
na adimu. Ni azma yangu kuwaona wananchi wa Zanzibar na Bara wakifurahia
matunda ya Muungano wetu badala ya kuwa kikwazo kwa ustawi wao na ustawi wa
nchi yetu.
Aidha, kwa kushirikiana na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar na wadau wa siasa hususan vyama vya CUF na CCM
tutahakikisha kuwa majaribu ya kisiasa yanayoikabili Zanzibar yanamalizika kwa
salama na amani. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujalie busara na hekima tumalize
kwa utulivu na amani.
Serikali nitakayoiunda itafanya kila
lililo ndani ya uwezo wake kuendelea kuimarisha Muungano wetu. Nina faraja kuwa
Mheshimiwa Samia Suluhu, Makamu wa Rais anao uzoefu mkubwa kutokana na nafasi
yake ya awali ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia
Muungano, na pia akiwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba. Mimi pamoja na
Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu na Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein
tutahakikisha tunasimamia na kuimarisha Muungano wetu.
Kuimarisha
Mihimili ya Serikali
Mheshimiwa
Spika;
Serikali ya Awamu ya Tano itaheshimu
na kuendeleza utamaduni mzuri uliojengeka nchini wa kuheshimu mihimili ya dola.
Tutafanya hivyo kwa kuhakikisha kuwa mihimili yetu ya Bunge na Mahakama inapata
fedha za kutosha kuendesha shughuli zake kwa uhuru kupitia Mfuko wa Bunge na
Mfuko wa Mahakama. Kwa upande wa Bunge, tutahakikisha fedha za Mfuko wa
Maendeleo ya Jimbo zinapatikana kwa wakati ili Waheshimiwa Wabunge
mkashirikiane na wananchi wenu kusukuma maendeleo. Kwa upande wa Mahakama,
tutalipa uzito mkubwa suala la uboreshaji wa Mahakama kwa kusogeza huduma za
Mahakama karibu na wananchi, kuongeza kasi ya utoaji haki na kuboresha maslahi
ya watumishi wa Mahakama zetu.
Mchakato
wa Katiba
Mheshimiwa
Spika;
Serikali yangu imepokea kiporo cha
mchakato wa Katiba ambao haukuweza kukamilika katika Awamu iliyopita kutokana
na kutokukamilika kwa wakati kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura. Napenda
kuwahakikishia kuwa tunatambua na kuthamini kazi kubwa ya kizalendo iliyofanywa
na wananchi walioshiriki hatua ya awali ya ukusanyaji wa maoni kuhusu Katiba
mpya, Tume ya Marekebisho ya Katiba na Bunge la Katiba lililotupatia Katiba
Inayopendekezwa. Tutatekeleza wajibu wetu kama ulivyoainishwa katika Sheria ya
Marekebisho ya Katiba.
Uchumi na
Matarajio ya Wananchi
Mheshimiwa
Spika;
Serikali ya Awamu ya Tano inaingia
madarakani kukiwa na msingi imara wa kiuchumi uliojengwa katika Awamu
inayomaliza muda wake. Uchumi wa nchi yetu umekuwa ukiimarika na kukua wastani
wa asilimia 7. Katika kipindi hicho fursa mbalimbali za kiuchumi
zilizopo nchini mwetu zimezidi kufunguliwa. Hii ni kutokana na jitihada
zilizofanywa na Serikali za Awamu zilizopita za kujenga miundombinu ya kiuchumi
kama vile barabara, uimarishaji wa bandari, uimarishaji wa reli, na ukuzaji wa
sekta za mawasiliano ya simu na mitandao, ukuzaji na uongezaji wa uwezo wetu wa
kuzalisha na kusambaza umeme.
Napenda kuwahakikishia kuwa
tutaendeleza na kuimarisha ujenzi wa miundombinu mipya na kuiimarisha iliyopo
ili kuvutia na kushawishi wawekezaji wa ndani na wa nje.
Mheshimiwa
Spika;
Nasema hivi kwa sababu miongoni mwa
ahadi tulizowaahidi Watanzania ni kuendeleza ujenzi wa barabara mbalimbali za
kuunganisha miji yetu mikuu ya mikoa na wilaya; barabara ziendazo kwenye maeneo
muhimu ya kimkakati na kiuchumi; na upanuaji wa barabara za miji kama Dar es
Salaam kwa kujenga flyovers, barabara za pete (ring
roads), n.k. Uboreshaji wa barabara na njia nyingine za uchukuzi na
usafirishaji kuingia na kutoka Dar es Salaam ni muhimu sana kwa sababu bandari
ya Dar es salaam ni lango kuu la biashara kwa nchi yetu na nchi jirani.
Mheshimiwa
Spika;
Katika jitihada hizo hizo za
kuboresha na kuimarisha miundombinu ya kiuchumi Serikali ya Awamu ya Tano,
katika kipindi cha miaka mitano ijayo itaelekeza nguvu zake katika ujenzi wa
reli mpya katika kiwango cha kimataifa (yaani standard gauge). Reli ambazo
tunakusudia zianze kujengwa ni:
o Dar es Salaam – Tabora – Kigoma/Mwanza
o Uvinza – Msongati (Burundi) na Isaka – Kigali (Rwanda)
o Mtwara – Songea – Mbamba Bay na matawi ya kwenda Mchuchuma
na Liganga;
o Tanga – Arusha – Musoma
o Kaliua – Mpanda – Karema
o
Mheshimiwa
Spika;
Nchi yetu pia imejaliwa kuwa na
madini na maliasili nyingi. Ugunduzi wa gesi asilia umeongeza matumaini ya watu
wetu wengi juu ya uwezo wetu wa kiuchumi katika miaka ijayo. Serikali
itahakikisha kwamba madini na maliasili zetu zinatumika kwa manufaa ya Taifa
letu kwa kusimamia Sheria na Taratibu zilizopo. Aidha, napenda kuipongeza kwa
dhati kabisa Serikali ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Bunge la 10 kwa
kupitisha Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi yaani The
Oil and Gas Revenues Management Act, 2015. Serikali yangu itasimamia
utekelezaji wa sheria hiyo kwa uaminifu na umakini mkubwa.
Ujenzi wa
Viwanda
Mheshimiwa
Spika;
Serikali ya Awamu ya Tano itaweka
mkazo mkubwa katika ujenzi wa Viwanda. Natambua kwamba sekta binafsi ndiyo
muhimili mkubwa wa kujenga uchumi wa viwanda. Hatuna njia nyingine kama kweli
tunataka kujenga msingi wa uchumi endelevu katika nchi yetu utakaopaisha uchumi
na maisha ya watu wetu. Dira ya Maendeleo ya 2025 inatutaka tuwe nchi ya watu
wenye kipato cha kati. Tunaweza tukafika huko, na dalili zipo, lakini pia
tunaweza tukafika huko kitakwimu tu wakati ukweli na uhalisia wa mambo ni tofauti.
Utofauti ninaouzungumzia ni pale takwimu zitakapoonyesha kwamba sisi ni nchi ya
kipato cha kati wakati mapato halisi na hali za maisha ya watu wengi hazifanani
na takwimu hizo. Tamaa yangu na kwa kweli jitihada za Serikali ya Awamu ya
Tano, zitakuwa katika ujenzi wa uchumi wa kipato cha kati ambapo sura na maisha
ya Watanzania walio wengi yafanane fanane na nchi ya kipato cha kati. Njia moja
ya kutufikisha huko ni uendelezaji wa viwanda.
Mheshimiwa
Spika;
Tutahakikisha suala la viwanda
linasimamiwa vizuri na tunafanikiwa. Matarajio yangu ni kuwa Bunge lako Tukufu
litatuunga mkono mimi na Serikali nitakayoiunda katika kufikia lengo hili.
Mheshimiwa
Spika;
Kama nilivyosema wakati wa Kampeni,
na nataka nirudie hapa, tutaanza na viwanda vilivyopo na kuhakikisha vinafanya
kazi. Wale wote ambao walibinafsishiwa viwanda vilivyokuwa vya umma kwa
makubaliano kwamba wataviendeleza niliwataka wafanye hivyo mapema. Na hapa
nataka nisisitize wito wangu huo kwao. Najua huko nyuma ufuatiliaji na
usimamizi wa utekelezaji wa mikataba ya aina hiyo umekuwa ukilegalega na watu
wamejifanyia mambo watakavyo. Wapo walioacha kabisa uzalishaji na kufumua hata
mitambo ya uzalishaji. Mimi niliahidi, na nataka niseme hapa kwa wazi kabisa,
kwamba wale waliobinafsishiwa viwanda hivyo waanze kazi, waanze kazi mara moja.
Wakishindwa basi tutavitwaa viwanda hivyo kwa kuzingatia sheria na taratibu za
nchi na kuwapa watu wengine wenye nia ya kuviendeleza. Hatuwezi kuwa na watu
wanajiita wawekezaji tunawapa viwanda vyetu halafu wanaviatamia tu. Mimi hilo
sitalikubali na wala sitalivumilia. Nimeielekeza Ofisi ya Msajili wa Hazina
kuanza kushughulikia suala hili mara moja. Naomba Bunge lako lituunge mkono.
Mheshimiwa
Spika;
Njia ya pili ya kuendeleza viwanda
ni kuhimiza na kushawishi wawekezaji kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya nchi
yetu. Kama nilivyoeleza miundombinu ya kufanya hivyo tayari ipo na baada ya
muda itakuwa bora zaidi. Najua wapo watu wanaotaka kuwekeza Tanzania sasa,
katika viwanda, na wamekuwepo hata miaka ya nyuma kidogo, lakini wakati
mwingine sisi humu humu – tukiwemo sisi viongozi kwa kushirikiana na
wafanyabiashara matapeli na laghai – tumehujumu mipango na shauku ya wawekezaji
wa nanma hiyo. Pamoja na shauku na utayari wao wa kuwekeza Tanzania tumewawekea
vikwazo na kuwapiga vita na hivyo kuwalazimisha kwenda kuwekeza katika nchi
jirani. Sisi katika Serikali ya Awamu ya Tano tutajitahidi sana kuondoa
usumbufu na urasimu wa aina hiyo na kuongeza bidii ya kuwashawishi wawekezaji wa
ndani na wa nje kuja kuwekeza viwanda hapa nchini. Kwa watendaji wa Serikali
watakaokwamisha jitihada za uwekezaji na ujenzi wa viwanda hapa nchini
hatutawavumilia.
Mheshimiwa
Spika;
Ni viwanda
vya aina ipi hasa tunavyovikusudia? Sura
ya kwanza ya viwanda tunavyovikusudia ni vile ambavyo sehemu kubwa ya malighafi
yake itatoka ndani, hususan kweye sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, na madini –
na maliasili nyingine. Viwanda vya aina hii vitatupa fursa ya kujenga mfumo wa
uzalishaji ndani ya nchi uliofungamana na kushikamana. Viwanda vya aina hii
vitahitaji na kutegemea malighafi toka kwa wazalishaji wa sekta nilizozitaja,
na kwa kufanya hivyo wazalishaji hao watakuwa na soko la uhakika humu humu
ndani ya nchi. Sura ya pili ya viwanda hivi ni kuzalisha bidhaa ambazo
zinatumiwa na watu wengi humu nchini (mass consumption) – yaani bidhaa kama
vile nguo, viatu, mafuta ya kupikia, n.k. kwa hivyo viwanda hivi vitakuwa na
uhakika wa soko la ndani kabla ya kufikiria soko la nje. Viwanda hivi
vitatarajiwa kuzalisha ziada kwa ajili ya masoko ya nje. Yote mawili yakitokea,
yaani kuzalisha kwa ajili ya soko la ndani na nje, itatuongezea akiba yetu ya
fedha za kigeni na kutuwezesha kutekeleza na kuendeleza mipango mingine kwa
ajili ya ustawi wa uchumi wetu. Sura ya tatu ya viwanda tunavyovikusudia ni
kuzalisha ajira nyingi. Shabaha yetu ni kuwa ifikapo mwaka 2020 idadi ya ajira
itokanayo na viwanda ifikie asilimia 40 ya ajira zote
zitakazokuwepo nchini wakati huo.
Mheshimiwa
Spika;
Nimeamua kulisema hili kwa kirefu
sana kwa sababu ili tufanikiwe lazima tuelewane na tusaidiane kulisukuma kwa
pamoja jambo hili.
Kilimo,
Mifugo na Uvuvi
Mheshimiwa
Spika;
Sekta nyingine ambazo lazima
tutazitilia mkazo mkubwa na kuziendeleza ni kilimo, mifugo na uvuvi.
Tutaziangalia sekta hizi kwa mtazamo wa kibiashara na viwanda kwa lengo la kuwa
na viwanda vya kisasa vya kuongeza thamani mazao yatokanayo na kilimo, mifugo
na uvuvi. Nchi yetu kwa kiasi kikubwa ni nchi ya kilimo, ufugaji na uvuvi. Hii
inatokana na ukweli kwamba sehemu kubwa ya watu wetu wapatao asilimia
75wanaishi vijijini na wanategemea kilimo, ufugaji na uvuvi kwa ajili ya
maisha yao. Wakulima, wafugaji na wavuvi wanatumia zana na mbinu duni katika
shughuli zao na wanazalisha zaidi ya asilimia 95 ya chakula
chote kinacholiwa hapa nchini, na kutoa mchango wa asilimia 25kwenye
pato la taifa yaani GDP, na asilimia 30 ya mapato yetu ya
fedha za kigeni. Kwa takwimu hizi chache ni wazi kwamba mchango wa sekta ya
kilimo, mifugo na uvuvi katika uchumi wetu na maisha yetu ni mkubwa sana.
Nichukue nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru wakulima, wafugaji na wavuvi
wote wa Tanzania kwa mchango wao mkubwa katika maisha yetu na uchumi wa nchi
yetu. Nataka kuahidi kwao sitawaangusha.
Mheshimiwa
Spika;
Pamoja na umuhimu wa kilimo, mifugo
na uvuvi katika uchumi wetu wakulima, wafugaji na wavuvi wetu wengi bado ni
watu maskini. Mapato yao yako chini na wanaishi maisha duni. Lengo letu ni
kuuimarisha sekta hizi ili ziweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa
nchi lakini pia ziweze kuwanufaisha wakulima, wafugaji na wavuvi katika
kuyabadili maisha yao. Tukiweza kuboresha sekta hizi vijana wengi zaidi
watavutiwa kujiunga nazo na hivyo kupunguza tatizo la upatikanaji wa ajira.
Nataka niwahakikishie wakulima, wafugaji na wavuvi wetu kwamba ahadi zetu kwao
tutahakikisha zinatekelezwa. Serikali ya Awamu ya Tano itazisimamia kwa dhati
ahadi hizo ili kuhakikisha kwamba kilimo, ufugaji na uvuvi unakuwa wa kisasa
zaidi na wenye tija. Baadhi ya mambo tuliyowaahidi kuyatekeleza ni pamoja na
haya yafuatayo:
o Kuwapatia mafunzo ya kilimo, ufugaji na uvuvi wa kisasa
ikiwa pamoja na ufugaji wa samaki,
o Kuwapatia pembejeo,
o Kuwapatia zana za kisasa za kilimo, ufugaji na uvuvi,
o Kuwapatia wataalamu wa ugani,
o Kuwawezesha kupata masoko ya uhakika ya mazao yao,
o Kuwapatia mikopo, na kwa hili Benki ya Kilimo itasaidia sana
kufikia lengo hili,
o Kuondoa ushuru, kodi na kero mbalimbali za mazao ya kilimo,
mifugo na uvuvi zinazosababisha bei ya mazao hayo kuwa chini (mfano. Kahawa,
kule Kagera ina kodi 26 ambazo husababisha wananchi kuuza kahawa yao Uganda
ambako bei iko juu, tutapunguza kama sio kuondoa kabisa ushuru hizo ili
wakulima wapate bei nzuri. Tutafanya hivyo pia kwa mazao mengine kama
mahindi, chai, pamba, korosho, mkonge, ngozi, nyama, maziwa, samaki, n.k.),
o Kuwahakikishia umiliki wa ardhi na kuwaondolea usumbufu wa
wao kuondolewa kwenye ardhi zao kupisha wawekezaji,
o Kuhakikisha kwamba migogoro ya ardhi baina ya wakulima na
wafugaji tunaitatua na kuikomesha kwa kuhakikisha kuwa vyanzo vya msingi vya
migogoro hiyo tunaviondosha haraka,
o 10. Kuhakikisha kwamba tatizo la wavuvi kuvamiwa
na majambazi na uvuvi haramu linashughulikiwa kikamilifu.
o
Tatizo la
Umaskini na Ajira
Mheshimiwa
Spika;
Nimezungumzia umuhimu wa kuendeleza
viwanda, kilimo, mifugo na uvuvi kwa sababu ya matatizo makubwa mawili
yanayoikabili nchi yetu kwa sasa. Kwanza, ni tatizo la UMASIKINI na
pili ni tatizo la AJIRA. Ni kweli uchumi wetu umekuwa ukikua kwa
kasi ya kuridhisha, lakini kasi hiyo haijawiana na kasi ya kuondoa umasikini na
uzalishaji wa ajira za kutosha kwa vijana wetu wanaoingia kwenye soko la ajira
kila mwaka.
Mheshimiwa
Spika;
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo zaidi
ya asilimia 28.2 ya Watanzania ni maskini. Na kwamba kwa namna
na kadri uchumi wetu unavyokuwa pengo baina ya matajiri (walionacho) na maskini
(wasionacho) linazidi kukua. Tukiendelea hivi tunavyoendelea sasa hatutakuwa
tunaitakia mema nchi yetu kwa sababu mgawanyiko mkubwa wa kimapato na tofauti
kubwa za kimaisha baina ya matajiri na maskini ukiachiwa uendelee na kuzidi
kukua utachochea chuki na uhasama baina ya walionacho na wasionacho. Lazima
tujizatiti na kutumia akili, maarifa na nguvu zetu zote kukabiliana na
kuibadilisha hali hii. Kwanza, lazima tushughulike na UMASIKINI wa
watu wetu. Na njia moja kama nilivyokwisha eleza ni uendelezaji wa sekta ya
viwanda na uboreshaji wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Mheshimiwa
Spika;
Tatizo la pili ni AJIRA.
Kama nilivyokwisha kugusia, ukuaji wa uchumi wetu haujaenda sambamba na kasi ya
watu wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka. Tatizo la ajira ni kwa vijana
wote waliosoma viwango mbalimbali vya elimu na wasio na ujuzi. Hii inamaana
kwamba sekta zinazochangia kukua kwa uchumi wa nchi yetu sizo zinazozalisha
ajira kwa wingi. Ndio maana ya kuweka msisitizo kwenye sekta ya viwanda hasa
vile vinavyoajiri watu wengi, na sekta ya kilimo, uvuvi na mifugo ambavyo ndio
mwajiri mkubwa hivi sasa.
Mheshimiwa
Spika;
Pamoja na kuweka msisitizo katika
Viwanda, Kilimo, Mifugo na Uvuvi hatuna budi kuwawezesha vijana wetu kuanzisha
shughuli mbalimbali za uzalishaji kwa viwango mbalimbali. Ili hili liwezekane,
na sisi tutalifanya, linahitaji mambo mawili makubwa.
Kwanza, kuwaandaa vijana wetu vizuri kielimu na kiujuzi. Hatuna
budi kuweka mkazo katika viwango vya ubora vya elimu na stadi za kazi
wanazopata vijana wetu. Nalisema hili kwa sababu hatuwezi kuzungumzia
uendelezaji wa viwanda ikiwa hatujaandaa vijana wenye uwezo, ujuzi, na stadi za
kufanya kazi hizo kwa ubora na ufanisi wa hali ya juu; hatuwezi kutaka kuwekeza
katika viwanda vya nguo au samani ikiwa hatuna wahandisi wa mitambo wazuri,
wabunifu wa zuri na wenye viwango vinavyotakiwa na kukubalika. Aidha
hatuwezi kuwa na vijana wenye uthubutu wa kuanzisha shughuli za uzalishaji kama
hawana elimu na maarifa ya kubuni miradi na kuiendeleza. Kwa hivyo tutaelekeza
nguvu zetu katika kuhakikisha kuwa shule na vyuo vyetu katika ngazi mbalimbali
vinafundisha na kutoa vijana wenye viwango vya hali ya juu vya elimu, maarifa, ujuzi
na ufundi.
Mheshimiwa
Spika;
Pili, ni suala la uwezeshaji wa vijana hasa wale watakaotaka
kujiajiri. Katika kutekeleza lengo hili Serikali ya Awamu ya Tano itachukua na
kutekeleza hatua mbalimbali ikiwemo:
o Kuwawezesha vijana wanaohitimu Elimu ya Juu na Vyuo vya
Ufundi kupata mitaji ya kuwasaidia kuanzisha makampuni yao kulingana na fani
walizosomea;
o Kuwawezesha vijana kuanzisha SACCOS zao na kupitia
SACCOS hizo kuwawezesha kupata mikopo;
o Kuwawezesha vijana wajasiriamali kujiunga na Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii ili waweze kupata mikopo na kunufaika na mafao mengine katika
mifuko hiyo.
Mheshimiwa
Spika;
Tatu, ni kuzitambua na kuziheshimu kazi na shughuli mbalimbali
zinazofanywa na makundi mbalimbali ya kinamama na vijana. Hapa namaanisha
shughuli za kina Mama lishe, wachuuzi mbalimbali, Machinga, waendesha Boda Boda
na Maguta, na vijana wa kike na wa kiume wanaojitafutia kazi mbalimbali halali
za kujipatia mapato kwa ajili ya kuendesha maisha yao, n.k. Shughuli za makundi
haya zinatusaidia sana katika kupunguza makundi ya vijana wetu ambao wangekaa
tu na kuzurura zurura ovyo bila shughuli ya kufanya. Na kwa kuwa kwa sasa uwezo
wetu wa kuwapatia ajira tofauti ni mdogo ni jukumu letu kuwasaidia na
kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa utilivu bila bugudha. Niliahidi, na nataka
nirudie hapa, kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ikishirikiana na Halmashauri
zetu, pamoja na Wakuu wa Mikoa na Wilaya itaweka mipango na taratibu nzuri na
rafiki kwa aina ya shughuli ambazo baadhi nimezigusia. Aidha, ushuru usio wa
lazima na wenye usumbufu kwa wafanyabiashara wadogo wadogo utokanao na shughuli
nilizozitaja tutauondoa. Tunaamini ikiwa tutaweza kuongeza ukusanyaji mapato,
na kuziba mianya ya wakwepaji wakubwa wa kodi ambao huipotezea Serikali
mabilioni ya fedha tutakuwa hatuna sababu ya kufukuzana na kina mama na vijana
mitaani. Viongozi na watendaji wa Serikali na hasa wa Halmashauri watenge
maeneo kwa ajili ya wafanyabishara wadogo na waandae mipango ya kupunguza
ushuru usio wa lazima.
Afya
Mheshimiwa
Spika;
Dhamira ya kujenga uchumi wa kisasa
na suala la kupambana na umasikini linakwenda sambamba na kuwa na wananchi
wenye afya bora. Kwa kutambua ukweli huu na mahitaji ya huduma bora za wananchi
wetu Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kwamba wananchi wanapata huduma bora
za afya kwa kufanya baadhi ya mambo yafuatayo:
o Kwanza,
kuimarisha huduma za afya pale zilipo na kuanzisha pale ambapo hazipo. Lengo ni
kuhakisha kwamba kila kijiji kinakuwa na Zahanati, kila Kata inakuwa na Kituo
cha Afya, kila wilaya inakuwa na Hospitali, na kila Mkoa unakuwa na hospitali
ya Rufaa.
o Pili, tutaimarisha
na kuboresha huduma za afya kwa kuongeza utaalamu katika Nyanja za afya kwa
kuwapatia mafunzo watumishi wake ndani na nje ya nchi; kwa kuzipatia vifaa bora
na vya kisasa hospitali, vituo vya afya na zahanati zetu. Lengo la kufanya
hivyo ni kuwezesha upatikanaji wa huduma mahsusi hapa hapa nchini na hivyo
kutolazimika kupeleka watu wetu kutibiwa nchi za nje.
o Tatu, tutaongeza
bajeti ya dawa na kuboresha mfumo wa upatikanaji ili kuhakikisha dawa
zinapatikana katika hospitali, vituo vya afya na zahanati zetu. Aidha,
tutahamasisha wananchi wajiunge na Bima ya Afya.
Elimu
Mheshimiwa
Spika;
Natambua juhudi kubwa zimefanyika katika upanuzi wa elimu ya awali, msingi,
sekondari na vyuo vikuu. Serikali ya Awamu ya Tano itajielekeza katika
kuongeza ubora wa elimu inayotolewa ikiwa pamoja na na kuongeza mkazo katika
masomo ya sayansi. Aidha, tutahakikisha kwamba vifaa vya kufundishia na
kujifunzia vinapatikana ikiwa ni pamoja na maabara, vitabu, madawati, n.k.
Tutahakikisha kuanzia Januari mwakani elimu kuanzia darasa la kwanza hadi
kidato cha nne inatolewa bure, kama tulivyoahidi kwenye kampeni. Tutahakikisha
kwamba wanafunzi wengi zaidi wa elimu ya juu wanapata mikopo kwa wakati.
Tutashughulikia maslahi na kero za walimu wa ngazi zote ikiwa ni pamoja na
kujenga nyumba za walimu vijijini na kuiunga mkono Benki ya walimu ili iweze
kuwanufaisha zaidi.
Maji
Mheshimiwa
Spika;
Wakati wa kampeni nimekutana na malalamiko mengi sana ya ukosefu wa maji.
Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kwamba inaongeza kiwango cha upatikanaji
wa maji kufikia asilimia 85 kwa maeneo ya vijijini na asilimia
95 kwa maeneo ya mijini ifikapo 2020. Tutakamilisha miradi
iliyokwishaanza na kuanzisha miradi mipya mikubwa na midogo ya maji kutoka
katika mito, maziwa na vyanzo vingine vya uhakika vya maji ikiwa
pamoja na kuvuna maji ya mvua. Tunataka tuwatue akina mama ndoo kichwani.
Tunatambua umaskini hauwezi kuondoka nchini kama wananchi hawapati maji safi na
salama.
Umeme
Mheshimiwa
Spika;
Suala la upatikanaji wa umeme limeendelea kuwa tatizo katika
nchi yetu pamoja na jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali zilizopita.
Hatuwezi kuzungumzia suala la kujenga viwanda wakati umeme hautoshi. Serikali
yangu itahakikisha kwamba umeme unapatikana wa kutosha na wa uhakika.
Tutakamilisha miradi ya umeme iliyopo na kujenga mingine mingi mipya ili
wananchi wengi zaidi wanufaike na nishati ya umeme na viwanda vingi zaidi
vidogo vidogo, vya kati na vikubwa vianzishwe.
Madawa ya
Kulevya
Mheshimiwa
Spika;
Madawa ya kulevya yamekuwa ni janga kubwa kwa taifa letu na kundi
linaloathirika zaidi ni vijana wa kiume na kike. Familia nyingi zimeathirika na
nguvu kazi ya taifa imepotea. Tutaushughulikia mtandao huo hususan
wafanyabiashara wakubwa wanaojihusisha na madawa ya kulevya bila ajizi.
Mheshimiwa
Spika;
Masuala mengine tutakayoyawekea
mkazo katika utawala wa Awamu ya Tano ambayo ninaamini yatasaidia katika
kujenga uchumi wetu ni pamoja na masuala ya Utalii, Mawasiliano, Madini, Ardhi
na Makazi, Ujenzi na Miundombinu, Bandari, Barabara, Ulinzi na Usalama,
utunzaji wa mazingira, Vijana, Wanawake, Watu wenye Ulemavu na Ualbino, Wazee,
Wafanyakazi, Wasanii na Wanamichezo, wanahabari, wafanyabiashara, wawekezaji,
wajasiriamali, sekta binafsi, n.k. Utekelezaji wa masuala haya umefafanuliwa
vizuri katika Ilani ya CCM ya mwaka 2015. Tutayatekeleza ipasavyo.
Mapambano
Dhidi ya Rushwa na Ufisadi
Mheshimiwa
Spika;
Jambo moja nililolisemea kwa nguvu
kubwa wakati wa kampeni ni mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Sikufanya
hivyo kwa sababu nilitaka tu kuwarubuni wananchi ili wanipe kura zao na
kunifanya kuwa Rais wao. Nililiongea jambo hili kwa dhati kabisa, na nilichokisema
na kuwaahidi wananchi ndicho hasa nilichokikusudia.
Mheshimiwa
Spika;
Wananchi wanachukia sana rushwa na
ufisadi, na wamechoshwa na vitendo hivyo. Mimi pia ninachukia rushwa na
ufisadi. Sifurahishwi kabisa na vitendo vya rushwa na ufisadi vinavyoendelea
hapa nchini. Vitendo vya rushwa na ufisadi vinawanyima haki wananchi na kuitia
hasara serikali kwa mamilioni ya fedha ambazo zingeweza kutumika kwa ajili ya
kujenga miradi ya maendeleo kwa ajili ya watu wetu.
Mheshimiwa
Spika;
Chama changu, Chama cha Mapinduzi,
kimejengwa katika misingi ya kukataa rushwa na ufisadi. Ndio maana moja ya
Imani kuu za CCM ni ile isemayo: “Rushwa ni adui wa haki, sitatoa wala
kupokea rushwa”
Kwa Mtanzania mwaminifu kwa imani
yake hatakuwa na kigugumizi katika kuwa mstari wa mbele katika kupambana na
rushwa na ufisadi.
Mheshimiwa
Spika;
Mmoja wa waasisi wa Taifa letu, Baba
wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kuifananisha rushwa
na ufisadi ‘Kama Adui Mkubwa wa Watu’. Akiongea Bungeni Mei
1960, Mwalimu Nyerere alisema yafuatayo kuhusu rushwa:
“Rushwa [na ufisadi] havina budi
kushughulikiwa bila huruma kwa sababu naamini wakati wa Amani rushwa na ufisadi
ni adui mkubwa kwa ustawi wa watu kuliko vita.”
Mheshimiwa
Spika;
Haya ni maneno makali ya mtu na kiongozi
aliyeichukia na kuikemea rushwa katika maisha yake yote ya uongozi. Ni maneno
yanayotukumbusha tu nini kinaweza kikatutokea kama taifa endapo tutaendekeza
rushwa na ufisadi. Chuki za wananchi dhidi ya rushwa na ufisadi ni dhahiri,
wamechoka kabisa, wamechoka sana, hawako tayari kuvumilia upuuzi wa serikali
itayoonea haya rushwa na kulea mafisadi.
Mheshimiwa
Spika;
Mimi nimewaahidi wananchi, na nataka
niirejee ahadi yangu kwao mbele ya Bunge lako tukufu, kwamba nitapambana na
rushwa na ufisadi bila kigugumizi na bila haya yoyote. Dawa ya jipu ni
kulitumbua, na mimi nimejipa kazi ya kuwa mtumbua jipu. Najua kutumbua jipu
kuna maumivu lakini bahati mbaya halina dawa nyingine. Hivyo ninaomba
Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mniombee na muniunge mkono wakati
natumbua majipu haya.
Mheshimiwa
Spika;
Ninafahamu ugumu wa vita niliyoamua
kuipigana. Nasema nafahamu ugumu na changamoto zake kwa sababu wanaojihusisha
na rushwa sio watu wadogo wadogo. Vitendo vya rushwa na ufisadi vyenye madhara
makubwa kwa nchi na ustawi wa nchi yetu hutendwa na watu wenye dhamana kubwa za
uongozi na utumishi ambazo wamezipata kutokana na ridhaa ya watu. Kwa
hivyo ili niweze kufanikiwa lazima nipate ushirikiano mkubwa toka kwa Bunge
lako tukufu na vyombo vingine vilivyopo na vyenye majukumu ya kupambana na
vitendo hivi.
Aidha, tutashinda vita hii endapo
wananchi pia watatuunga mkono. Sina mashaka kuwa kwa vile wao, kwa wingi wao,
wanachukia rushwa na ufisadi, watakuwa tayari kutoa ushirikiano wao katika
mapambano haya dhidi ya rushwa na ufisadi.
Mheshimiwa
Spika;
Katika kushugulikia tatizo hili
nimeahidi kuunda mahakama ya Rushwa na Ufisadi. Ni matumaini yangu vyombo
husika katika jambo hili havitanikwamisha.
Aidha, nataka niahidi mbele ya Bunge
lako tukufu kwamba, kiongozi yeyote wa kuteuliwa, ambaye mimi nitakuwa
nimemteua kwa mamlaka niliyonayo kikatiba, na ninayo mamlaka ya kumwajibisha,
pindi tu nikibaini na kujiridhisha kuwa anajihusisha na vitendo vya rushwa na
ufisadi nitamtimua mara moja. Baada ya mimi kuchukua hatua hizo hatua na
taratibu zingine za kisheria zitafuata.
Mheshimiwa
Spika;
Ninachotaka kusema ni kuwa Serikali
yangu itafuatilia kwa karibu mienendo ya viongozi na watendaji wake ili kubaini
kwa haraka nani anajihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi. Na
tukishajiridhisha hatutasubiri, tutachukua hatua. Ni imani yangu wengine pia
katika ngazi mbalimbali mtafanya hivyo. Kwa sababu bila kufanya hivyo rushwa na
ufisadi vitazoeleka na kuwa wimbo unaoburudisha badala ya kuudhi na kukera.
Muundo wa
Serikali na Utumishi
Mheshimiwa
Spika;
Nilipokuwa nazunguka na kuzungumza
na wananchi wakati wa Kampeni za Uchaguzi, niliahidi kuwa nitaunda serikali
ndogo ya wachapa kazi.
Aidha, niliahidi pia kuunda serikali
ambayo itawatumikia watu na hasa wananchi wa kawaida. Serikali nitakayounda,
nataka iwe inawahudumia wananchi kwa haraka na sio kuwasumbua sumbua na
kuwazungusha. Natoa rai kwa watumishi wa serikali, hasa ambao ni wazembe na
wavivu, kujiandaa. Wamevumiliwa kwa muda mrefu sasa basi. Kwa sababu watumishi
wa aina hiyo hawatavumuliwa katika serikali nitakayoiongoza. Lugha za “hiyo
ni changamoto tutaishughulikia”, au “Mchakato unaendeela” hazitavumiliwa
katika Serikali ya Awamu ya Tano. Mimi nataka watu wa Kazi Tu.
Hatuwezi kulea watu ambao wanalipwa mishahara lakini hawafanyi kazi
wanazotakiwa kufanya, au wamegeuza ofisi za umma kuwa ni mahala pa kuchuma bila
kufanya kazi.
Mheshimiwa
Spika;
Pamoja na kuwataka watumishi wa
Serikali kufanya kazi hatuna budi kuyaangalia na kuboresha mishahara na maslahi
yao na mazingira yao ya kufanyia kazi kwa kuwapatia vitendea kazi bora
na vya kisasa. Na jambo moja tutakalolitekeleza ni kuangalia namna ya
kupunguza kodi ya mapato katika mishahara ya wafanyakazi yaani PAYE.
Pia tutajitahidi kuwatambua na kuwapa motisha wafanya kazi wachapa kazi.
Kuongeza
Mapato na Kupunguza Matumizi ya Serikali
Mheshimiwa
Spika;
Kwa zaidi ya miaka mitatu sasa
ukusanyaji wa mapato umekuwa chini ya makadirio kwa sababu mbalimbali. Serikali
ya Awamu ya Tano itaongeza nguvu katika upanuzi wa wigo wa kodi na kuongeza
ufanisi katika ukusanyaji wa mapato. Tutahakikisha kwamba kila mtu anayestahili
kulipa kodi analipa kodi stahiki. Hatutasita kumchukulia hatua mtu yoyote
atakaye kwepa kulipa kodi. Tunawaomba wananchi mhakikishe mnapewa risiti kila
mnaponunua bidhaa au huduma. Kodi ni kitu muhimu lazima kila mtu anayestahili
kulipa kodi alipe.
Aidha, tutahakikisha kwamba kila
senti inayoongezeka katika mapato ya Serikali inaelekezwa katika kutoa huduma
bora zaidi kwa wananchi. Tutaziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali ambayo
inaipunguzia Serikali uwezo wake wa kuwahudumia wananchi.
Mheshimiwa
Spika;
Nitataja baadhi tu ya maeneo ambayo
tutayasimamia kwa lengo la kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuziba mianya
ya uvujaji wa fedha za Serikali:
Kwanza, safari zote zisizo za lazima nje ya nchi Serikalini
tutazidhibiti na badala yake tutawatumia mabalozi wetu kutuwakilisha kwenye
mikutano ya aina hiyo. Na pale inapolazimu kiongozi au mtumishi mwandamizi
kusafiri tutahakikisa kwamba haandamani na msururu wa watu wengi ambao hawana
umuhimu wala shughuli za kufanya katika safari hizo.
Katika kusisitiza hili napenda
niwape takwimu za fedha zilizotumika ndani ya Serikali, Mashirika ya Umma na
Taasisi nyingine za Serikali kwa safari za nje kati ya mwaka 2013/14 na
2014//2015. Jumla ya shilingi bilioni 356.324 zilitumika
kwa ajili ya safari za nje kama ifuatavyo:
o Tiketi za ndege (Air ticket) zilitumia shilingi
bilioni 183.160;
o Mafunzo nje ya nchi (Training Foreign) zilitumia shilingi
bilioni 68.612;
o Posho za kujikimu (Per Diem Foreign) zilitumia shilingi
bilioni 104.552;
Wizara na Taasisi zinazoongoza kwa
matumizi ya safari za nje ni pamoja na Bunge, Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikano wa Kimataifa, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Taifa
ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT), Wizara ya Mambo ya Ndani, n.k.
Hizi fedha zingeweza kutumika vizuri kuboresha huduma za wananchi wa maisha ya
chini, kama afya, maji, elimu, umeme n.k. Mfano; fedha hizi zingetosha
kutengeneza kilometa 400 za barabara za lami, tujiulize
zingeweza kutengeneza zahanati ngapi?, nyumba za walimu ngapi?, madawati
mangapi? n.k. Hivyo tunapodhibiti safari za nje tunawaomba Waheshimiwa Wabunge
na Watanzania wote mtuelewe na mtuunge mkono.
Pili, tutahakikisha tunadhibiti safari na ziara za mafunzo nje
ya nchi zinazogharamiwa na serikali ambayo yanapatikana hapa nchini.
Tatu, tutadhibiti warsha, semina, makongamano, na matamasha
ambayo kwa kweli yanatumia fedha nyingi tu za serikali lakini hayana tija na
wala hayaongezi ufanisi katika utekelezaji na usimamizi wa sera na mipango ya
Serikali.
Nne, tutasimamia kwa ukamilifu Sheria ya Manunuzi ya Umma ili
kuhakikisha kwamba mianya yote ya fedha za umma inayotokana na usimamizi hafifu
tunaiziba. Ni matarajio yangu kutakapoleta Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya
Manunuzi ya Umma Waheshimiwa Wabunge mtatuunga mkono.
Tano, tutasimamia na kudhibiti ukiukwaji wa maagizo na maelekezo
mbalimbali yaliyokwisha kutolewa na Serikali siku za nyuma kuhusu ununuzi wa
bidhaa kama samani kwa ajili ya matumizi ya Serikali. Samani zote kwa ajili ya
matumizi ya Serikali zinatakiwa ziwe zile zinazozalishwa hapa hapa nchini.
Sita, Serikali ya Awamu ya Tano itasimamia kwa karibu na
kuthibiti ununuzi wa magari ya gharama kwa ajili ya Viongozi na Watumishi
waandamizi wa Serikali; na
Saba, tutaendelea kuchunguza na kudhibiti matumizi ya Serikali na
Taasisi zake zote yasiyo na tija kwa uchumi wa taifa letu.
Mheshimiwa
Spika;
Kwa ajili hiyo, vipaumbele vya Serikali ninayotarajia
kuiunda vitakuwa ni: kupunguza urasimu ili kuongeza kasi ya utekelezaji
wa maamuzi na miradi ya Serikali; kubana matumizi kwa kupunguza
yale ambayo kutokana na hali yetu ya uchumi kwa sasa yanaweza kuepukika;na
kurejesha nidhamu ya Serikali na utumishi wa umma kwa kuongeza uwazi na
uwajibikaji.
Tutatekeleza vipaumbele hivyo kwa kufanya pamoja na mambo mengine kupunguza
ukubwa wa Baraza la Mawaziri; kuongeza usimamizi katika ukusanyaji wa mapato ya
kodi na maduhuli ya Serikali kwa kuziba mianya ya ukwepaji kodi, tutahakikisha
kwamba wale wote wanaotakiwa kulipa kodi wanalipa ipasavyo. Tutaongeza nidhamu
ya matumizi ya Serikali ili kuhakikisha fedha zinazookolewa zinakwenda kwenye
miradi ya maendeleo; na kusimamia sheria, kanuni na taratibu za uwajibikaji wa
viongozi na watumishi wa umma ili wawajibike kwa wananchi ambao ndio wateja na
waajiri wakuu wa watumishi wa umma. Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea
kubainisha maeneo mengine ya matumizi yasiyo ya lazima ambayo yanaigharimu
Serikali fedha nyingi na kuyadhibiti. Aidha, nitoe wito kwa Watanzania wote
kila mmoja wetu afanye kazi iwe shambani, ofisini, kiwandani, sokoni, n.k.
Badala ya tabia ya sasa iliyoanza kujengeka kwa Watanzania kutokupenda
kufanya kazi na hivyo kupoteza muda mwingi vijiweni, muda ambao ungetumika
kufanya kazi ndiyo maana kauli mbiu yangu ni HAPA KAZI TU!
Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa
Kikanda na
Kimataifa
Mheshimiwa
Spika;
Nchi yetu imepata mafanikio makubwa katika Nyanja ya diplomasia na ushirikiano
wa kimataifa katika awamu zilizotangulia za uongozi. Serikali yangu itaendeleza
sifa hiyo kwa kujenga juu ya msingi imara uliowekwa na awamu zilizotangulia na
awamu ya nne chini ya Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Tutaendelea kuwa
waumini na tutaendeleza sera ya ujirani mwema na nchi zinazotuzunguka kwa lengo
la ustawi wa watu wetu na maslahi mapana ya nchi yetu. Tutaendelea kuwa
waaminifu wa utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na daima
tutatekeleza wajibu wetu kwa mujibu wa Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki, itifaki zake na maamuzi ya vikao vya nchi wanachama.
Tutaendelea kutekeleza matakwa ya Mkataba huu wa kujenga utengamano wetu hatua
kwa hatua.
Mheshimiwa
Spika;
Tanzania itaendelea kuwa mwanachama
mwaminifu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na kuendelea
kushirikiana kwa karibu na nchi wanachama ambao tunauhusiano wa kihistoria na
kidugu. Tutaendelea kuamini katika Umoja wa Afrika (AU) na azma ya ndoto ya
waasisi wetu ya kuunganisha bara la Afrika. Tutaendelea pia kushiriki
kikamilifu katika Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) na kushirikiana na
nchi wenzetu wanachama kutafuta majawabu ya kudumu ya amani, usalama na
maendeleo katika eneo la maziwa makuu.
Tutaendeleza na kustawisha mahusiano na marafiki zetu wote Magharibi, Mashariki
ya Mbali na Mashariki ya Kati kwa lengo la kushirikiana kwa maslahi ya nchi
zetu na watu wetu. Tutapenda kutumia fursa nzuri ya mahusiano yetu mazuri
kisiasa kukuza mahusiano yetu ya uchumi kwa kutumia diplomasia ya uchumi.
Tutafanya hivyo pia kwa ushirikiano wa kimataifa kwa kuendeleza mahusiano yetu
na Umoja wa Mataifa (UN) na taasisi zake, Jumuiya ya Madola, Benki ya Dunia,
Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), n.k.
Aidha, tutazitaka Balozi zetu
zionyeshe matunda yanayolingana na thamani ya fedha tunazowapelekea hususan
katika kuvutia uwekezaji, biashara, utalii na mchango wao katika ukuzaji wa
sekta ya viwanda. Tunataka kuona diplomasia yetu na Sera yetu ya nje ikijibu
changamoto zetu za ndani za ajira, miundombinu, masoko ya mazao ya wakulima,
viwanda n.k.
Hitimisho
Mheshimiwa
Spika;
Naomba kabla ya kuhitimisha nitoe
wito kwa Waheshimiwa Wabunge, Bunge hili linalo nafasi ya kuweka historia ya
kuwa kitu kimoja na kuweka masilahi ya Taifa mbele. Kama kuna kitu ambacho
wananchi wanachukia ni lugha za vijembe, mipasho, na ushabiki wa vyama bungeni.
Kwanza, tukumbuke wote bila kujali itikadi za vyama vyetu sisi ni kitu kimoja;
na pili tumechaguliwa kuwawakilisha wenzetu. Baada ya miaka mitano kila mmoja
atarudi kwenye jimbo lake kuomba kura na huko atapimwa kwa maendeleo
aliyopeleka.
Tusimame pamoja, Tanzania ni yetu
sote tutangulize masilahi ya nchi mbele, na kwa mara ya kwanza Watanzania waone
Bunge tofauti na sio Bunge la kuzomea, kutoka nje, kutukanana, mipasho, n.k.
Tunaitwa Waheshimiwa kwa heshima ya dhamana tuliyopewa na Bunge hili Tukufu,
tutunze heshima hiyo ili tuzidi kuheshimiwa.
Aidha, napenda kusisitiza kuwa kazi
iliyoko mbele yetu ni kubwa. Matarajio na matumaini ya Watanzania waliotuchagua
na kutupa ridhaa ya kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni
makubwa. Wanachotaka kuona ni nchi yetu kupiga hatua kubwa za maendeleo
zitakazojibu matumaini yao na kutatua shida na kero zao. Nyie na mimi, baada ya
miaka mitano toka sasa, tutapimwa kwa namna tutakavyokuwa tumetekeleza mambo
ambayo tumewaahidi Watanzania wenzetu. Mimi nina amini kabisa kwa ushirikiano
wetu na kwa kufanya kazi kwa bidii na ubunifu tutaweza kuzitimiza ndoto za Watanzania
wenzetu.
Mheshimiwa
Spika;
Sasa natamka kwamba nimelifungua
rasmi Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Asanteni kwa
kunisikiliza!
Mungu
libariki Bunge letu na Wabunge wake!
Mungu
Ibariki Afrika!
Mungu
Ibariki Tanzania!
Ahsanteni kwa kunisikiliza
No comments:
Post a Comment