(Makala hii ipo katika toleo la gazeti la habarileo la may 9
2015)
MICHEZO ni afya walisema wahenga
tangu enzi za mababu zetu. Nami sina budi kukubaliana na msemo wa wahenga hawa
kwani nimeshuhudia michezo ikijenga afya na kudumisha undugu ama kujenga
urafiki.
Mafanikio na maendeleo ya michezo
Tanzania ni matokeo ya muda mrefu ya juhudi za serikali kwa kushirikiana na
wadau wengine kuhakikisha taifa linapata wanamichezo wenye vipaji na
kuwaendeleza ili wafikie ndoto za kutwaa ubingwa kwenye mashindano mbalimbali
ndani na nje ya nchi.
Katika kuzungumzia mafanikio haya
ya michezo na maendeleo ya taaluma hii, makala haya yatajikita zaidi katika
kuzungumzia chuo pekee cha kuzalisha wataalamu na walimu wa michezo Tanzania,
Chuo cha Michezo cha Malya.
Chuo hiki cha michezo kabla ya
kuanzishwa kwake, eneo la Malya lilianzishwa na wakoloni wa Kijerumani waliotawala
Tanganyika kuanzia mwaka 1914 hadi 1918.
Katika kipindi hicho, Malya
ilikuwa ndio makao makuu na makazi ya Kamishina Msaidizi Kanda ya Ziwa kwa
Wajerumani. Baada ya kupata Uhuru, Malya ikawa makao makuu ya wilaya mpya ya
Kwimba na sehemu ambayo machifu wote wa Kanda ya Ziwa wa kabila la Wasukuma
walikutana na kufanya mikutano yao.
Kwa kuwa makao makuu ya wilaya,
majengo na miundombinu yote ilikuwa ni mali ya Serikali ya Tanzania chini ya
mamlaka ya Mkoa wa Mwanza.
Jengo ambalo machifu walilitumia
kukutana, kufanya mikutano ya mwaka na kuendesha shughuli nyingine linaendelea
kutunzwa kama sehemu ya urithi wa historia kwa Chuo cha Maendeleo ya Michezo
Malya, mji wa Malya na Wasukuma.
Baadaye makao makuu ya Wilaya ya
Kwimba yalihamishiwa mji wa Ngudu, na mwaka 1979, Wizara ya Utamaduni na Vijana
wakati huo, iliomba na kupewa kibali cha kutumia miundombinu ya majengo ili
itumike kama nyumba za watumishi, vyumba vya madarasa, bwalo la chakula, jiko
pamoja na ofisi mbalimbali na kiwanja cha mpira wa miguu kwa ajili ya maendeleo
ya michezo pamoja na maendeleo ya vijana.
Lengo kubwa la chuo hiki ni kuwa
kitovu cha kuzalisha wataalamu wa kimataifa katika nyanja za ukocha, utawala
bora katika michezo, uamuzi na wachezaji mahiri. Kwa kipindi cha miaka 50
ijayo, chuo kinaazimia kuwa na miundombinu muhimu na yenye hadhi ya kuzalisha
wataalamu wa michezo wenye ubora wa kimataifa na hata kuandaa mashindano yenye
hadhi ya Olimpiki na michezo mingine ya burudani kitaifa na kimataifa.
Kwa sasa chuo kinatoa mafunzo
bora ya michezo, kuendesha na kufanya tafiti za michezo na kutoa huduma kwa
jamii kwa kuendeleza vijana katika kukuza vipaji vyao kwenye fani mbalimbali
pia kuhamashisha vijana wa Tanzania kuendeleza kupenda michezo na kuitangaza
nchi yetu kupitia michezo.
Mafunzo ya michezo yalianza
kutolewa rasmi 1990 ambapo chuo kilianza na kozi moja tu ya elimu ya ukocha
(coaching education) kwa ngazi ya cheti na waliopata mafunzo hayo walikuwa ni
wanafunzi 27. Mwaka 2005/2006, chuo kilianza kutoa mafunzo kwa ngazi ya Stashahada.
Kuongezeka kwa kozi ya Stashahada
kumesaidia kuongeza idadi ya wanachuo kutoka kutoka 27 mwaka 1990 na kufikia 32
mwaka wa masomo 2005/2006. Katika mwaka wa masomo 2006/2007, chuo kilipanua
mafunzo ya michezo ya elimu ya ukocha kutoka mchezo mmoja wa mpira wa mikono na
kufikia sita ambayo ni, netiboli, wavu, kikapu, soka na riadha.
Mwaka wa masomo wa 2007/2008,
chuo kiliongeza utoaji wa Stashahada ya Usimamizi na Utawala katika Michezo na
Stashahada ya Ufundishaji Elimu kwa Michezo iliyoanza mwaka wa masomo
2013/2014.
Kwa sasa chuo hiki kinatoa kozi
tatu kwa ngazi ya Stashahada ikiwa ni Stashahada ya Elimu ya Ukocha, Stashahada
ya Usimamizi na Utawala katika Michezo na Stashahada ya Elimu kwa Michezo.
Kutokana na kumalizika kwa miradi
mikubwa ya majengo ya maktaba na sehemu ya jengo la hosteli ya wanachuo,
udahili wa wanachuo wanaojiunga na masomo ulitegemea kupanuka kutoka wanachuo
60 mwaka 2011/2012 hadi kufikia wanachuo 120 kulingana na upanuzi wa
miundombinu unavyoendelea.
Miundombinu ya kufundishia iliyopo
ni mizuri na inavutia kwa wanachuo wanaofika kujipatia mafunzo. Hii inahusisha
madarasa, maktaba zilizojaa vitabu vya kila aina vitakavyowawezesha wanachuo
kupata mafunzo yaliyobora, maabara ya kompyuta, viwanja vya kuchezea vya ndani
na nje.
Miundombinu mingine ni zahanati,
makazi ya wanachuo, pamoja na bwalo la chakula na jiko. Kwa sasa chuo kina
madarasa manne yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 150. Darasa moja lina uwezo wa
kuchukua wanachuo 45 na madarasa matatu yanaweza kuchukua wanachuo 35 kwa kila
moja.
Jengo lililokamilika la maktaba
lina uwezo wa kuchukua wanafunzi 70 kwa wakati, maabara ya kompyuta ina uwezo
wa kuchukua wanafunzi 48. Chuo kina kiwanja kimoja kwa ajili ya mpira wa miguu
pia viwanja vya ndani ambavyo hujumuisha michezo kama vile mpira wa mikono,
netiboli, kikapu na wavu.
Baadaye, michezo kama kunyanyua
vitu vizito, tenisi, mpira wa meza na mpira wa vinyoya pia utakuwa ukichezwa.
Pamoja na mafunzo ya ngazi ya Stashahada yanayotolewa, chuo pia kinatoa mafunzo
ya kozi za muda mfupi katika michezo mbalimbali kama vile mpira wa kengele na
soka kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na vyama husika.
Katika kutekeleza mpango wa
kuwajengea wanachuo uwezo mkubwa katika ufundishaji wa michezo na
kuwatambulisha wahitimu kwa vyama husika, chuo kupitia Kaimu Mkuu wa Chuo,
Richard Mganga, kimeendesha kozi ya mpira wa kengele (Goalball) mchezo ambao
huchezwa na watu wasioona, kuanzia Januari 5 hadi 10, mwaka huu, ikihudhuriwa
na washiriki 66 wanachuo na walimu kutoka katika halmashauri mbalimbali nchini.
Lengo kubwa ni kuwawezesha
wanachuo kutambuliwa na mashirikisho na vyama husika na kufuata utaratibu wa
mashirikisho utakaowawezesha kuwa na vyeti vinavyowaruhusu kufanya mafunzo
mbalimbali kwa kuzingatia viwango vya mashirikisho na kuendelea kupata mafunzo
zaidi.
Akizungumzia manufaa yatokanayo
na mafunzo ya kozi fupi zinazotolewa hapo, Mganga alisema manufaa ni mengi
ikiwemo wanaojiunga ni watumishi wa umma na wanahitaji kurudi kuendelea na
majukumu mengine huku wakitumia mafunzo hayo kuendeleza michezo na kuwaandaa
wanafunzi kushiriki katika mashindano ya Umisseta na Umitashumita.
Aliongeza kuwa, “Maofisa michezo
wengi wa wilaya pia ni matunda ya chuo hiko kama vile Ofisa Michezo Wilaya ya
Kwimba, Namtumbo na wengine wanaofanya kazi katika vyama au mashirikisho
mbalimbali ya michezo.”
Alitoa mwito kwa Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo izungumze na vyama vya ndani vya michezo
ili waone ni namna gani wanavyoweza kuendesha mafunzo ya kozi fupi chuoni hapo
ili kuleta ufanisi mkubwa wa ufundishaji michezo kwa kuzingatia viwango vya
mashirikisho ya michezo duniani.
No comments:
Post a Comment