Saturday, February 20, 2016

NGUDU NYUMBANI BLOG NA USHIRIKI WA WADAU.


Ngudu nyumbani blog ni moja kati ya blogu za jamii iliyojikita zaidi wilayani KWIMBA. Kuhakikisha habari zinawafikia wananchi mathalani wanaotumia mitandao ya kijamii habari, chambuzi, mitazamo mbalimbali na mawazo kwa ujumla juu ya wilaya yetu.

Lengo lake la awali lilikuwa ni kupeleka wazo hili la kuendesha hii blogu kuwa chini ya serikali kwa maana ya halmashauri ya wilaya. Lengo lilikuwa ni kukuza nasaba kati ya serikali na wananchi ambapo serikali ingewajibika kumpatia mwananchi habari zote muhimu zinazomhusu.

Sababu kubwa ya kupeleka wazo hili ni baada ya kuona, kama serikali bado ina ombwe au tatizo kubwa haswa katika sekta hii ya upashaji habari. Na njia rahisi niliyopendekeza kama mwanzilishi wa blogu hii ilikuwa ni kuwapa wao sababu za kulipa uzito suala hili na kulitekeleza kwa manufaa ya wengi.

Wazo lilikwama kwa sababu zinazosemekana kuwa kuna maandalizi ya mwisho kabisa katika kuanzisha tovuti rasmi ya wilaya ambayo itatoa habari na mengine mengi kama zifanyavyo tovuti nyinginezo za serikali. Japo walihitaji pendekezo langu juu ya kuanzisha blogu pengine tovuti ikachua muda mpaka kuanza kutumika.

Pendekezo liliandaliwa na kutumwa kwa njia ya barua pepe, lakini tangu litumwe mwaka jana mwezi april hakuna majibu ya kukataliwa au kukubaliwa kwa pendekezo hili. Na tovuti rasmi bado haijaandaliwa mpaka sasa. Sina hakika kama ‘wakala wa serikali mtandao’ ndio kikwazo katika hili au ni uongozi wenyewe ndio haujawa tayari na kulipa uzito jambo hili.

Lengo lilikuwa sio kuelezea yote haya, bali ni kutoa maelezo machache juu ya hii blogu mpaka hapa ilipofikia.

Kwa sasa blogu inazidi kuongeza wasomaji wa habari zinazoihusu wilaya yetu. Japo changamoto ni nyingi katika kufanikisha hili. Ningependa ifahamike kuwa blogu hii inajiendesha yenyewe na hakuna nasaba yoyote na serikali ya wilaya yetu. Hivyo ni blogu ya jamii kila mmoja wetu anao uhuru wa kuchangia katika mawazo, mijadala, kuandaa na kuleta tafiti mbalimbali juu ya wilaya, mapendekezo, ili mwisho wa siku tuwe na jamii inayowajibika katika kujua yale yanayoendelea katika mazingira yao.

Ushiriki wa wadau katika mawazo, upatikanaji wa habari, mijadala na mengine mengi ni mdogo au pengine naweza kusema haupo kabisa. Nasema hivi kwa maana kuwa asilimia zote POST zote zinazohusu blogu zimetolewa na mwanzilishi wa blogu hii. Na lengo la blogu hii sio la kibiashara ama namna yeyote, bali ni la kijamii zaidi kupata mawazo ya kila mmoja wetu kushiriki kuwaza kwa pamoja.

Wana KWIMBA tunashiriki mijadala katika mitandao kadhaa ya kijamii. Ila lengo la blogu hii ni kuunganisha mawazo yote ili kuwa na platform moja itakayoweza kuunganisha jamii yote ya wana Kwimba kirahisi zaidi pengine tofauti na magroup yetu ya ‘Facebook, whatsapp na mengineyo ambapo yanakuwepo mengi na sio kila mmoja anaweza kushiriki katika magroup hayo kwa wakati.
Nadhani ushiriki wetu ndio changamoto kubwa zaidi, nyingine ni ndogondogo zinawezeka kutatuliwa.

 Pia nikijaribu kupitia takwimu za wasomaji/watembeleaji wa blogu naona kuna raia wa Tanzania waishio  nje kama Marekani, Kenya, Uholanzi, India, Ujerumani na nchi nyinginezo husoma blogu hii mara kwa mara. Nao pia kwa nafasi yao wanao wajibu wa kuchangia mawazo yao katika platform hii.

 Na tukio moja nililokutana nalo juzi kati ni DEVICE  moja kutoka Nairobi Kenya yenye IP ADDRESS ‘141.0.13.113’ ilijaribu kutaka ku-access akaunti ya blogu hii kama Adminstrator. Kama atapata kusoma hapa huyo mwenye address hiyo bila shaka atatakiwa kujua kuwa blogger ni mtaalamu wa IT kwa hiyo asipende kujaribu kila kitu maana hii address yake ni kigezo tosha cha kumfunza adabu. Hii inawahusu wote wenye tabia kama hii.

Kingine, kulingana na majukumu ya kila mmojawetu katika ujenzi wa taifa popote alipo, mara nyingi unaweza kuona post zinawekwa siku za mapumziko(weekend). Ambapo mwandaaji anakuwa na muda wa kutafakari jambo na upande mwingine wadau wanakuwa wengi wamepumzika na majukumu yao ya kuchakarika na maisha. Kwa mara chache sana inaweza tokea kwenye siku za kazi.

Rai yangu kwa wasomaji wa blogu hii pia facebook page inayohusiana na blogu hii ni kuwa, ushiriki wetu sote ndio mafanikio katika hili. Ningependa kushauri kwa wote wenye kupenda kuandika lolote juu ya wilaya yetu na jamii ikaelewa ni vyema wakafanya hivyo kwa faida ya jamii. Tusikomee kulaumu wilaya yetu ni maskini na mwisho wa siku hautoi mawazo ya nini kifanyike kuhakikisha tunatoka hatua tuliyopo na kwenda hatua bora zaidi.

Kuna wadau baadhi wamenihakikishia ushiriki katika hili, pia ningependa kila mwenye kuweza kufanya hivyo na afanye kwa moyo wa dhati yake kabisa akiamini jamii kubwa inafatilia kwa umakini atakachokisema au kukiwasilisha.

Kufanya hivyo tunatimiza matakwa ya katiba yetu ya JMT ya mwaka 1977 kwenye ibara ya 18 inayosema;
(1) Bila kuathiri sheria za nchi, Kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na  kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.
(2) Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbali mbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.

Japo kwa maelezo hayo machache na imani nitakuwa nimeeleweka vyema. Lengo ni kuamsha hisia tofauti, kuongeza msukumo ndani ya jamii zetu kwa lengo la kujenga zaidi bila kuathiri wengine.
Wilaya yetu ina wasomi wa kada mbalimbali hivyo kila mmoja wetu anaweza kutoa mchango wake kupitia kada yake. Sio mahsusi sana mada, mawazo, makala zetu zihusu siasa moja kwa moja bali kuna mazingira mengi ya kuzungumzika pia ya uchumi, kijamii, teknolojia japo siasa inaonekana kuteka na pengine kuwa mhimili mkubwa katika haya mengine.

Naamini hakuna jambo muhali kwenye jamii yetu lisilo na majibu au mawazo mbadala wa kulifanya. Na lengo la kusisitiza ushiriki wetu katika hili ni kuepuka ‘shere’ zinazofanyika mara kwa mara kwenye groups zetu. Huku hazitofanyika kwa maana yak u-post au share habari zisizo na maadili au zisizokuwa na mwamko wowote kwenye jamii yetu.

Mawasiliano kwa watakaokuwa tayari kushirikiana na ngudu nyumbani blog yapo wazi kabisa, hivyo ni jukumu la kila mwenye uhitaji katika hili kuhakikisha anafanya kulingana na hisia, muono na busara zake.

Tafakari.
nguduone@gmail.com


No comments:

Post a Comment

Previous Page Next Page Home