BY NGUDU NYUMBANI BLOG
27/02/2016.
MATOKEO ya kidato cha
nne yaliyotolewa Feb 18 mwaka huu yameonesha kuporomoka kwa ufaulu,
ikilinganishwa na mwaka jana. Ambapo ni anguko la asilimia 1.85 kwa watahiniwa
wa shule.
Matokeo hayo
yalipangwa katika mfumo wa madaraja (Division) badala ya ule wa wastani wa
alama (GPA) kama ambavyo iliagizwa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na
Ufundi hivi karibuni.
Katika shule zilizopo
wilaya ya KWIMBA, kwa wale waliopata kuyaona matokeo ya shule hizo wanaweza
kukubaliana nami kwamba kuna mwendelezo wa kuporomoka huku Mkoa ukibeba sifa ya
mikoa iliyofanya vizuri kitaifa. Mkoa umetoa shule 3 kati ya shule 10 bora
yaani ALLIANCE GIRLS(2), ALLIANCE BOYS(4) na ALLIANCE ROCK ARMY(7) zote za
binafsi.
Nilipata wasaa wa
kuyapitia matokeo ya takriban shule 28 za wilaya yetu japo kuona ufaulu kwa ujumla
tu, nikagundua hayana tofauti sana na ya miaka miwili au mitatu iliyopita.
Nikaja na jibu moja kwamba tunajitahidi kuongeza idadi ya vijana wasio na
sifa(waliofeli) mitaani na pengine tusijue wanachokifanya baada ya
matokeo haya na hakuna anayejali katika hili.
BAADHI YA SHULE ZA
SEKONDARI ZILIZOJITAHIDI.
Shule ya sekondari SUMVE
GIRLS ndiyo inaongoza kwa shule zilizopo wilayani ambapo ipo nafasi ya 48/231
Kimkoa. Ambapo, Div i-0, Div ii-9, Div iii-40, Div iv-71 na Div 0-2. Ni
ajabu kwa shule inayoongoza ki-wilaya hakuna mwenye daraja la kwanza hata
mmoja, na pia pongezi kwao kwa sababu waliopata daraja la sifuri ni wawili tu
kati ya watahiniwa 122. Shule hii ina uhakika wa kupeleka wanafunzi 49
kidato cha 5. Mwaka jana walipeleka wanafunzi 56 kidato cha 5.
Shule ya sekondari
BUJIKU SAKILA ipo nafasi ya 52/231 Kimkoa, kwa shule zenye watahiniwa zaidi ya
40. Jumla ya watahiniwa ni 109 waliofanya mtihani huo ambapo Div i-4,
Div ii-17, Div iii-16, Div iv-55 na Div 0-17. Kwa ufupi ni kwamba
watahiniwa 37(daraja la 1-3) wana uhakika wa kuendelea na kidato cha tano.
Ikumbukwe kuwa
waliochaguliwa kujiunga na kidato cha 5 mwaka jana kwa shule hii ni 25, kwahiyo
kuna ongezeko la wanafunzi 12 katika awamu hii.
Shule kongwe kama NGUDU,
NYAMILAMA na MWAMASHIMBA zinazidi kupotezwa na hizi (zilizoanzishwa mwanzoni
mwa awamu ya 4 na mwishoni mwa awamu ya 3) taratibu na hakuna anayejali na
kujiuliza kulikoni. Shule hizi za zamani kidogo ndiyo zimepata kupika wasomi na
viongozi wengi tulionao katika nchi yetu kwenye ngazi mbalimbali. Wataalamu
wabobezi wanapenda kuzitofautisha hizi shule kama shule za serikali, na shule
za jamii(kata).
Kwamba katika shule ya
sekondari NGUDU, kati ya watahiniwa 139 waliofanya mtihani, ni 24 tu wanaweza
kuendelea na kidato cha 5. Wakati waliobaki(daraja la iv na 0) ni watahiniwa
115, wengi wao wasijue hatima yao. Huku ikishika nafasi ya 148/231 kimkoa.
Mwaka jana ilipeleka wanafunzi 22 kwenda kidato cha 5.
Aidha, inazidiwa
na mwang’halanga(97/231) na Igongwa (81/231), shule ambazo bado zina changamoto
lukuki katika sekta ya elimu ukilinganisha na shule ya NGUDU. Ambayo
imeanzishwa miaka mingi iliyopita, walau haina changamoto kubwa kama za walimu,
maabara na miundombinu kwa ujumla. Hii ni AIBU kubwa kwa shule mama
ya wilaya.
Shule ya sekondari
NYAMILAMA, kati ya watahiniwa 162 waliofanya mtihani huo, wenye uhakika
wa kwenda kidato cha tano ni 36 tu. Tena kwa hawa hakuna aliyepata daraja la
kwanza. Huku wale wenye div 4 na 0 ni 126, na shule imeshika nafasi ya
134/231 Kimkoa. Mwaka jana ilipeleka wanafunzi 22 kwenda kidato cha 5.
Shule ya sekondari
MWAMASHIMBA, kati ya watahiniwa 89 waliofanya mtihani huo, wenye uhakika wa
kuendelea kidato cha tano ni 32. Huku wale wenye div 4 na 0 wapo 57, na shule
ikishika nafasi ya 61/231 kimkoa. Bila shaka hii ndiyo inafuata kwa kufanya
vizuri kiwilaya baada ya Sumve girls na Bujiku. Mwaka jana ilifanikiwa kupeleka
wanafunzi watano tu kwenda kidato cha 5. Wamefanya vizuri walau kuongeza idadi
hiyo.
Shule ya sekondari MALYA
, kati ya watahiniwa 82 waliofanya mtihani huo, wenye uhakika wa kwenda kidato cha
tano ni 15. Huku wenye Div 4 na 0 wapo 67 kati ya hao wenye Div 0 ni watano tu.
Kimkoa imeshika nafasi ya 63/231 kwa maana ya kwamba ni shule ya 4 kiwilaya kwa
zilizofanya vizuri. Mwaka jana waliochaguliwa kwenda kidato cha 5 walikuwa 15.
Hii pia ni moja kati ya shule zenye watahiniwa wachache kwenye daraja la sifuri
kama ilivyo kwa Sumve girls, Mwamala, Lyoma, na Mwakilyambiti.
BAADHI YA SHULE
ZILIZOFANYA VIBAYA.
Shule ya sekondari
TALLO, ambapo kati ya watahiniwa 45, Div i-0, Div ii-1, Div iii-0, Div
iv-19 na Div 0-25. Hii ina maana kwamba shule itapeleka mwanafunzi “mmoja”
tu kidato cha 5 kati ya 45. Kimkoa ipo nafasi ya 221/231. Mwaka jana ilipeleka
wanafunzi 10, sijui nini kimewasibu mwaka huu na kuwa na matokeo mabovu
kupindukia, bila shaka ndiyo ya mwisho kiwilaya kama sikosei.
Shule ya sekondari
MWANDU, kati ya watahiniwa 48 waliofanya mtihani huo, hakuna Div i,
hakuna Div ii, Div iii-4, Div iv-18, na Div 0- 26. Kwamba ni wanafunzi
wanne ndiyo watajiunga na kidato cha 5. Mwaka jana waliochaguliwa walikuwa
wanne pia. Nafasi yao kimkoa ni 217/231.
Shule ya sekondari
NGULA, iliyokuwa na watahiniwa 63, kati yao wenye Div i-0, Div ii-4,
Div iii-3, Div iv-24 na Div 0-32. Hii inamaanisha itapeleka wanafunzi 7
kidato cha 5. Mwaka jana ilipeleka wanafunzi 7 pia. Nafasi kimkoa ni 168/231.
Shule ya sekondari
MWAGI. Kati ya watahiniwa 84 waliofanya mtihani huo, Div i-0, Div ii-1,
Div iii-4, Div iv-40 na Div 0-39. Hawa wanategemea kupeleka wanafunzi
watano kidato cha 5, mwaka jana walipeleka wanafunzi watano pia. Nafasi yao
kimkoa ni 212/231.
Shule ya sekondari
MANTARE. Kati ya watahiniwa 45 waliofanya mtihani, Div i-0, Div
ii-2, Div iii-2, Div iv=25 na Div 0-16. Kwamba itapeleka wanafunzi wanne
kidato cha 5, mwaka jana ilipeleka wanafunzi 7. Nafasi kimkoa ni 165/231
Shule ya sekondari
MHANDE, waliofanya mtihani ni 60, ambapo Div i-1, Div ii-1, Div iii-8,
Div iv-27 na Div 0-23. Wanatarajia kupeleka wanafunzi 10 kidato cha 5,
kwa mwaka jana walipeleka wanafunzi watatu. Kimkoa ipo nafasi ya 167/231.
TUNAJIFUNZA NINI JUU YA
MATOKEO HAYA?
Kwa maoni na tathmini
yangu nimeweza kugundua na pengine kujifunza mambo kadhaa..
Moja, asilimia 60 na zaidi, ya wahitimu wanapata
“Division” IV na 0. Ambapo katika kundi hili kuna wanaopata bahati ya kuendelea
katika taasisi mbalimbali mathalan, vyuo vya elimu, afya, VETA na taasisi
nyingine nyingi kusoma kozi hasa za astashahada na kozi za ufundi.
Kundi jingine
katika hiyo asilimia linakuwa na vyeti ambavyo hutumika mara chache sana kusoma
baadhi ya kozi ikitegemeana na hali ya uchumi wa mzazi. Na kundi la mwisho wao
hata vyeti hawapati. Unaweza jiuliza mwisho wa siku, hili kundi linakuwa linachukuliwa
vipi katika jamii. Hakuna anayejali!
Pili, shule kama SUMVE GIRLS na BUJIKU zimeonekana
walau kufanya vizuri katika mfululizo wa takribani miaka 3 sasa. Japo sio kwa
kiwango kinachotakiwa lakini hatuna budi kuwasifia na kuwatia moyo zaidi. Wakati
shule kubwa kama NGUDU, NYAMILAMA, MWAMASHIMBA na nyinginezo zimeendelea
kuzorota kadri miaka inavyokwenda. Hawapaswi kubweteka hata kidogo japo kwa
ufaulu huu mdogo, inawapasa kutia bidii na juhudi zaidi. Hakuna
anayejali!
Tatu, Mkoa umeendelea kubeba sifa katika kufanya
vizuri kitaifa kwa miaka kadhaa sasa, huku wilaya ikimezwa katika mafanikio
hayo. Japo ukifatilia ufaulu kwa ngazi ya wilaya, wilaya hii imekuwa ikiburuza
mkia mara kwa mara. Viongozi wanayajua haya fika na hakuna hatua wanayochukua
pengine kunusuru hali hii. Hakuna anayejali!
Nne, wenye dhamana ya kusimamia hii elimu yetu
naweza kusema wanajiita wanaharakati waliojipambanua. Kwamba kufeli kwa shule
za wilaya hii sio sababu na pengine hawastuki kabisa, bali wanachukulia
mafanikio ya mkoa zaidi. Sina imani kama matokeo mabovu haya yanachagizwa na
mrundikano wa madai ya walimu juu ya stahiki zao. Na kama pengine ndivyo ilivyo
nani anapaswa kunyooshewa kidole, serikali, CWT na walimu kwa ujumla, au nani?
Sikuona ajabu nilipoona
taarifa mwishoni mwa mwaka jana kwamba, zaidi ya walimu 300 wakitishia kugoma
kufundisha kushinikiza stahiki zao toka serikalini. Na viongozi wao wapo
pengine wameshindwa kufuatilia masuala haya kiundani au pengine ni ugumu wa
serikali katika kuwasikiliza na kutatua changamoto zao. Hakuna
anayejali!
Kila mmoja wetu
anahusika kwa namna moja au nyingine katika kushauri na kuchangia namna bora ya
kupata mafanikio.
Sasa tupo katika awamu
mpya ya HAPA KAZI TU. Iliyojipambanua kinagaubaga kuhakikisha elimu inatolewa
bure kuanzia msingi hadi sekondari. Japo cha kujiuliza ni kwamba, je, ni kweli
kwamba matokeo yetu mabovu yataondolewa kwa kuwapo kwa elimu bure pekee?
Kama elimu bure
itazingatia na kumjali mwalimu kwa kumtengenezea mazingira mazuri katika kazi
yake, pia kuiboresha kiasi cha kumfanya mwanafunzi kufuata taratibu na sheria.
Kama elimu hii itatatua changamoto zote kwa ujumla zinazoikabili sekta hii,
bila shaka matunda tutayaona.
Vinginevyo kama ni
katika kupunguza mzigo kwa mzazi katika michango, ada na mengineyo siamini kama
tutapiga hatua mbele zaidi ya kuzidi kurudi nyuma miaka yote daima dawamu.
WATAALAMU KATIKA SEKTA
HII NA WACHAMBUZI WANASEMAJE?
Itawawia vigumu mno
wanafunzi hawa waliofeli(Div iv na 0) kupata ajira kwani hawana maarifa ya
msingi ya kusoma, kuandika na kuhesabu. Pia wanakosa stadi za msingi za maisha
kama kujiamini, ubunifu na mbinu za kutatua matatizo. .
Walimu ni sehemu muhimu
katika kuleta elimu bora. Elimu bora inahusiana moja kwa moja na ufundishaji
bora na ujifunzaji bora. Kuna
mambo mengi yanayoukilia ufundishaji bora, miongoni mwayo ni sifa na uzoefu wa
waalimu, kiwango cha hamasa waliyo nayo, moyo wa kujituma na hisia za
kufundisha na mazingira ya kazi.. (HAKI ELIMU).
Sababu kadhaa zimetajwa
kuwa chanzo cha hali duni ya elimu hapa nchini. Mosha (2011) ameeleza kwa
muhtasari sababu hizo, akiziweka katika makundi makuu mawili, ambayo ni:
sababu za kimazingira na sababu za vitendea kazi.
Kwa mujibu wa Mosha, sababu za kimazingira hujumuisha mazingira ya kisiasa,
kiuchumi, kisheria, kidemografia, kiutamaduni na kimataifa. Sababu za
vitendea kazi hujumuisha uongozi duni katika taasisi, ufadhili duni kwa
sekta ya elimu, hali duni ya miundombinu ya kufundishia na kujifunzia,
walimu wenye sifa duni na matatizo ya mitaala....(MOSHA 2011)
Mabadiliko katika elimu
barani Afrika yamelenga zaidi kuongeza idadi ya watu wanaopata elimu,
huku ubora wa elimu inayotolewa ukipewa umakini mdogo.. (Odulo, Dachi &
Fertig, 2008)
Ni imani yangu
kwamba, tathmini na maelezo yangu kwa ujumla yatakuwa yamewafikia na kueleweka
wana KWIMBA popote mlipo, iwe chachu kwa wadau na wataalamu katika sekta hii
kutoa ushauri bora juu ya kuinusuru elimu yetu na vijana/wadogo zetu ambao ndio
mwanga na taifa la leo na kesho katika kuleta maendeleo endelevu kwenye jamii
yetu.
Mwandishi maarufu wa
marekani, Magret mead, aliwahi kutamka "never doubt that a small group of
thoughtful, committed citizens can change the world; indeed, it's the only
thing that ever has"
akiwa na maana kwamba,
tusiwe na shaka kwamba kikundi kidogo cha wananchi wenye fikra, wenye kujituma
kinaweza kugeuza dunia.kawaida wanaweza kuungana, kupashana habari, kujifunza,
kupanga na kutenda kwa ajili ya kuleta maendeleo.
Tafakari!
KWIMBA TUITAKAYO
nguduone@gmail.com
DUUUUUU MAJANGA
ReplyDelete