Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Kwimba, Mkoa wa
Mwanza, Cosberth Byabato, juzi alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya Naibu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula kumbana ampatie
maelezo kuhusu idara hiyo kuchukua fedha kutoka kwa wananchi bila ya kuwagawia
viwanja.
Ofisa huyo alipata ‘kibano’ hicho mbele ya
wananchi waliomlalamikia Mabula kuwa licha ya kulipa fedha za viwanja,
halmashauri imeshindwa kuwakabidhi.
Baada ya kupokea malalamiko hayo, Mabula
alimtaka Byabata kueleza sababu zilizoifanya halmashauri itoe jumla ya hekari
2,500 zimilikiwe na taasisi za dini na magereza ambao toka wagawiwe 1998,
wameshindwa kuziendeleza.
Pia, inadaiwa kuwa wamiliki hao
huwakodisha wananchi kwa Sh25,000 kwa kila heka kwa ajili ya kulima.
Baadhi ya wananchi walimlalamikia naibu
waziri huyo alipozungumza nao katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika
Kijiji cha Maliya wilayani Kwimba.
Akizungumza kwenye mkutano huo mmoja wa
wananchi hao, Mery Vicent alimuomba naibu waziri huyo awasaidie kupata ardhi.
“Wanatupatia ahadi kila siku tuje wakati
wameshakula Sh800,000 zetu,” alidai Vicent.
Alipotakiwa kujibu malalamiko hayo ya
wananchi, Byabato alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kukatishwa kila mara
na Mabula aliyekuwa akimtaka atoe ufafanuzi wa kina.
Hata hivyo, alikiri wananchi kutopatiwa
viwanja na kuahidi kuwapa kesho.
Akizungumzia hekari 2,500 zilizotolewa kwa
taasisi za dini, alisema: “Eneo linalolalamikiwa na wananchi, mwaka 2008
lilipata wawekezaji ambao ni Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)
hekari 1,000, Kanisa Katoliki 1,000 na Magereza 500.
“Eneo hilo lilianza kutambuliwa mwaka 2011
kisheria na hati zake zilitolewa mwaka jana.
Tatizo wananchi wanaona mashamba hayo
hayaendelezwi, lakini sheria inasema baada ya miaka mitano kama yatakuwa
hayajaendelezwa yachukuliwe na Serikali, muda huo bado haujafika,” alifafanua.
Chanzo: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment