BY NGUDU NYUMBANI BLOG
13/03/2016
NYASECO ALUMINAE, hili ni kundi la wadau
waliopata kusoma shule ya sekondari Nyamilama iliyopo talafa ya
Nyamilama, kata ya Nyamilama wilaya ya KWIMBA.
Wadau hawa licha ya uchache wao lakini
walipata kujipanga na kwenda kuitembelea shule waliyopata kusoma miaka kadhaa
iliyopita. Lengo ni kujua maendeleo ya shule yao hiyo, changamoto zinazoikabili
shule hiyo na mambo yote yanayoihusu shule kwa ujumla.
Sijabahatika kupata taarifa zao zaidi,
japo kwa “Video clip” ya dakika chache inatosha kuonesha malengo na
Mipango waliyokuwa nayo kutaka kuitembelea shule yao. Shauku yao kubwa
ilikuwa ni kuona mabadiliko ya shule hiyo kipindi wanasoma na hali ilivyo kwa
kipindi wameitembelea.
Kuweza kuongea na vijana na kuwapa ushauri
ambao kwa namna moja ni msaada mkubwa kwa wanafunzi hao. Ushauri unaoweza
kuwajenga kiuwezo na kifikra pia kuelekea kwenye mafanikio yao.
Wadau kadhaa pia kupitia NADSO waliwahi
kutembelea shule ya sekondari NGUDU na kufanikisha baadhi ya maazimio
waliyokusudia kuyafikisha shuleni hapo, ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wa
vitabu n.k.
WADAU WENGINE WANA NAFASI GANI?
Kila mmoja wetu anaweza kuguswa kwa namna
yake, kiasi cha kupelekea kuhamasika au pengine kuwaza siku moja anaweza
kuitembelea ama shule aliyowahi kusoma au taasisi yoyote iliyopata kumlea hapo
kabla.
kundi la wadau wanaweza kupanga namna ya
kuweza kuikumbuka shule waliyosoma kipindi cha nyuma. Wakajadili kupitia namna
mbalimbali za mawasiliano, kisha wakapata wawakilishi baadhi wanaoweza kubeba
ujumbe wa jumla juu ya lengo lao la msingi.
Ujumbe wao unaweza kuwa kwenye
maandishi mahsusi kuwafikia walengwa. Au pengine unaweza kuwasilishwa kwa namna
yoyote iliyo bora ikiwa na lengo lile lile.
Niliwahi kuwa na wazo hili kabla, japo ni
kwa namna tofauti kidogo kwamba, nilipata kuaandaa baadhi ya ripoti kadhaa
nikilenga hasa matokeo ya shule husika. Kuna shule kadhaa nimepata kuandaa kila
napopata muda wa kufanya hivyo.
Changamoto ikawa ni namna gani naweza pata
wadau, tukaweza unganisha mawazo na kupata mwafaka wa pamoja namna ya kulifanya
jambo hili kwa ufasaha zaidi. Kuna mambo mengi na ya msingi ya kujadili kabla
ya kuwaza na kuamua kwenda kutembelea jamii mliyokulia na kusoma.
Changamoto ya mazingira tofauti
baina yetu pia, japo hii sikuona kama ni kikwazo sababu kupitia mitandao ya
kijamii mnaweza kujadili kwa ufasaha pia. Na wakapatikana wadau walio karibu na
eneo la ”tukio” wakawakilisha. Au mkakubaliana mathalan, kukutana na kujadili
kipindi cha likizo ambapo wengi hupenda kurudi nyumbani kusalimia ndugu, jamaa
na marafiki.
Tunaweza kama jamii, kutumia mitandao hii
ya kijamii kushauri na kushauriana namna bora ya kufanya mambo, kujadili, na
kuweka kumbukumbu nzuri na sahihi juu ya jamii tunazotoka.
Mwitiko wa wadau katika mambo kama hayo
huwa ni hafifu sana, ikizingatiwa kwamba kila mmojawetu anakuwa na mambo
yake ya msingi katika ujenzi wa taifa. Lakini sidhani pamoja na kuwa busy
unaweza kukosa muda wa kujadili mambo kadhaa yanayoigusa jamii yako uliyokulia.
Uchache wa wanaoguswa katika mambo kama
haya haupaswi kuwa kikwazo katika kufanikisha Mipango. Nyaseco walikuwa wadau
wachache na walifanikiwa, kwahiyo wingi wa watu sio kigezo cha kufanikisha azma
yenu.
Makundi yanaweza kuwa mengi kadri ya
mnavyoweza kujipanga, ikiwa tu lengo la msingi ni moja. Ningependa ujenzi wa
nasaba yenye siha njema baina yetu na jamii tunayotoka na tunayoishi iwe
katika kila mmojawetu kwa wana Kwimba wote popote pale mlipo.
Wasomi , watu maarufu na viongozi wakubwa
katika taifa hili wametokana na jamii tunazoishi. Lakini wengi wao wana mchango
mdogo sana mathalan, katika jamii waliyokulia na pengine kusoma. Hawataki
kuwekeza mawazo, miradi au mali zao kwenye jamii walizokulia, na mwisho wa siku
huishia kulaumu kuwa jamii wanayotoka bado ni maskini bila ya kujua wao wana
mchango gani katika kuleta maendeleo kwenye jamii hiyo.
Ukiachilia sababu nyingine zinazopelekea
wilaya yetu kubaki nyuma siku zote na pengine kuwa na ukuaji mdogo wa hali ya
maisha na maendeleo kwa ujumla. Kundi la wasomi na wazaliwa wote ambao hawaipi
jamii yao kipaumbele kwenye uwekezaji wao ndio sababu mojawapo ya umasikini wa
jamii yao.
Katika hili kuna mifano mingi lakini
haitokuwa busara kama nitaanza kutaja mtu kwa jina au cheo chake lakini nafsi
ya kila mmoja wetu inajua ipo katika nafasi ipi katika ujenzi wa jamii yetu.
Ningeweza kuongea zaidi ya hapa lakini
inatosha kusema ujumbe umetufikia sote inabakia upande wetu katika kuamua namna
bora ya kufanya.
Tafakari!
KWIMBA TUITAKAYO
nguduone@gmail.com.
No comments:
Post a Comment