Mgombea wa CCM ngazi ya udiwani ndugu Jonathan Malifedha akiwa jukwaani kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana 2015 |
23/04/2016
Kata ya NGUDU ni mojawapo ya kata 15 zinazounda
jimbo la KWIMBA, ambapo halmashauri ya wilaya inaundwa na majimbo mawili ya
uchaguzi, Kwimba na Sumve na kila jimbo likiwa na kata 15.
Unapozungumzia wilaya ya KWIMBA ni lazima uzungumzie kitovu cha wilaya, makao makuu ya wilaya na picha au muonekano halisi wa wilaya ndipo utagundua NGUDU ndiyo inabeba sifa zote hizo. Ngudu kama tarafa inayounganisha maeneo kadhaa ya kata, pia ni kama kata inayounganisha maeneo kadhaa ya vijiji, vitongoji n.k
Kata ya Ngudu(Mamlaka ya mji mdogo wa ngudu) Inaundwa
na vitongoji kama, Chamhela, Ngudu mjini, Kakora, Igoma, Sokoni, Ngudulugulu,
Budula, Bugakama, Ngumo, Shuleni,Ilamba, Kilyaboya, na Welamasonga
Makadirio ya wakazi wa kata ya Ngudu kwa mwaka jana(2015)
ni watu 29,837 na idadi iliyokadiliwa kwa watu wenye miaka 18 na kuendelea ni
14,428, haya makadilio yalifanyika kwamba, kufikia mwezi October kata itakuwa
na idadi hiyo. Ikumbukwe pia katika Sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka
2012, kata hii ilikuwa na jumla ya wakazi
27,630.
Kata ya NGUDU ina Shule za msingi kama, Budula,
Chamhela, Igoma. Kilyaboya, Kakora, Welamasonga, Ngudulugulu, Ilumba na Ngumo. Kwa
upande wa shule za sekondari kuna Bujiku Sakila na Ngudu sekondari
Kwa
mujibu wa jumuiya ya tawala za mitaa nchini (ALAT) kwenye KIONGOZI CHA
MADIWANI, ngazi ya Kata, kwa mujibu wa Sheria,
siyo mamlaka ya utawala bali ni ngazi inayowezesha Mamlaka za Kijiji na
Halmashauri ya eneo lake, kwa kutekeleza shughuli za uratibu kupitia Kamati ya
Maendeleo ya Kata.
Kamati ya
Maendeleo ya Kata
Katika Ngazi ya Kata utendaji wake huwezeshwa kupitia kamati ya maendeleo ya
kata
ambayo sura 287 na 288 za sheria zimeelekeza kuwa na muundo ufuatao.
Wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Kata ni wafuatao:-
- Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata ambaye ni Diwani anayewakilisha
Kata;
- Wenyeviti wa Vijiji/Mitaa yote katika Kata;
- Diwani wa Viti maalum Mkazi wa Kata husika;
- Watu walioteuliwa na Kamati ya Maendeleo ya Kata kutoka Mashirika yasiyo ya
Serikali na vikundi vya kijamii (lakini hawaruhusiwi kupiga kura);
- Afia Mtendaji wa Kata – Katibu.
ambayo sura 287 na 288 za sheria zimeelekeza kuwa na muundo ufuatao.
Wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Kata ni wafuatao:-
- Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata ambaye ni Diwani anayewakilisha
Kata;
- Wenyeviti wa Vijiji/Mitaa yote katika Kata;
- Diwani wa Viti maalum Mkazi wa Kata husika;
- Watu walioteuliwa na Kamati ya Maendeleo ya Kata kutoka Mashirika yasiyo ya
Serikali na vikundi vya kijamii (lakini hawaruhusiwi kupiga kura);
- Afia Mtendaji wa Kata – Katibu.
Pia wameelezea aina za kamati za kudumu
kwenye halmashauri ya wilaya kuwa ni; Fedha, Utawala na Mipango, Afya, Elimu na
Maji. Pia kuna Uchumi, ujenzi na mazingira. Kuna kamati ambazo sio za kudumu
kama Kamati ya maadili, kamati ya UKIMWI bali ni kamati za majukumu maalum
katika halmashauri ingawaje zinafanya kazi kwa utaratibu wa kamati za kudumu.
Uundaji wa
kamati ndogo ya kudumu ulisitishwa na unahitaji kibali maalumu kutoka kwa
waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa.
Inashauriwa na kuelekezwa kwamba,
kikao/mkutano wa kamati ya maendeleo ya kata kukutana kila baada ya miezi
mitatu na wakati mwingine wowote kulingana na dharura.
KUHUSU DIWANI
Kuna dhana kadhaa zinazomwelezea diwani kuwa ni mtu
wa aina gani. Kwanza Diwani ni mwakilishi wa wananchi kwenye kata. Pili, diwani
ni mjumbe wa mamlaka za serikali za mitaa(halmashauri ya wilaya/mji). Na pia
diwani anaelezewa kama mwenyekiti wa maendeleo wa kata.
Majukumu ya Diwani yapo wazi, ambapo kubwa ni
kusimamia rasilimali na sheria. Pia kuwakilisha wananchi kwenye shughuli zote
za maendeleo kwenye kata na halmashauri kwa ujumla.
“Diwani si mwajiriwa wa
Halmashauri, bali ni “Mwakilishi wa watu”, na hivyo anawajibika kwa watu
anaowawakilisha na wakazi wa eneo la Halmashauri yake.” (policy forum)
Diwani si Mtendaji, bali ni Kiongozi
na Mwakilishi wa wananchi hivyo hapaswi kuingilia utendaji wa idara yoyote
katika Halmashauri kwa maslahi yake binafsi
Diwani pia analo jukumu zito la
Kuwashirikisha wananchi katika kuainisha vyanzo vya mapato, mahitaji, fursa na
vipaumbele vyao. Kuhakikisha ukusanyaji na matumizi sahihi ya mapato n.k
Awe ni mtu wa kusimamia misingi na sifa
za utawala bora. Nikimaanisha Demokrasia, Ushirikishwaji, Utawala wa Sheria, Uwazi,
Uwajibikaji, haki, usawa na uadilifu na wakala wa mabadiliko ya kweli.
Hali Kadhalika,
kwa kata ya NGUDU diwani wa kuchaguliwa ni Mh. Malifedha. Japo kuna diwani wa
kuteuliwa(viti maalum) atakuwepo bila shaka. Kwa wilaya nzima ya Kwimba kuna
viti maalumu 11, ambapo 9 ni kutoka CCM, mmoja kutoka CDM halafu mmoja
alisubiriwa kupatikana baada ya uchaguzi kata ya Bupamwa. Hii ni kulingana na
maelezo ya NEC na kama uchaguzi kata ya Bupamwa umekwisha fanyika basi kuna
utaratibu wao kujua ni kutoka chama gani.
Mantiki yangu ni kwamba, tukizungumzia kata ya NGUDU
lazima tujue kuna wawakilishi zaidi ya mmoja. Kwamba katika hao 9 wa CCM kuna
ama mmoja anatoka kata ya Ngudu. Pengine nahisi(japo sina uhakika) Mh. Lucy
Cypriani Nchangwe akawa anatokea kata hii sababu jina hili sio geni sana. Pia
kwa waliofatilia orodha ya viti maalum kwa wilaya yetu wanaweza kutusaidia ni
nani hasa anawakilisha/anatokea kata yetu, na kama hakuna pia tujue.
HARAKATI ZA UCHAGUZI.
Kata ya NGUDU ni mojawapo ya ngome ya chama tawala
kwa miaka yote. Sina taarifa kwa miaka ya nyuma walipata kuongoza wakina nani,
ila najua kuanzia enzi za kina NGASA akaja FAISAL na sasa MALIFEDHA.
Mchakato wa kumpata mrithi wa diwani aliyemaliza
muda wake kata hii ndani ya CCM ulihusisha
makada kadhaa, ambapo mwisho wa siku matokeo yalikuwa kama ifuatavyo;
1-JONATHAN MALIFEDHA (MFURUKI)-124.
2-JOHN IBRAHIM NGASA-51.
3-MUSA TEMBE-26.
4-RICHARD CHARLES-21.
5-SIRAJI KABYEMELA-17.
6-JOSEPH NCHANGWE-6.
7-MUSA BULUBA (FATHER KISS)-6.
2-JOHN IBRAHIM NGASA-51.
3-MUSA TEMBE-26.
4-RICHARD CHARLES-21.
5-SIRAJI KABYEMELA-17.
6-JOSEPH NCHANGWE-6.
7-MUSA BULUBA (FATHER KISS)-6.
Unaweza kuona ndugu Malifedha aliwaacha wenzie
kwa mbali(kura zake ni karibia mara mbili ya jumla ya kura za wagombea wenzake
6) hivyo kuipeperusha bendera ya chama ngazi ya udiwani. Upande wa upinzani
napo ulipita mchujo kumpata mmoja wa kugombea kwa nafasi hiyo.
Kipindi cha kampeni vyama vyenye wagombea
vilijinadi majukwaani kuomba ridhaa ya wananchi kutaka kuongoza kata ya Ngudu.
Nilipata kuhudhuria mikutano baadhi
kuwasikiliza wagombea wakinadi sera zao juu ya uwakilishi wa kata yetu.
Kiukweli sikupenda zile kampeni zilizojaa dhihaka, ndaro na shere hasa
ukizingatia propaganda chafu(naziita za kishamba) zilizoendeshwa na wananchama
na (wakati mwingine wagombea wenyewe) hasa wa CDM na CCM.
Binafsi nilibaki na imani yangu kwamba sio tu Kata
bali Jimbo zima hatujapata watu wazuri(washindani) katika nafasi hizi kama
tukitumia vigezo vya kuwasikiliza wanavyojinadi majukwaani. Japo wapo wachache
wanaojitahidi ila wengi wao bado sana licha ya kuwa na ufuasi mkubwa lakini
ukiwapima kwa wanachosema(sera, hoja, mikakati yao n.k) unaweza ungana na mimi
kama tu sio mkeleketwa wa chama. Kulikuwa na arijojo nyingi sana kimsingi.
Propaganda nyingi zilikuwa za kipuuzi, mara
mgombea Fulani hajaoa kwahiyo hafai, mwingine kalazimishwa kubadili dini ili
apate nafasi kwenye chama. Mwingine mara ana madeni kibao anadaiwa hivyo hafai.
Wengine wanadiliki kutumia kigezo cha jinsia kumnadi mgombea wao kama ni bora
kwa sababu anapambana na jinsia tofauti na mengine mengi.
Kwa jinsi ushabiki ulivyokuwa hasa kwa vyama
hivi viwili vyenye wafuasi wengi, upepo ulivuma sana CDM alipokuwa Mama
Senga(Thereza Jackson) na wengi tukaamini kwa mara ya kwanza kata inaenda
upinzani. Hata wana CCM wengi walianza kuamini hivyo, lakini chini ya usimamizi
wa diwani aliyemaliza muda wake na chama kwa ujumla waliweza kutumia nguvu za
ziada ama kwa njia halali au laa ilimradi mgombea wao aibuke kidedea.
Matokeo ya mwisho ya udiwani Kata ya Ngudu malifedha
john(CCM) kura 4451, thereza Jackson(cdm) kura 3836, Augustine Lusimbya(Act)
kura 54.
Baada ya uchaguzi
kuisha, ndipo zikabaki stori mitaani kila mmoja akiwa na lake kuhusu uchaguzi.
Kuna mtazamo mmoja
kwamba wengi waliamini, mgombea wa CDM hakupewa ushirikiano na wanawake wenzie
ambao kwa kiasi kikubwa ndio mara zote hujitokeza kupiga kura. Kwa upande
mwingie pia vijana wengi walikuwa hawamkubali mgombea wa CCM ambaye ni kijana
mwenzao pia.
Sambamba na hilo kuna
kauli kadhaa zilisikika na kuandikwa kutoka pande tofauti. Mojawapo iliyoleta
msisimko nimeinukuu hapa..“WANANGUDU
HUYO KIJANA HATUFAI KUWA DIWANI WETU WA NGUDU HUYO MALIFEDHA KAWEKWA KUWA
DARAJA LA MASULI NA FEISA WAMEUNDA PEMBE TATU WANANGUDU BILA SISI KUJUA NIHIVI
MASULI AKIPITA KATIBU WA MBUNGE FEISA NA DIWANI MALIFEDHA AWA DARAJA TUMPIGENI
CHINI WANANGUDU HUYO BONGE LA FALA ” Chambilecho Bundalah Simon.
Kwa kauli hii na
nyinginezo zilikuwa na mitazamo tofauti miongoni mwa wafuasi wa vyama hivi na
hata wasio na vyama. Wengine wakiungana nazo na wengine wakipingana nazo, japo
sio kwa aliyepinga wala kuunga mkono
kauli alikuwa na sababu za kufanya hivyo bali wengi walifanya kwa mapenzi yao
binafsi.
Aidha, siku moja nikiwa zangu kwenye ofisi ya
WEO nilijikuta katika mazungumzo na mtu ambaye baada ya kumsikiliza kwa muda
nikagundua alikuwa ni mgombea mmojawapo kwenye nafasi ya udiwani. Japo sikuweza kufahamu ni kutoka chama gani,
sababu kubwa ikiwa kwamba sikupata kumwona jukwaani wakati wa kampeni na pia
mimi sikuwa mmoja ya waliopiga kura kwenye uchaguzi kwa sababu ambazo
hazikuweza kupatiwa ufumbuzi. Hasa ukizingatia nilijiandikishia sehemu tofauti
kabisa na wilaya yetu.
Katika maelezo yake alisema aliamua kutokupiga
kampeni kwa sababu aliamini kwa muda huo hatapata kusikilizwa kama ilivyo kwa
wagombea kutoka vyama vikubwa. Ila lengo lake lilikuwa kuweka utambulisho ili
awamu nyingine iwe rahisi kwake.
Hali hii naambiwa ilijitokeza pia kwenye kura
za maoni ndani ya CCM pale Ndugu Musa Tembe. Baada ya kuchukua fomu,
inasemekana alikatazwa ama na ndugu au watu wake wa karibu kujihusisha na siasa
hasa kugombea nafasi hiyo. Lakini cha ajabu akashika nafasi ya 3 licha ya
kutofanya harakati zozote kujinadi kwa wana CCM wenzie.
Kingine ninachokikumbuka, baada ya wagombea wa
CCM kushinda kwenye Ubunge na udiwani. Wanachama wanazi(hasa wanawake
wakiambatana na watoto) walifanya maandamano kuzunguka maeneo kadhaa(soko la
zamani-soko mjinga na kwingineko) huku wakiwa wamebeba mfano wa jeneza
wakimaanisha wanakizika chama cha upinzani(CDM) na baadae kuliteketeza.
Kwa
mtazamo wangu walikuwa sawa kufanya walichofanya, japo sikuona mantiki ya kubeba lile
jeneza, sababu wao ndiyo wameongoza miaka yote hivyo kama angeshinda wa
upinzani basi ingeleta maana kimsingi. Eniwei waliofurahi walifurahi na
waliochukia walifanya hivyo pia na maisha yakaendelea.
Sasa ni wakati wa
kufanya kazi kwa kuwa uchaguzi na harakazi zote zimepita. Ila ni vyema
kumbukizi kama hizi tukazieleza na pengine kuzitunza kwa matumizi ya baadae
endapo zitahitajika.
USHAURI NA MAPENDEKEZO YANGU..
Kuna mambo baadhi ambayo ningependa kuyagusia katika
kata yetu ya NGUDU nikimhusisha diwani moja kwa moja.
UTEKELEZAJI WA MIRADI NA UWAJIBIKAJI
Diwani anawajibika kusimamia miradi yote iliyo chini
ya kata yake akishirikiana vizuri na viongozi wa chini yake nikimaanisha
uongozi wa kijiji, kitongoji na mtaa. Na katika kila hatua mwananchi anapaswa
kushirikishwa kujua Mipango inavyoenda na pengine kupewa nafasi ya kutoa
ushauri nini kifanyike katika kuboresha mambo. Mbali na kata diwani anapaswa
kuisimamia halmashauri yote kwa ujumla.
Kwa takwimu jinsi zilivyo, kata ya Ngudu ndiyo kata
yenye wakazi wengi zaidi kuliko kata zote zinazounda halmashauri ya wilaya.
Hivyo hata kwenye mfuko wa jimbo fungu lake lazima litofautiane na kata nyingine.
Lakini(kwenye maeneo mengi) mwananchi ashirikishwi kujua mapato na matumizi
ndani eneo lake. Kwa hatua hiyo ndipo viongozi hujipangia na kutumia fedha za
miradi kwa sababu wanajua wananchi hawajui kinachoendelea. Na imani awamu hii
mambo hayatafanyika kwa mazoea bali yatafanyika kwa ufanisi na uwazi zaidi.
Ukisoma ripoti kadhaa za CAG kuhusu ukaguzi wa
taarifa za fedha za mamlaka za serikali za mitaa utangundua uzembe mwingi
umekuwa ukifanyika na baraza wa wawakilishi(madiwani) ama kwa kujua au
kutokujua wamekuwa wakikaa kimya bila kupinga na pengine kuchukua hatua juu ya
vitendo viovu vinavyofanyika.
Mfano taarifa moja inaonesha halmashauri ya wilaya ya KWIMBA inaongoza kuwa na matumizi yasiyo na hati za malipo. Pia malipo yasiyo na vibali(malipo hayakuidhinishwa na baraza la madiwani), ushindanishaji wa zabuni, kununua vifaa bila kuviingiza katika leja.
Pia ripoti inaonesha takwimu za utoaji wa hati
ambapo kwa halmashauri yetu ilipata hati inayoridhisha mwaka 2009/10 na
2011/12. Ikapata hati zisizoridhisha(hati yenye shaka) kwa mwaka 2010/11,
2012/13 na mwaka 2013/14. Baraza linawajibika katika kuisimamia halmashauri
hivyo diwani wangu hapaswi kufanya mambo kwa mazoea bali afanye kile ambacho
watangulizi wake walishindwa kukisimamia.
Na bahati nzuri ni kwamba wizara
inayohusika(TAMISEMI) sasa ipo chini ya mtumbua majipu mkuu. Na katika hatua za
mwanzo katika kubaini watumishi hewa, Mkoa wa MWANZA ndiyo unaongoza kuwa na
watumishi hewa wengi zaidi.
JUKWAA LA KWIDECO
Kwa maoni yangu na wadau waliogusia suala la Jukwaa
la Kwideco, Diwani anakuwa kiongozi wa kwanza kuhusika katika kulifuatilia na
kulitatua tatizo hili. Kwa sababu yeye anaweza kuonana na wahusika wote(Mbunge,
mkuu wa wilaya, Afisa michezo, baraza la madiwani, Mkurugenzi n.k) kuwafikishia
pendekezo juu ya ukarabati wa jengo na mengine mengi yahusuyo uwanja wetu wa
wilaya. Kwangu mimi nitampima katika kulifanikisha hilo ndani ya miaka mitatu
ya mwanzo kwenye uongozi wake.
Mbali na ukarabati wa jengo, suala la michezo
lichukuliwe kama suala zito na muhimu sana. Nasema hivi kwa sababu kupitia
michezo ndipo tunatengeneza ajira kwa vijana wetu, ila ajabu vijana hawa
huletewa jezi kipindi cha kampeni na kuwa na ligi ila mhusika akifanikisha
kushinda ndio imetoka. Inabidi tuwekeze kwenye michezo kwa ngazi ya wilaya tupo
nyuma sana na sio kama hakuna watu wazuri ama timu nzuri bali hatuna uongozi
mzuri. Hata ule ukumbi wa KWIDECO
unaendeshwa visivyo tofauti na ilivyokuwa zamani hii ni kwa mujibu wa
wadau.
Mgombea wa CDM Thereza Jackson aliapa endapo
atashinda uchaguzi kipindi kile, jukwaa la KWIDECO ataanza nalo katika
vipaumbele vyake.
FURSA ZA UJASIRIAMALI
Kiongozi yeyote anayo nafasi kubwa
katika kuona fursa zilizopo kwenye eneo lake na kuweka mikakati ili ziwanufaishe
wananchi wake. Hivyo ni imani yangu kwamba, diwani kabla hata hajawaza kugombea
lazima alikuwa anajua maeneo ambayo yakitiliwa mkazo yanaweza kutengeneza ajira
na fursa kwa wakazi wa Ngudu. Baadhi ya maeneo kama kilimo cha umwagiliaji,
ufugaji wa kuku n.k
Vikundi kadhaa vinaweza kuundwa na
kiongozi kuweza kuangalia namna ya vikundi hivyo kuwezeshwa ili vifanye kazi
mbalimbali za kijasiriamali. Niliwahi kuongelea mambo ya KWIWODE, SHIKOME na vikundi vingine kujua maendeleo yake
lakini hakuna anayejua na vilikuwepo wilaya yetu.
SOKO JIPYA NA MNADA
Katika mpango wa muda mrefu wa halmashauri katika
sera ya mpango miji wapo sahihi kabisa kutanua eneo japo sina hakika kama lile
eneo lilikuwa sahihi kujenga. Lakini licha ya Mipango ya muda mrefu lazima kuwe
na Mipango ya muda mfupi ambayo inapaswa kutekelezwa. Soko lile mara moja moja
utakuta wafanyabiashara wadogo wadogo wanauza licha ya uchache wao. Pia kuna
bucha inahudumia pale japo bado haijazoeleka na kuwekewa mazingira mazuri ya
biashara kwa wakazi wa kata hii na wilaya kwa ujumla.
Kwenye suala la mnada, baadhi yetu wanasema gulio
letu liboreshwe liwe na muonekano mzuri ili watu waweze kufanya biashara zao
kwa uwazi. Japo siafik kwamba lifanyike kwa siku mbili ndani ya wiki moja kama
ilivyowahi kusemwa kutoka kwa mdau mmoja.
JUKWAA LA WANA KWIMBA
Hili wazo nimekuwa nalo tangu zamani
kwamba, kuna haja ya kuwepo kwa jukwaa la wanaKwimba la wazi ambapo litahusisha
lika zote kujadili masuala yetu kwa uwazi na upana zaidi. Kunakuwa na mijadala
ambayo shabaha yake kubwa ni kuibua ari na kuchochea utendaji kazi wa kila
mmojawetu kwa nafasi yake. Kunakuwa na eneo maalumu(mfano ukumbi wa Kwideco),
siku maalum na muda maalum kwa wote wanaopenda kujadili kukutana pamoja na
kubadilishana mawazo kuhusu jamii yetu.
Mbali na hilo linaweza kuwepo jukwaa
la mtandaoni(social network forum) ambapo kunakuwa na utaratibu maalum katika
kujadili masuala mbalimbali, hapa litawahusu hata walio mbali na nyumbani
kushiriki kwa ukamilifu zaidi.
Pia tunaweza kuanzisha toleo la KWIMBA kwa maana ya gazeti, jarida au kitu kama hicho kila baada ya muda Fulani(mfano kila mwisho wa wiki) linalojadili mambo ya Kwimba katika nyanja mbalimbali. Haya yote yanaweza kwenda sambamba na uwepo wa tovuti ya wilaya kama ambavyo naliongelea hili suala kila leo.
Pia tunaweza kuanzisha toleo la KWIMBA kwa maana ya gazeti, jarida au kitu kama hicho kila baada ya muda Fulani(mfano kila mwisho wa wiki) linalojadili mambo ya Kwimba katika nyanja mbalimbali. Haya yote yanaweza kwenda sambamba na uwepo wa tovuti ya wilaya kama ambavyo naliongelea hili suala kila leo.
Wapo wachache miongoni mwetu walioweza
kuona kazi na umuhimu wa NGUDU NYUMBANI BLOG kwa inachokifanya na kutoa pongezi
zao. Ila kama kiongozi anatakiwa kula yamini juu ya suala hili naamini hakuna
litakaloshindikana. Napenda nieleweke kwamba nimeongelea kwa diwani wetu japo
nikilenga kwa kata zote kuhusika katika hili kwa maana ya wilaya nzima.
SUALA LA ELIMU.
Katika tathmini yangu niliyowahi kuiandika
huko nyuma, nikiongelea matokeo ya kidato channe. Nilizungumzia shule kongwe ya
NGUDU kama moja ya shule zenye matokeo mabovu kupindukia licha ya kuwa na
mazingira mazuri tofauti na shule nyingine katika wilaya yetu. Pia shule ya
Bujiku imeendelea kujitahidi japo si kwa kiwango kinachotakiwa.
Hivyo ni jukumu la diwani kushirikiana na wahusika katika sekta hii kusaidia shule zetu zifanye vizuri. Mbali na sekondari kuna shule za msingi pia ambazo nazo changamoto zipo lukuki ikiwa ni pamoja na matokeo mabovu. Zoezi hili ningependa lihusishe shule zote za wilaya yetu.
Hivyo ni jukumu la diwani kushirikiana na wahusika katika sekta hii kusaidia shule zetu zifanye vizuri. Mbali na sekondari kuna shule za msingi pia ambazo nazo changamoto zipo lukuki ikiwa ni pamoja na matokeo mabovu. Zoezi hili ningependa lihusishe shule zote za wilaya yetu.
KUGAWANYWA KWA HALMASHAURI ZIWE MBILI.
Kupitia baraza la wajumbe(madiwani),
anaweza kuwa na hoja hiyo ya kugawanywa kwa halmashauri yetu tuwe na
halmashauri mbili yaani halmashauri za Kwimba na Sumve. Suala hili pia nimewahi
kuliongelea huko nyuma ila likaonekana kuwa zito miongoni mwetu. Naamini kama
baadae watagawanya, kutakuwa na hatua nzuri zaidi ya kuwasogezea wananchi
huduma na kuhalakisha maendeleo.
Kuna mengine mengi ambayo anaweza
kuyafanya ambayo kwa upande wangu naona yapo kwenye majukumu yake muhimu ya
kila siku kama kusimamia zoezi la ugawaji na upimaji wa viwanja, kusuluhisha
migogoro, masuala ya afya na mengine mengi ambayo ni lazima ayasimamie
kikamilifu.
Mwisho, natambua uwepo wa mawazo
kinzani katika kila mtazamo. Mimi ni muumini mzuri wa dhana ya KUKUBALI
KUTOKUKUBALIANA. Ila sifurahii mtu anaposhindwa kujadili kilichowasilishwa na
hatimaye ama kumshambulia mtoa hoja au mwandishi. Siku zote tunajadili
kilichopo mbele yetu na sio kumjadili aliyekileta. Tunapinga vitu kwa hoja na
tunasifia pia alipokugusa na kumwelewa mwandishi.
Nimtakie uwakilishi mwema diwani wa
kata ya NGUDU, panapo majaliwa. Japo nitahitaji aniaminishe(kupitia uwajibikaji
wake) kuwa tatizo la baraza letu(madiwani) sio chama cha mapinduzi bali ni
mwakilishi mmoja mmoja. Vinginevyo nitaendelea kuamini kuwa CCM ndiyo
inatuletea viongozi dhaifu na ndio sababu ya kuwa nyuma siku zote hivyo
tusikubali(awamu nyingine) hata wakibadilisha wagombea bali tujipange kuindoa
kama suruhu ya matatizo yetu na mwanzo mpya wa KWIMBA TUITAKAYO.
Mimi kama kijana naamini katika kijana
mwenzangu katika kuleta maendeleo ya kweli. Makala hii iwakilishe na kata
nyingine zote lengo ni kuona jamii yetu kwa ujumla inasonga mbele. mnisamehe kwa maelezo yangu marefu yenye kuchosha..
Tafakari!
nguduone@gmail.com
No comments:
Post a Comment