Chanzo: Mwananchi
Akiwa anaendelea na ngoma yake wananchi wa Kijiji cha Sekke
waliibiwa ng’ombe wengi sana na watu kutoka Kabila la Wamasai ambao walienda
kuwahifadhi katika Pori la Mwanima karibu na Kijiji cha Bubiki.
Ng’wanamalundi na kikosi chake waliondoka Wilaya ya Kwimba
mkoani Mwanza na kuelekea Sekke wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kwa lengo la kusaidia
kuzikomboa ng’ombe zilizoibwa.
Hata hivyo kabla hawajafika uwanja wa vita, Ng’wanamalundi
alifanya utabiri wake uliotokana na nguvu ambazo alizipata kutoka kwa Bibi
Kizee wa porini.
Sitta anasema aliwaambia kuwa kabla ya vita, itatokea mvua
kubwa sana na ikikatika watakuja ndege hai aina ya mwewe watakaokuwa
wanazungukazunguka kwenye zile ng’ombe na hapo sasa wafuasi wake wakate miti
mifupi mifupi (Lubugu).
Sitta anasema utabiri huo ulitimia, kwani mvua ilinyesha
kubwa sana na baada ya kukatika wale mwewe walijitokeza wengi sana wakawa
wanazunguka kwenye zile ng’ombe na ndipo yale mapigano ya Wamasai na wafuasi
wake yalipoanza.
Aliwaeleza kuwa baada ya kuwa na fimbo ya Lubugu wale wenye
upinde na mishale watakaa nyuma na kazi yao watakuwa wanazipiga zile ngao za
Kimasai na zikidondoka chini ndipo wenye pinde na mishale waanze kushambulia.
Mwanamalundi alipigana hiyo vita ya Wamasai mpaka
akazirejesha zile ng’ombe na aliwatokomeza Wamasai mpaka kwenye mpaka wa Mto
Manonga unaotenganisha Tinde Shinyanga na Nzega mkoani Tabora.
Hapo ndipo ilibainika Wamasai hao walikuwa wametumwa kuiba
ng’ombe Usukumani na Mtemi Tinginya wa Busongo Nzega, ambapo baada ya vita hiyo
Ng’wanamalundi na kundi lake walirudi Sekke na kupewa jina la Kishosha
Mang’ombe tafsiri ikiwa ni mrudisha ng’ombe.
Baada ya vita hiyo Ng’wanamalundi alirudi nyumbani kwao
wilayani Kwimba kuoa, lakini bahati mbaya ilimkuta, kwani kila mke
aliyejifungua, mtoto alikufa. Baba yake Bugomola akaenda Ntuzu kwa sasa Bariadi
kufanyiwa tambiko kuhusu uzazi kwa mwanaye.
Akiwa huko Ntuzu, Bugomola alielezwa mwanaye Ng’wanamalundi
hatapata mtoto kwa wake zake alionao. Hivyo aoe msichana atakayempata upande wa
Mashariki ambaye atakuwa akiitwa Nkamba na atazaa watoto watatu; wa kwanza
ataitwa Sitta, wa pili Ngassa na wa tatu Marieta.
Baada ya kurudi Bugomola, haikumchukua muda mwanaye
Ng’wanamalundi akapata msichana akaoa na akaendelea na shughuli yake ya
kuendesha kikundi cha ngoma.
Ng’wanamalundi kuwekwa kizuizini
Akiwa anaendelea na ngoma zake katika maeneo ya Kanda ya
Ziwa, Sitta anasema siku moja yeye na kikundi chake walipokuwa wakiburudisha
katika maeneo ya Bukumbi mkoani Mwanza, wafuasi wake walipumzika kwenye mti
mkubwa ambapo pia kilikuwa Kituo cha Wajerumani, Ng’wanamalundi aliwaambia
wafuasi wake waondoke waende kwenye ngoma, wafuasi wake waligoma wakadai
wanapumzika kwenye kivuli hicho ili wavute sigara.
Baada ya kuwabembeleza vya kutosha akabaini hawataki
kumsikiliza ndipo alipounyooshea kidole ule mti akisema “Ngh’walemelaga hanti
gunugo aliyo gumaga,” akiwa na maana “Mmekatalia kwenye mti huo huku ukiwa
umekauka.” Ghafla mti huo wote ulikauka.
Kuona hivyo wafuasi wake wakaondoka wote kwenye huo mti
wakaenda kuendelea na ngoma yao ambayo walicheza katika eneo la Bukumbi na
Busagara karibu na Mji wa Mwanza na walipomaliza walirejea Kwimba.
Akiwa Kwimba alicheza ngoma moja na Gindu Nkima, ngoma hiyo
ilikuwa ngumu kwake ilichezwa sehemu za Mwanagwa. Baada ya kuwa amezidiwa
Ng’wanamalundi, wapishi wake walimfuata na kumtaka awasaidie namna ya kupata
kuni za kupikia.
Kutokana na uharaka aliokuwa nao Ng’wanamalundi alielekeza
kidole chake kwenye miti ya minyaa iliyokuwa mbele yake huku akisema “Batemagi
pye abenababa mkazugile,” akiwa na maana “Yakateni yote haya mkapikie.” Baada
ya kauli hiyo minyaa yote ilikauka na kuwa kuni na wafuasi wake walikata
wakaenda kupikia chakula.
Akiwa katika ngoma hiyo wakati huo barabara ya kutoka
Shinyanga kwenda Mwanza ilikuwa inachongwa na manamba waliokuwa wakikamatwa na
Wajerumani kwa ajili ya kazi hiyo, Gavana wa Kijerumani wa eneo la Mwanza
alipita eneo hilo akiwa amepanda punda alikuta kazi imesimama, alipohoji
kwanini kazi imesimama alielezwa wananchi wote wamekwenda kwenye ngoma ya
Ng’wanamalundi.
Kitendo hicho kilimchukiza sana Mjerumani huyo, ambaye
aliondoka akaenda Mwanza na baada ya siku mbili walikuja askari waliomkamata
Ng’wanamalundi na kumfunga mnyororo na watuhumiwa wengine walipelekwa Mwanza na
kuwekwa gerezani.
Kosa hilo kwa utawala wa Ujerumani lilihesabiwa kuwa ni
uhaini wa kupinga utawala wao hivyo alitakiwa kupewa adhabu ya kunyongwa. Kabla
hajapelekwa Mwanza, kwa kuwa ilikuwa ni safari ya kwenda kunyogwa, alipelekwa
nyumbani kwa wazazi wake kuaga.
Alipofika nyumbani kwao alimpa mama yake shoka aliloliweka
pembezoni mwa ukuta chumbani na maziwa, huku akitoa maelekezo.
“Mayu imbasa yeneye ulu yulina ng’wigulya mumhonatwalwa ulu
yika hase mumhonashoka amabele genaya ulu guganda mumhonacha, ulu gita lububhi
mumhonasata.” Akiwa na maana hii shoka ikipanda juu basi nitakuwa nimepelekwa
ikishuka chini nitakuwa nimerudishwa.”
Sitta anasema Ng’wanamalundi aliendelea kumpa maelekezo mama
yake kuwa haya maziwa yakiganda atakuwa amekufa na pindi yakipata utando
atakuwa anaumwa, baada ya maelezo hayo Ng’wanamalundi alipelekwa Mwanza
gerezani ambako alikutana na Mtemi Makongoro wa Mwanza.
Siku iliyofuata walitolewa wote ambapo Sitta alieleza kuwa
walikutana pia na mganga aliyemtabiria kuzaa watoto watatu ambaye naye alikuwa
amekamatwa kwa kosa la kupiga ramli iliyosababisha mauaji ya kishirikina.
Asubuhi kila mmoja alisomewa mashtaka yake ambapo
Ng’wanamalundi alisomewa mashtaka matatu, shtaka la kwanza kuukausha mti
uliokuwa ukitumiwa na maofisa wa utawala wa Wajerumani kama kituo cha
kupumzikia huko Bukumbi Mwanza.
Shtaka la pili kuwatungia na kuwaimbia nyimbo mbaya
Wajerumani na la tatu ni kukwamisha ujenzi wa Barabara ya Mwanza kwenda
Shinyanga.
Ng’wanamalundi alidaiwa kuchezesha ngoma eneo la Mwanangwa
hali iliyosababisha wafanyakazi wa manamba waliokuwa wakilima barabara hiyo
kuacha na kwenda kuangalia ngoma yake hali iliyowachukiza Wajerumani…
Inaendelea...