(Hizi ni salamu zangu kwenu viongozi na wananchi wa
Kwimba katika awamu hii ya HAPA KAZI TU)
BY NGUDU NYUMBANI BLOG
14/08/2016
Ni imani yangu kuwa wote tu wazima wa afya,
tunaendelea na ujenzi wa taifa letu. Leo NGUDU NYUMBANI ingependa kuwakaribisha
rasmi viongozi mbalimbali waliopewa majukumu mazito kuiongoza wilaya yetu
kongwe ya KWIMBA katika awamu hii ya 5.
Bila shaka wengi wetu tunawafahamu viongozi wetu
kuanzia ngazi ya vijiji, vitongoji, mitaa, kata, tarafa na hadi ngazi ya
wilaya.
Kwa faida ya wengine ambao hawajui, Mkuu wa
wilaya(DC) ya Kwimba kwa sasa ni Mhandisi
Mtemi Msafiri Simeon, Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya(DED) ni Pendo
Anangisye Malabeja na Katibu tawala wa wilaya(DAS) ni Andrea Izziga Ng’hwani. DED si mgeni kwetu
sababu amewahi kuhudumu katika nafasi hiyo kabla.
Kuhusu wabunge wa majimbo ya Kwimba na Sumve bila
shaka tunawajua, madiwani wetu na viongozi wengine wote wa ngazi zote
tunawafahamu.
Awamu ya tano imeingia na kasi ya aina yake katika
kuhakikisha inatoa majibu ya changamoto zinazowakabili wananchi wake, ikiongozwa
vema na Rais wa JMT, Dr John Pombe Magufuli.
Katika mambo ambayo Rais amekuwa akisisitiza kufanyiwa kazi na viongozi
aliowateua katika ngazi mbalimbali hasa ngazi ya halmashauri za
wilaya(mkurugenzi, Mkuu wa wilaya na Katibu tawala n.k) ni pamoja na;
Usuluhishaji wa migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji au wakulima
dhidi ya mwekezaji au viongozi wa serikali na wananchi. Mfano mzuri ni mwezi wa
pili mwaka huu pale Naibu waziri wa Ardhi, Nyumba na Maelndeleo ya Makazi
Angelina Mabula alipombana Afisa ardhi wa wilaya ampatie maelezo kuhusu idara
hiyo kuchukua fedha ya wananchi bila ya kuwagawia viwanja. Hayo na mengine
mengi yanapaswa kupatiwa majawabu ya kudumu.
Tatizo la elimu hasa upungufu wa madawati ambalo kwa
kiasi kikubwa limeshughulikiwa. Nilisoma taarifa moja ikimnukuu mkurugenzi wa
wilaya akisema wilaya ya Kwimba ina nakisi ya madawati 5,314 sawa na asilimia
15 kumaliza tatizo la uhaba kufikia julai 30 mwaka huu. Hayo aliyazungumza wakati wa hafla fupi ya kupokea
msaada wa madawati 60 yenye thamani ya Sh milioni 5 iliyofanyika shule ya
msingi Kakora Kata ya Ngudu Mjini, kutoka kwa uongozi wa Benki ya CRDB tawi la
Nyerere jijini Mwanza. Hivyo hadi kufikia julai 21 kulikuwa na upungufu wa
madawati 5,254.
Maagizo mengine ya Rais ni pamoja na kukabiliana na
baa la njaa pamoja na milipuko ya magonjwa katika mikoa na wilaya zote nchini.
Pia kupitia maagizo ya RC Mongella ya june 04 mwaka
huu alipokuwa akiwaapisha wakuu wa
wilaya, ambapo pamoja na yote
alisisitiza wakasimamie shughuli za kuhimiza maendeleo, suala la ulinzi na
usalama huku akitilia mkazo ukomeshwaji wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa
ngozi na vikongwe.
Katika kuwakaribisha huko NGUDU NYUMBANI ingependa
kuwakumbusha machache yaliyopo ndani ya wilaya yetu.
ELIMU
Pamoja na kukabiliana na tatizo la madawati, zoezi
lililofanikiwa kwa kiasi kikubwa. Wilaya yetu bado ipo nyuma sana katika suala
la elimu. Ningependa kulielezea hili kwa kuhusianisha na matokeo ya vijana wetu
kwenye shule za msingi na sekondari.
Bahati nzuri teknolojia imekua kiasi hata cha
matokeo ya upimaji wa kitaifa darasa la nne(SFNA), Matokeo ya darasa la saba,
ya kidato cha pili yote yanawekwa kwenye mtandao. Ukipitia blogu yetu utayaona
na kukubaliana nami.
Tatizo ni kubwa sana katika ufaulu wa shule zetu,
mathalani vijana wanaohitimu kidato cha nne. Niliandika makala yenye jina
‘IDADI YA WALIOCHAGULIWA KIDATO CHA TANO KWA KILA SHULE ZILIZOPO WILAYA YA
KWIMBA’ pia NGUDU NYUMBANI ilifanya tathmini ya matokeo ya kidato cha 4 mwaka
2015. Kwa waliofuatilia matokeo kwa ujumla au walau kusoma tathmini wanaweza kukubaliana
nami kuwa bado tuna safari ndefu katika elimu yetu.
Shule za A-level zilizopo wilaya ya Kwimba walau
zinafanya vizuri katika matokeo yao. Ambapo katika matokeo ya mwaka huu, Mwamashimba H/school wameshika nafasi ya 2/25
kimkoa(ina division 1-3, hakuna four na zero), Sumve ikishika nafasi ya 11/25
kimkoa na Ngudu H/school nafasi ya 12/25 Kimkoa.
Mbali na matokeo, bado sekta ya elimu ina changamoto
lukuki, ikiwemo uhaba wa nyumba za walimu, madarasa, uhaba wa walimu n.k. ‘Elimu ni walimu’ kauli hii imewahi kutolewa
maelezo jadidi na mujarabu na Prof Kitila
Mkumbo katika moja ya makala zake kwenye gazeti la Raia mwema, pia wadau
wengine wamepata kusisistiza kauli hii. Bila kuwekeza katika changamoto
zinazowakabili waalimu bado elimu yetu itabaki nyuma daima dawamu.
Pamoja na yote hayo wilaya yetu inaburuza mkia
katika ufaulu kimkoa kwa muda sasa. Hivyo viongozi wenye dhamana ya kusimamia
sekta hii wasifanye kazi kwa mazoea tungependa kuona mabadiliko.
KILIMO NA HALI YA UCHUMI
MWANZA ni miongoni mwa mikoa(mitano)
inayoongoza kwa umaskini Tanzania na asilimia ya umaskini(35.3 %) hii ni
kulingana na mpango wa maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/167.
kupitia gazeti la mwananchi
waliandika kwamba, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dr, Tibeza alisema taarifa
alizonazo zinatofautiana na alizopewa zinaonyesha kuwa Mkoa wa Mwanza ni
miongoni mwa mikoa mitano inayokabiliwa na upungufu wa chakula.
Alinukuliwa akisema “Taarifa
nilizopewa na mthamini wa chakula zinasema Mwanza ni miongoni mwa (mikoa)
inayokabiliwa na upungufu wa chakula, hivyo itakuwa na njaa, lakini wewe
(Mongella-Mkuu wa Mkoa wa Mwanza) unaniambia kuna chakula cha kutosha,”.
Pamoja na yote hayo,asilimia kubwa
ya wakazi wa Kwimba ni wakulima na wafugaji. wakulima wanaotegemea zaidi mvua za masika ambazo mara
nyingi hazieleweki na sio za kutegemea sana katika kilimo chao.
Mazao kama pamba, alizeti, mpunga,
mahindi n.k ndiyo huliwa na wakulima japo ni kwa uchache ambao wengi wengi wao
hulima kukidhi mahitaji ya familia na wachache hutegemea kuuza kujipatia
kipato.
Changamoto zilizopo hasa kwenye zao la pamba mikoa ya kanda ya ziwa ni
nyingi na hazijapata ufumbuzi wa kudumu. Licha ya kuwa vinu kadhaa vya
kuchambulia pamba bado zao hili halimnufaishi ipasavyo mkulima.
Bwawa la mahiga maalumu kwa kilimo
cha umwagiliaji na uvuvi, kunapaswa kuwepo mipango mizuri katika kulitumia
bwawa hili ili liweze kuwanufaisha wananchi na serikali kwa ujumla.
Elimu inapaswa kutolewa kwa
wakulima, hasa kulima mazao yenye kuhimili ukame, utumiaji bora wa zana bora za
kilimo n.k
UKUAJI WA TEKNOLOJIA
Ukuaji wa sekta ya teknolojia ya habari na
mawasiliano kwa miaka ya hivi karibuni, imekuwa ikikua kwa kasi ukilinganisha
na uhitaji wa watumiaji wa huduma zihusianazo na sekta hiyo. Kumekuwa na
uwekezaji mkubwa katika hili, hali ambayo inatia moyo japo sio kwa kiwango
kinachotakiwa lakini walau inaridhisha.
Ukuaji wa TEHAMA umesababisha
mabadiliko ya uendeshaji wa shughuli za serikali na jamii kwa ujumla.
Ukuaji wa sekta hii unahusisha na vitu vingi ambapo
baadhi ni kama matumizi bora, sahihi na salama ya vifaa na mifumo ya
TEHAMA serikalini. Mbali na hilo pia,
lengo jingine kubwa ni kurahisisha upatikanaji wa habari, uhuru wa kupata
habari na kusambaza kwa wengine bila kuathiri, kuingilia, kukiuka au kuvunja
katiba na sheria zote za nchi zinazolinda uhuru huo.
Kwa leo nitaongelea zaidi kuhusu
matumizi bora na sahihi ya vyombo vya Tehama hasa kwenye matumizi ya mitandao
na intaneti(tovuti, barua pepe n.k)
Kuna uhitaji mkubwa kwa taasisi ama za serikali au
binafsi kuwa na tovuti katika hatua mojawapo ya kurahisisha upatikanaji wa
mambo muhimu yahusuyo taasisi husika. Hasa nikiongelea upande wa serikali,
mamlaka zake nyingi zinatunza na kutoa taarifa zao kwenye tovuti. Ofisi ya
Rais, na ofisi nyingine nyingi kubwa zinafanya hivyo pia.
Ni utaratibu mzuri unaokubalika katika kukuza secta
ya TEHAMA, ambapo unarahisisha upatikanaji wa habari muhimu kwa wale wenye
uwezo wa kutumia mitandao na intaneti kwa ujumla.
Ombi langu kwa hawa viongozi wetu ni kuhakikisha
wilaya inakuwa na tovuti rasmi ambapo, habari zote muhimu za wilaya yetu zenye
kupaswa kuwafikia wananchi ziweke kupatikana kule.
Sambamba na uanzishwaji wa hiyo tovuti, itasaidia
viongozi waandamizi wa serikali ngazi ya wilaya kutumia barua pepe za serikali.
Mwongozo wa matumizi bora, sahihi na salama ya vifaa
na mifumo ya Teknolojia ya habari na mawasiliano(TEHAMA) serikalini toleo la
julai 2012, umesisitiza matumizi wa anwani za barua pepe hasa usajiri wa barua
pepe za serikali.
Anwani za
barua pepe binafasi mfano ‘yahoo.com’, ‘hotmail.com’,
‘gmail.com’ n.k hazipaswi kutumika katika mawasiliano ya shughuli za serikali.
Sasa sijui viongozi wetu wanatumia anwani zipi maana
inaelekezwa taasisi za serikali anwani za barua pepe zao ziwe zenye kikoa cha
mfumo wa ‘.go.tz’ na mfumo wa kifupisho
cha cheo jina la taasisi na kikoa husika. Mfano anwani ya barua pepe ya
mkurugenzi inaweza kuwa.. md@kwimbadc.go.tz
na sio dedkwimba@yahoo.com
iliyokuwa inatumika kabla.
Hiyo kwimbadc.go.tz
ndio tovuti inayopaswa iwepo hewani kwa maana ya kupatikana muda wote(umiliki
wa domain name).
Kuna shida katika tovuti ya mkoa(www.mwanza.go.tz)
hasa katika viungo(links) za wilaya, waliopata kutembelea tovuti hii wanaweza
jua ninachomaanisha.
Mfano ukifungua kwenye link ya ‘Kwimba DC’
utafunguliwa ukurasa ukiwa wazi na ujumbe ukisema ‘Ukurasa huu upo kwenye matengenezo’ ni zaidi ya miaka miwili na zaidi sasa, enewei
pengine matengenezo yanahitaji mwongo mzima tuendelee kusubiri.
Pamoja na hayo yote, kuna blogu moja(www.kwimbadc.blogspot.com)
inayoripoti baadhi ya taarifa za halmashauri, japo sina hakika kama ndiyo
inayotambulika. Kupitia blogu hiyo kuna ‘jarida la Kwimba’ toleo la 45 lenye
jina ‘IJUE KWIMBA’.
Kwa ambao hamjapata kusoma ni vema mkapitia kuna mambo
mazuri ya kuyajua mule japo kwa ufupi. Pia kuna Documentary ya miaka 10 ya
maendeleo ya KWIMBA 2005-2015.
Ningependa kumaliza kwa leo, kwa kunukuu baadhi ya
maneno kwenye kitabu cha Uhuru na Maendeleo kilichoandikwa na Baba wa Taifa
hayati Mwl J.K Nyerere, alisema;
Kama maendeleo yanaongeza uhuru wa watu, basi lazima
yawe maendeleo yanayowafaidia watu. Lazima maendeleo hayo yawe na faida kwao,
na kumaliza shida zao. kila mpango uamuliwe kwa kupima kama unatimiza shabaha
ya maendeleo, na shabaha ya maendeleo ni
watu. Lakini kama mpango unasaidia maendeleo ya watu na kama unatimizwa
na watu kwa hiari yao, mpango huo utatimiza haja za watu, mradi masharti matatu
yametimizwa. Kwanza, kama watu wanaelewa shida zao. Pili, kama wanaelewa jinsi
shida hizo zinavyoweza kumalizwa. Na tatu, kama wana uhuru wa kujiamulia
mipango yao, na kuitimiza.
Itaendelea……
Tafakari!
nguduone@gmail.com