Sunday, February 15, 2015

SAUTI YA NYIKANI KWIMBA ……….. (1)




























NA AKIDA MAJENGA.
Nilipokuwa nyumbani ngudu mwishoni mwa mwaka jana nilifanya udukuzi na kutizama hali ya mambo ya kisiasa wilayani.Inatosha kusema mbegu ya mwamko imepandwa,mwamko wa wakazi wa wilaya kuacha kupelekwa na historia na wao kuamua kusema kulingana na matakwa yao,la muhimu ni matunzo ya mbegu hiyo mpaka kukua kwake na kuashiria mwanzo mpya wa wilaya ya kwimba katika namna ya tofauti ,moja kati ya wilaya za mwanzo kabisa mkoani mwanza lakini yenye maendeleo hafifu yanayokwenda sege mnege.
Ni mwamko mpya kwa maana ya mageuzi ya ushindi wa kitongoji cha ngudu mjini kwa umoja wa UKAWA kupitia chadema, kwamba eneo ambalo ndiyo kiungo cha wilaya nzima kisiasa la ngudu mjini lipo chini ya chama cha upinzani na kwamba inafahamika ushawishi wa ngudu mjini una nafasi katika kuchagiza mageuzi kwa eneo la wilaya nzima.Ushindi huo ni mwamko kwa wananchi wengi kwamba mageuzi yanawezekana na maisha yakaendelea.
Japo kuna nadharia niliambiwa kwamba kupoteza nafasi kwa chama tawala kwa ngudu mjini katika uchaguzi huo wa vitongoji kunachangiwa na tabia ile ile ya chama tawala kupenda kung’ang’ania wagombea ambao hawana mvuto kijamii,na kwamba kama ccm ingekuwa imechanga karata zake vyema labda mambo yangekuwa tofauti.kwa minajiri ya mipango ya baadaye kwa UKAWA na CCM kuna ukweli kwenye hili.
Lakini la muhimu zaidi ni kwamba tunapata funzo gani hasa vijana kizazi kipya kutokana na hali hii ya mambo wilayani kwetu na ukiashiria kwamba kipenga cha mbio za ubunge na udiwani kimatendo kimepulizwa wilayani na tayari watu wazima wapo bussy. Nimesikia habari za bwana mansuri kutetea kiti chake,bwana Nape Nauye katibu mwenezi cha ccm taifa anatajwa kuwania nafasi hiyo pia,sina uhakika na Bi.Leticia Nyerere kurejea katika kugombea nafasi hiyo kulingana na mteguko wake kisiasa wakati wa bunge la katiba na chama chake.
Mwingine ni mwalimu mahewa anatajwa kuwania nafasi hiyo na watu wengine kadha wa kadha ambao kutokana na uchache wa muda sikufanikiwa kufahamu,japo kuna jambo lilinistua kwamba mbunge wa zamani na ninayemuheshimu sana ana mpango wa kugombea ubunge tena.washauri wake waongee naye nadhani nyakati zimepita sana.
Nimejaribu kuwataja wagombea wa chama tawala cha ccm zaidi kwa nafasi ya ubunge sababu naamini kitakwimu na kimfumo mgombea ambaye atapitishwa na chama hicho ndiye mwenye nafasi kubwa ya kushinda, hii ikichangiwa na ukweli kwamba Mgombea pekee toka UKAWA Bi. Leticia Nyerere ambaye kwa maoni yangu ndiye alikuwa na nguvu na ubavu wa kupambana na chama cha ccm wilayani kwimba aliteguka msimamo wakati wa bunge la katiba na kumuacha na ‘walakini ‘ wa kisiasa na kufanya kupoteza mvuto wake ambao aliujenga kwa muda mrefu.
Ifahamike pia kitakwimu kulingana na uchaguzi uliopita wa vitongoji ni kwamba UKAWA walipata asilimia 20% ya viti vyote na CCM asilimia 80% ya viti vyote kiwilaya,hivyo kimantiki CCM ndiyo wana nafasi kubwa ya kushinda ubunge kuliko UKAWA ila Udiwani upinzani wanayo nafasi pia(nipo tayari kusahihishwa).
Hivyo basi kwa minajiri hiyo nitawajadili zaidi chama cha CCM katika nafasi ya ubunge kwa kuwaangalia wagombea wote wanaotajwa kuwania nafasi kupitia chama tawala wilayani na baadaye nitaoanisha nguvu za kila mgombea na mahitaji ya wilaya ili kuweza kuona nani anafaa kubeba jahazi kwa maendeleo ya wilaya.Katika nafasi ya Udiwani nitawajadili UKAWA pia na nitasisitiza vijana siyo katika UKAWA tu bali pia katika chama tawala ccm wajitokeze kubadili historia.
Katika ukawaida wa mambo mwenye nguvu kwa sasa na kwa jicho la haraka ni Ndugu Mansouri ambaye anatetea kiti chake.Huyu ana nguvu mbili au tatu,kwanza ni wazi ana nguvu ya pesa kama ambavyo chaguzi nyingi Afrika hasa zikihusisha tabaka la watu maskini na hohehahe watu huchangamkia pesa kwanza,nguvu ya pili ni kwamba anatetea nafasi yake na hivyo chama kinawiwa kumlinda zaidi badala ya kuleta mwingine vinginevyo wathibitishe udhaifu wake wa kumuacha , na tatu amejibebesha agenda ya kuleta ngudu maji ya ziwa victoria.
Kwa ambao hamfahamu mji wa ngudu sasa maji ni masaa 24 toka mradi mkubwa wa maji ya ziwa victoria,ifahamike maji ya ziwa victoria ni mradi wa taifa zima na uliasisiwa toka zama za Edward lowasa ni waziri wa maji. Udhaifu mkubwa wa bwana mansouri ni kwanza anategema pesa kushinda,pili mfumo ambao ulimsaidia kuingia madarakani unamaliza ngwe yake na hivyo kurejea kwake ama la kunategemea na nguvu ya mgombea urais kwa ccm awamu hii kama itambeba pia,vinginevyo na yeye pia anaweza kushindwa kutetea kiti chake.
Nguvu za bwana mansouri haziendani na mahitaji ya wanakwimba kwa sasa na hata baadaye labda abadili sana taswira yake na sera zake,lakini kwa uchache wake ni kwamba haitawahi kutokea apiganie maendeleo ya wanakwimba kwa dhati kabisa ya uvungu wa moyo wake,kipaumbele chake ni biashara zake za mafuta na wala si maendeleo ya wanakwimba.
Nape Nauye katibu mwenezi ccm taifa anatajwa pia kuweka nia kugombea ubunge wilayani kwimba,japo kuna hadidu za rejea nimezipata pia ameweka nia hiyo kwenye jimbo la Mh.Bernard Membe waziri wa mambo ya nje ambaye anatajwa kugombea nafasi ya urais,ni katika jimbo la mtama mtwara,nadhani kwa sasa anapima upepo na joto la kisiasa kati ya pande hizo mbili japo binafsi naamini kama ana nia kweli atagombea ngudu,maana kusini kuna joto na hasira ya kisiasa hasa masuala ya gesi, hali si rahisi kwa mtu kuanza kwa mara ya kwanza katika purukushani kama hiyo.
Nguvu ya nape ni kwamba anazifahamu siasa za Tanzania,ni rahisi kupambana nazo hasa kwa eneo kama ngudu ambalo bado halina wabishi wa kisiasa,pili anaweza kushinda uteuzi kama ataungana na kambi ya mgombea urais wa kiti cha ccm awamu hii imbebe katika harakati zake hizo,uzuri mwingine wa nape ni kijana na anaongea lugha moja na vijana wenzake,wakati fulani nilionana naye Dodoma akiimba na kupiga vyombo vya mziki katika bendi ya Dodoma mjini wakati wa uzinduzi wa website ya chama chao,hivyo kwa maisha yake ni rahisi kumtafuta na kuonana naye.
Udhaifu wa Nape ni ule ule wa vijana viongozi,atapenda atutumie wanakwimba kupata madaraka ya juu kama uwaziri na kusahau agenda ya kusaidia wanakwimba maana bado ana ndoto za uongozi katika taifa hili kwa anavyoonekana.
Mgombea mwingine ni Ndugu Mahewa,ni mwalimu wangu na ninamheshimu sana kwani alinifundisha akiwa field muda fulani nikiwa darasa la saba shule ya msingi Ngudulugulu.Wakati naondoka ngudu baada ya likizo kurejea dar nilimuacha katika harakati za kutetea nafasi ya mwenyekiti CWT,sifahamu matokeo yake.Mwalimu mahewa na kama washauri wake wapo karibu au wanasoma hapa,wanafahamu ana tatizo moja tu tangu akiwa mwalimu wangu,wazungu wanaita SUPERIORITY COMPLEX au tuseme OVER-CONFIDENCE,maana nakumbuka muda fulani wakati anakuja darasani kutufundusha alikuwa kabla hajafanya lolote ni lazima anyanyue dawati la sehemu ya mwalimu juu kama mara tano au apige pushapu mbele ya wanafunzi ndiyo aanze kufundisha.
Kwa masimulizi ya watu wa ngudu bado shida ya mwalimu mahewa ni hiyo hiyo,kujiamini kupita kiasi katika mambo ambayo yanahitaji usawa wa kawaida .Kama washauri wake wangekuwa wanaweza kumshauri mwalimu mahewa ,ni kwamba ana nguvu na mtaji mkubwa sana kisiasa wilayani kwimba labda tofauti na wagombea wengine wote,unapokuwa mwenyekiti wa walimu wote wilaya unakosa nini? Tiketi yako kubwa ni kufanya kazi kwa juhudi,maarifa na kupigania haki za walimu wako ili wawe mabalozi katika kila kona ya wilaya na walibebe jina lako vyema na kufanya ujilikane kila mahali,sidhani kama mtaji wa walimu anaufahamu.kama ameshinda uenyekiti wa CWT kwa mara nyingine naomba afikishiwe salamu za mtaji huu na kama ana nia kweli ya kuwa mgombea wa wilaya.Ila kama la walimu tu litamshinda sidhani kama kwa nafasi ya ubunge ataweza.
Sasa tujiulize swali,unadhani ili wilaya ya kwimba iendelee inahitaji nini hasa? Naomba tufahamu ukweli wa mambo,mawaziri au wizara za Tanzania au serikali kuu haziwezi kuendeleza wilaya ya kwimba,zitatoa mwongozo tu ila kazi kubwa inabaki kwa wanakwimba wenyewe.Kwimba inaendelezwa na mtu ambaye anaweza kuja akatia pressure kwenye HALMASHAURI YETU YA KWIMBA na WATENDAJI WAKE huku sisi wananchi tukimsaidia.Mtu ambaye atapambana na watendaji wachovu wa wilaya ya kwimba awaamshe wafanye kazi, wawe wabunifu,wakifanya mipango itekelezeke na siyo leo wanapima eneo na wanahamisha stendi ya wilaya na kesho wenye magari wanajichagulia stendi yao wenyewe eneo la hospitali na wanaachwa tu.watendaji uchwara ambao wanatangaza kupima maeneo ya ardhi watu wapewe hati za viwanja na inapita miaka miwili hawajafanya kitu na hakuna anayehoji wala kuwapa pressure,tungepata hizo hati si tungekopa hata benki tukaendelea.
Tunataka mtu wa kuwatia pressure wakuu wa mashule na maofisa elimu,wanafunzi wakawa na malengo mapana ya kujisomea na siyo kwamba leo ukifika Ngudu Sec haufahamu ni muda gani watoto wanajisomea na muda gani wapo mapumziko,wilaya nzima ni “zunzaga zunzaga”,tunahitaji kiongozi wa kuwatia pressure vijana wa ngudu wasimsubiri Emmanuel kasalali karejea ngudu wamuombe pesa ila wajiajili katika kilimo na ufugaji,ufundi seremala na uashi,tunahitaji kiongozi wa kutia pressure waganga wa hospitali za wilaya kwamba kwanini madawa hayaonekani hospitali lakini katika maduka binafsi dawa haziishi?
Kihistoria dunia nzima,uongozi katika ngazi yeyote iwe familia,shule,kijiji,wilaya,wizara au taifa lazima kiongozi mkubwa uwe na uwezo wa kuwatia pressure na kuwauliza watu wawajibike kulingana na nafasi na majukumu yao. Binadamu wote tuna hulka mbaya ya kujisahau na bila kukumbushwa na kuwajibishwa hakuna ambalo tunafanya.Ndivyo alifanya Waziri mama na chuma wa uingereza Bi Magreth Thatcher,ndivyo alifanya Nyerere na Mkapa,ndivyo anafanya mwakyembe na Magufuli. Katika dunia ya leo maendeleo unajiletea mwenyewe na watu wa Kwimba wanapaswa kufahamu ukweli huu,hakuna mtu anakuletea maendeleo,ana pesa kiasi gani akujengee barabara? ila mtu anaweza kuja kusimamia shughuli za maendeleo, na ndiyo wajibu wa wabunge,madiwani na vitongoji kuwasimamia watendaji na kuwapa pressure.
Huu ndiyo wito wangu kwa watu wote wa kwimba na hasa vijana,tunahitaji mtu ambaye ana nguvu ya kututia pressure watu wote kuanzia mkurugenzi wa wilaya,watendaji wake na wananchi kwa ujumla. Unadhani kati ya wagombea niliowajadili hapo juu kuna hata mmoja mwenye sifa hizo? Kuwa sehemu ya mabadiriko ambayo wewe ungependa uone.
1.Katika makala yangu wiki ijayo,sehemu ya pili nitaeleza vijana ambao bado hawana majina kisiasa ila wana nia safi za kiuongozi wafanye nini? Nitaeleza kwa nini vijana wajitokeze nafasi ya udiwani zaidi badala ya ubunge,mfano Ashrafu Omary toka UKAWA (CHADEMA ) alivyo na nafasi ya kushinda udiwani ngudu mjini.
Angalizo langu ni kwamba vijana mnapopata uongozi lazima muonyeshe utofauti na kujituma dhidi ya kile ambacho mlikuwa mnakilalamikia, anayetakiwa kuanza ni Casmiry na tumsaidie.Niombe radhi kama kuna mtu nitamkwaza kwa uandishi wangu,ila naomba tufahamu kwamba ukichagua kuwa kiongozi wa umma,umekubali watu wajenge hoja juu yako na kwa kutaja majina yako kama mimi ninavyofanya hapa,hoja ijibiwe kwa hoja na wachangiaji watumie lugha ya staha kupata wito bora kwa kwimba.Kila la heri..WAKATABAHU!

MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2014


Akitangaza matokeo ya Kidato cha Nne ya mwaka 2014  jijini Dar es salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa Dkt Charles Msonde amesema kati ya waliofaulu, wasichana ni 89,845 sawa na asilimia 66.61 wakati wavulana ni 106,960.

   Akizitaja shule kumi bora kwa ufaulu, Dkt Msonde amesema shule hizo ni;

       1.  Kaizirege mkoa wa Kagera
       2.  Mwanza Alliance mkoa wa Mwanza
       3. Marian Boys mkoa wa Pwani
       4.  St. Francis Girls mkoa wa Mbeya
       5. Abbey mkoa wa Mtwara
       6. Feza Girls mkoa wa Dar es salaam
      7. Canossa Mkoa wa Dar es salaam
      8. Bethel sabs Girls mkoa wa Iringa
      9. Marian Girls mkoa wa Pwani
      10. Feza Boys mkoa wa Dar es salaam.


     Shule 10 za mwisho ni

       1. Manolo mkoa wa Tanga
       2. Chokocho mkoa wa Pemba
       3. Kwalugulu mkoa wa Tanga
       4. Relini mkoa wa Dar es salaam
       5. Mashindei mkoa wa Tanga
       6. Njelekela Islamic Seminary mkoa wa Kigoma
       7. Vudee mkoa wa Kilimanjaro
        8. Mnazi mkoa wa Tanga
       9. Ruhembe mkoa wa Morogoro
      10. Magoma mkoa wa Tanga.

      Dkt Msonde pia ametaja watahiniwa 10 waliofanya vizuri kuwa ni

       1. Nyakaho Marungu kutoka Baobab Pwani
       2. Elton Sadock Jacob kutoka Feza Boys Dar es salaam
       3. Samwel M Adam kutoka Marian Boys Pwani
       4.Fainess John Mwakisimba kutoka kutoka St Francis Girls Mbeya
       5. Mugisha Reynold Lukambuzi kutoka Bendel Memorial Kilimanjaro
       6. Paul W Jijimya kutoka Marian Boys Pwani
       7. Angel Lundgreen Mcharo kutoka St Francis Girls Mbeya
       8. Atuganile Cairo Jimmy kutoka Canossa
       9. Jenifa Lundgreen Mcharo kutoka St Francis Girls Mbeya
      10. Mahmoud Dadi Bakili kutoka Feza Boys


  Kwa upande wa shule za wilayani Kwimba baadhi za matokeo yao kwa ujumla ni kama ifuatavyo






Monday, February 9, 2015

SHIRIKA LA MAALBINO DUNIANI LAMSUTA MBUNGE WA KWIMBA

Mkurugenzi wa shirika la Under The Same Sun (UTSS), Peter Ash

SHIRIKA la Under The Same Sun (UTSS) limeeleza kusikitishwa kwake na viongozi wa kisiasa pamoja na mbunge wa jimbo la kwimba kutofika kumjulia hali na kumfariji mama wa motto mwenye ulemavu wa ngozi, Pendo Emmanuel (4) aliyeporwa na watu wasiojulikana mwishoni mwa mwaka jana.
Hayo yalielezwa jana na Mkurugenzi wa Mwanzilishi wa shirika hilo, Peter Ash wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza ziara yake kwenye mikoa ya Mwanza na Shinyanga
“Nimefika kwenye kijiji cha Ndami wilayani Kwimba, motto pendo alipotekwa na kuzungumza na  wazazi wake ambaye alieleza kuwa mbunge wa jimbo hilo hajaenda kumtembelea ili kujua  motto wake yupo  wapi na anashangaa yeye kutoka Canada amefika”, alisema na kuongeza kwanini mbunge ambaye yeye anampigia kura hajaenda kumsikiliza.
Alisema January 6, mwaka huu katika eneo la Nyakato, motto mwingine mwenye ulemavu wa ngozi , karim kassimalinusurika kutekwa ambapo familia yake nayo inasema hakuna kiongozi wa siasa wala Mbunge walioenda kuwajulia hali.
Ash alisema watu wenye ulemavu wa ngozi wamekuwa wakiwindwa na wanaendelea kuwindwa hasa wakati huu kuelekea uchaguzi ambapo Tanzania na Burundi zinafanya uchaguzi mwaka huu na kuhoji kwa nini vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi vinazidi kuongezeka kipindi hiki.
Alisema kumekuwepo na matukio 152 yakiwemo ya utekaji nyara, kubakwa na mauaji ambayo yametokea kwa kipindi cha miaka 14 nchini Tanzania; lakini ni asilimia tano tu ya kesi ndio zimefikishwa mahakamani ambazo hazilingani na idadi ya matukio na watu waliofanyiwa ukatili.
Alisema viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi vinauzwa kwa bei juu, lakini cha kujiuliza ni nani atakuwa na maelfu ya dola ili kununua hivyo viungo isipokuwa wale watu ambao ni matajiri, Watanzania wengi ni masikini.
Mtoto Pendo Emmanuel (4) aliporwa na watu wasiojulikana December 27, mwaka jana wakati akiwa amelala na wazazi wake katika kijiji cha Ndami, tarafa ya Mwamashimba wilayani Kwimba, majira ya saa 4 usiku.


 Chanzo: Habari leo

HOTUBA YA MHE. WAZIRI MKUU PINDA YA KUAHIRISHA MKUTANO WA 18 WA BUNGE



HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P.  PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO
WA 18 WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
TAREHE 7 FEBRUARI, 2015

I:          UTANGULIZI 

(a)      Masuala ya jumla

1.     Mheshimiwa Spika, Tumekuwepo hapa kwa takriban siku 12 katika shughuli za Mkutano wa 18 wa Bunge lako Tukufu. Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo.

2.     Lakini tumekutana hapa tukiwa tumeshuhudia mabadiliko katika Baraza la Mawaziri na Wenyeviti wa baadhi ya Kamati za Kudumu za Bunge. Niruhusu nitumie nafasi hii ya awali kuwapongeza Mawaziri na Naibu Mawaziri wote ambao wameteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali katika mabadiliko hayo. Aidha, napenda niwapongeze Wenyeviti watatu pamoja na Makamu mmoja kwa kuchaguliwa kuongoza Kamati za Kudumu za Bunge ikiwemo Kamati ya Bajeti, Kamati ya Nishati na Madini na Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala. Tunawatakia afya njema Mawaziri, Naibu Mawaziri na Wenyeviti wote katika kutekeleza majukumu yao mapya.

3.     Mheshimiwa Spika,Tangu tulipomaliza Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge lako Tukufu, kumetokea majanga katika sehemu mbalimbali Nchini ikiwemo mafuriko na mapigano ya Wakulima na Wafugaji kule Morogoro, pamoja na ajali za barabarani. Naomba nitumie nafasi hii kuwapa pole wote walioathirika na majanga, maafa na ajali za barabarani.  Kwa wale waliopoteza maisha tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahala pema peponi Amina.



b)      Maswali

4.  Mheshimiwa Spika,  Katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge             wamepata fursa ya kuuliza maswali ya kawaida na yale ya papo papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Jumla ya maswali 122 ya msingi na 313 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali.  Aidha, Maswali 15 ya msingi na 13 ya nyongeza yaliulizwa na kujibiwa kwa utaratibu wa maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

(c)     Miswada na Taarifa Mbalimbali

5. Mheshimiwa Spika, Tunahitimisha Mkutano huu tukiwa tumekamilisha kazi kubwa ya kusoma na kujadili taarifa mbalimbli za Kamati za Bunge za Kisekta na zisizo za Kisekta. Kamati za Kisekta ambazo Taarifa zake zimewasilishwa na kujadiliwa na Waheshimiwa Wabunge ni zifuatazo:

                                                                                 i.            Kamati ya Miundombinu;
                                                                              ii.            Kamati ya Nishati na Madini;
                                                                            iii.            Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira;
                                                                            iv.            Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji;
                                                                              v.            Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala;
                                                                            vi.            Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa;
                                                                         vii.            Kamati ya Masuala ya UKIMWI;
                                                                       viii.            Kamati ya Ulinzi na Usalama;
                                                                            ix.            Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa;
                                                                              x.            Kamati ya Huduma na Jamii; na
                                                                            xi.            Kamati ya Maendeleo ya Jamii.

6.   Aidha, Bunge Lako Tukufu lilipokea na kujadili Taarifa za Kamati zisizo za Kisekta zinazosimamia Fedha za Umma zifuatazo:

                                              i.            Kamati ya Hesabu za Serikali;
                                            ii.            Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa; na
                                         iii.            Kamati za Bajeti.



UBUNGE JIMBO LA KWIMBA

Hayati musobi mageni musobi

1. MUSOBI MAGENI MUSOBI
Mwenyekiti wa Chama awamu ya pili (1995 – 1999),
 aliyejiunga na chama cha wananchi CUF mwaka 1994
amefariki akiwa na umri wa miaka 81, amezaliwa April 01, 1931,

·        Wakati wa uhai wake alipata elimu ya Msingi katika Shule ya Kakola wilayani Kwimba, na baadae alipata elimu ya kati na Sekondari Dole iliyopo Zanzibar. Baada ya hapo 1950 alirudi wilayani Kwimba na mwaka mmoja baadae 1951 alipata kazi ya ukarani (Area Secretary) katika Halmashuri ya Maswa, na baadae 1954 akahamia Halmashauri ya Kwimba kama Muhasibu na mnamo 1957 akahamishiwa ukarani tena katika Halmashauri hiyohiyo ya Kwimba hadi 1961 alipoacha kazi na kufanya shughuli za ukulima.

·         Ilipofika mwaka 1965 aliamua kugombea ubunge jimbo la Mwamashimba wilaya ya Kwimba, alifanikiwa kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa awamu mbili hadi mwaka 1975, wakati huo akiwa mbunge alifanikiwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Aridhi, Nyumba na Maendeleo Mijini mwaka 1972 na aliutumikia hadi 1975, kabla hajateuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Chunya mwaka 1978, wilaya ya Kahama 1983 na wilaya ya Muleba 1988 hadi 1990.
Kitaaluma, pamoja na mafunzo ya Uhasibu na Ukarani, lakini pia alibahatika kupata mafunzo ya Uandishi wa Habari katika chuo cha Cambrige University mwaka 1968 na Chuo cha Social Training Centre cha Nyegezi, mkoani Mwanza.

Thursday, February 5, 2015

SIKU 40 ZAKATIKA ALBINO ALIYEIBWA HAJAONEKANA


Ni simanzi na majonzi katika kijiji cha Ndami, wilayani Kwimba ikiwa ni siku 40 sasa, tangu mtoto Pendo Emmanuel (4), atekwe na watu ambao hawajajulikana hadi sasa.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Mwandu Madirisha, anasema wananchi wake hawapo vizuri kiakili tangu aibwe mtoto Pendo na kwamba “hawaamini kama mtoto yule hajaonekana mpaka leo.”

Anasema kijiji hicho kina barabara kuu tatu zinazoingia na kutoka katika vitongoji vya Misasi, Nyahonge na Chibwiji, hali inayochangia kuwapo na ulinzi wa jadi (sungusungu).

“Hata hivyo, hawa sungusungu wanalinda katika njia zile kuu tu…siku ya tukio la kuibiwa mtoto 

Pendo, hakuna aliyefahamu wala kuhisi chochote kwani tumezoea kuishi kwa amani kwa miaka mingi,” anasema.

Anasema kutokuwapo kwa matukio ya ‘ajabu’ katika kijiji hicho, ndiko kulikochangia watu wasio wema kutumia nafasi hiyo kumuiba Pendo na kutoweka naye kusikojulikana mpaka sasa. Madirisha anasema wakati watu hao wanatekeleza unyama wao kwa Pendo, kijiji kilikuwa hakina uongozi licha ya kuchaguliwa na wananchi, kutokana na kuchelewa kuapishwa mara baada ya kufanyika uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa na vitongoji.

Mwenyekiti huyo anasema inawezekana watu hao walitumia hali hiyo kufanya ‘uhalifu’ wa kuvamia nyumba yao iliyopo mbali kidogo na barabara zinazolindwa na sungusungu.

“Naamini ni tukio la imani za kishirikina linalowahusu zaidi wafanyabiashara wa migodini pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali ambao wanahitaji madaraka,” anasema.

MAMA PENDO
Mama mzazi wa Pendo, Sophia Juma, ambaye kwa sasa amehamishwa katika makazi yake na kupelekwa wilayani Misungwi, hakuwa na mengi ya kusema kutokana na kumfikiria mtoto wake.

“Namkumbuka sana mwanangu, sielewi huko alipo kipi kimemtokea, lakini namwamini Mungu waliotenda jambo hilo, uso wa Mungu utawaumbua,” anasema Sophia.

Anasema siku ya tukio akiwa na watoto wake wawili akiwamo Pendo, walilala chumbani na muda wa saa 4:00 usiku, walishitukia watu wameingia ndani na kumchukua mtoto kinguvu na kutoweka naye.

Hata hivyo, mama huyo hakuweza kuzungumza sana kutokana na simanzi alizonazo kuhusu mwanaye. 

MAJIRANI
Shigilu Kuya (70), ambaye nyumba yake ipo umbali wa mita 100 toka alipoibwa mtoto Pendo anasema alikuwa msibani wakati watekaji wanatimiza azma hiyo.

“Nilipokuwa msibani na mwanangu, usiku wa manane nilipigiwa simu na kuambiwa mtoto wa jirani Pendo amechukuliwa na watu wasiojulikana … nilishtuka na kuishiwa nguvu kabisa,” anasema mzee Kuya.

“Nilikuwa namfahamu sana Pendo maana amekuwa akicheza hapa kwangu na wajukuu zangu, kutoonekana kwake kumetufanya tukose raha lakini tukiamini Mungu ipo siku watamuona tu,” anasema.

Mzee Kuya anasema licha tukio hilo kushughulikiwa na kikosi kazi cha polisi, naye amefanikiwa kuisaidia polisi kwa kuwekwa mahabusu kutokana na tukio hilo.

Hata hivyo, anasema hafahamu kwa nini mtoto huyo ameibwa kwani hajawahi kusikia kijijini hapo kutokea kwa matukio kama hayo kwa miaka yake yote aliyoishi.

Kwa upande wake, Ngollo Maduka (50), jirani wa alipokuwa akiishi mtoto Pendo na wazazi wake, anasema anashikwa na hofu kubwa akimkumbuka mtoto huyo kutokana na jinsi walivyokuwa wakiishi naye na kucheza na wajukuu zake.

“Hatuamini kama tumempoteza Pendo, lakini naamini vyombo husika vitafanya kazi zake kiufasaha kuhakikisha wanafahamika na kufikishwa katika sheria wahusika wote wa tukio hilo bila upendeleo,” anasema Ngollo.

VIONGOZI WA DINI
Mwinjilisti Hagai Mkumbo wa kanisa la AICT Ndami, kiongozi wa kanisa alilokuwa akiabudu mtoto Pendo na wazazi wake anasema:

“Pendo amekuwa mshirika wetu tangu wazazi wake wahamie hapa, tena walikuwa katika mafundisho ya ubatizo…tumehuzunika na kusikitishwa sana baada ya kusikia tukio hilo.”

Anasema baada ya kupata taarifa ya watu kumuiba Pendo, kanisa lilifunga na kuomba kwa ajili yake ili Mungu asaidie kupatikana kwake, na wanaamini atapatikana.

Anasema wakati wa tukio hilo, baadhi ya waumini walienda nyumbani kwao kutoa msaada ingawa ilikuwa ngumu kuonana na mama yake kutokana na kuwapo na polisi wengi waliokuwa wakilinda eneo la nyumba yao.

Hata hivyo, anasema walipopata taarifa ya kuhamishwa mama Pendo nyumbani kwake, walifarijika na kumshukuru Mungu.

Mkumbo anasema tangu limetokea tukio hilo, limekuwa likiwaumiza na kuwakosesha amani, ingawa wanaamini Mungu ataingilia kati jambo hilo na kuweza kupatikana kwake.

David Mashimba ambaye ni mzee wa kanisa hilo, anasema walikuwa wakihitaji kupata mawazo ya Pendo na mama yake, lakini wamekosa hilo na kubaki kutafakari zaidi.

“Walikuwa wameanza mafundisho kwa ajili ya kubatizwa, lakini shetani amechukua nafasi yake kwa kuwaondoa katika nyumba ya Bwana,” anasema Mashimba.

MKUU WA MKOA
Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, baada ya tukio hilo alitembelea kijiji cha Ndama kilichopo tarafa ya Mwamashimba wilaya ya Kwimba na kuzungumza na wananchi wake.

Mulongo alitaka kuwafahamu hatua iliyofikiwa na viongozi na wananchi katika kuwabaini waliotenda unyama huo kwa mtoto Pendo.

Anasema tukio hilo linasikitisha kwani halijawahi kutokea tangu 2007 wilayani humo wakati lilipomkumba mwananchi mmoja wa wilaya hiyo akisafiri kwenda mkoani Shinyanga kwa shughuli binafsi.

“Kiburi cha watekaji kimo humu humu haiwezekani mtu kutoka mbali aje atekeleze tukio kijijini bila yakuwa na wenyeji, lazima kuna mtu ama watu walioshirikiana na wahalifu hao. Mbona mifugo inapoibiwa hupatikana, iweje mtu asipatikane,” anahoji Mulongo.

Hata hivyo, Mulongo pamoja na kutoa siku tano kwa waliofanya tukio hilo kupatikana, laini siku hizo zimeisha huku jeshi la polisi likiendelea kuwachunguza waliokamatwa kwa tuhuma hizo akiwamo baba mzazi wa Pendo, Emmanuel Shilinde.

MWENYEKITI WA ALBINO MWANZA
Mwenyekiti wa chama cha watu wenye ulemavu wa ngozi mkoani Mwanza, Alfred Kapole, amesema chama kinasikitisha kuona wanadamu wakiwaua wenzao kama wanyama na bila woga wowote.

“Inasikitisha kuona miongoni mwa kesi 72 zilizopo mahakamani, ni tatu tu ndizo zilizotolewa hukumu, lakini zingekuwa kesi ya wanasiasa kama wabunge wanashindana masuala ya uchaguzi wangetoa hukumu muda mrefu. Lakini si kwa walemavu wa ngozi,” anasema Kapole.

Anasema hata kama wanadamu wanashindwa kutoa hukumu, Mungu atawahukumu na kutoa maandikio katika kitabu cha Biblia Takatifu, Mika 3.3-7, kinachoelezea hukumu watakayopata watu walao nyama za watu bila woga. 

Mwenyekiti Kapole amewaomba wasamaria wema wanaofahamu alipo Pendo wamrejeshe ama hata kama wamemdhuru basi mwili wake upatikane kwa ajili ya matanga na waliotenda jambo hilo wahukumiwe.

UNDER THE SAME SUN
Mkurugenzi mtendaji wa shirika la kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), Under the Same Sun (UTSS), lenye makazi yake Canada, Peter Ash, ameshangazwa na vyombo vya dola kushindwa kuwakamata wanunuzi wa viungo vya albino licha ya kutajwa na waganga na wauaji.

Ash anasema viungo vya albino vinanunuliwa kwa bei kubwa ambayo mwananchi wa kawaida hawezi, lakini vyombo vya dola vinapowakamata wauaji na kuwahoji wanaelekezwa waliowatuma, bado vyombo vya dola vinashindwa kuwakamata.

“Inashangaza kuona licha ya kukamatwa kwa waganga ama wapiga ramli na wauaji wa albino, wakihojiwa na kuwataja wanaowauzia, wanashindwa kuwachukulia hatua…hali hii ni mbaya kwani bila jamii kusimama yenyewe ‘mchezo’ huo utanedelea,” anasema Ash.

POLISI MWANZA
Awali akizungumza na NIPASHE, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola, amesema kikosi kazi cha polisi kinaendelea na kazi ya upelelezi ili kuhakikisha waliotenda unyama huo wanapatikana.

“Tuliwakamata watu 15 akiwamo baba wa mtoto Pendo, Emmanuel Shilinde, lakini katika mchujo uliopitishwa ni watu wanane wanaoshikiliwa na jeshi hilo mpaka sasa,” anasema Mlowola.

Anasema pia jeshi hilo limefanikiwa kuinasa pikipiki (bodaboda) iliyotumika kufanya unyama huo.

“Mlowola anasema licha ya kuendelea kuwahoji watu hao, lakini huo siyo mwisho kosa la jinai kutokana na kutokuwa na mwisho hata baada ya miaka 20 tukio hili litaendelea kuchunguzwa.

Aidha, amewataka wananchi kuendelea kufanya ushirikiano na polisi kwa kile wanachofahamu kuhusiana na kuibiwa Pendo huku akisisitiza jeshi lake likitangaza dau la Sh. milioni 3 kwa atakayefanikisha kupatikana kwake. 

Pendo ni miongoni mwa albino 74 waliopo wilayani Kwimba, huku akiwa namba tisa katika suala la kupatiwa ulinzi.

TAKWIMU
Takwimu za kimataifa zinaonyesha kuwa ni asilimia mbili  tu ya watu ambao huzaliwa na ulemavu wa ngozi ndiyo wanaosherehekea miaka 40 ya kuzaliwa kwao, huku takwimu hizo zikionyesha nchi za Afrika ni mtu mmoja kati ya 2,000 huzaliwa wakiwa albino wakati Marekani mtu mmoja kati ya 17,000 huzaliwa na ulemavu wa ngozi.

Mauaji ya albino nchini yanaonekana kukithiri zaidi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kutokana na imani za kishirikina, yakifuatiwa na mauaji ya vikongwe tangu yaliposhamiri mwaka 2006/07.

CHANZO: NIPASHE


Previous Page Next Page Home