Sunday, February 15, 2015

SAUTI YA NYIKANI KWIMBA ……….. (1)




























NA AKIDA MAJENGA.
Nilipokuwa nyumbani ngudu mwishoni mwa mwaka jana nilifanya udukuzi na kutizama hali ya mambo ya kisiasa wilayani.Inatosha kusema mbegu ya mwamko imepandwa,mwamko wa wakazi wa wilaya kuacha kupelekwa na historia na wao kuamua kusema kulingana na matakwa yao,la muhimu ni matunzo ya mbegu hiyo mpaka kukua kwake na kuashiria mwanzo mpya wa wilaya ya kwimba katika namna ya tofauti ,moja kati ya wilaya za mwanzo kabisa mkoani mwanza lakini yenye maendeleo hafifu yanayokwenda sege mnege.
Ni mwamko mpya kwa maana ya mageuzi ya ushindi wa kitongoji cha ngudu mjini kwa umoja wa UKAWA kupitia chadema, kwamba eneo ambalo ndiyo kiungo cha wilaya nzima kisiasa la ngudu mjini lipo chini ya chama cha upinzani na kwamba inafahamika ushawishi wa ngudu mjini una nafasi katika kuchagiza mageuzi kwa eneo la wilaya nzima.Ushindi huo ni mwamko kwa wananchi wengi kwamba mageuzi yanawezekana na maisha yakaendelea.
Japo kuna nadharia niliambiwa kwamba kupoteza nafasi kwa chama tawala kwa ngudu mjini katika uchaguzi huo wa vitongoji kunachangiwa na tabia ile ile ya chama tawala kupenda kung’ang’ania wagombea ambao hawana mvuto kijamii,na kwamba kama ccm ingekuwa imechanga karata zake vyema labda mambo yangekuwa tofauti.kwa minajiri ya mipango ya baadaye kwa UKAWA na CCM kuna ukweli kwenye hili.
Lakini la muhimu zaidi ni kwamba tunapata funzo gani hasa vijana kizazi kipya kutokana na hali hii ya mambo wilayani kwetu na ukiashiria kwamba kipenga cha mbio za ubunge na udiwani kimatendo kimepulizwa wilayani na tayari watu wazima wapo bussy. Nimesikia habari za bwana mansuri kutetea kiti chake,bwana Nape Nauye katibu mwenezi cha ccm taifa anatajwa kuwania nafasi hiyo pia,sina uhakika na Bi.Leticia Nyerere kurejea katika kugombea nafasi hiyo kulingana na mteguko wake kisiasa wakati wa bunge la katiba na chama chake.
Mwingine ni mwalimu mahewa anatajwa kuwania nafasi hiyo na watu wengine kadha wa kadha ambao kutokana na uchache wa muda sikufanikiwa kufahamu,japo kuna jambo lilinistua kwamba mbunge wa zamani na ninayemuheshimu sana ana mpango wa kugombea ubunge tena.washauri wake waongee naye nadhani nyakati zimepita sana.
Nimejaribu kuwataja wagombea wa chama tawala cha ccm zaidi kwa nafasi ya ubunge sababu naamini kitakwimu na kimfumo mgombea ambaye atapitishwa na chama hicho ndiye mwenye nafasi kubwa ya kushinda, hii ikichangiwa na ukweli kwamba Mgombea pekee toka UKAWA Bi. Leticia Nyerere ambaye kwa maoni yangu ndiye alikuwa na nguvu na ubavu wa kupambana na chama cha ccm wilayani kwimba aliteguka msimamo wakati wa bunge la katiba na kumuacha na ‘walakini ‘ wa kisiasa na kufanya kupoteza mvuto wake ambao aliujenga kwa muda mrefu.
Ifahamike pia kitakwimu kulingana na uchaguzi uliopita wa vitongoji ni kwamba UKAWA walipata asilimia 20% ya viti vyote na CCM asilimia 80% ya viti vyote kiwilaya,hivyo kimantiki CCM ndiyo wana nafasi kubwa ya kushinda ubunge kuliko UKAWA ila Udiwani upinzani wanayo nafasi pia(nipo tayari kusahihishwa).
Hivyo basi kwa minajiri hiyo nitawajadili zaidi chama cha CCM katika nafasi ya ubunge kwa kuwaangalia wagombea wote wanaotajwa kuwania nafasi kupitia chama tawala wilayani na baadaye nitaoanisha nguvu za kila mgombea na mahitaji ya wilaya ili kuweza kuona nani anafaa kubeba jahazi kwa maendeleo ya wilaya.Katika nafasi ya Udiwani nitawajadili UKAWA pia na nitasisitiza vijana siyo katika UKAWA tu bali pia katika chama tawala ccm wajitokeze kubadili historia.
Katika ukawaida wa mambo mwenye nguvu kwa sasa na kwa jicho la haraka ni Ndugu Mansouri ambaye anatetea kiti chake.Huyu ana nguvu mbili au tatu,kwanza ni wazi ana nguvu ya pesa kama ambavyo chaguzi nyingi Afrika hasa zikihusisha tabaka la watu maskini na hohehahe watu huchangamkia pesa kwanza,nguvu ya pili ni kwamba anatetea nafasi yake na hivyo chama kinawiwa kumlinda zaidi badala ya kuleta mwingine vinginevyo wathibitishe udhaifu wake wa kumuacha , na tatu amejibebesha agenda ya kuleta ngudu maji ya ziwa victoria.
Kwa ambao hamfahamu mji wa ngudu sasa maji ni masaa 24 toka mradi mkubwa wa maji ya ziwa victoria,ifahamike maji ya ziwa victoria ni mradi wa taifa zima na uliasisiwa toka zama za Edward lowasa ni waziri wa maji. Udhaifu mkubwa wa bwana mansouri ni kwanza anategema pesa kushinda,pili mfumo ambao ulimsaidia kuingia madarakani unamaliza ngwe yake na hivyo kurejea kwake ama la kunategemea na nguvu ya mgombea urais kwa ccm awamu hii kama itambeba pia,vinginevyo na yeye pia anaweza kushindwa kutetea kiti chake.
Nguvu za bwana mansouri haziendani na mahitaji ya wanakwimba kwa sasa na hata baadaye labda abadili sana taswira yake na sera zake,lakini kwa uchache wake ni kwamba haitawahi kutokea apiganie maendeleo ya wanakwimba kwa dhati kabisa ya uvungu wa moyo wake,kipaumbele chake ni biashara zake za mafuta na wala si maendeleo ya wanakwimba.
Nape Nauye katibu mwenezi ccm taifa anatajwa pia kuweka nia kugombea ubunge wilayani kwimba,japo kuna hadidu za rejea nimezipata pia ameweka nia hiyo kwenye jimbo la Mh.Bernard Membe waziri wa mambo ya nje ambaye anatajwa kugombea nafasi ya urais,ni katika jimbo la mtama mtwara,nadhani kwa sasa anapima upepo na joto la kisiasa kati ya pande hizo mbili japo binafsi naamini kama ana nia kweli atagombea ngudu,maana kusini kuna joto na hasira ya kisiasa hasa masuala ya gesi, hali si rahisi kwa mtu kuanza kwa mara ya kwanza katika purukushani kama hiyo.
Nguvu ya nape ni kwamba anazifahamu siasa za Tanzania,ni rahisi kupambana nazo hasa kwa eneo kama ngudu ambalo bado halina wabishi wa kisiasa,pili anaweza kushinda uteuzi kama ataungana na kambi ya mgombea urais wa kiti cha ccm awamu hii imbebe katika harakati zake hizo,uzuri mwingine wa nape ni kijana na anaongea lugha moja na vijana wenzake,wakati fulani nilionana naye Dodoma akiimba na kupiga vyombo vya mziki katika bendi ya Dodoma mjini wakati wa uzinduzi wa website ya chama chao,hivyo kwa maisha yake ni rahisi kumtafuta na kuonana naye.
Udhaifu wa Nape ni ule ule wa vijana viongozi,atapenda atutumie wanakwimba kupata madaraka ya juu kama uwaziri na kusahau agenda ya kusaidia wanakwimba maana bado ana ndoto za uongozi katika taifa hili kwa anavyoonekana.
Mgombea mwingine ni Ndugu Mahewa,ni mwalimu wangu na ninamheshimu sana kwani alinifundisha akiwa field muda fulani nikiwa darasa la saba shule ya msingi Ngudulugulu.Wakati naondoka ngudu baada ya likizo kurejea dar nilimuacha katika harakati za kutetea nafasi ya mwenyekiti CWT,sifahamu matokeo yake.Mwalimu mahewa na kama washauri wake wapo karibu au wanasoma hapa,wanafahamu ana tatizo moja tu tangu akiwa mwalimu wangu,wazungu wanaita SUPERIORITY COMPLEX au tuseme OVER-CONFIDENCE,maana nakumbuka muda fulani wakati anakuja darasani kutufundusha alikuwa kabla hajafanya lolote ni lazima anyanyue dawati la sehemu ya mwalimu juu kama mara tano au apige pushapu mbele ya wanafunzi ndiyo aanze kufundisha.
Kwa masimulizi ya watu wa ngudu bado shida ya mwalimu mahewa ni hiyo hiyo,kujiamini kupita kiasi katika mambo ambayo yanahitaji usawa wa kawaida .Kama washauri wake wangekuwa wanaweza kumshauri mwalimu mahewa ,ni kwamba ana nguvu na mtaji mkubwa sana kisiasa wilayani kwimba labda tofauti na wagombea wengine wote,unapokuwa mwenyekiti wa walimu wote wilaya unakosa nini? Tiketi yako kubwa ni kufanya kazi kwa juhudi,maarifa na kupigania haki za walimu wako ili wawe mabalozi katika kila kona ya wilaya na walibebe jina lako vyema na kufanya ujilikane kila mahali,sidhani kama mtaji wa walimu anaufahamu.kama ameshinda uenyekiti wa CWT kwa mara nyingine naomba afikishiwe salamu za mtaji huu na kama ana nia kweli ya kuwa mgombea wa wilaya.Ila kama la walimu tu litamshinda sidhani kama kwa nafasi ya ubunge ataweza.
Sasa tujiulize swali,unadhani ili wilaya ya kwimba iendelee inahitaji nini hasa? Naomba tufahamu ukweli wa mambo,mawaziri au wizara za Tanzania au serikali kuu haziwezi kuendeleza wilaya ya kwimba,zitatoa mwongozo tu ila kazi kubwa inabaki kwa wanakwimba wenyewe.Kwimba inaendelezwa na mtu ambaye anaweza kuja akatia pressure kwenye HALMASHAURI YETU YA KWIMBA na WATENDAJI WAKE huku sisi wananchi tukimsaidia.Mtu ambaye atapambana na watendaji wachovu wa wilaya ya kwimba awaamshe wafanye kazi, wawe wabunifu,wakifanya mipango itekelezeke na siyo leo wanapima eneo na wanahamisha stendi ya wilaya na kesho wenye magari wanajichagulia stendi yao wenyewe eneo la hospitali na wanaachwa tu.watendaji uchwara ambao wanatangaza kupima maeneo ya ardhi watu wapewe hati za viwanja na inapita miaka miwili hawajafanya kitu na hakuna anayehoji wala kuwapa pressure,tungepata hizo hati si tungekopa hata benki tukaendelea.
Tunataka mtu wa kuwatia pressure wakuu wa mashule na maofisa elimu,wanafunzi wakawa na malengo mapana ya kujisomea na siyo kwamba leo ukifika Ngudu Sec haufahamu ni muda gani watoto wanajisomea na muda gani wapo mapumziko,wilaya nzima ni “zunzaga zunzaga”,tunahitaji kiongozi wa kuwatia pressure vijana wa ngudu wasimsubiri Emmanuel kasalali karejea ngudu wamuombe pesa ila wajiajili katika kilimo na ufugaji,ufundi seremala na uashi,tunahitaji kiongozi wa kutia pressure waganga wa hospitali za wilaya kwamba kwanini madawa hayaonekani hospitali lakini katika maduka binafsi dawa haziishi?
Kihistoria dunia nzima,uongozi katika ngazi yeyote iwe familia,shule,kijiji,wilaya,wizara au taifa lazima kiongozi mkubwa uwe na uwezo wa kuwatia pressure na kuwauliza watu wawajibike kulingana na nafasi na majukumu yao. Binadamu wote tuna hulka mbaya ya kujisahau na bila kukumbushwa na kuwajibishwa hakuna ambalo tunafanya.Ndivyo alifanya Waziri mama na chuma wa uingereza Bi Magreth Thatcher,ndivyo alifanya Nyerere na Mkapa,ndivyo anafanya mwakyembe na Magufuli. Katika dunia ya leo maendeleo unajiletea mwenyewe na watu wa Kwimba wanapaswa kufahamu ukweli huu,hakuna mtu anakuletea maendeleo,ana pesa kiasi gani akujengee barabara? ila mtu anaweza kuja kusimamia shughuli za maendeleo, na ndiyo wajibu wa wabunge,madiwani na vitongoji kuwasimamia watendaji na kuwapa pressure.
Huu ndiyo wito wangu kwa watu wote wa kwimba na hasa vijana,tunahitaji mtu ambaye ana nguvu ya kututia pressure watu wote kuanzia mkurugenzi wa wilaya,watendaji wake na wananchi kwa ujumla. Unadhani kati ya wagombea niliowajadili hapo juu kuna hata mmoja mwenye sifa hizo? Kuwa sehemu ya mabadiriko ambayo wewe ungependa uone.
1.Katika makala yangu wiki ijayo,sehemu ya pili nitaeleza vijana ambao bado hawana majina kisiasa ila wana nia safi za kiuongozi wafanye nini? Nitaeleza kwa nini vijana wajitokeze nafasi ya udiwani zaidi badala ya ubunge,mfano Ashrafu Omary toka UKAWA (CHADEMA ) alivyo na nafasi ya kushinda udiwani ngudu mjini.
Angalizo langu ni kwamba vijana mnapopata uongozi lazima muonyeshe utofauti na kujituma dhidi ya kile ambacho mlikuwa mnakilalamikia, anayetakiwa kuanza ni Casmiry na tumsaidie.Niombe radhi kama kuna mtu nitamkwaza kwa uandishi wangu,ila naomba tufahamu kwamba ukichagua kuwa kiongozi wa umma,umekubali watu wajenge hoja juu yako na kwa kutaja majina yako kama mimi ninavyofanya hapa,hoja ijibiwe kwa hoja na wachangiaji watumie lugha ya staha kupata wito bora kwa kwimba.Kila la heri..WAKATABAHU!

No comments:

Post a Comment

Previous Page Next Page Home