Ndugu waandishi wa
habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari, ninayo furaha kubwa kuwakaribisha
katika ofisi za Baraza. Lengo la kuwaita hapa leo ni kuwapa taarifa juu ya
maamuzi yaliyofikiwa na Baraza ikiwa ni katika jitihada za kuinua ubora wa
elimu ya ufundi nchini.
Ndugu Waandishi wa
Habari
Baraza la Taifa la Elimu
ya Ufundi ni chombo kilichoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Sura ya 129, kwa lengo
la kusimamia na kuratibu taaluma zinazotolewa na taasisi na vyuo vva elimu ya
ufundi nchini, ambavyo siyo vyuo vikuu au vyuo vikuu vishiriki. Jukumu kubwa la
Baraza ni kuendeleza na kuinua ubora wa elimu ya ufundi nchini kwa kusimamia
kikamilifu shughuli za kuendesha mafunzo ili tuzo zinazotolewa na taasisi na
vyuo ziwe na ubora unaokubalika kitaifa na kimataifa.
Kwa kutumia Sheria na
Kanuni za Baraza za Usajili (2001) na zile za Ithibati na Utambuzi (2001),
mnamo tarehe 20 Februari 2015, Baraza lilitoa notisi ya siku 30 kwa taasisi na
vyuo vilivyokiuka taratibu na vyenye mapungufu makubwa ya Usajili na Ithibati kupitia
taarifa yake kwa Umma. Notisi hii ililenga kuzipa taasisi na vyuo nafasi ya
kujirekebisha.
Baraza linakiri kuwa
taasisi na vyuo vingi kama vilivyoorodheshwa kwenye Jedwali Na. 1, Jedwali Na.
3, na baadhi kwenye Jedwali Na. 5 vimechukua hatua mbalimbali za kurekebisha
mapungufu yaliyojitokeza. Hata hivyo, hadi kufikia leo tarehe 24 Juni 2015
yaani siku 124 baada ya Notisi ya Baraza, kuna vyuo ambavyo havijachukua hatua
yoyote ya kurekebisha mapungufu yake kama inavyooneshwa kwenye Jedwali Na. 2 na
Jedwali Na. 4.
Tamko la Baraza
Kutokana na mapungufu
hayo Baraza limeamua kuchukua hatua kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zake kwa
taasisi na vyuo vyote vilivyoorodheshwa katika Jedwali Na. 2 na Jedwali Na. 4
kwa makosa yafuatayo:
a) Ama
kumalizika kwa muda wa Usajili wa Awali (Preparatory Registration) na
Usajili wa Muda (Provisional Registration); au
b)
Kutoanza mchakato wa kupata Ithibati baada ya kupata Usajili Kamili; au
c)
Kumalizika kwa muda wa Ithibati na kutochukua hatua ya kuomba upya Ithibati
(re-affirmation); na
d) Taasisi
na Vyuo kuamua vyenyewe kusitisha kutoa mafunzo kwa sababu mbalimbali.