OFISI
YA WAZIRI MKUU TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
OFISI
YA MKUU WA MKOA WA MWANZA TAARIFA KWA UMMA TAREHE 18/11/2015
Ndugu
Wanahabari.
Mkoa wa Mwanza kwa kawaida hupata misimu miwili ya
mvua kwa mwaka. Misimu hiyo ni ya mvua za vuli na masika ambapo mvua za vuli
huanza kunyesha mwezi Septema/Oktoba hadi kufikia mwezi Januari; na msimu wa
mvua za masika hunyesha Kuanzia mwezi Machi hadi Mei ya kila mwaka. Wastani wa
mvua ni mm 720 hadi mm 1200 kwa mwaka ambazo hutawanyika kati ya mm 570 mm kwa
mwaka hadi mm 1800 kwa mwaka.
Ndugu
Wanahabari.
Mkoa wa
Mwanza unatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani kwa maana ya mvua
za juu ya wastani wa mm 1300 katika kipindi hicho cha Oktoba – Desemba, 2015.
Hii ni kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Kwa kuzingatia utabiri huo wa hali ya hewa,
tunawashauri wakulima na wananchi katika Mkoa wa Mwanza kufanya yafuatayo:-
Kulima mazao ya chakula aina ya wanga yanayohitaji
au kustahimili mvua za wastani hadi mvua za juu ya wastani na pia kukomaa kwa
muda mfupi kiasi cha kuweza kukomaa kufikia mwezi Desemba, 2015/Januari, 2016.
Mkazo zaidi utiliwe kwenye mazao ya:-
Viazi vitamu hasa mbegu (Variety) zisizolikishwa
(Non-Orange Fortified) aina ya Polista na Ukerewe, “Kishiga Mdege” na
matembele; pamoja na mbegu zilizolikishwa (Orange Fortified) kama Ejumla,
Karotoda na Kabode.
Mazao mengine ni mahindi hasa katika ukanda wa mazao
(agro-ecological zone) unaopata mvua za wastani wa mm 1100 hadi 1200 kwa mwaka
au Zaidi ukanda ambao unajumuisha Tarafa za Ukara na Ilangala katika Wilaya ya
Ukerewe na Tarafa za Kahunda na Buchosa katika Halmashauri ya Wilaya ya
Buchosa. Aina ya mbegu (variety) za mahindi zinazopendekezwa ni:-
(i) Aina ya mbegu ya mahindi chotara (hybrid) ni
pamoja na SeedCo yenye alama ya pundamilia (SC 513), Pannar inayokomaa kwa muda
mfupi (PAN 4M-19) na kati PAN 15), Delkab (DKC 8053).
(ii) Aina ya
mbegu ya mahindi isiyochotara/ya chavua huria (OPV) ni pamoja na Kilima, Stuka,
TAN 600H, Kitale na TMV 1. Mpunga hususan mbegu aina ya SARO 5 (TXD 306) na
Supa inayolimwa mabondeni (low land rice); na NERICA 2 na 4 zinazolimwa nchi
kavu.
Ndugu
Wanahabari.
Tunawashauri wananchi wetu kutenga fedha na kununua
pembejeo za kilimo hasa mbegu, mbolea na dawa za kilimo mapema kwa kuzingatia
kuwa matumizi ya pembejeo yanaweza kuongezeka kutokana na mvua hizo ambazo
zinaweza kusababisha kuoshwa ama dawa za kudhibiti wadudu waharibifu na
magonjwa au mfumuko wa magonjwa hasa ya ukungu kutokana na mazingira ya
unyevunyevu mwingi katika ardhi na hewani. Aidha, pembejeo zinaweza kupanda bei
na kuwa adimu kutokana na kutopatikana kwa wingi na kwa urahisi kwa sababu ya
mvua kuharibu miundombinu ya barabara hasa katika maeneo ya vijijini na
kuathiri usafirishaji mazao. Ili kupunguza gharama za uzalishaji kutokana na
mvua, wakulima wanaweza kugawanya kiasi cha mbolea kinanchohitajika kwa eneo na
kuweka kwa awamu lakini pia tunawashauriwa kuwatumia Maafisa Ugani katika
Wilaya.
Vilevile tunawashauri wakulima kulima kwa kukinga au
kuzuia mmomonyoko wa udongo kutokana na mvua hasa katika maeneo yenye miinuko
na vilima. Mmomonyoko wa udongo unaweza kukingwa au kuzuiliwa kwa kutumia mbinu
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulima kilimo cha matuta kwa kukinga/kukata
mteremko, kulima na kuacha mistari (strip) ya nyasi au kufanya kilimo hifadhi.
Zaidi, wakulima katika maeneo yanayo hifadhi unyevu kwa wingi au kutwaamisha
maji (mabonde) wanaweza kulima kwa kufuata uelekeo wa maji kwa kuacha mistari
ya nyasi kuzuia mmomonyoko wa udongo au kulima kilimo hifadhi kinachopunguza
ukwatuaji wa udongo.
Ndugu
wanahabari.
Tunawashauri wananchi kujiwekea akiba ya chakula
hasa cha aina ya wanga kutokana na sababu kwamba mvua zinazotarajiwa katika
kipindi hicho cha Oktoba na Desemba, 2015 zinaweza kuharibu miundombinu ya
barabara na kusababisha ugumu wa usafirishaji wa vyakula hivyo kuleta uhaba wa
vyakula katika masoko. Msisitizo wa kujiwekea akiba ya chakula unatolewa Zaidi
kwa kuzingatia ukweli kwamba, Mkoa wa Mwanza wenye wakazi 2,772,509 huhitaji
jumla ya Tani 708,376 za chakula aina ya wanga kwa mwaka mzima, ambapo, katika
msimu wa kilimo wa 2014/2015 Mkoa ulizalisha Tani 495,863.2 za chakula aina ya
wanga hivyo kuuwezesha kujitosheleza kwa 70% tu kwa chakula aina ya wanga.
Aidha, tunahimiza wafanyabishara kuleta chakula
kutoka kwenye maeneo yenye ziada ya chakula aina ya wanga , lakini pia wananchi
kutumia chakula kwa umakini na kuuza sehemu ya mazao ya biashara na mifugo ili
kuweza kununua chakula. Aidha, Mkoa unasisitiza kuwa wafanyabiashara
walioidhinishwa kununua na kuuza chakula kutoka katika maghala ya Wakala wa
Taifa wa Hifadhi ya Chakula Sumbawanga kufanya hivyo kwani mkoa umeutengewa
jumla ya Tani 5,400 za mahindi kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa nafaka
katika masoko ya Mkoa wa Mwanza hii nikutokana na tathmini iliyofanywa na
wadau.
Ndugu
wanahabari
Kupitia kwenu
tunawaomba wananchi kujiwekea akiba ya chakula aina ya wanga katika ngazi ya
kaya, kwa kuzingatia kuwa wastani wa watu katika kaya ya watu 6 katika mkoa
wetu, tunawashauri kuhifadhi magunia 3 ya mahindi yenye uzito wa kilo 100
lakini pia magunia 5 ya muhogo mkavu yenye uzito wa kilo 60 kila moja sawa na
kilo 314.64 katika kipindi cha Novemba 2015 na Januari 2016 endapo kaya hiyo
itatumia mahindi au muhogo kama chakula cha wanga katika kipindi hicho.
Kwa upande wa
wakulima wanaotumia miundombinu ya umwagiliaji katika
Skimu ya Umwagiliaji Mahiga kwenye Wilaya ya Kwimba tunawashauri kuchukua
tahadhari kwani mabwawa yanaweza kukatika kutokana na mvua zinazotarajiwa na
inaweza kusababisha mmomonyoko wa udongo, kusombwa mazao shambani, kukosa maji
ya kumwagilia, kuongezeka kwa gharama za ukarabati wa mabwawa na hata kupoteza
maisha ya watu na mali zao.
Mwisho
wakulima na wananchi kwa ujumla tunawashauri kuchukua tahadhari dhidi ya
madhara yanayoweza kusababishwa na mvua zinazotarajiwa na kuzitumia vizuri mvua
hizo katika kuzalisha mazao yanayopendekezwa ili Mkoa uzalishe chakula cha
kuutosheleza katika msimu wa 2016/2017. Mara baada yakusema hayo niwashukuru
sana kwakuja lakini zaidi sana kuweza kuchukua taarifa hii na kutufikishia kwa
umma wa watanzania kupitia vyombo vyenu vya habari.
Mungu Awabariki Sana , Ahsanteni kwa
Kunisikiliza!
Chanzo:HAPA