Friday, April 22, 2016

DIWANI JONATHAN MALIFEDHA NA KATA YA NGUDU

Mgombea wa CCM ngazi ya udiwani ndugu Jonathan Malifedha akiwa jukwaani kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana 2015
BY NGUDU NYUMBANI BLOG.
23/04/2016

Kata ya NGUDU ni mojawapo ya kata 15 zinazounda jimbo la KWIMBA, ambapo halmashauri ya wilaya inaundwa na majimbo mawili ya uchaguzi, Kwimba na Sumve na kila jimbo likiwa na kata 15.

Unapozungumzia wilaya ya KWIMBA ni lazima uzungumzie kitovu cha wilaya, makao makuu ya wilaya na picha au muonekano halisi wa wilaya ndipo utagundua NGUDU ndiyo inabeba sifa zote hizo. Ngudu kama tarafa inayounganisha maeneo kadhaa ya kata, pia ni kama kata inayounganisha maeneo kadhaa ya vijiji, vitongoji n.k
Kata ya Ngudu(Mamlaka ya mji mdogo wa ngudu) Inaundwa na vitongoji kama, Chamhela, Ngudu mjini, Kakora, Igoma, Sokoni, Ngudulugulu, Budula, Bugakama, Ngumo, Shuleni,Ilamba, Kilyaboya, na Welamasonga

Makadirio ya wakazi wa kata ya Ngudu kwa mwaka jana(2015) ni watu 29,837 na idadi iliyokadiliwa kwa watu wenye miaka 18 na kuendelea ni 14,428, haya makadilio yalifanyika kwamba, kufikia mwezi October kata itakuwa na idadi hiyo. Ikumbukwe pia katika Sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2012, kata hii ilikuwa na jumla ya wakazi  27,630.
Kata ya NGUDU ina Shule za msingi kama, Budula, Chamhela, Igoma. Kilyaboya, Kakora, Welamasonga, Ngudulugulu, Ilumba na Ngumo. Kwa upande wa shule za sekondari kuna Bujiku Sakila na Ngudu sekondari

Wednesday, April 13, 2016

JUST A DEMO, ITAZAME KISHA TOA MAONI

TANGAZO MAALUM VIJANA WA KUJITOLEA 2016-JKT


Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, anawatangazia vijana wenye sifa za kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa kujitolea kwa mwaka 2016.
Barua zilizoainisha sifa za kijana kujiunga na mafunzo ya JKT zimetumwa kwa Waheshimiwa Wakuu wa mikoa. Mchakato wa zoezi la kuwapata vijana wenye sifa unaanza Aprili 2016 hadi tarehe 20 Mei 2016.
Sifa za mwombaji ni kama zifuatazo:-
1. Awe raia halisi wa Tanzania.
2. Umri. Kwa vijana wenye elimu ya Darasa la saba hadi kidato cha sita ni miaka 18 hadi 23.Vijana wenye elimu ya Stashahada umri ni miaka 18 hadi 26 na Vijana wenye elimu ya Shahada na kuendelea umri ni miaka 18 hadi 30.
3. Awe na afya njema, akili timamu.
4. Asiwe na alama yeyote ya michoro mwilini (Tattoo).
5. Mwenye tabia nzuri, hajapatikana na hatia Mahakamani na hajawahi kufungwa.
6. Kwa vijana waliomaliza elimu ya Sekondari kidato cha nne wawe waliomaliza kuanzia mwaka 2010, 2011, 2012, 2013 na 2014 wenye ufaulu ufuatao:-
      (a) Waliomaliza 2010 hadi 2012 wawe wamefaulu na wawe na alama (Points) zisizopungua 32.
      (b) Waliomaliza 2013 wawe wamefaulu na wawe na alama (Points) zisizopungua 38.
      (c) Waliomaliza 2014 wawe wamefaulu na wawe na GPA isiyopungua 0.6.
7. Awe na elimu ya msingi aliyehitimu darasa la saba.
8. Awe na cheti halisi cha kuzaliwa (Original Birth Certificate).
9. Awe na cheti halisi cha kumaliza shule (School Leaving Certificate)
10. Awe na cheti halisi cha matokeo (Original Academic Certificate/Transcript).
11. Asiwe ametumikia Jeshi la Polisi, Magereza, Chuo cha Mafunzo au KMKM wala kuajiriwa na Idara nyingine Serikalini.
12. Asiwe amepitia JKT Operesheni za nyuma.
13. Asiwe amejihusisha na matumizi ya madawa ya kulevya, bangi na yanayofanana na hayo..

Waombaji wenye sifa wapeleke maombi yao kwa Waheshimiwa wakuu wa mikoa. Makao Makuu ya JKT hayatapokea na hayapokei maombi yoyote, kwa vijana watakaoomba nafasi hizo wazingatie maelekezo yatakayotolewa kuepuka usumbufu.


Imetolewa na:
Kurugenzi ya Habari na Uhusiano
Makao Makuu ya JKT
Tarehe 05 Aprili 2016


Sunday, April 10, 2016

WADAU WAFUFUA MATUMAINI YA WANYONGE MAGU

UKOMBOZI wa wananchi masikini na wazee wilayani Magu, Mwanza umeanza kuonekana baada ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf III), Shirika la Maperece na Jeshi la Polisi kuunganisha nguvu za kuwaondolea madhila yanayoyakabili katika jamii.
Taasisi hizo zimepania kushirikiana kwa hali na mali katika kuyakomboa makundi hayo ya jamii kiuchumi, kiafya na kiusalama kwa dhana ya kuyafungulia ukurasa mpya wa maisha bora.

Katika juhudi hizo, Tasaf III  imeyaidhinisha makundi hayo kwenye mpango maalumu wa kutambuliwa, kuthaminiwa na kuwezeshwa kupata mahitaji ya msingi ya chakula, malazi, mavazi, matibabu na elimu.

Wazee wanapewa kipaumbele cha ziada cha kuimarishiwa ulinzi dhidi ya vitendo vya uonevu, dhuluma, kujeruhiwa na kuuawa kutokana na imani potofu za kichawi zinazochochewa na waganga wa jadi, hususan wapiga ramli chonganishi.
Mkuu wa Wilaya (DC), Karen Yunus na Mbunge wa Magu, Bonaventura Kiswaga, wameahidi kuzipatia taasisi hizo ushirikiano wa dhati katika kuyaondolea makundi hayo ya jamii hali ya unyonge na vikwazo vya kufurahia maisha yao duniani.
Tasaf na kaya masikini

Mratibu wa Tasaf Wilaya ya Magu, Philip Msangi, amelieleza Raia Mwema wiki hii kwamba kaya 5,937 zimeingizwa kwenye mpango wa kuwezeshwa kujikimu katika mahitaji ya msingi ya chakula, mavazi na malazi. Pia mahitaji ya sare na vifaa vya shule kwa wanafunzi ambao wazazi wao ni walengwa wa mpango huo wa kunusuru kaya masikini.

Walengwa hao pia watawezeshwa kupata matibabu, kiingilio katika Bima ya Afya ya Jamii (CHF), kuweka akiba na kuwekeza katika miradi midogo ya uzalishaji mali kuongeza kipato cha familia na kujenga mazingira endelevu hata baada ya kuondolewa kwenye mpango huo.
Msangi anasema mpango huo umetengewa Sh bilioni 4.879 kutoka serikalini kwa kipindi cha miaka mitatu na kwamba matumizi yake yanahusisha malipo taslimu kwa walengwa na gharama za uendeshaji katika ngazi ya wilaya, kata na vijiji.
“Hadi sasa Tasaf III Wilaya ya Magu tumeshapokea shilingi 1,355,517,000 kati ya shilingi 4,879,861,200 zilizotengwa kwa ajili ya walengwa 5,937,” anabainisha mratibu huyo.
Malipo kwa walengwa hufanywa kila baada ya miezi miwili kwa ratiba maalumu ya kitaifa inayojulikana kama Dirisha la Malipo. Fedha hupelekwa vijijini chini ya ulinzi wa askari polisi na viongozi wote ngazi ya kijiji hushirikishwa kusimamia kazi ya ulipaji.
Mratibu huyo wa Tasaf anafafanua kwamba kuna ruzuku za aina mbili; ile isiyo na masharti wanayopatiwa walengwa wote 5,937 na ya masharti wanayopatiwa walengwa wenye watoto wenye mahitaji ya shule na matibabu.
“Utaratibu umeweka wa kufanya ufuatiliaji katika shule za msingi, sekondari, zahanati, vituo vya afya na hospitali kuratibu mahudhurio na maendeleo ya watoto wanaopata ruzuku ya masharti,” anasema.
Mmoja wa walengwa hao, Asha Shibugulu (61) mkazi wa Itumbili, Magu anasema “Ninapokea shilingi 40,000 kutoka Tasaf  kila baada ya miezi miwili, ambazo zimenisaidia kuanzisha biashara ya karanga inayoniwezesha kujikimu katika chakula, mavazi na kulipa kodi ya nyumba.”
Tasaf inavyowatambua wazee
Msangi anasema ingawa wazee si walengwa wa moja kwa moja, mpango wa kunusuru kaya masikini unaotekelezwa na Tasaf III unawanufaisha baadhi yao kulingana na vigezo vya umasikini na nafasi zao za uwajibikaji katika familia.
Kati ya kaya 5,937 zinazopokea ruzuku ya fedha kutoka Tasaf, 2,652 sawa na asilimia 44.6 ni za wazee, ambapo kaya za wazee wanawake ni 2,219 (83.6%) na za wanaume ni 433 sawa na 16.4% ya wazee wote wanaolengwa na mpango huo wilayani Magu.
Changamoto zilizoonekana katika utekelezaji wa mpango huo ni pamoja na wazee wengi kutokujua kusoma na kuandika, hivyo kushindwa kuendesha miradi yao kikamilifu na baadhi ya wanajamii kutokutambua umuhimu wa wazee, hivyo kuwanyima fursa zinazopatikana katika jamii.
Changamoto nyingine ni baadhi ya wazee, hasa wanaume kuwanyanyasa wazee wenzao wanawake kwa kuwanyang’anya fedha walizolipwa na Tasaf na baadhi yao kuzitumia visivyo kama vile kununua pombe.
“Lakini pia, baadhi ya wazee wamekuwa na wategemezi wengi, hivyo kufanya fedha wanazolipwa kutotosha kugharimia mahitaji ya familia zao,” anaongeza mratibu huyo wa Tasaf.
Hata hivyo, anasema Tasaf III inaendelea kuhamasisha jamii kuwathamini wazee na kutoa elimu ya ujasiliamali, uwekaji wa akiba na uwekezaji kwa walengwa wote wa mfuko huo. Pia kuhimiza ushiriki wa wazee katika shughuli za maendeleo na uzalishaji mali, kuunda vikundi vyao waweze kutambulika na kupata fursa za kufadhiliwa na wahisani.
Maperece inavyowatetea wazee
Mratibu na Mweka Hazina wa Shirika la Maperece, Julius Mwengela, anaamini kwamba masuala ya wazee yatapata ufumbuzi iwapo serikali na wadau wengine zikiwamo taasisi za kiraia zitayaingiza kwenye mipango yao ya maendeleo.
Mwengela anasema Shirika la Maperece linalotambuliwa kama kinga ya wazee linakusudia kuwafanyia wazee mambo mazuri zaidi kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano.
“Tuwaone wazee kama ni rasilimali katika jamii yetu. Sisi Maperece ni wadau wa kusukuma masuala ya wazee, tunaomba madiwani, mbunge na viongozi wa Serikali kwa jumla mtuunge mkono ili pia tuweze kutokomeza mauaji dhidi ya wazee wetu,” anasema.
Shirika la Maperece lilianzishwa mwaka 1993 na kupata usajili kamili mwaka 1994 kwa ajili ya kutetea haki za wazee chini ya ufadhili wa Shirika la HelpAge International.
Kauli ya DC, Mbunge Magu
Mkuu wa Wilaya ya Magu, Yunus, anakiri kuwa Shirika la Maperece limepanda mbegu nzuri inayozaa matunda ya kuwanasua wazee kutoka kwenye matatizo yanayowaandama katika jamii.
“Watu wengi kutoka wilaya na mikoa mbalimbali na hata nje ya nchi wanakuja Magu kujifunza namna ya kushughulikia masuala ya wazee kwa ufanisi. Maperece imeifanya Magu kuwa mfano mzuri wa kuigwa,” anasema na kuongeza: “Wazee ni suluhu ya jamii, tusiwasahau kwenye bajeti zetu kwani wana mchango mkubwa katika jamii ikiwa ni pamoja na kulea wajukuu. Tukiwatambua wazee na mahitaji yao wataishi kwa faraja.”
Kwa upande mwingine, wazee wamekuwa wakiomba kuimarishiwa ulinzi wasiendelee kuuawa kutokana na imani za kishirikina, lakini pia Sera ya Taifa ya Wazee ya Mwaka 2003 itungiwe sheria itakayowapa nguvu ya kudai haki zao.
Mbunge wa Magu (CCM), Kiswaga, anaunga mkono msukumo huo akisema; “Sheria ya wazee inatakiwa kutungwa haraka ili matakwa yao yatimizwe ikiwa ni pamoja na kulipwa pensheni jamii. Mimi hili nitalibeba, nitalipeleka bungeni ili kuwasaidia wazee wasiendelee kuishi katika mazingira magumu.”
Hoja ya kwamba baadhi ya wazee wamekuwa wakibebeshwa mzigo wa kulea wajukuu imethibitishwa na Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Magu, Coletha Sanga, akisema juhudi za kupiga vita kasumba hiyo zinaendelea. “Tunapiga vita kasumba ya watu kuwapeleka watoto wao kulelewa na babu na bibi zao vijijini, kisha wao kurudi mijini kuendelea kutafuta watoto wengine,” anasisitiza.
Juhudi za Jeshi la Polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Justus Kamugisha, anasema jeshi hilo linaendelea kukazania suala la kuishawishi jamii kuondokana na imani potofu za kuwahusisha wazee na matukio mabaya yanatokea katika jamii.
Anasema jitihada hizo zitahusisha ushirikiano wa karibu na wadau wengine zikiwemo asasi za kiraia na madhehebu ya dini ili pia kuwahimiza wanajamii kuepuka kasumba ya kujichukulia sheria mkononi.
“Tutaendelea kuimarisha vikosi kazi vyetu ili viweze kufanya kazi kwa weledi na ufanisi mkubwa katika kuwalinda wazee dhidi ya vitendo vya kushambuliwa na kuuawa,” anasema.
Mganga wa jadi azungumza
Mwenyekiti wa waganga wa tiba asilia wilayani Magu, Makoye Kanyerere, ameahidi kusimamia kwa dhati maazimio ya kuwafichua wapiga ramli ili washughulikiwe kisheria, lakini akiomba usiwepo unyanyasaji unaofanywa na askari polisi dhidi ya waganga wa jadi wasiyo na hatia.
“Niko tayari, nitashirikiana na polisi kupambana na wauaji wa wazee na albino, tutadhibiti upigaji ramli miongoni mwetu, lakini polisi nao wafanye kazi kwa haki, wasionee na kunyanyasa waganga wa tiba asilia wasiyo na tatizo,” anasema Kanyerere.
Mapendekezo ya HelpAge International
Shirika la HelAge International linaamini kwamba kukosekana kwa mipango thabiti, fedha na nguvu ya pamoja baina ya wizara na mashirika husika kunadhoofisha mapambano dhidi ya mauaji ya wazee nchini.
“Mauaji ya wazee yanachukuliwa kwa sura ya imani za uchawi, hivyo kujenga dhana kuwa haiwezekani kuyathibitisha mahakamani kama ilivyo kwa kesi nyingine,” anasema Mratibu wa HelpAge International nchini, Joseph Mbasha.
Anaendelea; “Mara nyingi viongozi wa serikali, wanasiasa na asasi za kiraia hukaa kimya wakati makosa makubwa dhidi ya binadamu kama haya (mauaji ya wazee) yanapofanyika. Lakini pia, Sera ya Taifa ya Wazee ya Mwaka 2003 imecheleweshwa kutungiwa sheria kwa miaka 13 sasa.”
Shirika hilo linapendekeza kwamba wadau muhimu wakiwamo Jeshi la Polisi, Mahakama, Usalama wa Taifa na watetezi wa haki za binadamu kuhakikisha wanakuwa na mpango maalum unaopimika wa kupambana na mauaji ya wazee.
“Mahakama zifikirie namna ya kuwa na utaratibu maalumu wa kuharakisha kesi za mauaji ya wazee na agenda ya mauaji hayo iwe ya kudumu katika vikao na mikutano, hasa maeneo yanayoathirika zaidi,” anaongeza Mbasha.
Hata hivyo, mapambano dhidi ya mauaji ya wazee yamekuwa yakikabiliwa na vikwazo mbalimbali ikiwa ni pamoja na waathirika wa matukio hayo kutokuwa tayari kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kuwabaini wahalifu husika kutokana na baadhi ya mauaji kupangwa na wanandugu/wanafamilia.
Pia kumekuwepo na vitisho vya kuuawa kwa wahanga wanaojaribu kufichua taarifa za kuwezesha kuwakamata watuhumiwa, lakini pia baadhi ya viongozi wa kijamii wamekuwa sehemu ya tatizo kutokana na wao kuamini masuala ya ushirikina.
Aidha, katika baadhi ya maeneo, hususan vijijini kumekuwepo na kikwazo cha miundombinu mibovu isiyopitika kwa urahisi, hivyo kusababisha upelelezi wa mauaji ya wazee na uhalifu mwingine kuchukua muda mrefu na kuwakatisha tamaa waathirika.
Lakini pia, kumekuwepo na kikwazo cha uelewa mdogo miongoni mwa jamii husika na wengi wao hawana imani ya dini na hofu ya Mungu. Vikwazo hivyo vinahitaji nguvu ya pamoja kuvipatia ufumbuzi wa haraka ili kunusuru maisha ya wazee katika jamii.

Chanzo: RAIA MWEMA

Saturday, April 9, 2016

WATU NINAOJIVUNIA KATIKA TASNIA YA SANAA KWIMBA KWETU (SEHEMU YA PILI)


BY NGUDU NYUMBANI BLOG
09/04/2016

 Huu ni mwendelezo wa makala iliyopita juu ya kukubali na kupenda vipaji vya watu hususan kwenye tasnia Sanaa. Ikiwa wengi wao walifanya na baadae wakaacha, ila wengine wanajihusisha na mambo hayo hadi leo.

Lengo kubwa na la msingi katika kuyajua haya yote, ni kutaka kuiandika historia ya wilaya yetu iweze kukumbukwa na wengi japo pengine isiwe imekamilika kwa asilimia zote.
Kipindi cha nyuma kuliwahi kuwapo na kundi la HIP HOP lililojulikana kwa jina la MASOKWE FAMILY liliundwa na vichwa vitatu  likiongozwa Mwl. Wawa a.k.a CRAZY V.
Kwa sasa Wawa ni mwalimu anayefundisha watoto wenye special needs kakora s/m.

Pia kulikuwa na kundi la muziki la BLESSED BOYS baadae likabadilishwa na kuwa BLESSED ARMY.  kundi hili liliundwa na Renatus Mahuyu(ray m), Deogratias Igonzela(yung skills), Samwel Musobi(samu 4 real), Yahya (yq), Shaina(lady shao), Zephania festo(zf), pia kulikia na dogo felali. Kwa sasa wengi wao kama sio wote ni waheshimiwa kulingana na nafasi walizonazo.
 Na pengine ukiwakumbusha wakupe stori kidogo juu ya harakati zao enzi hizo, vijana wa mjini wanasema ‘ilikuwa ni shiida’ enzi hizo.

Ukiachilia mbali makundi ya muziki, naambiwa pia FRED  SWAGG ni KWIMBA product. Huyu jamaa anajulikana sana hasa kwa wafuatiliaji wazuri wa muziki wetu. Amewahi kufanya ngoma kama  THE LYRICS akiwashirikisha Young killer(msodoki) na Kad go(kadi ya mchezo). Pia nyingine akimshirikisha Baraka Da prince kwenye track ya ‘Kikomo’, na nyingine nyingi.

Unaweza kuona muziki hasa wa Hip Hop uliweza kuvutia vijana wengi sana, hata leo bado unavutia wengi pia. Zamani kulikuwa na changamoto nyingi tofauti na sasa katika kuufanya. Muziki huu umeendelea kutambulika kama muziki wa harakati ambapo kwa wafuatiliaji wazuri wanajua kuna Misingi na Nguzo zinazoongoza mziki huu.

Ukiachana na hilo, harakati za kuukuza mziki huu ni nyingi, ambapo kumekuwepo na vitu kama KILINGE CHA NADHALIA kwa wakazi wa Dar(New msasani club chini ya usimamizi wa tamaduni muzik), S.U.A kwa wakazi wa Arusha(kijenge juu, chini ya watengwa rec) kama waanzilishi ambapo kwa sasa ni karibu kila mkoa kuna haya mambo. Pia kwa Mwanza kuna S.U.A  maeneo ya nyamagana.

Dj Venture, ni moja ya watu muhimu kabisa kipindi hicho miaka ya 2002 hivi. Ikumbukwe ndiye aliyefanikisha kuwaleta wasanii wengi wakubwa  Bob Haisa, Inspecta Haroun na wengine wengi ambao baadhi niliwaongelea kwenye sehemu ya kwanza ya makala hii.
Mbali na kufanikisha kwa kiasi kikubwa kuleta wasanii kufanya show wilayani, pia anaongelewa kufanikisha kwa kiasi kikubwa kuletwa na kuanzishwa kwa MISS KWIMBA.

Katika kufanikisha hilo kulikuwa na kamati maalumu ya kupanga na kufanikisha tukio hilo. Ambapo inasemekana waliounda kamati hiyo ni pamoja na Dj jigga, Idd ghati, Daniel Magobe, Mbialo na wengineo.

Baada ya muda, tukio la Miss KWIMBA  lilizoeleka na kupata wafuasi na washiriki wengi pia. Itakumbukwa hadi watoto wa sekondari walihusika hapo. Ndiyo kipindi cha kina NYABAZENDA MATENGANE kuwatoa kimasomaso vijana wa NGOYAI pale Ngudu sec, pale aliponyakua taji hilo.

Pia katika ma-DJ vijana wanaochipukia na kukubalika vema  nilisahau jina la bwana mdogo Nestory Samson. Ni moja ya vijana mahiri kabisa katika eneo hilo la kuchezea vyombo vya muziki.

Kwenye sanaa, upande wa wachoraji na wapaka rangi bora kabisa enzi hizo pengine hadi leo. Utakutana na Mwenyekiti wa sasa wa NGUDU MJINI, mh Casmiry Antony, bila kumsahau J4 kama tulivyomjua wengi.

WASANII WASUKUMA(nyimbo za asili)

Katika kanda ya ziwa, hasa sehemu ambazo zinakaliwa na kabila la wasukuma nikihusisha na eneo letu pia. Kumekuwepo na mwamko mkubwa wa wasanii wa nyimbo za asili hasa nikimaanisha nyimbo za kisukuma.

Kuna wasanii wengi ambao wanafanya vizuri katika anga hiyo kama, Bhulemela, Bhudagala, Senghi milembe, Inaga Myambelele, Juma Marko, Kundi wa Moto, Madebe, Steven Maneno, Misoji sabhujo, Nyanda Lunduma, Kisima, Koper head, Elias mnyamwezi, Mwana kwela, Shinje makala, Mchelemchele, Jeledi, Malingita, Shilango na wengine wengi.
Utajiuliza nimewajuaje wote hao, ila ukweli ni kwamba nimewafahamu kupitia nyimbo zao nilizonazo. Japo mimi nae ni mmoja kati ya wavivu wengi wa kusikiliza ladha adhimu hii kutoka usukumani. Na katika wote niliowataja hapo juu sina hakika kama kuna hata mmoja anatokea KWIMBA kwetu. Katika kundi kama hilo, pia kuna wacheza ngoma maarufu ambapo wamekuwa wakifanya mashindano mara kadhaa hasa viwanja vya KWIDECO na MAHIGA na maeneo mengine ndani na nje ya wilaya.

‘Kila ng’wene na ka nyengele gakwe’, moja ya misemo maarufu ya kisukuma. Ikilenga kumaanisha kila mmoja kwa nafasi yake katika kutoka au kufanya kitu.  Panapo majaliwa WAKATABAHU.

KWIMBA TUITAKAYO
nguduone@gmail.com



Tuesday, April 5, 2016

WATU NINAOJIVUNIA KATIKA TASNIA YA SANAA KWIMBA KWETU(SEHEMU YA 1)


BY NGUDU NYUMBANI BLOG
05/04/2016.
(SEHEMU YA KWANZA)

KATIKA maisha, hali ya kujiamini juu ya kile unachokifanya na kukifanya kwa utashi na utulivu mkubwa ndiyo silaha muhimu kuelekea mafanikio. Licha ya kujiamini ni lazima kukubaliana na matokeo kwa kukubali changamoto zinazokukabili na kujua namna bora ya kuzikabili ili usonge mbele.

Leo nimeamua kuwakumbuka baadhi ya ndugu zangu hasa kwenye tasnia ya sanaa kwa ujumla wake. Nimejaribu kuwazungumzia vijana baadhi waliojihusisha na sanaa hasa ‘wasanii’ kipindi cha nyuma.  Ambapo wengi wao walifanya kama hobby(kwa kipindi hicho baadae wakaachana nayo) na wengine waliwekeza muda mwingi kuhakikisha wanaendelea na utaratibu huo na leo tunawatambua kama wasanii.

Nakumbuka kipindi hicho, vijana wengi walikuwa wanapenda hasa kuimba. Jamaa zangu,  Omary Kigoda na Juma Damas( mwenyezi amlaze mahala pema)  walikuwa ni watu wa kuandika mashairi mara kadhaa ila changamoto ilikuwa namna ya kupata au kuvifikia vyombo vya kurekodia mashairi hayo, kipindi hicho hapakuwa/hawakuwa na simu za kurekodi japo sauti kama ilivyo leo. Mbali na kuimba bwana omary alipenda kuigiza pia.

Kwa sasa Omary licha ya kuwa mtumishi wa serikali lakini anajihusisha na sanaa pia(kuigiza na kuandaa filamu), ambapo amehusika kwenye baadhi ya filamu  ikiwemo ‘MADNESS’  iliyopo sokoni kwa sasa unaweza kuitafuta na kuitazama. Mdogo wake pia msharo (Shaban) ni msanii anayewakilisha kundi la THE WINNERS ambapo naye amepata kufanya kazi kadhaa ikiwemo ‘Bolingo nangaye’ akimshirikisha  Man M the winner. Video yao na video nyingine unaweza kuzipitia HAPA

Friday, April 1, 2016

MBUNGE WA JIMBO LA SUMVE APANDISHWA KIZIMBANI KWA TUHUMA ZA RUSHWA

Richard Ndasa, mbunge wa jimbo la SUMVE

RICHARD Ndasa, Mbunge wa Sumve, (CCM) amepandishwa kizimbani katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu shtaka la tuhuma ya kuomba rushwa ya Shilingi milioni 30, 
Akisoma mashtaka hayo wakili wa Taasisi ya Kuzia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Denis Lukayo mbele ya hakimu, Amilisi Mchaura amesema kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo akiwa kama mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma.
Amesema kwamba mbunge huyo anatuhumiwa kwa kosa la kuomba Rushwa kwa Mkurugenzi wa Shirika la Umeme (Tanesco), Felichesmi Mramba ila amsaidie kuandika mapendekezo safi ya shirika hilo.
Mbunge huyo anakuwa wa nne kupandishwa kizimbani kwa kosa la rushwa ambako tayari jana walipandishwa wengine wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ambao ni Ahmad Saddiq (53) mbunge wa Mvomero, Kangi Lugola (54) mbunge wa Mwibara na Victor Mwambalaswa (63) mbunge wa Lupa.
Kutokana na uchunguzi unaoendelea upo uwezekano wa wabunge zaidi kufikishwa mahakani kujibu tuhuma hizo ambazo zimetikisa taasisi ya Bunge ambacho ndicho chombo kikuu cha kutunga sheria.
Mbunge huyo alifikishwa majira ya saa mbili asubuhi huku idadi kubwa ya watu wakiwa wamefurika kushuhudia kesi hiyo ambayo imekuwa na mvuto kwa wananchi wengi wa jiji la Dar es Salaam.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo mbunge Ndasa alikana kutenda kosa hilo ambako upande wa serikali ulisema upelelezi bado unaendelea.

Chanzo: MWANAHALISI


Previous Page Next Page Home