Tuesday, January 6, 2015

ZIFAHAMU SIFA, MAJUKUMU YA DIWANI WAKO, KISHA JITOKEZE KULETA MABADILIKO KWENYE JAMII YAKO.

Diwani ni mwakilishi aliyechaguliwa kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Serikali za Mitaa.  Madiwani ndio wanaounda Halmashauri za Serikali za Mitaa na ndio wenye mamlaka ya kutekeleza majukumu ya Serikali za Mitaa.  Sheria za Serikali za Mitaa zimeainisha majukumu ya kutekelezwa na Mamlaka hizi kuwa ni ya kuwaletea wananchi maendeleo kwa kuwapatia huduma bora na kwa gharama nafuu. Majukumu hayo ya Serikali za Mitaa ni haya yafuatayo:
             i.                Kulinda na kutunza utulivu na amani na kusimamia Utawala Bora;

      ii.           Kuendeleza ustawi wa jamii na kuinua uchumi wa wananchi wake ikiwemo kuimarisha afya, elimu, utamaduni, burudani na ustawi wa wananchi wake;

           iii.                Kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii yanapatikana kwa mujibu wa Sera za Taifa za Maendeleo Mijini na Maendeleo Vijijini;

           iv.                Kuhakikisha na kuchukua hatua zozote zinazofaa katika kuzuia au kuondoa uhalifu na kulinda watu pamoja na mali zao;

            v.                Kuimarisha na kuendeleza kilimo, viwanda na biashara;

           vi.                Kuuondoa umaskini na kero nyingine katika jamii hususan kwa kuzingatia makundi ya vijana, wazee na walemavu wa aina mbalimbali na wale wasiojiweza;

         vii.                Kuhimiza dhana ya ushirikishwaji wa wananchi, vyama vya hiari na visivyo vya hiari katika kujiletea maendeleo;

        viii.                Kubuni vyanzo mbalimbali vya mapato vya kuwezesha Halmashauri kutekeleza majukumu yake niliyoyataja hivi punde.


Hayo ndiyo majukumu ya Serikali za Mitaa ambayo msimamizi mkuu katika halmashauri ni Diwani.

SIFA ZA KUGOMBEA UDIWANI
Mtu anaweza kugombea na kuchaguliwa kuwa Diwani iwapo anakidhi
sifa zifuatazo:
(i) Awe ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

(ii) Awe ametimiza umri wa miaka ishirini na moja au zaidi;

(iii) Awe na akili timamu;

(iv) Awe ni mkazi wa kawaida wa eneo la Mamlaka ya Serikali za
Mtaa husika;

(v) Anaweza kusoma na kuandika Kiswahili na Kiingereza;

(vi) Awe ni mwanachama wa chama cha siasa kilichosajiliwa kwa
mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 na chama
chake kimemteua akiwakilishe kwenye uchaguzi husika;

(vii) Awe na njia halali za kujipatia kipato;

(viii) Asiwe amehukumiwa kwa kosa la ukwepaji kodi ndani ya kipindi
cha miaka mitano kabla ya uchaguzi.

(ix) Asiwe amehukumiwa kifo au amehukumiwa kifungo cha zaidi ya
miezi sita jela


Mimi kama mwananchi ninapaswa kutathmini majukumu ya kiongozi na kupima uwajibikaji wake katika kuleta maendeleo kwenye jamii yangu.
Ikiwa ni mmoja ya wanaoamini katika mabadiliko, ambapo huanzia ngazi ya uongozi.Sasa basi kama diwani wako hajatimiza wajibu wake kwa maana ya kushindwa kusimamia ipasavyo miradi ya maendeleo katika kata yako kwenye miaka yake mitano ya uongozi ni wazi yanahitajika mabadiliko makubwa ili kufikia malengo ya kuwa na kiongozi bora mchapakazi na mpenda mabadiliko.
AMKA MWANA KWIMBA, AMKA MTANZANIA, VIJANA TUJITOKEZE KUWANIA UONGOZI!


No comments:

Post a Comment

Previous Page Next Page Home