Sunday, February 28, 2016

Naibu Waziri ampa kibano ofisa ardhi-KWIMBA


Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Kwimba, Mkoa wa Mwanza, Cosberth Byabato, juzi alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula kumbana ampatie maelezo kuhusu idara hiyo kuchukua fedha kutoka kwa wananchi bila ya kuwagawia viwanja.

Ofisa huyo alipata ‘kibano’ hicho mbele ya wananchi waliomlalamikia Mabula kuwa licha ya kulipa fedha za viwanja, halmashauri imeshindwa kuwakabidhi.
Baada ya kupokea malalamiko hayo, Mabula alimtaka Byabata kueleza sababu zilizoifanya halmashauri itoe jumla ya hekari 2,500 zimilikiwe na taasisi za dini na magereza ambao toka wagawiwe 1998, wameshindwa kuziendeleza.
Pia, inadaiwa kuwa wamiliki hao huwakodisha wananchi kwa Sh25,000 kwa kila heka kwa ajili ya kulima.
Baadhi ya wananchi walimlalamikia naibu waziri huyo alipozungumza nao katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Maliya wilayani Kwimba.
Akizungumza kwenye mkutano huo mmoja wa wananchi hao, Mery Vicent alimuomba naibu waziri huyo awasaidie kupata ardhi.
“Wanatupatia ahadi kila siku tuje wakati wameshakula Sh800,000 zetu,” alidai Vicent.
Alipotakiwa kujibu malalamiko hayo ya wananchi, Byabato alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kukatishwa kila mara na Mabula aliyekuwa akimtaka atoe ufafanuzi wa kina.
Hata hivyo, alikiri wananchi kutopatiwa viwanja na kuahidi kuwapa kesho.
Akizungumzia hekari 2,500 zilizotolewa kwa taasisi za dini, alisema: “Eneo linalolalamikiwa na wananchi, mwaka 2008 lilipata wawekezaji ambao ni Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) hekari 1,000, Kanisa Katoliki 1,000 na Magereza 500.

“Eneo hilo lilianza kutambuliwa mwaka 2011 kisheria na hati zake zilitolewa mwaka jana.
Tatizo wananchi wanaona mashamba hayo hayaendelezwi, lakini sheria inasema baada ya miaka mitano kama yatakuwa hayajaendelezwa yachukuliwe na Serikali, muda huo bado haujafika,” alifafanua.
Chanzo: MWANANCHI


Saturday, February 27, 2016

TATHMINI YANGU KUHUSU MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2015.

BY NGUDU NYUMBANI BLOG
27/02/2016.

MATOKEO ya kidato cha nne yaliyotolewa Feb 18 mwaka huu yameonesha kuporomoka kwa ufaulu, ikilinganishwa na mwaka jana. Ambapo ni anguko la asilimia 1.85 kwa watahiniwa wa shule.

 Matokeo hayo yalipangwa katika mfumo wa madaraja (Division) badala ya ule wa wastani wa alama (GPA) kama ambavyo iliagizwa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi hivi karibuni.

Katika shule zilizopo wilaya ya KWIMBA, kwa wale waliopata kuyaona matokeo ya shule hizo wanaweza kukubaliana nami kwamba kuna mwendelezo wa kuporomoka huku Mkoa ukibeba sifa ya mikoa iliyofanya vizuri kitaifa. Mkoa umetoa shule 3 kati ya shule 10 bora yaani ALLIANCE GIRLS(2), ALLIANCE BOYS(4) na ALLIANCE ROCK ARMY(7) zote za binafsi.

Nilipata wasaa wa kuyapitia matokeo ya takriban shule 28 za wilaya yetu japo kuona ufaulu kwa ujumla tu, nikagundua hayana tofauti sana na ya miaka miwili au mitatu iliyopita. Nikaja na jibu moja kwamba tunajitahidi kuongeza idadi ya vijana wasio na sifa(waliofeli) mitaani na  pengine tusijue wanachokifanya baada ya matokeo haya na hakuna anayejali katika hili.

BAADHI YA SHULE ZA SEKONDARI ZILIZOJITAHIDI.

Shule ya sekondari SUMVE GIRLS ndiyo inaongoza kwa shule zilizopo wilayani ambapo ipo nafasi ya 48/231 Kimkoa. Ambapo, Div i-0, Div ii-9, Div iii-40, Div iv-71 na Div 0-2. Ni ajabu kwa shule inayoongoza ki-wilaya hakuna mwenye daraja la kwanza hata mmoja, na pia pongezi kwao kwa sababu waliopata daraja la sifuri ni wawili tu kati ya watahiniwa 122.  Shule hii ina uhakika wa kupeleka wanafunzi 49 kidato cha 5. Mwaka jana walipeleka wanafunzi 56 kidato cha 5.

Saturday, February 20, 2016

NGUDU NYUMBANI BLOG NA USHIRIKI WA WADAU.


Ngudu nyumbani blog ni moja kati ya blogu za jamii iliyojikita zaidi wilayani KWIMBA. Kuhakikisha habari zinawafikia wananchi mathalani wanaotumia mitandao ya kijamii habari, chambuzi, mitazamo mbalimbali na mawazo kwa ujumla juu ya wilaya yetu.

Lengo lake la awali lilikuwa ni kupeleka wazo hili la kuendesha hii blogu kuwa chini ya serikali kwa maana ya halmashauri ya wilaya. Lengo lilikuwa ni kukuza nasaba kati ya serikali na wananchi ambapo serikali ingewajibika kumpatia mwananchi habari zote muhimu zinazomhusu.

Sababu kubwa ya kupeleka wazo hili ni baada ya kuona, kama serikali bado ina ombwe au tatizo kubwa haswa katika sekta hii ya upashaji habari. Na njia rahisi niliyopendekeza kama mwanzilishi wa blogu hii ilikuwa ni kuwapa wao sababu za kulipa uzito suala hili na kulitekeleza kwa manufaa ya wengi.

Wazo lilikwama kwa sababu zinazosemekana kuwa kuna maandalizi ya mwisho kabisa katika kuanzisha tovuti rasmi ya wilaya ambayo itatoa habari na mengine mengi kama zifanyavyo tovuti nyinginezo za serikali. Japo walihitaji pendekezo langu juu ya kuanzisha blogu pengine tovuti ikachua muda mpaka kuanza kutumika.

Pendekezo liliandaliwa na kutumwa kwa njia ya barua pepe, lakini tangu litumwe mwaka jana mwezi april hakuna majibu ya kukataliwa au kukubaliwa kwa pendekezo hili. Na tovuti rasmi bado haijaandaliwa mpaka sasa. Sina hakika kama ‘wakala wa serikali mtandao’ ndio kikwazo katika hili au ni uongozi wenyewe ndio haujawa tayari na kulipa uzito jambo hili.

Lengo lilikuwa sio kuelezea yote haya, bali ni kutoa maelezo machache juu ya hii blogu mpaka hapa ilipofikia.

Kwa sasa blogu inazidi kuongeza wasomaji wa habari zinazoihusu wilaya yetu. Japo changamoto ni nyingi katika kufanikisha hili. Ningependa ifahamike kuwa blogu hii inajiendesha yenyewe na hakuna nasaba yoyote na serikali ya wilaya yetu. Hivyo ni blogu ya jamii kila mmoja wetu anao uhuru wa kuchangia katika mawazo, mijadala, kuandaa na kuleta tafiti mbalimbali juu ya wilaya, mapendekezo, ili mwisho wa siku tuwe na jamii inayowajibika katika kujua yale yanayoendelea katika mazingira yao.

Ushiriki wa wadau katika mawazo, upatikanaji wa habari, mijadala na mengine mengi ni mdogo au pengine naweza kusema haupo kabisa. Nasema hivi kwa maana kuwa asilimia zote POST zote zinazohusu blogu zimetolewa na mwanzilishi wa blogu hii. Na lengo la blogu hii sio la kibiashara ama namna yeyote, bali ni la kijamii zaidi kupata mawazo ya kila mmoja wetu kushiriki kuwaza kwa pamoja.

Wana KWIMBA tunashiriki mijadala katika mitandao kadhaa ya kijamii. Ila lengo la blogu hii ni kuunganisha mawazo yote ili kuwa na platform moja itakayoweza kuunganisha jamii yote ya wana Kwimba kirahisi zaidi pengine tofauti na magroup yetu ya ‘Facebook, whatsapp na mengineyo ambapo yanakuwepo mengi na sio kila mmoja anaweza kushiriki katika magroup hayo kwa wakati.
Nadhani ushiriki wetu ndio changamoto kubwa zaidi, nyingine ni ndogondogo zinawezeka kutatuliwa.

 Pia nikijaribu kupitia takwimu za wasomaji/watembeleaji wa blogu naona kuna raia wa Tanzania waishio  nje kama Marekani, Kenya, Uholanzi, India, Ujerumani na nchi nyinginezo husoma blogu hii mara kwa mara. Nao pia kwa nafasi yao wanao wajibu wa kuchangia mawazo yao katika platform hii.

 Na tukio moja nililokutana nalo juzi kati ni DEVICE  moja kutoka Nairobi Kenya yenye IP ADDRESS ‘141.0.13.113’ ilijaribu kutaka ku-access akaunti ya blogu hii kama Adminstrator. Kama atapata kusoma hapa huyo mwenye address hiyo bila shaka atatakiwa kujua kuwa blogger ni mtaalamu wa IT kwa hiyo asipende kujaribu kila kitu maana hii address yake ni kigezo tosha cha kumfunza adabu. Hii inawahusu wote wenye tabia kama hii.

Kingine, kulingana na majukumu ya kila mmojawetu katika ujenzi wa taifa popote alipo, mara nyingi unaweza kuona post zinawekwa siku za mapumziko(weekend). Ambapo mwandaaji anakuwa na muda wa kutafakari jambo na upande mwingine wadau wanakuwa wengi wamepumzika na majukumu yao ya kuchakarika na maisha. Kwa mara chache sana inaweza tokea kwenye siku za kazi.

Rai yangu kwa wasomaji wa blogu hii pia facebook page inayohusiana na blogu hii ni kuwa, ushiriki wetu sote ndio mafanikio katika hili. Ningependa kushauri kwa wote wenye kupenda kuandika lolote juu ya wilaya yetu na jamii ikaelewa ni vyema wakafanya hivyo kwa faida ya jamii. Tusikomee kulaumu wilaya yetu ni maskini na mwisho wa siku hautoi mawazo ya nini kifanyike kuhakikisha tunatoka hatua tuliyopo na kwenda hatua bora zaidi.

Kuna wadau baadhi wamenihakikishia ushiriki katika hili, pia ningependa kila mwenye kuweza kufanya hivyo na afanye kwa moyo wa dhati yake kabisa akiamini jamii kubwa inafatilia kwa umakini atakachokisema au kukiwasilisha.

Kufanya hivyo tunatimiza matakwa ya katiba yetu ya JMT ya mwaka 1977 kwenye ibara ya 18 inayosema;
(1) Bila kuathiri sheria za nchi, Kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na  kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.
(2) Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbali mbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.

Japo kwa maelezo hayo machache na imani nitakuwa nimeeleweka vyema. Lengo ni kuamsha hisia tofauti, kuongeza msukumo ndani ya jamii zetu kwa lengo la kujenga zaidi bila kuathiri wengine.
Wilaya yetu ina wasomi wa kada mbalimbali hivyo kila mmoja wetu anaweza kutoa mchango wake kupitia kada yake. Sio mahsusi sana mada, mawazo, makala zetu zihusu siasa moja kwa moja bali kuna mazingira mengi ya kuzungumzika pia ya uchumi, kijamii, teknolojia japo siasa inaonekana kuteka na pengine kuwa mhimili mkubwa katika haya mengine.

Naamini hakuna jambo muhali kwenye jamii yetu lisilo na majibu au mawazo mbadala wa kulifanya. Na lengo la kusisitiza ushiriki wetu katika hili ni kuepuka ‘shere’ zinazofanyika mara kwa mara kwenye groups zetu. Huku hazitofanyika kwa maana yak u-post au share habari zisizo na maadili au zisizokuwa na mwamko wowote kwenye jamii yetu.

Mawasiliano kwa watakaokuwa tayari kushirikiana na ngudu nyumbani blog yapo wazi kabisa, hivyo ni jukumu la kila mwenye uhitaji katika hili kuhakikisha anafanya kulingana na hisia, muono na busara zake.

Tafakari.
nguduone@gmail.com


Thursday, February 18, 2016

MATOKEO YA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE(CSEE) 2015- WILAYA YA KWIMBA


Baraza la Mitihani (NECTA) leo Februari 18, 2016 limetoa Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne uliofanyika mwishoni mwa mwaka 2015.

Akitangaza Matokeo hayo katibu Mtendaji wa Baraza hilo Dkt Charles Msone amesema jumla watahiniwa 272,947 sawa na 67.53% ya watahiniwa waliofanya mtihani wa kidato cha nne 2015 wamefaulu tofauti na mwaka 2014 ambapo ufaulu ulikuwa 68.33%.

Upande wa watahiniwa wa shule, waliofaulu ni 240,996 sawa na asilimia 67.91 ya waliofanya mtihani, wasichana wakiwa 11,125 (64.84) na wavulana wakiwa 124,871 (71.09). 

Friday, February 12, 2016

WILAYA MBILI AU HALMASHAURI MBILI NDANI YA WILAYA MOJA?


BY NGUDU NYUMBANI BLOG
12/02/2016

WILAYA ya KWIMBA ni moja kati ya wilaya 7 zinazounda mkoa wa MWANZA. Katika sensa ya mwaka 2012, idadi ya wakazi wa wilaya ya KWIMBA ilihesabiwa kuwa 406,509. Pia makadirio ya idadi ya watu kwa mwaka 2015 takwimu zinaonesha majimbo mawili yanayopatikana wilaya ya KWIMBA  yana jumla ya wakazi 438,984 ambapo jimbo la Kwimba ni 235,818 na Sumve ni 203,166.

Nimejaribu kuandaa majedwali yanayohusisha sensa ya mwaka 2012, pia makadirio ya idadi ya watu mwaka 2015 kwa majimbo ya KWIMBA na SUMVE kama ifuatavyo;


Wednesday, February 10, 2016

SHIKOME, KWIWODE, NADSO NA NGO’s NYINGINEZO KWIMBA RIPOTI ZA MAENDELEO YAO ZIPO VIPI?


BY NGUDU NYUMBANI BLOG

Japo kwa ufupi tupate kujua maelezo machache juu ya taasisi hizi zisizo za kiserikali kwa faida ya wasiojua, kisha kama kuna wahusika au wadau wa maendeleo wanaojua kinachoendelea ndani ya taasisi hizi waujuze umma wa wana Kwimba maendeleo yake yako vipi japo kwa muhtasari kufikia mwezi huu.

 Nikimaanisha miradi ya maendeleo kupitia taasisi hizo, mwitiko wa watu kushirikiana na taasisi na mchango wa serikali pamoja na wafadhili kutoka ndani na nje umewezesha kwa kiasi gani kuikuza taasisi husika na hatimaye kufikia malengo yake. Na kama kuna utaratibu maalumu wa kupata taarifa husika hizo pia ni vema ikajulikana wenye nia ya kujua wakafuata..



1. SHIKOME ORGANISATION GROUP
Previous Page Next Page Home