Sunday, February 28, 2016

Naibu Waziri ampa kibano ofisa ardhi-KWIMBA


Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Kwimba, Mkoa wa Mwanza, Cosberth Byabato, juzi alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula kumbana ampatie maelezo kuhusu idara hiyo kuchukua fedha kutoka kwa wananchi bila ya kuwagawia viwanja.

Ofisa huyo alipata ‘kibano’ hicho mbele ya wananchi waliomlalamikia Mabula kuwa licha ya kulipa fedha za viwanja, halmashauri imeshindwa kuwakabidhi.
Baada ya kupokea malalamiko hayo, Mabula alimtaka Byabata kueleza sababu zilizoifanya halmashauri itoe jumla ya hekari 2,500 zimilikiwe na taasisi za dini na magereza ambao toka wagawiwe 1998, wameshindwa kuziendeleza.
Pia, inadaiwa kuwa wamiliki hao huwakodisha wananchi kwa Sh25,000 kwa kila heka kwa ajili ya kulima.
Baadhi ya wananchi walimlalamikia naibu waziri huyo alipozungumza nao katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Maliya wilayani Kwimba.
Akizungumza kwenye mkutano huo mmoja wa wananchi hao, Mery Vicent alimuomba naibu waziri huyo awasaidie kupata ardhi.
“Wanatupatia ahadi kila siku tuje wakati wameshakula Sh800,000 zetu,” alidai Vicent.
Alipotakiwa kujibu malalamiko hayo ya wananchi, Byabato alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kukatishwa kila mara na Mabula aliyekuwa akimtaka atoe ufafanuzi wa kina.
Hata hivyo, alikiri wananchi kutopatiwa viwanja na kuahidi kuwapa kesho.
Akizungumzia hekari 2,500 zilizotolewa kwa taasisi za dini, alisema: “Eneo linalolalamikiwa na wananchi, mwaka 2008 lilipata wawekezaji ambao ni Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) hekari 1,000, Kanisa Katoliki 1,000 na Magereza 500.

“Eneo hilo lilianza kutambuliwa mwaka 2011 kisheria na hati zake zilitolewa mwaka jana.
Tatizo wananchi wanaona mashamba hayo hayaendelezwi, lakini sheria inasema baada ya miaka mitano kama yatakuwa hayajaendelezwa yachukuliwe na Serikali, muda huo bado haujafika,” alifafanua.
Chanzo: MWANANCHI


No comments:

Post a Comment

Previous Page Next Page Home