Sunday, March 13, 2016

UNA MCHANGO GANI KWENYE SHULE ULIYOPATA KUSOMA NA KUKUFIKISHA HAPO ULIPO LEO?


BY NGUDU NYUMBANI BLOG
13/03/2016

NYASECO ALUMINAE, hili ni kundi la wadau waliopata kusoma shule ya sekondari  Nyamilama iliyopo talafa ya Nyamilama, kata ya Nyamilama wilaya ya KWIMBA.

Wadau hawa licha ya uchache wao lakini walipata kujipanga na kwenda kuitembelea shule waliyopata kusoma miaka kadhaa iliyopita. Lengo ni kujua maendeleo ya shule yao hiyo, changamoto zinazoikabili shule hiyo na mambo yote yanayoihusu shule kwa ujumla.

Sijabahatika kupata taarifa zao zaidi, japo kwa “Video clip” ya dakika chache inatosha kuonesha  malengo na Mipango waliyokuwa nayo kutaka  kuitembelea shule yao. Shauku yao kubwa ilikuwa ni kuona mabadiliko ya shule hiyo kipindi wanasoma na hali ilivyo kwa kipindi wameitembelea. 


Kuweza kuongea na vijana na kuwapa ushauri ambao kwa namna moja ni msaada mkubwa kwa wanafunzi hao. Ushauri unaoweza kuwajenga kiuwezo na kifikra pia kuelekea kwenye mafanikio yao. 
Wadau kadhaa pia kupitia NADSO waliwahi kutembelea shule ya sekondari NGUDU  na kufanikisha baadhi ya maazimio waliyokusudia kuyafikisha shuleni hapo, ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wa vitabu  n.k.

WADAU WENGINE WANA NAFASI GANI?

Kila mmoja wetu anaweza kuguswa kwa namna yake, kiasi cha kupelekea kuhamasika au pengine kuwaza siku moja anaweza kuitembelea ama shule aliyowahi kusoma au taasisi yoyote iliyopata kumlea hapo kabla.
kundi la wadau wanaweza kupanga namna ya kuweza kuikumbuka shule waliyosoma kipindi cha nyuma. Wakajadili kupitia namna mbalimbali za mawasiliano, kisha wakapata wawakilishi baadhi wanaoweza kubeba ujumbe wa jumla juu ya lengo lao la msingi.

 Ujumbe wao unaweza kuwa kwenye maandishi mahsusi kuwafikia walengwa. Au pengine unaweza kuwasilishwa kwa namna yoyote iliyo bora ikiwa na lengo lile lile.

Niliwahi kuwa na wazo hili kabla, japo ni kwa namna tofauti kidogo kwamba, nilipata kuaandaa baadhi ya ripoti kadhaa nikilenga hasa matokeo ya shule husika. Kuna shule kadhaa nimepata kuandaa kila napopata muda wa kufanya hivyo.

Changamoto ikawa ni namna gani naweza pata wadau, tukaweza unganisha mawazo na kupata mwafaka wa pamoja namna ya kulifanya jambo hili kwa ufasaha zaidi. Kuna mambo mengi na ya msingi ya kujadili kabla ya kuwaza na kuamua kwenda kutembelea jamii mliyokulia na kusoma.

 Changamoto ya mazingira tofauti baina yetu pia, japo hii sikuona kama ni kikwazo sababu kupitia mitandao ya kijamii mnaweza kujadili kwa ufasaha pia. Na wakapatikana wadau walio karibu na eneo la ”tukio” wakawakilisha. Au mkakubaliana mathalan, kukutana na kujadili kipindi cha likizo ambapo wengi hupenda kurudi nyumbani kusalimia ndugu, jamaa na marafiki.

Tunaweza kama jamii, kutumia mitandao hii ya kijamii kushauri na kushauriana namna bora ya kufanya mambo, kujadili, na kuweka kumbukumbu nzuri na sahihi juu ya jamii tunazotoka. 

Mwitiko wa wadau katika mambo kama hayo huwa ni hafifu sana, ikizingatiwa kwamba kila mmojawetu anakuwa  na mambo yake ya msingi katika ujenzi wa taifa. Lakini sidhani pamoja na kuwa busy unaweza kukosa muda wa kujadili mambo kadhaa yanayoigusa jamii yako uliyokulia.

Uchache wa wanaoguswa katika mambo kama haya haupaswi kuwa kikwazo katika kufanikisha Mipango. Nyaseco walikuwa wadau wachache na walifanikiwa, kwahiyo wingi wa watu sio kigezo cha kufanikisha azma yenu.
Makundi yanaweza kuwa  mengi kadri ya mnavyoweza kujipanga, ikiwa tu lengo la msingi ni moja. Ningependa ujenzi wa nasaba  yenye siha njema baina yetu na jamii tunayotoka na tunayoishi iwe katika kila mmojawetu kwa wana Kwimba wote popote pale mlipo.
Wasomi , watu maarufu na viongozi wakubwa katika taifa hili wametokana na jamii tunazoishi. Lakini wengi wao wana mchango mdogo sana mathalan, katika jamii waliyokulia na pengine kusoma. Hawataki kuwekeza mawazo, miradi au mali zao kwenye jamii walizokulia, na mwisho wa siku huishia kulaumu kuwa jamii wanayotoka bado ni maskini bila ya kujua wao wana mchango gani katika kuleta maendeleo kwenye jamii hiyo.

Ukiachilia sababu nyingine zinazopelekea wilaya yetu kubaki nyuma siku zote na pengine kuwa na ukuaji mdogo wa hali ya maisha na maendeleo kwa ujumla. Kundi la wasomi na wazaliwa wote ambao hawaipi jamii yao kipaumbele kwenye uwekezaji wao ndio sababu mojawapo ya umasikini wa jamii yao.

Katika hili kuna mifano mingi lakini haitokuwa busara kama nitaanza kutaja mtu kwa jina au cheo chake lakini nafsi ya kila mmoja wetu inajua ipo katika nafasi ipi katika ujenzi wa jamii yetu.

Ningeweza kuongea zaidi ya hapa lakini inatosha kusema ujumbe umetufikia sote inabakia upande wetu katika kuamua namna bora ya kufanya.

Tafakari!
KWIMBA TUITAKAYO
nguduone@gmail.com.





No comments:

Post a Comment

Previous Page Next Page Home