Saturday, February 27, 2016

TATHMINI YANGU KUHUSU MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2015.

BY NGUDU NYUMBANI BLOG
27/02/2016.

MATOKEO ya kidato cha nne yaliyotolewa Feb 18 mwaka huu yameonesha kuporomoka kwa ufaulu, ikilinganishwa na mwaka jana. Ambapo ni anguko la asilimia 1.85 kwa watahiniwa wa shule.

 Matokeo hayo yalipangwa katika mfumo wa madaraja (Division) badala ya ule wa wastani wa alama (GPA) kama ambavyo iliagizwa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi hivi karibuni.

Katika shule zilizopo wilaya ya KWIMBA, kwa wale waliopata kuyaona matokeo ya shule hizo wanaweza kukubaliana nami kwamba kuna mwendelezo wa kuporomoka huku Mkoa ukibeba sifa ya mikoa iliyofanya vizuri kitaifa. Mkoa umetoa shule 3 kati ya shule 10 bora yaani ALLIANCE GIRLS(2), ALLIANCE BOYS(4) na ALLIANCE ROCK ARMY(7) zote za binafsi.

Nilipata wasaa wa kuyapitia matokeo ya takriban shule 28 za wilaya yetu japo kuona ufaulu kwa ujumla tu, nikagundua hayana tofauti sana na ya miaka miwili au mitatu iliyopita. Nikaja na jibu moja kwamba tunajitahidi kuongeza idadi ya vijana wasio na sifa(waliofeli) mitaani na  pengine tusijue wanachokifanya baada ya matokeo haya na hakuna anayejali katika hili.

BAADHI YA SHULE ZA SEKONDARI ZILIZOJITAHIDI.

Shule ya sekondari SUMVE GIRLS ndiyo inaongoza kwa shule zilizopo wilayani ambapo ipo nafasi ya 48/231 Kimkoa. Ambapo, Div i-0, Div ii-9, Div iii-40, Div iv-71 na Div 0-2. Ni ajabu kwa shule inayoongoza ki-wilaya hakuna mwenye daraja la kwanza hata mmoja, na pia pongezi kwao kwa sababu waliopata daraja la sifuri ni wawili tu kati ya watahiniwa 122.  Shule hii ina uhakika wa kupeleka wanafunzi 49 kidato cha 5. Mwaka jana walipeleka wanafunzi 56 kidato cha 5.



Shule ya sekondari BUJIKU SAKILA ipo nafasi ya 52/231 Kimkoa, kwa shule zenye watahiniwa zaidi ya 40. Jumla ya watahiniwa ni 109 waliofanya mtihani huo ambapo Div i-4, Div ii-17, Div iii-16, Div iv-55 na Div 0-17. Kwa ufupi ni kwamba watahiniwa 37(daraja la 1-3) wana uhakika wa kuendelea na kidato cha tano.

Ikumbukwe kuwa waliochaguliwa kujiunga na kidato cha 5 mwaka jana kwa shule hii ni 25, kwahiyo kuna ongezeko la wanafunzi 12 katika awamu hii.

Shule kongwe kama NGUDU, NYAMILAMA na MWAMASHIMBA zinazidi kupotezwa na hizi (zilizoanzishwa mwanzoni mwa awamu ya 4 na mwishoni mwa awamu ya 3) taratibu na hakuna anayejali na kujiuliza kulikoni. Shule hizi za zamani kidogo ndiyo zimepata kupika wasomi na viongozi wengi tulionao katika nchi yetu kwenye ngazi mbalimbali. Wataalamu wabobezi wanapenda kuzitofautisha hizi shule kama shule za serikali, na shule za jamii(kata).

Kwamba katika shule ya sekondari NGUDU, kati ya watahiniwa 139 waliofanya mtihani, ni 24 tu wanaweza kuendelea na kidato cha 5. Wakati waliobaki(daraja la iv na 0) ni watahiniwa 115, wengi wao wasijue hatima yao. Huku ikishika nafasi ya 148/231 kimkoa. Mwaka jana ilipeleka wanafunzi 22 kwenda kidato cha 5.

 Aidha, inazidiwa na mwang’halanga(97/231) na Igongwa (81/231), shule ambazo bado zina changamoto lukuki katika sekta ya elimu ukilinganisha na shule ya NGUDU. Ambayo imeanzishwa miaka mingi iliyopita, walau haina changamoto kubwa kama za walimu, maabara na  miundombinu kwa ujumla. Hii ni AIBU  kubwa kwa shule mama ya wilaya.

Shule ya sekondari NYAMILAMA, kati ya watahiniwa 162 waliofanya mtihani huo,  wenye uhakika wa kwenda kidato cha tano ni 36 tu. Tena kwa hawa hakuna aliyepata daraja la kwanza.  Huku wale wenye div 4 na 0 ni 126, na shule imeshika nafasi ya 134/231 Kimkoa. Mwaka jana ilipeleka wanafunzi 22 kwenda kidato cha 5.

Shule ya sekondari MWAMASHIMBA, kati ya watahiniwa 89 waliofanya mtihani huo, wenye uhakika wa kuendelea kidato cha tano ni 32. Huku wale wenye div 4 na 0 wapo 57, na shule ikishika nafasi ya 61/231 kimkoa. Bila shaka hii ndiyo inafuata kwa kufanya vizuri kiwilaya baada ya Sumve girls na Bujiku. Mwaka jana ilifanikiwa kupeleka wanafunzi watano tu kwenda kidato cha 5. Wamefanya vizuri walau kuongeza idadi hiyo.

Shule ya sekondari MALYA , kati ya watahiniwa 82 waliofanya mtihani huo, wenye uhakika wa kwenda kidato cha tano ni 15. Huku wenye Div 4 na 0 wapo 67 kati ya hao wenye Div 0 ni watano tu. Kimkoa imeshika nafasi ya 63/231 kwa maana ya kwamba ni shule ya 4 kiwilaya kwa zilizofanya vizuri. Mwaka jana waliochaguliwa kwenda kidato cha 5 walikuwa 15. Hii pia ni moja kati ya shule zenye watahiniwa wachache kwenye daraja la sifuri kama ilivyo kwa Sumve girls, Mwamala, Lyoma, na Mwakilyambiti.

BAADHI YA SHULE ZILIZOFANYA VIBAYA.

Shule ya sekondari TALLO, ambapo kati ya watahiniwa 45, Div i-0, Div ii-1, Div iii-0, Div iv-19 na Div 0-25. Hii ina maana kwamba shule itapeleka mwanafunzi “mmoja” tu kidato cha 5 kati ya 45. Kimkoa ipo nafasi ya 221/231. Mwaka jana ilipeleka wanafunzi 10, sijui nini kimewasibu mwaka huu na kuwa na matokeo mabovu kupindukia, bila shaka ndiyo ya mwisho kiwilaya kama sikosei.

Shule ya sekondari MWANDU, kati ya watahiniwa 48 waliofanya mtihani huo, hakuna Div i, hakuna Div ii, Div iii-4, Div iv-18, na Div 0- 26. Kwamba ni wanafunzi wanne ndiyo watajiunga na kidato cha 5. Mwaka jana waliochaguliwa walikuwa wanne pia. Nafasi yao kimkoa ni 217/231.

Shule ya sekondari NGULA, iliyokuwa na watahiniwa 63, kati yao wenye Div i-0, Div ii-4, Div iii-3, Div iv-24 na Div 0-32. Hii inamaanisha itapeleka wanafunzi 7 kidato cha 5. Mwaka jana ilipeleka wanafunzi 7 pia. Nafasi kimkoa ni 168/231.

Shule ya sekondari MWAGI. Kati ya watahiniwa 84 waliofanya mtihani huo, Div i-0, Div ii-1, Div iii-4, Div iv-40 na Div 0-39. Hawa wanategemea kupeleka wanafunzi watano kidato cha 5, mwaka jana walipeleka wanafunzi watano pia. Nafasi yao kimkoa ni 212/231.

Shule ya sekondari MANTARE. Kati ya watahiniwa 45 waliofanya mtihani,  Div i-0, Div ii-2, Div iii-2, Div iv=25 na Div 0-16. Kwamba itapeleka wanafunzi wanne kidato cha 5, mwaka jana ilipeleka wanafunzi 7. Nafasi kimkoa ni 165/231

Shule ya sekondari MHANDE, waliofanya mtihani ni 60, ambapo Div i-1, Div ii-1, Div iii-8, Div iv-27 na Div 0-23. Wanatarajia kupeleka wanafunzi 10 kidato cha 5, kwa mwaka jana walipeleka wanafunzi watatu. Kimkoa ipo nafasi ya 167/231.

TUNAJIFUNZA NINI JUU YA MATOKEO HAYA?

Kwa maoni na tathmini yangu nimeweza kugundua na pengine kujifunza mambo kadhaa..

Moja, asilimia 60 na zaidi, ya wahitimu wanapata “Division” IV na 0. Ambapo katika kundi hili kuna wanaopata bahati ya kuendelea katika taasisi mbalimbali mathalan,  vyuo vya elimu, afya, VETA na taasisi nyingine nyingi kusoma kozi hasa za astashahada na kozi za ufundi.
 Kundi jingine katika hiyo asilimia linakuwa na vyeti ambavyo hutumika mara chache sana kusoma baadhi ya kozi ikitegemeana na hali ya uchumi wa mzazi. Na kundi la mwisho wao hata vyeti hawapati. Unaweza jiuliza mwisho wa siku, hili kundi linakuwa linachukuliwa vipi katika jamii. Hakuna anayejali!

Pili, shule kama SUMVE GIRLS na BUJIKU zimeonekana walau kufanya vizuri katika mfululizo wa takribani miaka 3 sasa. Japo sio kwa kiwango kinachotakiwa lakini hatuna budi kuwasifia na kuwatia moyo zaidi. Wakati shule kubwa kama NGUDU, NYAMILAMA, MWAMASHIMBA  na nyinginezo zimeendelea kuzorota kadri miaka inavyokwenda. Hawapaswi kubweteka hata kidogo japo kwa ufaulu huu mdogo, inawapasa kutia bidii na juhudi zaidi.  Hakuna anayejali!

Tatu, Mkoa umeendelea kubeba sifa katika kufanya vizuri kitaifa kwa miaka kadhaa sasa, huku wilaya ikimezwa katika mafanikio hayo. Japo ukifatilia ufaulu kwa ngazi ya wilaya, wilaya hii imekuwa ikiburuza mkia mara kwa mara. Viongozi wanayajua haya fika na hakuna hatua wanayochukua pengine kunusuru hali hii.  Hakuna anayejali!

Nne, wenye dhamana ya kusimamia hii elimu yetu naweza kusema wanajiita wanaharakati waliojipambanua. Kwamba kufeli kwa shule za wilaya hii sio sababu na pengine hawastuki kabisa, bali wanachukulia mafanikio ya mkoa zaidi. Sina imani kama matokeo mabovu haya yanachagizwa na mrundikano wa madai ya walimu juu ya stahiki zao. Na kama pengine ndivyo ilivyo nani anapaswa kunyooshewa kidole, serikali, CWT na walimu kwa ujumla, au nani?

Sikuona ajabu nilipoona taarifa mwishoni mwa mwaka jana kwamba, zaidi ya walimu 300 wakitishia kugoma kufundisha kushinikiza stahiki zao toka serikalini. Na viongozi wao wapo pengine wameshindwa kufuatilia masuala haya kiundani au pengine ni ugumu wa serikali katika kuwasikiliza na kutatua changamoto zao. Hakuna anayejali!

Kila mmoja wetu anahusika kwa namna moja au nyingine katika kushauri na kuchangia namna bora ya kupata mafanikio.

Sasa tupo katika awamu mpya ya HAPA KAZI TU. Iliyojipambanua kinagaubaga kuhakikisha elimu inatolewa bure kuanzia msingi hadi sekondari. Japo cha kujiuliza ni kwamba, je, ni kweli kwamba matokeo yetu mabovu yataondolewa kwa kuwapo kwa elimu bure pekee?

Kama elimu bure itazingatia na kumjali mwalimu kwa kumtengenezea mazingira mazuri katika kazi yake, pia kuiboresha kiasi cha kumfanya mwanafunzi kufuata taratibu na sheria. Kama elimu hii itatatua changamoto zote kwa ujumla zinazoikabili sekta hii, bila shaka matunda tutayaona. 

Vinginevyo kama ni katika kupunguza mzigo kwa mzazi katika michango, ada na mengineyo siamini kama tutapiga hatua mbele zaidi ya kuzidi kurudi nyuma miaka yote daima dawamu.

WATAALAMU KATIKA SEKTA HII NA WACHAMBUZI WANASEMAJE?

Itawawia vigumu mno wanafunzi hawa waliofeli(Div iv na 0) kupata ajira kwani hawana maarifa ya msingi ya kusoma, kuandika na kuhesabu. Pia wanakosa stadi za msingi za maisha kama kujiamini, ubunifu na mbinu za kutatua matatizo. .

Walimu ni sehemu muhimu katika kuleta elimu bora. Elimu bora inahusiana moja kwa moja na ufundishaji bora na ujifunzaji bora. Kuna mambo mengi yanayoukilia ufundishaji bora, miongoni mwayo ni sifa na uzoefu wa waalimu, kiwango cha hamasa waliyo nayo, moyo wa kujituma na hisia za kufundisha na mazingira ya kazi.. (HAKI ELIMU).

Sababu kadhaa zimetajwa kuwa chanzo cha hali duni ya elimu hapa nchini. Mosha (2011) ameeleza kwa muhtasari sababu hizo, akiziweka katika makundi  makuu mawili, ambayo ni: sababu za kimazingira na sababu za vitendea kazi. Kwa mujibu wa Mosha, sababu za kimazingira hujumuisha mazingira ya kisiasa, kiuchumi, kisheria, kidemografia,  kiutamaduni na kimataifa. Sababu za vitendea kazi hujumuisha uongozi duni katika taasisi, ufadhili duni kwa sekta  ya elimu, hali duni ya miundombinu ya kufundishia na kujifunzia, walimu wenye sifa duni na matatizo ya mitaala....(MOSHA 2011)

Mabadiliko katika elimu barani Afrika yamelenga zaidi kuongeza idadi ya  watu wanaopata elimu, huku ubora wa elimu inayotolewa ukipewa umakini mdogo.. (Odulo, Dachi & Fertig, 2008)

 Ni imani yangu kwamba, tathmini na maelezo yangu kwa ujumla yatakuwa yamewafikia na kueleweka wana KWIMBA popote mlipo, iwe chachu kwa wadau na wataalamu katika sekta hii kutoa ushauri bora juu ya kuinusuru elimu yetu na vijana/wadogo zetu ambao ndio mwanga na taifa la leo na kesho katika kuleta maendeleo endelevu kwenye jamii yetu.

Mwandishi maarufu wa marekani, Magret mead, aliwahi kutamka "never doubt that a small group of thoughtful, committed citizens can change the world; indeed, it's the only thing that ever has"
akiwa na maana kwamba, tusiwe na shaka kwamba kikundi kidogo cha wananchi wenye fikra, wenye kujituma kinaweza kugeuza dunia.kawaida wanaweza kuungana, kupashana habari, kujifunza, kupanga na kutenda kwa ajili ya kuleta maendeleo.


Tafakari!
KWIMBA TUITAKAYO
nguduone@gmail.com





1 comment:

Previous Page Next Page Home