Friday, April 22, 2016

DIWANI JONATHAN MALIFEDHA NA KATA YA NGUDU

Mgombea wa CCM ngazi ya udiwani ndugu Jonathan Malifedha akiwa jukwaani kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana 2015
BY NGUDU NYUMBANI BLOG.
23/04/2016

Kata ya NGUDU ni mojawapo ya kata 15 zinazounda jimbo la KWIMBA, ambapo halmashauri ya wilaya inaundwa na majimbo mawili ya uchaguzi, Kwimba na Sumve na kila jimbo likiwa na kata 15.

Unapozungumzia wilaya ya KWIMBA ni lazima uzungumzie kitovu cha wilaya, makao makuu ya wilaya na picha au muonekano halisi wa wilaya ndipo utagundua NGUDU ndiyo inabeba sifa zote hizo. Ngudu kama tarafa inayounganisha maeneo kadhaa ya kata, pia ni kama kata inayounganisha maeneo kadhaa ya vijiji, vitongoji n.k
Kata ya Ngudu(Mamlaka ya mji mdogo wa ngudu) Inaundwa na vitongoji kama, Chamhela, Ngudu mjini, Kakora, Igoma, Sokoni, Ngudulugulu, Budula, Bugakama, Ngumo, Shuleni,Ilamba, Kilyaboya, na Welamasonga

Makadirio ya wakazi wa kata ya Ngudu kwa mwaka jana(2015) ni watu 29,837 na idadi iliyokadiliwa kwa watu wenye miaka 18 na kuendelea ni 14,428, haya makadilio yalifanyika kwamba, kufikia mwezi October kata itakuwa na idadi hiyo. Ikumbukwe pia katika Sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2012, kata hii ilikuwa na jumla ya wakazi  27,630.
Kata ya NGUDU ina Shule za msingi kama, Budula, Chamhela, Igoma. Kilyaboya, Kakora, Welamasonga, Ngudulugulu, Ilumba na Ngumo. Kwa upande wa shule za sekondari kuna Bujiku Sakila na Ngudu sekondari

MUUNDO WA KATA
Kwa mujibu wa jumuiya ya tawala za mitaa nchini (ALAT) kwenye KIONGOZI CHA MADIWANI, ngazi ya Kata, kwa mujibu wa Sheria, siyo mamlaka ya utawala bali ni ngazi inayowezesha Mamlaka za Kijiji na Halmashauri ya eneo lake, kwa kutekeleza shughuli za uratibu kupitia Kamati ya Maendeleo ya Kata.
Kamati ya Maendeleo ya Kata
Katika Ngazi ya Kata utendaji wake huwezeshwa kupitia kamati ya maendeleo ya kata
ambayo sura 287 na 288 za sheria zimeelekeza kuwa na muundo ufuatao.
Wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Kata ni wafuatao:-
- Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata ambaye ni Diwani anayewakilisha
Kata;
- Wenyeviti wa Vijiji/Mitaa yote katika Kata;
- Diwani wa Viti maalum Mkazi wa Kata husika;
- Watu walioteuliwa na Kamati ya Maendeleo ya Kata kutoka Mashirika yasiyo ya
Serikali na vikundi vya kijamii (lakini hawaruhusiwi kupiga kura);
- Afia Mtendaji wa Kata – Katibu.
Pia wameelezea aina za kamati za kudumu kwenye halmashauri ya wilaya kuwa ni; Fedha, Utawala na Mipango, Afya, Elimu na Maji. Pia kuna Uchumi, ujenzi na mazingira. Kuna kamati ambazo sio za kudumu kama Kamati ya maadili, kamati ya UKIMWI bali ni kamati za majukumu maalum katika halmashauri ingawaje zinafanya kazi kwa utaratibu wa kamati za kudumu.

Uundaji wa kamati ndogo ya kudumu ulisitishwa na unahitaji kibali maalumu kutoka kwa waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa.
 Inashauriwa na kuelekezwa kwamba, kikao/mkutano wa kamati ya maendeleo ya kata kukutana kila baada ya miezi mitatu na wakati mwingine wowote kulingana na dharura.

KUHUSU DIWANI
Kuna dhana kadhaa zinazomwelezea diwani kuwa ni mtu wa aina gani. Kwanza Diwani ni mwakilishi wa wananchi kwenye kata. Pili, diwani ni mjumbe wa mamlaka za serikali za mitaa(halmashauri ya wilaya/mji). Na pia diwani anaelezewa kama mwenyekiti wa maendeleo wa kata.
Majukumu ya Diwani yapo wazi, ambapo kubwa ni kusimamia rasilimali na sheria. Pia kuwakilisha wananchi kwenye shughuli zote za maendeleo kwenye kata na halmashauri kwa ujumla.
Diwani si mwajiriwa wa Halmashauri, bali ni “Mwakilishi wa watu”, na hivyo anawajibika kwa watu anaowawakilisha na wakazi wa eneo la Halmashauri yake.” (policy forum)
Diwani si Mtendaji, bali ni Kiongozi na Mwakilishi wa wananchi hivyo hapaswi kuingilia utendaji wa idara yoyote katika Halmashauri kwa maslahi yake binafsi
Diwani pia analo jukumu zito la Kuwashirikisha wananchi katika kuainisha vyanzo vya mapato, mahitaji, fursa na vipaumbele vyao. Kuhakikisha ukusanyaji na matumizi sahihi ya mapato n.k
Awe ni mtu wa kusimamia misingi na sifa za utawala bora. Nikimaanisha Demokrasia, Ushirikishwaji, Utawala wa Sheria, Uwazi, Uwajibikaji, haki, usawa na uadilifu na wakala wa mabadiliko ya kweli.
Hali Kadhalika, kwa kata ya NGUDU diwani wa kuchaguliwa ni Mh. Malifedha. Japo kuna diwani wa kuteuliwa(viti maalum) atakuwepo bila shaka. Kwa wilaya nzima ya Kwimba kuna viti maalumu 11, ambapo 9 ni kutoka CCM, mmoja kutoka CDM halafu mmoja alisubiriwa kupatikana baada ya uchaguzi kata ya Bupamwa. Hii ni kulingana na maelezo ya NEC na kama uchaguzi kata ya Bupamwa umekwisha fanyika basi kuna utaratibu wao kujua ni kutoka chama gani.

Mantiki yangu ni kwamba, tukizungumzia kata ya NGUDU lazima tujue kuna wawakilishi zaidi ya mmoja. Kwamba katika hao 9 wa CCM kuna ama mmoja anatoka kata ya Ngudu. Pengine nahisi(japo sina uhakika) Mh. Lucy Cypriani Nchangwe akawa anatokea kata hii sababu jina hili sio geni sana. Pia kwa waliofatilia orodha ya viti maalum kwa wilaya yetu wanaweza kutusaidia ni nani hasa anawakilisha/anatokea kata yetu, na kama hakuna pia tujue.

HARAKATI ZA UCHAGUZI.
Kata ya NGUDU ni mojawapo ya ngome ya chama tawala kwa miaka yote. Sina taarifa kwa miaka ya nyuma walipata kuongoza wakina nani, ila najua kuanzia enzi za kina NGASA akaja FAISAL na sasa MALIFEDHA.
Mchakato wa kumpata mrithi wa diwani aliyemaliza muda wake  kata hii ndani ya CCM ulihusisha makada kadhaa, ambapo mwisho wa siku matokeo yalikuwa kama ifuatavyo;
1-JONATHAN MALIFEDHA (MFURUKI)-124.
2-JOHN IBRAHIM NGASA-51.
3-MUSA TEMBE-26.
4-RICHARD CHARLES-21.
5-SIRAJI KABYEMELA-17.
6-JOSEPH NCHANGWE-6.
7-MUSA BULUBA (FATHER KISS)-6.
Unaweza kuona ndugu Malifedha aliwaacha wenzie kwa mbali(kura zake ni karibia mara mbili ya jumla ya kura za wagombea wenzake 6) hivyo kuipeperusha bendera ya chama ngazi ya udiwani. Upande wa upinzani napo ulipita mchujo kumpata mmoja wa kugombea kwa nafasi hiyo.
Kipindi cha kampeni vyama vyenye wagombea vilijinadi majukwaani kuomba ridhaa ya wananchi kutaka kuongoza kata ya Ngudu.

Nilipata kuhudhuria mikutano baadhi kuwasikiliza wagombea wakinadi sera zao juu ya uwakilishi wa kata yetu. Kiukweli sikupenda zile kampeni zilizojaa dhihaka, ndaro na shere hasa ukizingatia propaganda chafu(naziita za kishamba) zilizoendeshwa na wananchama na (wakati mwingine wagombea wenyewe) hasa wa CDM na CCM.

Binafsi nilibaki na imani yangu kwamba sio tu Kata bali Jimbo zima hatujapata watu wazuri(washindani) katika nafasi hizi kama tukitumia vigezo vya kuwasikiliza wanavyojinadi majukwaani. Japo wapo wachache wanaojitahidi ila wengi wao bado sana licha ya kuwa na ufuasi mkubwa lakini ukiwapima kwa wanachosema(sera, hoja, mikakati yao n.k) unaweza ungana na mimi kama tu sio mkeleketwa wa chama. Kulikuwa na arijojo nyingi sana kimsingi.

Propaganda nyingi zilikuwa za kipuuzi, mara mgombea Fulani hajaoa kwahiyo hafai, mwingine kalazimishwa kubadili dini ili apate nafasi kwenye chama. Mwingine mara ana madeni kibao anadaiwa hivyo hafai. Wengine wanadiliki kutumia kigezo cha jinsia kumnadi mgombea wao kama ni bora kwa sababu anapambana na jinsia tofauti na mengine mengi.

Kwa jinsi ushabiki ulivyokuwa hasa kwa vyama hivi viwili vyenye wafuasi wengi, upepo ulivuma sana CDM alipokuwa Mama Senga(Thereza Jackson) na wengi tukaamini kwa mara ya kwanza kata inaenda upinzani. Hata wana CCM wengi walianza kuamini hivyo, lakini chini ya usimamizi wa diwani aliyemaliza muda wake na chama kwa ujumla waliweza kutumia nguvu za ziada ama kwa njia halali au laa ilimradi mgombea wao aibuke kidedea.
Matokeo ya  mwisho ya udiwani Kata ya Ngudu  malifedha john(CCM) kura 4451, thereza Jackson(cdm) kura 3836, Augustine Lusimbya(Act) kura 54.
Baada ya uchaguzi kuisha, ndipo zikabaki stori mitaani kila mmoja akiwa na lake kuhusu uchaguzi.
Kuna mtazamo mmoja kwamba wengi waliamini, mgombea wa CDM hakupewa ushirikiano na wanawake wenzie ambao kwa kiasi kikubwa ndio mara zote hujitokeza kupiga kura. Kwa upande mwingie pia vijana wengi walikuwa hawamkubali mgombea wa CCM ambaye ni kijana mwenzao pia.
Sambamba na hilo kuna kauli kadhaa zilisikika na kuandikwa kutoka pande tofauti. Mojawapo iliyoleta msisimko nimeinukuu hapa..“WANANGUDU HUYO KIJANA HATUFAI KUWA DIWANI WETU WA NGUDU HUYO MALIFEDHA KAWEKWA KUWA DARAJA LA MASULI NA FEISA WAMEUNDA PEMBE TATU WANANGUDU BILA SISI KUJUA NIHIVI MASULI AKIPITA KATIBU WA MBUNGE FEISA NA DIWANI MALIFEDHA AWA DARAJA TUMPIGENI CHINI WANANGUDU HUYO BONGE LA FALA ” Chambilecho Bundalah Simon.

Kwa kauli hii na nyinginezo zilikuwa na mitazamo tofauti miongoni mwa wafuasi wa vyama hivi na hata wasio na vyama. Wengine wakiungana nazo na wengine wakipingana nazo, japo sio kwa  aliyepinga wala kuunga mkono kauli alikuwa na sababu za kufanya hivyo bali wengi walifanya kwa mapenzi yao binafsi.
Aidha, siku moja nikiwa zangu kwenye ofisi ya WEO nilijikuta katika mazungumzo na mtu ambaye baada ya kumsikiliza kwa muda nikagundua alikuwa ni mgombea mmojawapo kwenye nafasi ya udiwani.  Japo sikuweza kufahamu ni kutoka chama gani, sababu kubwa ikiwa kwamba sikupata kumwona jukwaani wakati wa kampeni na pia mimi sikuwa mmoja ya waliopiga kura kwenye uchaguzi kwa sababu ambazo hazikuweza kupatiwa ufumbuzi. Hasa ukizingatia nilijiandikishia sehemu tofauti kabisa na wilaya yetu.
Katika maelezo yake alisema aliamua kutokupiga kampeni kwa sababu aliamini kwa muda huo hatapata kusikilizwa kama ilivyo kwa wagombea kutoka vyama vikubwa. Ila lengo lake lilikuwa kuweka utambulisho ili awamu nyingine iwe rahisi kwake.
Hali hii naambiwa ilijitokeza pia kwenye kura za maoni ndani ya CCM pale Ndugu Musa Tembe. Baada ya kuchukua fomu, inasemekana alikatazwa ama na ndugu au watu wake wa karibu kujihusisha na siasa hasa kugombea nafasi hiyo. Lakini cha ajabu akashika nafasi ya 3 licha ya kutofanya harakati zozote kujinadi kwa wana CCM wenzie.
Kingine ninachokikumbuka, baada ya wagombea wa CCM kushinda kwenye Ubunge na udiwani. Wanachama wanazi(hasa wanawake wakiambatana na watoto) walifanya maandamano kuzunguka maeneo kadhaa(soko la zamani-soko mjinga na kwingineko) huku wakiwa wamebeba mfano wa jeneza wakimaanisha wanakizika chama cha upinzani(CDM) na baadae kuliteketeza.
 Kwa mtazamo wangu walikuwa sawa kufanya walichofanya, japo sikuona mantiki ya kubeba lile jeneza, sababu wao ndiyo wameongoza miaka yote hivyo kama angeshinda wa upinzani basi ingeleta maana kimsingi. Eniwei waliofurahi walifurahi na waliochukia walifanya hivyo pia na maisha yakaendelea.

Sasa ni wakati wa kufanya kazi kwa kuwa uchaguzi na harakazi zote zimepita. Ila ni vyema kumbukizi kama hizi tukazieleza na pengine kuzitunza kwa matumizi ya baadae endapo zitahitajika.

USHAURI NA MAPENDEKEZO YANGU..
Kuna mambo baadhi ambayo ningependa kuyagusia katika kata yetu ya NGUDU nikimhusisha diwani moja kwa moja.

UTEKELEZAJI WA MIRADI NA UWAJIBIKAJI
Diwani anawajibika kusimamia miradi yote iliyo chini ya kata yake akishirikiana vizuri na viongozi wa chini yake nikimaanisha uongozi wa kijiji, kitongoji na mtaa. Na katika kila hatua mwananchi anapaswa kushirikishwa kujua Mipango inavyoenda na pengine kupewa nafasi ya kutoa ushauri nini kifanyike katika kuboresha mambo. Mbali na kata diwani anapaswa kuisimamia halmashauri yote kwa ujumla.

Kwa takwimu jinsi zilivyo, kata ya Ngudu ndiyo kata yenye wakazi wengi zaidi kuliko kata zote zinazounda halmashauri ya wilaya. Hivyo hata kwenye mfuko wa jimbo fungu lake lazima litofautiane na kata nyingine. Lakini(kwenye maeneo mengi) mwananchi ashirikishwi kujua mapato na matumizi ndani eneo lake. Kwa hatua hiyo ndipo viongozi hujipangia na kutumia fedha za miradi kwa sababu wanajua wananchi hawajui kinachoendelea. Na imani awamu hii mambo hayatafanyika kwa mazoea bali yatafanyika kwa ufanisi na uwazi zaidi.

Ukisoma ripoti kadhaa za CAG kuhusu ukaguzi wa taarifa za fedha za mamlaka za serikali za mitaa utangundua uzembe mwingi umekuwa ukifanyika na baraza wa wawakilishi(madiwani) ama kwa kujua au kutokujua wamekuwa wakikaa kimya bila kupinga na pengine kuchukua hatua juu ya vitendo viovu vinavyofanyika.

Mfano taarifa moja inaonesha halmashauri ya wilaya ya KWIMBA inaongoza kuwa na matumizi yasiyo na hati za malipo. Pia malipo yasiyo na vibali(malipo hayakuidhinishwa na baraza la madiwani), ushindanishaji wa zabuni, kununua vifaa bila kuviingiza katika leja.

Pia ripoti inaonesha takwimu za utoaji wa hati ambapo kwa halmashauri yetu ilipata hati inayoridhisha mwaka 2009/10 na 2011/12. Ikapata hati zisizoridhisha(hati yenye shaka) kwa mwaka 2010/11, 2012/13 na mwaka 2013/14. Baraza linawajibika katika kuisimamia halmashauri hivyo diwani wangu hapaswi kufanya mambo kwa mazoea bali afanye kile ambacho watangulizi wake walishindwa kukisimamia.

Na bahati nzuri ni kwamba wizara inayohusika(TAMISEMI) sasa ipo chini ya mtumbua majipu mkuu. Na katika hatua za mwanzo katika kubaini watumishi hewa, Mkoa wa MWANZA ndiyo unaongoza kuwa na watumishi hewa wengi zaidi.

JUKWAA LA KWIDECO
Kwa maoni yangu na wadau waliogusia suala la Jukwaa la Kwideco, Diwani anakuwa kiongozi wa kwanza kuhusika katika kulifuatilia na kulitatua tatizo hili. Kwa sababu yeye anaweza kuonana na wahusika wote(Mbunge, mkuu wa wilaya, Afisa michezo, baraza la madiwani, Mkurugenzi n.k) kuwafikishia pendekezo juu ya ukarabati wa jengo na mengine mengi yahusuyo uwanja wetu wa wilaya. Kwangu mimi nitampima katika kulifanikisha hilo ndani ya miaka mitatu ya mwanzo kwenye uongozi wake.

Mbali na ukarabati wa jengo, suala la michezo lichukuliwe kama suala zito na muhimu sana. Nasema hivi kwa sababu kupitia michezo ndipo tunatengeneza ajira kwa vijana wetu, ila ajabu vijana hawa huletewa jezi kipindi cha kampeni na kuwa na ligi ila mhusika akifanikisha kushinda ndio imetoka. Inabidi tuwekeze kwenye michezo kwa ngazi ya wilaya tupo nyuma sana na sio kama hakuna watu wazuri ama timu nzuri bali hatuna uongozi mzuri. Hata ule ukumbi wa KWIDECO  unaendeshwa visivyo tofauti na ilivyokuwa zamani hii ni kwa mujibu wa wadau.

Mgombea wa CDM Thereza Jackson aliapa endapo atashinda uchaguzi kipindi kile, jukwaa la KWIDECO ataanza nalo katika vipaumbele vyake.

FURSA ZA UJASIRIAMALI
Kiongozi yeyote anayo nafasi kubwa katika kuona fursa zilizopo kwenye eneo lake na kuweka mikakati ili ziwanufaishe wananchi wake. Hivyo ni imani yangu kwamba, diwani kabla hata hajawaza kugombea lazima alikuwa anajua maeneo ambayo yakitiliwa mkazo yanaweza kutengeneza ajira na fursa kwa wakazi wa Ngudu. Baadhi ya maeneo kama kilimo cha umwagiliaji, ufugaji wa kuku n.k

Vikundi kadhaa vinaweza kuundwa na kiongozi kuweza kuangalia namna ya vikundi hivyo kuwezeshwa ili vifanye kazi mbalimbali za kijasiriamali. Niliwahi kuongelea mambo ya KWIWODE, SHIKOME  na vikundi vingine kujua maendeleo yake lakini hakuna anayejua na vilikuwepo wilaya yetu.

SOKO JIPYA NA MNADA
Katika mpango wa muda mrefu wa halmashauri katika sera ya mpango miji wapo sahihi kabisa kutanua eneo japo sina hakika kama lile eneo lilikuwa sahihi kujenga. Lakini licha ya Mipango ya muda mrefu lazima kuwe na Mipango ya muda mfupi ambayo inapaswa kutekelezwa. Soko lile mara moja moja utakuta wafanyabiashara wadogo wadogo wanauza licha ya uchache wao. Pia kuna bucha inahudumia pale japo bado haijazoeleka na kuwekewa mazingira mazuri ya biashara kwa wakazi wa kata hii na wilaya kwa ujumla.

Kwenye suala la mnada, baadhi yetu wanasema gulio letu liboreshwe liwe na muonekano mzuri ili watu waweze kufanya biashara zao kwa uwazi. Japo siafik kwamba lifanyike kwa siku mbili ndani ya wiki moja kama ilivyowahi kusemwa kutoka kwa mdau mmoja.

JUKWAA LA WANA KWIMBA
Hili wazo nimekuwa nalo tangu zamani kwamba, kuna haja ya kuwepo kwa jukwaa la wanaKwimba la wazi ambapo litahusisha lika zote kujadili masuala yetu kwa uwazi na upana zaidi. Kunakuwa na mijadala ambayo shabaha yake kubwa ni kuibua ari na kuchochea utendaji kazi wa kila mmojawetu kwa nafasi yake. Kunakuwa na eneo maalumu(mfano ukumbi wa Kwideco), siku maalum na muda maalum kwa wote wanaopenda kujadili kukutana pamoja na kubadilishana mawazo kuhusu jamii yetu.

Mbali na hilo linaweza kuwepo jukwaa la mtandaoni(social network forum) ambapo kunakuwa na utaratibu maalum katika kujadili masuala mbalimbali, hapa litawahusu hata walio mbali na nyumbani kushiriki kwa ukamilifu zaidi. 
Pia tunaweza kuanzisha toleo la KWIMBA kwa maana ya gazeti, jarida au kitu kama hicho kila baada ya muda Fulani(mfano kila mwisho wa wiki) linalojadili mambo ya Kwimba katika nyanja mbalimbali. Haya yote yanaweza kwenda sambamba na uwepo wa tovuti ya wilaya kama ambavyo naliongelea hili suala kila leo.

Wapo wachache miongoni mwetu walioweza kuona kazi na umuhimu wa NGUDU NYUMBANI BLOG kwa inachokifanya na kutoa pongezi zao. Ila kama kiongozi anatakiwa kula yamini juu ya suala hili naamini hakuna litakaloshindikana. Napenda nieleweke kwamba nimeongelea kwa diwani wetu japo nikilenga kwa kata zote kuhusika katika hili kwa maana ya wilaya nzima.

SUALA LA ELIMU.
Katika tathmini yangu niliyowahi kuiandika huko nyuma, nikiongelea matokeo ya kidato channe. Nilizungumzia shule kongwe ya NGUDU kama moja ya shule zenye matokeo mabovu kupindukia licha ya kuwa na mazingira mazuri tofauti na shule nyingine katika wilaya yetu. Pia shule ya Bujiku imeendelea kujitahidi japo si kwa kiwango kinachotakiwa. 
Hivyo ni jukumu la diwani kushirikiana na wahusika katika sekta hii kusaidia shule zetu zifanye vizuri. Mbali na sekondari kuna shule za msingi pia ambazo nazo changamoto zipo lukuki ikiwa ni pamoja na matokeo mabovu. Zoezi hili ningependa lihusishe shule zote za wilaya yetu.

KUGAWANYWA KWA HALMASHAURI ZIWE MBILI.
Kupitia baraza la wajumbe(madiwani), anaweza kuwa na hoja hiyo ya kugawanywa kwa halmashauri yetu tuwe na halmashauri mbili yaani halmashauri za Kwimba na Sumve. Suala hili pia nimewahi kuliongelea huko nyuma ila likaonekana kuwa zito miongoni mwetu. Naamini kama baadae watagawanya, kutakuwa na hatua nzuri zaidi ya kuwasogezea wananchi huduma na kuhalakisha maendeleo.

Kuna mengine mengi ambayo anaweza kuyafanya ambayo kwa upande wangu naona yapo kwenye majukumu yake muhimu ya kila siku kama kusimamia zoezi la ugawaji na upimaji wa viwanja, kusuluhisha migogoro, masuala ya afya na mengine mengi ambayo ni lazima ayasimamie kikamilifu.

Mwisho, natambua uwepo wa mawazo kinzani katika kila mtazamo. Mimi ni muumini mzuri wa dhana ya KUKUBALI KUTOKUKUBALIANA. Ila sifurahii mtu anaposhindwa kujadili kilichowasilishwa na hatimaye ama kumshambulia mtoa hoja au mwandishi. Siku zote tunajadili kilichopo mbele yetu na sio kumjadili aliyekileta. Tunapinga vitu kwa hoja na tunasifia pia alipokugusa na kumwelewa mwandishi.

Nimtakie uwakilishi mwema diwani wa kata ya NGUDU, panapo majaliwa. Japo nitahitaji aniaminishe(kupitia uwajibikaji wake) kuwa tatizo la baraza letu(madiwani) sio chama cha mapinduzi bali ni mwakilishi mmoja mmoja. Vinginevyo nitaendelea kuamini kuwa CCM ndiyo inatuletea viongozi dhaifu na ndio sababu ya kuwa nyuma siku zote hivyo tusikubali(awamu nyingine) hata wakibadilisha wagombea bali tujipange kuindoa kama suruhu ya matatizo yetu na mwanzo mpya wa KWIMBA TUITAKAYO.

Mimi kama kijana naamini katika kijana mwenzangu katika kuleta maendeleo ya kweli. Makala hii iwakilishe na kata nyingine zote lengo ni kuona jamii yetu kwa ujumla inasonga mbele. mnisamehe kwa maelezo yangu marefu yenye kuchosha..

Tafakari!
nguduone@gmail.com


No comments:

Post a Comment

Previous Page Next Page Home