Monday, May 11, 2015

Diwani CUF Mbaroni kwa Tuhuma za Kuomba na Kupokea Rushwa ya Sh 150,000 wilaya ya KWIMBA


DIWANI wa Kata ya Ngula wilayani Kwimba, Palu Mashagu (CUF), anashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya Sh 150,000.

Taarifa kutoka Kwimba na kuthibitishwa jana na Kamanda wa Takukuru, Faustine Maijo, ilisema Mashagu alikamatwa Mei 6, mwaka huu mchana katika ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Ngula akidaiwa kuomba na kupokea Sh 150,000 kutoka kwa mtumishi wa Halmashauri ya Kwimba, Nyabugumba Jonathan.

Mashagu ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF wilaya ya Kwimba anadaiwa kuomba na kupokea kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kumsaidia mtumishi huyo pamoja na wenzake wanne waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma za ubadhirifu wa Sh milioni 72 za mradi wa usafi na mazingira.

Kutokana na tuhuma hizo kufika katika vikao vya Halmashauri ya Kwimba, kikao cha Baraza la Madiwani kiliazimia kufanya uchunguzi wa tuhuma hizo na kuunda kamati ya madiwani watano chini ya uenyekiti wa Diwani wa Nkalalo, Enos Ntwale, kuchunguza wizi wa fedha hizo kabla ya hatua nyingine dhidi ya wahusika kuchukuliwa.

Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Shija Malando (Kata ya Hungumalwa), Peter Msalaba (Kata ya Nyambiti), Tabu Samson (Viti Maalumu) na Mashagu.

Akizungumzia taarifa za diwani wake kutiwa mbaroni kwa kosa la rushwa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kwimba, Zephania Masangu, alisema amepokea taarifa hizo lakini hajui undani wake na kubainisha alikuwa miongoni mwa wajumbe wa kamati yake aliyounda Aprili 29, mwaka huu.

“Kamati niliyounda ilishakamilisha kazi yake na taarifa kukabidhiwa sasa maelezo zaidi nadhani wanajua waliomkamata mngewauliza wao,”alisema Masangu.

Akizungumzia suala hilo mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo aliyekataa jina lake kuandikwa  alidai taarifa walizopokea katika kamati yao zimedai Mashagu aliomba rushwa ya Sh 500,000 kwa Ofisa Afya Msaidizi aliyetoa taarifa Takukuru ndipo ukawekwa mtego na kumnasa akipokea Sh 150,000.


Chanzo:  mpekuzihuru

No comments:

Post a Comment

Previous Page Next Page Home