Monday, June 8, 2015

MWANZA : Takukuru yawaburuza kortini vigogo watatu wa Serikali


TAASISI ya Kupambana na Kudhibiti Rushwa nchini (TAKUKURU) imewaburuza mahakamani vigogo watatu  wa Serikali  kwa makosa mawili ya matumizi mabaya ya madaraka na   kutumia nyaraka mbalimbali kumtapeli mwajiri wao.

Vigogo hao ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Mkoa wa Shinyanga, Patrick Karangwa (45), Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mkoa wa Mwanza, Ntinika Paul (51) na Mhasibu Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mathayo Masuka.

Walifikishwa wiki iliyopita katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana Mkoa wa Mwanza,  mbele ya Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Janeth Masesa.

Ilidaiwa kuwa watuhumiwa hao walitenda makosa hayo mwaka 2009 wakati wakiwa wafanyakazi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

Ilielezwa kuwa wakati wakitenda makosa hayo, Karangwa alikuwa Mchumi Mkuu Jiji la Mwanza, Paul   alikuwa mweka hazina mkuu  wa jiji hilo wakati  Masuka alikuwa mkaguzi wa ndani wa jiji la Mwanza.

Watuhumiwa hao walikana mashtaka hayo na wapo nje kwa dhamana na  kesi hiyo inatarajiwa kutajwa tena Juni 11 mwaka huu.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Kasomambuto Mbengwa, alithibitisha taasisi hiyo kuwakifikisha vigogo hao mahakamni.




No comments:

Post a Comment

Previous Page Next Page Home