Wednesday, February 10, 2016

MCHANGO WA CHUO CHA MALYA KWA MAENDELEO YA MICHEZO


(Makala hii ipo katika toleo la gazeti la habarileo la may 9 2015)
MICHEZO ni afya walisema wahenga tangu enzi za mababu zetu. Nami sina budi kukubaliana na msemo wa wahenga hawa kwani nimeshuhudia michezo ikijenga afya na kudumisha undugu ama kujenga urafiki.
Mafanikio na maendeleo ya michezo Tanzania ni matokeo ya muda mrefu ya juhudi za serikali kwa kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha taifa linapata wanamichezo wenye vipaji na kuwaendeleza ili wafikie ndoto za kutwaa ubingwa kwenye mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Katika kuzungumzia mafanikio haya ya michezo na maendeleo ya taaluma hii, makala haya yatajikita zaidi katika kuzungumzia chuo pekee cha kuzalisha wataalamu na walimu wa michezo Tanzania, Chuo cha Michezo cha Malya.
Chuo hiki cha michezo kabla ya kuanzishwa kwake, eneo la Malya lilianzishwa na wakoloni wa Kijerumani waliotawala Tanganyika kuanzia mwaka 1914 hadi 1918.
Katika kipindi hicho, Malya ilikuwa ndio makao makuu na makazi ya Kamishina Msaidizi Kanda ya Ziwa kwa Wajerumani. Baada ya kupata Uhuru, Malya ikawa makao makuu ya wilaya mpya ya Kwimba na sehemu ambayo machifu wote wa Kanda ya Ziwa wa kabila la Wasukuma walikutana na kufanya mikutano yao.
Kwa kuwa makao makuu ya wilaya, majengo na miundombinu yote ilikuwa ni mali ya Serikali ya Tanzania chini ya mamlaka ya Mkoa wa Mwanza.
Jengo ambalo machifu walilitumia kukutana, kufanya mikutano ya mwaka na kuendesha shughuli nyingine linaendelea kutunzwa kama sehemu ya urithi wa historia kwa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, mji wa Malya na Wasukuma.
Baadaye makao makuu ya Wilaya ya Kwimba yalihamishiwa mji wa Ngudu, na mwaka 1979, Wizara ya Utamaduni na Vijana wakati huo, iliomba na kupewa kibali cha kutumia miundombinu ya majengo ili itumike kama nyumba za watumishi, vyumba vya madarasa, bwalo la chakula, jiko pamoja na ofisi mbalimbali na kiwanja cha mpira wa miguu kwa ajili ya maendeleo ya michezo pamoja na maendeleo ya vijana.
Lengo kubwa la chuo hiki ni kuwa kitovu cha kuzalisha wataalamu wa kimataifa katika nyanja za ukocha, utawala bora katika michezo, uamuzi na wachezaji mahiri. Kwa kipindi cha miaka 50 ijayo, chuo kinaazimia kuwa na miundombinu muhimu na yenye hadhi ya kuzalisha wataalamu wa michezo wenye ubora wa kimataifa na hata kuandaa mashindano yenye hadhi ya Olimpiki na michezo mingine ya burudani kitaifa na kimataifa.
Kwa sasa chuo kinatoa mafunzo bora ya michezo, kuendesha na kufanya tafiti za michezo na kutoa huduma kwa jamii kwa kuendeleza vijana katika kukuza vipaji vyao kwenye fani mbalimbali pia kuhamashisha vijana wa Tanzania kuendeleza kupenda michezo na kuitangaza nchi yetu kupitia michezo.
Mafunzo ya michezo yalianza kutolewa rasmi 1990 ambapo chuo kilianza na kozi moja tu ya elimu ya ukocha (coaching education) kwa ngazi ya cheti na waliopata mafunzo hayo walikuwa ni wanafunzi 27. Mwaka 2005/2006, chuo kilianza kutoa mafunzo kwa ngazi ya Stashahada.
Kuongezeka kwa kozi ya Stashahada kumesaidia kuongeza idadi ya wanachuo kutoka kutoka 27 mwaka 1990 na kufikia 32 mwaka wa masomo 2005/2006. Katika mwaka wa masomo 2006/2007, chuo kilipanua mafunzo ya michezo ya elimu ya ukocha kutoka mchezo mmoja wa mpira wa mikono na kufikia sita ambayo ni, netiboli, wavu, kikapu, soka na riadha.
Mwaka wa masomo wa 2007/2008, chuo kiliongeza utoaji wa Stashahada ya Usimamizi na Utawala katika Michezo na Stashahada ya Ufundishaji Elimu kwa Michezo iliyoanza mwaka wa masomo 2013/2014.
Kwa sasa chuo hiki kinatoa kozi tatu kwa ngazi ya Stashahada ikiwa ni Stashahada ya Elimu ya Ukocha, Stashahada ya Usimamizi na Utawala katika Michezo na Stashahada ya Elimu kwa Michezo.
Kutokana na kumalizika kwa miradi mikubwa ya majengo ya maktaba na sehemu ya jengo la hosteli ya wanachuo, udahili wa wanachuo wanaojiunga na masomo ulitegemea kupanuka kutoka wanachuo 60 mwaka 2011/2012 hadi kufikia wanachuo 120 kulingana na upanuzi wa miundombinu unavyoendelea.
Miundombinu ya kufundishia iliyopo ni mizuri na inavutia kwa wanachuo wanaofika kujipatia mafunzo. Hii inahusisha madarasa, maktaba zilizojaa vitabu vya kila aina vitakavyowawezesha wanachuo kupata mafunzo yaliyobora, maabara ya kompyuta, viwanja vya kuchezea vya ndani na nje.
Miundombinu mingine ni zahanati, makazi ya wanachuo, pamoja na bwalo la chakula na jiko. Kwa sasa chuo kina madarasa manne yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 150. Darasa moja lina uwezo wa kuchukua wanachuo 45 na madarasa matatu yanaweza kuchukua wanachuo 35 kwa kila moja.
Jengo lililokamilika la maktaba lina uwezo wa kuchukua wanafunzi 70 kwa wakati, maabara ya kompyuta ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 48. Chuo kina kiwanja kimoja kwa ajili ya mpira wa miguu pia viwanja vya ndani ambavyo hujumuisha michezo kama vile mpira wa mikono, netiboli, kikapu na wavu.
Baadaye, michezo kama kunyanyua vitu vizito, tenisi, mpira wa meza na mpira wa vinyoya pia utakuwa ukichezwa. Pamoja na mafunzo ya ngazi ya Stashahada yanayotolewa, chuo pia kinatoa mafunzo ya kozi za muda mfupi katika michezo mbalimbali kama vile mpira wa kengele na soka kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na vyama husika.
Katika kutekeleza mpango wa kuwajengea wanachuo uwezo mkubwa katika ufundishaji wa michezo na kuwatambulisha wahitimu kwa vyama husika, chuo kupitia Kaimu Mkuu wa Chuo, Richard Mganga, kimeendesha kozi ya mpira wa kengele (Goalball) mchezo ambao huchezwa na watu wasioona, kuanzia Januari 5 hadi 10, mwaka huu, ikihudhuriwa na washiriki 66 wanachuo na walimu kutoka katika halmashauri mbalimbali nchini.
Lengo kubwa ni kuwawezesha wanachuo kutambuliwa na mashirikisho na vyama husika na kufuata utaratibu wa mashirikisho utakaowawezesha kuwa na vyeti vinavyowaruhusu kufanya mafunzo mbalimbali kwa kuzingatia viwango vya mashirikisho na kuendelea kupata mafunzo zaidi.
Akizungumzia manufaa yatokanayo na mafunzo ya kozi fupi zinazotolewa hapo, Mganga alisema manufaa ni mengi ikiwemo wanaojiunga ni watumishi wa umma na wanahitaji kurudi kuendelea na majukumu mengine huku wakitumia mafunzo hayo kuendeleza michezo na kuwaandaa wanafunzi kushiriki katika mashindano ya Umisseta na Umitashumita.
Aliongeza kuwa, “Maofisa michezo wengi wa wilaya pia ni matunda ya chuo hiko kama vile Ofisa Michezo Wilaya ya Kwimba, Namtumbo na wengine wanaofanya kazi katika vyama au mashirikisho mbalimbali ya michezo.”
Alitoa mwito kwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo izungumze na vyama vya ndani vya michezo ili waone ni namna gani wanavyoweza kuendesha mafunzo ya kozi fupi chuoni hapo ili kuleta ufanisi mkubwa wa ufundishaji michezo kwa kuzingatia viwango vya mashirikisho ya michezo duniani.



No comments:

Post a Comment

Previous Page Next Page Home