Friday, April 1, 2016

MBUNGE WA JIMBO LA SUMVE APANDISHWA KIZIMBANI KWA TUHUMA ZA RUSHWA

Richard Ndasa, mbunge wa jimbo la SUMVE

RICHARD Ndasa, Mbunge wa Sumve, (CCM) amepandishwa kizimbani katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu shtaka la tuhuma ya kuomba rushwa ya Shilingi milioni 30, 
Akisoma mashtaka hayo wakili wa Taasisi ya Kuzia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Denis Lukayo mbele ya hakimu, Amilisi Mchaura amesema kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo akiwa kama mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma.
Amesema kwamba mbunge huyo anatuhumiwa kwa kosa la kuomba Rushwa kwa Mkurugenzi wa Shirika la Umeme (Tanesco), Felichesmi Mramba ila amsaidie kuandika mapendekezo safi ya shirika hilo.
Mbunge huyo anakuwa wa nne kupandishwa kizimbani kwa kosa la rushwa ambako tayari jana walipandishwa wengine wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ambao ni Ahmad Saddiq (53) mbunge wa Mvomero, Kangi Lugola (54) mbunge wa Mwibara na Victor Mwambalaswa (63) mbunge wa Lupa.
Kutokana na uchunguzi unaoendelea upo uwezekano wa wabunge zaidi kufikishwa mahakani kujibu tuhuma hizo ambazo zimetikisa taasisi ya Bunge ambacho ndicho chombo kikuu cha kutunga sheria.
Mbunge huyo alifikishwa majira ya saa mbili asubuhi huku idadi kubwa ya watu wakiwa wamefurika kushuhudia kesi hiyo ambayo imekuwa na mvuto kwa wananchi wengi wa jiji la Dar es Salaam.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo mbunge Ndasa alikana kutenda kosa hilo ambako upande wa serikali ulisema upelelezi bado unaendelea.

Chanzo: MWANAHALISI


No comments:

Post a Comment

Previous Page Next Page Home