Sunday, May 8, 2016

MBUNGE RICHARD NDASSA NA JIMBO LA SUMVE


BY NGUDU NYUMBANI BLOG
08/05/2016

JIMBO la Sumve ni moja kati ya majimbo mawili yanayounda halmashauri ya wilaya ya Kwimba. Ambapo linaundwa na tarafa mbili kati ya tano zinazounda halmashauri ya wilaya yaani Ngulla na Ibindo.
Jimbo pia linaundwa na kata 15, vijiji 60 na vitongoji  397. Wilaya ya KWIMBA inayoundwa na majimbo mawili ya KWIMBA na SUMVE ina  kata 30, vijiji 119 na vitongoji 870.

Kulingana na takwimu zilizotolewa mwaka jana(2015) juu ya makadilio ya idadi ya wapiga kura, jimbo hili lilikuwa na  Idadi ya watu 203,166 huku idadi ya watu wenye miaka 18 na kuendelea ni  87,993. Kata ya Maligisu ikionekana kuwa na wakazi wengi(22,449) na kata ya Bugando ndiyo yenye wakazi wachache zaidi(7,746).  

NAFASI ALIZOSHIKA
Mheshimiwa Ndassa kapata kuwa mjumbe katika kamati kadhaa zakudumu za bunge. Baadhi ya nafasi alizopata kuwapo ni kama ifuatavyo;

Kwenye bunge hili(bunge la 11) alipata kuwa  mwenyekiti wa kamati za kudumu bungeni kwenye kamati ya Uwekezaji wa mitaji ya umma(PIC).
Baadae akavuliwa  uwenyekiti na kuhamishwa katika kamati nyingine. Pia ana kesi inayomkabili ya kuomba rushwa ya mil 30(yeye na wenzake watatu), hivyo ana shitaka mahakamani.
Mwaka 2015 alipata kuwa mwenyekiti wa kamati ya nishati na madini, baada ya aliyekuwepo ndugu Victor Mwambalaswa kujiuzulu nafasi hiyo.

Mwaka 2000 alipata kuwa kaimu mwenyekiti wa PAC. Ambapo baada ya sakata la aliyekuwa waziri wa  Nchi ofisi ya Rais utawala bora Dk Hans Kitine kutumia fedha za serikali kumtibia mke wake nje ya nchi kwa kiwango cha dola za kimarekani 63,000 kinyume na utaratibu , yeye na wenzake walisimamishwa(kwa muda kuhudhulia vikao vya bunge) kwa kutoa taarifa za uongo.

 Hii ilikuwa katika bunge la mwaka 2001/2002. Kupitia kamati ya bunge ya hesabu za serikali(PAC) ambayo mh Ndasa alikuwa kaimu mwenyekiti, kamati iliandika barua Wizara ya afya ikiiagiza wizara hiyo kumrudishia mke wa Kitine pesa ambazo alikuwa ameshalipa kiasi cha dola 15,000. Kamati ilidai kugundua kwamba, Mama kitine alikuwa kweli anaumwa na alitibiwa nje ya nchi kwa kufuata utaratibu.

Ni katika kipindi ambacho ndugu Membe akiwa balozi wa Canada,  alisimama bungeni kueleza kwamba alikuwa na ushahidi bayana kuhusu ufisadi uliofanywa na Dk Kitine kwa jina la matibabu ya mke wake.
Alipopewa nafasi Membe akamwaga nyaraka muhimu zilikuwa zinaonesha jinsi fedha zilivyotumwa kwenye akaunti binafasi ya mama Kitine badala ya kutumwa katika akaunti ya ubalozi. Membe akiwa balozi wa Canada ndiye aliyepewa jukumu la kuchunguza uhalali wa matibabu na malipo ya mama Kitine. Mwisho wa siku katika hospitali zote zilizodaiwa kumtibu mama Kitine hawakupata ushahidi wowote  kwamba aliwahi hata kufika huko achilia mbali kutibiwa.

Kufuatia kuthibitika kwa kashfa ya Dr Kitine, ilionekana wazi kwamba kamati ya Bunge ilikuwa imetumika kujaribu kumsafisha Dr Kitine na familia yake. Kwa sababu hii wajumbe watatu wa kamati hii walifungiwa miezi miwili kuhudhulia vikao vya Bunge. Wajumbe hao walikuwa ni Richard Ndasa, Dk. Amani kaborou na Dk. Kitine mwenyewe.
Richard Ndasa ndiye mbunge wa kwanza kuomba wajumbe wa bunge la katiba kuongezewa posho zao za kila siku kutoka laki 3 hadi laki 7, sababu kubwa ikiwa ni kupanda kwa gharama za maisha. Ambapo katika ongezeko hilo lingeweza kusaidia kumudu mahitaji yao muhimu, pia kulipa madereva na mahitaji mengine binafsi pindi wakiwa Dodoma muda wa siku 90. Hii ilikuwa mwaka 2014 kwenye bunge la katiba. Mwanzoni hoja hii ililenga kuwasaidia wajumbe wale 201 walioteuliwa na Rais lakini baadae waliozidi kuunga mkono hoja hiyo waliibeba kama hoja ya wajumbe wote iwahusu.
Kupitia wizara ya fedha, ilitolewa taarifa iliyowataka wote wanaoona posho za sasa hazitoshi ni bora wakafungasha virago na kuondoka.

HARAKATI ZA UCHAGUZI.

Mheshimiwa Richard Ndassa kawa mbunge wa jimbo la Sumve katika awamu tano sasa ikiwemo na awamu hii. Yaani 1995-2000, 2000-2005, 2005-2010, 2010-2015, na 2015- mpaka sasa. Hii ina maana kwamba kawa mbunge katika awamu ya tatu yote chini Mkapa, kawepo kwenye awamu ya nne yote  chini ya Kikwete, na sasa yupo kwenye awamu ya 5 chini ya JPM.

Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, jimbo la Sumve lilikuwa na wagombea wanne.  NG'HOLO MALIMI LUBATULA- CHADEMA;  SHADRACK BONIPHAS GWEGWE- ADA TADEA;  MCHELE RICHARD NTUNDURU- CUF na  NDASSA RICHARD MGANGA- CCM
Matokeo ya mwisho kwenye uchaguzi huo,  Richard Ndasa (CCM) kura 20,002, Mchele Richard(CUF) kura 14,966 na Ng’holo  Malimi(CDM) kura 6,535.
Hivyo mgombea wa CCM akashinda ubunge kwa mara nyingine tena.

Mwaka 2010 kwenye uchaguzi mkuu, Richard Ndasa (CCM) alipata kura 18,705, mpinzani wake wa karibu ndugu Julius Samamba alipata kura 16,729.

Kwa mtizamo wangu, nadhani huyu ni mojawapo ya wanasiasa bora wenye kujua kucheza na akili za wananchi vyema.  Pia mwenye ushawishi mkubwa mathalan, kwenye bunge letu la JMT ndiyo maana utaona kapata kuongoza kamati kadhaa za kudumu za bunge.
Ni mwanasiasa  bora pia kwa kuweza kushinda uchaguzi katika awamu tano mfululizo au kwa maneno mengine naweza sema ni mshindi tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa kwenye jimbo la Sumve.  Jimbo lake ni mojawapo ya ngome kuu ya chama tawala ambayo haijapata kuyumbishwa hata mara moja.
Kushinda kwake katika chaguzi ndiyo kunaipa nguvu CCM kushinda katika nafasi nyingine za uwakilishi kama madiwani na Rais  na hata kwenye chaguzi  za serikali za mitaa.

Katika awamu zote alizoshinda uchaguzi na chama kupata madiwani wengi ambao wanakipa chama nafasi ya kuongoza Halmashauri wakiungana na wale wa jimbo la KWIMBA ambalo ni ngome kuu ya chama tawala pia.

Lakini pia  katika upande wa pili, ni moja kati ya wanasiasa mizigo wasiofaa kuigwa kama kiongozi kwenye jamii.

Nasema hivi kwa maana kwamba, hawezi na kashindwa kusimamia majukumu na wajibu wake ipasavyo kwa wananchi waliomchagua.  Huwezi nishawishi  kwamba, umeongoza jimbo miaka 20 lakini bado kuna changamoto nyingi ambazo nyingine zingeweza kutatuliwa kwenye miaka mitano tu ya mwanzo.

 Leo mbunge anaahidi kushughulikia tatizo la madawati mashuleni na yupo hapo miaka 20 kabla. Ndiyo kusema changamoto ya madawati imekuwa  mpya kwake hapo kabla haikuwepo?
Nimetolea mfano wa changamoto ya madawati, japo kuna changamoto nyingi ambazo kwa mwakilishi wenye sifa ya kuwa kiongozi anazijua na anaweza ama kuzitatua au kuzitolea ufafanuzi na ufumbuzi kwa kushirikiana na wananchi kuzipunguza na hatimaye kuzimaliza kabisa.
Na katika mambo yanayosababisha jimbo la Sumve na wilaya ya KWIMBA kubaki nyuma katika suala zima la maendeleo ukilinganisha na sehemu nyingine  ni uzembe wa ‘chama tawala’. Chama kilichopewa dhamana ya kuongoza jimbo,  halmashauri na serikali kwa ujumla. Ambapo wawakilishi wameshindwa  kutekeleza  wajibu wao ipasavyo wa kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika jamii yetu.

Changamoto na/au matatizo mengi yaliyopo kwenye jimbo hili  mengi ni yaleyale kama yaliyopo kwenye jimbo la Kwimba. Na chama tawala ndiyo kimeongoza majimbo haya kwa miaka yote mpaka sasa. Nilipata kuelezea baadhi nilipoongelea jimbo la Kwimba huko nyuma.
Mimi kama mwananchi wa kawaida nitapenda ama chama tawala kisifanye mambo kwa mazoea(hasa kupitisha makada wachovu) na kikubali mabadiliko ndani ya chama. Kuna watu wengi wazuri ndani ya chama ila wanakwama kwa sababu hawana rasilimali(fedha, na watu) ili kuweza kuaminiwa na chama.

 Pia nitafurahi kama upinzani utajiimalisha vizuri kiasi cha kusimamisha watu makini awamu nyingine ili kutoa ushindani mkubwa na ikiwezekana kukiondoa chama tawala katika majimbo haya kama kitaendelea na uzembe. Lengo letu sote ni kuona jamii inasonga mbele kimaendeleo na sio vinginevyo.

NAFASI YA UPINZANI.

Wapinzani katika jimbo hili wangeweza kuwa na nafasi kubwa ya kuchukua jimbo hili tangu mwaka 2010 kama wangeweza kuungana na kuonesha ari na nia ya dhati ya kutaka kumwondoa ndugu Ndasa. Unaweza kuona katika matokeo ya mwaka huo, tofauti ya kura za Ndasa na mpinzani wake ndugu Samamba ilikuwa ni kura tu 1976 katika kura zaidi ya elfu 35 zilizopigwa. Hapo hatujahesabu kura za wagombea wengine ambao pengine wangeweza kumuunga mkono ndugu Samamba na upepo ungebadilika.

Uchaguzi wa mwaka 2015 pia hali haikuwa tofauti sana, kwamba kura za wapinzani wake ambazo zilikuwa ni 21,501(CDM na CUF) dhidi ya kura 20,002 za ndugu Ndasa. Kama wangeungana(kama makubaliano yao ya awali) basi ungekuwa mwisho wa utawala wa ndugu Ndasa katika jimbo hilo.

Inasemekana upinzani hasa wale wanaounda UKAWA walikubaliana  kuachiana jimbo hili ili asimame mgombea mmoja kati ya vyama hivyo, vyama vingine vimuunge mkono. Lakini hawakuweza kukubaliana na kufikia hatua hiyo ya kila chama kusimamisha mgombea. Hatua hiyo ilimrahisishia kazi mgombea wa Ccm na hatimaye kuibuka kidedea. 
Uzembe huu ulifanyika hata jimbo la Kwimba na majimbo mengine mengi ambayo kama upinzani ungeungana vema basi chama tawala kingepoteza majimbo zaidi ya ilivyo sasa.

Kama wapinzani hawawezi kujifunza kwa makosa yao kwa vipindi viwili hivi basi msemo wa Mh. Ndasa utaendelea kutamalaki. Kwamba mgombea wa kumshinda bado hajazaliwa katika jimbo la Sumve, na kama chama kikiendelea kumwamini ataliongoza jimbo hilo kwa awamu nyingine nyingi zaidi.

Udhabidhabina, unafiki, na umimi mwingi umetawala kwenye vyama vya upinzani kiasi cha kushindwa kuheshimu taratibu wanazojiwekea na kuzisimamia haswa. Viongozi wengi kwenye chama wanamini wakigombea nafasi ndani ya chama mathalani kukiwakilisha chama kwenye ngazi flani(udiwani, ubunge) baadhi hutumia mabavu hata kama wamezidiwa na kujipitisha.

Hii ilitokea kwenye jimbo la Kwimba ambapo mgombea/mshindi wa 3(inasemekana ni mwenyekiti wa chama wilaya) kwanza hakusaini matokeo kukubaliana na pia akasimama yeye kwenye ngazi ya ubunge na kuachwa nafasi ya pili(katibu wa chama mkoa) na ya kwanza(mwanachama wa kawaida) bila sababu za kueleweka. Licha ya mshindi wa kwanza kuwaacha kwa mbali wenzake.

Pamoja na yote, kuna mengi ya kujifunza zaidi katika siasa hizi za ubabe. Hata CCM pia mgombea mmojawapo kwenye kura za maoni jimbo la Sumve hakulidhika na yale matokeo na kupelekea kuhama chama(kwenda CUF). Kule akapata nafasi ya kugombea ngazi ya ubunge na kuchuana na mpinzani wake(ambaye aliamini hakushinda kwa halali kwenye kura za maoni).

Pengine chama cha mapinduzi kingejilaumu sana endapo huyo mgombea aliyekihama angeshinda kupitia upinzani kwenye nafasi hiyo.

Panapo majaliwa mbunge wa Sumve, katika kuhakikisha unawatumikia wananchi wako kama ulivyowaahidi. Na Usisahau hoja yako ya kugawa wilaya iwe na halmashauri mbili kuifuatilia kwa ukaribu zaidi ili kuboresha maendeleo yetu kwa kusogeza huduma karibu na wananchi.

Tafakari!
nguduone@gmail.com.



No comments:

Post a Comment

Previous Page Next Page Home