Saturday, January 30, 2016

MBUNGE MANSOOR SHANIF HIRAN, JIMBO LA KWIMBA NA KWIMBA TUITAKAYO.

Mh Mansoor Shanif Hirani, Mbunge jimbo la KWIMBA(2015-2020)

By NGUDU NYUMBANI BLOG
30/01/2016.

NDUGU Mansoor Shanif Hirani alizaliwa Tar 05/05/1967, kwa maana hiyo ikifika Tarehe 05 may mwaka huu atafikisha miaka 49. Amesoma katika shule ya msingi “Nyakahoja” kuanzia 1975-1981, pia kasoma shule ya sekondari ya “Lake” kuanzia mwaka 1982-1986.

Kwa sasa ndiye Mbunge halali wa Jimbo la KWIMBA kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), pia ndiye mweka hazina wa mkoa wa Mwanza (Ccm) wadhifa aliokuwa nao tangu 2012. Pia ndiye katibu mkuu mtendaji wa kampuni la "Mansoor industries ltd". Bila kusahau kuwa ni mjumbe wa kamati za kudumu za bunge (bunge la 11) kwenye kamati ya “MIUNDOMBINU”. Anafahamika Kwa nick-name “MOIL”.

HISTORIA

“Mkoa wa mwanza ulianzishwa rasmi mwaka 1963 ukiwa na wilaya nne za Ukerewe. Geita, Mwanza na Kwimba. Mwaka 1972  baada ya sera ya madaraka mikoani wilaya zaidi  zilianzishwa kwa kuanza na Magu mwaka 1974. Wilaya ya  Sengerema ilianzishwa mwaka 1975 ambapo awali ilikuwa  ni tarafa mojawapo ya wilaya ya Geita.  Misungwi  ilianzishwa mwaka 1995 ambapo awali ilikuwa ni eneo la tarafa za wilaya ya Kwimba, Ilemela na Nyamagana  zilianzishwa mwaka 2002 ambazo zilikuwa zinaunda  wilaya ya mwanza”. [TAARIFA YA MKOA WA MWANZA WAKATI WA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA UHURU WA TANZANIA BARA 1961-2011]



Historia inaonesha kuwa wilaya ya Kwimba ilikuwa na jimbo moja la uchaguzi kipindi cha nyuma(Jimbo la mwamashimba). Ambapo ukifuatilia mlolongo wa wabunge waliopita utaona ndg Msobi Mageni aliongoza jimbo la Mwamashimba miaka ya 1965-1975.


 Ila haijaelezwa wazi ni lini kulifanyika mgawanyo wa majimbo tukawa na majimbo mawili ya uchaguzi (Sumve na Kwimba).  Pengine naweza kusema ni baada ya mfumo wa vyama vingi kuanzishwa mwaka 1992, maana jimbo la Sumve linaonekana kuanzia kwa ndg Mganga Ndasa (1995)

Jimbo la KWIMBA limepata kuongozwa na wabunge kadhaa katika nyakati tofauti, kuanzia mwaka 1965 mpaka leo. Ambapo Ndugu MUSOBI MAGENI MUSOBI(1965-1975),  Ndugu MASANJA FRANCIS NCHIMANI (1975-1985),  Balozi GEORGE NHIGULA(1985-1995),  Mh BUJIKU PHILIP SAKILA(1995-2010) na  Mh MANSOOR SHANIF HIRANI(2010- na kuendelea..). historia zao japo kwa ufupi unaweza zipata kupitia
 .. HAPA

Jimbo la Kwimba linaundwa Na kata 15 ambazo (pamoja na idadi ya wakazi kwa takwimu za mwaka 2015 kwenye mabano) ni;


Mwang'halanga(11,986),  Nyamilama(8,219),  Mwakilyambiti(17,364),  Hungumalwa(17,827),  Mwamala(11,427),  Kikubiji(23,792),  Mhande(21,197),  Bupamwa(18,753),  Fukalo(18,935),  Ng'hundi(9,994),  Igongwa(12,640),  Ngudu(29,837),  Mwankulwe(10,254),  Ilula(12,922) na Shilembo(10,671).  Zote kwa pamoja yakileta idadi ya wakazi 235,818


HARAKATI ZA SIASA


Ndugu Mansoor, kwa mara ya kwanza alijitokeza kuwania nafasi ya kuteuliwa na chama chake kwenye kura za maoni mwaka 2010 kuweza kuipeperusha bendera ya CCM kwenye uchaguzi mkuu. Kwenye mchakato huo alipata kupambana na baadhi ya makada kindakindaki akiwemo Ndugu Bujiku Sakila Mbunge aliyekuwa amemaliza muda wake, wengine ni kama Lameck Mahewa, Aaron Masalu na Wallace Nkanwa


Ndugu Mansoor alifanikiwa kushinda kwenye kura hizo za maoni ambapo alipata kura 7,333 huku ndugu Bujiku Sakila akiambulia kura 1.216 ya kura zote. hivyo Mansoor akasimamishwa na CCM kwenye nafasi ya ubunge akipambana na Leticia Nyerere(CDM) na wagombea kutoka vyama vingine vilivyoshiriki uchaguzi. Matokeo ya uchaguzi mkuu yalikuwa hivi;Shanif Mansoor wa CCM alishinda kwa kupata kura 19,703 na kufuatiwa na Leticia Nyerere wa Chadema aliyepata kura 7,823.


Katika awamu hii ndugu Mansoor alikuwa na vipaumbele kadhaa kama kuwaletea maji kutoka ziwa victoria wakazi wa jimbo la Kwimba, kusimamia miradi ya maendeleo kama uboreshaji wa vituo vya afya na ujenzi wa vituo vipya, kuleta mitambo ya kutengeneza barabara na kuhakikisha zinajengwa kiwango cha lami. Mitambo ya kuchimbia visima ili kupunguza tatizo la maji kwa baadhi ya maeneo na upatikanaji wa huduma nyingine nyingi za kijamii..


Awamu ya pili (2015-2020),Kwenye upande wa kura za maoni, ndugu Mansoor alichuana na makada wa chama hicho kama Bujiku Sakila, Dr Mgosha, Tumaini Shija Ruben, Lugodisha na Gwanchele. Alifanikiwa kuibuka kidedea katika mchuano huo hivyo kusimamishwa na chama chake kupeperusha bendera kwenye uchaguzi mkuu.


 Muda wa kampeni ulipofika aliandaa vipaumbele vipya katika kuliongoza jimbo la Kwimba, pia akibainisha mafanikio ya awamu iliyopita. Upande wa wapinzani wake kulikuwa na washiriki wanne, Mh Shilogela(CDM), Mh Ntiga otto(CUF), Mch. Yohana(Act) na Ndg Iswalala(UDP).


 Wagombea wa Cdm na Cuf walikuwa wanawakilisha UKAWA (Umoja wa katiba ya wananchi) unaohusisha muungano wa vyama vinne vya upinzani (Cuf, Cdm, Nccr-mageuzi na Nld). Ambapo walishindwa kufikia makubaliano ya pamoja kwamba wasimamishe mgombea mmoja atakayeungwa mkono na muungano huo hivyo kusimamisha wagombea kutoka vyama viwili. Japo taarifa za awali zinaonesha mgombea wa CUF ndiye alipitishwa na umoja huo, ila kadri siku zilivyozidi kwenda mgombea wa CDM nae alionekana kurudisha fomu na kuanza kampeni pia.


Matokeo ya mwisho
Mansoor Shanif Hiran alishinda kwa kura 39,357 huku Shilogela nganga wa CDM alipata 7,338 na Julius Otto wa CUF kura 4,076. Kwa matokeo hayo ndugu Mansoor alitangazwa kuwa Mbunge halali wa jimbo la Kwimba.Huku tukio la kufurahisha ni kuhusu mgombea wa UDP kupata kura “sifuri” kwa jimbo zima. Nilipata kuelezea sababu chache zilizopelekea Ndugu Mansoor kushinda uchaguzi huu kwenye andiko lenye kichwa “ILIKUWA NI LAZIMA MH MANSOOR ASHINDE UBUNGE JIMBO LA KWIMBA 2015”.


MAFANIKIO


Mafanikio ya awamu iliyopita (2010-2015) yalichagizwa Kwa kiasi kikubwa na wawakilishi wawili ambao ni Ndg Mansoor  na Leticia Nyerere (Cdm) mbunge wa viti maalumu mwenyezi MUNGU amlaze mahala pema.


Baadhi ya miradi ya muda mrefu ilipata kukamilika Kwa kiasi Fulani na kupata kufanya kazi. Mojawapo ya miradi hiyo ni ule wa kuleta maji ya ziwa Victoria hadi maeneo ya wilaya ya Kwimba- huu ulikuwa mradi wa muda mrefu ambao ulisuasua sana katika utekelezaji wake. Walau katika awamu iliyopita utekelezaji wake ulianza ambapo inakadiliwa vijiji 24 vimepatiwa huduma ya maji kwa awamu ya kwanza, awamu ya pili itahusisha vijiji kadhaa pia ikiwa lengo la serikali ni kumaliza tatizo la maji katika jimbo hili.


Mafanikio mengine ni usambazaji wa umeme vijijini, chini ya usimamizi wa shirika la umeme Tanzania (TANESCO) na wakala wa nishati vijijini (REA). Jimbo la Kwimba ni mojawapo ya wanufaika wa mradi huo ambapo vijiji kadhaa walipata kuunganishwa na huduma ya umeme katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo. Lengo ni kuvifikia vijiji vyote Tanzania kwa mpangilio wa awamu kadhaa inayoendelea.


Miradi mingine ya maendeleo ni kama kuanzishwa kwa tawi la benki ya CRDB, uanzishwaji ujenzi wa baadhi ya vituo vya afya kwenye baadhi ya kata. Pia uchimbwaji wa visima kadhaa vya maji kwenye baadhi ya maeneo.


Pia rafiki yangu Joel alipata kunielezea baadhi ya mafanikio katika awamu hii ambapo ni pamoja na kupungua kwa msongamano wa wagonjwa kwenye hospital ya wilaya kwa kuboresha “Kliniki ndogo ya wazazi”. Minara kadhaa imejengwa kwa ajiri ya kufikisha mawasiliano ya kimtandao sehemu nyingi zaidi, uboreshaji wa baadhi ya miundombinu mathalani barabara kadhaa jimboni na mengine mengi.


Japo ni ngumu kuthibitisha moja kwa moja kama ndugu mbunge alihusika kwa asilimia zote katika kufatilia utekelezaji wa miradi hii kama wajibu wake kikatiba ambapo anapaswa kusimamia serikali kikamilifu kwenye utekelezaji wa miradi na kuikosoa pale inaposhindwa kufanikisha kwa muda na kwa kiwango kinachostahili.


Maswali aliyopata kuuliza bungeni kwa kipindi cha kwanza kwenye uwakilishi wake unaweza yapata kupitia
 .. HAPA

MAPUNGUFU

Mbunge wangu amekuwa na madhaifu kadhaa katika awamu iliyopita na pengine akaendelea na utaratibu huu kwa awamu hii pia.

Utaratibu wa kufanya vikao na makada wenzie wa Ccm halafu kusahau kufanya vikao/mikutano na viongozi na wananchi kwa ujumla kila baada ya muda ili kujua changamoto wanazokabiliana nazo. Hili limekuwa ni tatizo kubwa. Atambue kuwa yeye ni mbunge wa wananchi wote wa jimbo hivyo anao wajibu wa kuwasikiliza na kutimiza ahadi zake.

Kujenga mazoea ya kuja jimboni mara kwa mara maana ndiko waajiri wake wapo kule. Hili limekuwa likilalamikiwa sana na wananchi wa jimbo hili kwamba Mh akishapata kuchaguliwa basi kuonekana jimboni ni kwa nadra sana, na hata akionekana ni kwa shida maalumu ama ihusuyo chama chake au ulazima wa shida husika na sio kuja kujumuika na wananchi kwenye mikakati ya kimaendeleo.

Wananchi huishia kulalamika na ukikaribia uchaguzi mheshimiwa ndio huongeza safari pengine kila kata,kijiji na kitongoji ndani ya jimbo ambapo wananchi husahau tabia aliyokuwa nayo kwa miaka ya nyuma na kumuamini kwa “vizawadi” vichache ambavyo lengo lake ni kuwaweka karibu kuelekea uchaguzi wabaki kuwa na imani naye.

“Jukumu la Mbunge alilopewa kikatiba ni kushirikiana na wananchi wa jimbo lake kuhakikisha kwamba serikali na halmashauri zinawajibika katika kutumia rasilimali fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya serikali ili maendeleo yaweze kupatikana kwa wananchi”.(policy forum)

Kwenye Mfuko wa maendeleo ya Jimbo ambao unakuwa chini ya usimamizi wa ofisi ya mbunge, mfuko huu umekuwa ukilalamikiwa sana na wadau wa maendeleo kwamba, fedha zake hazipo katika mtiririko mzuri kwenye matumizi yake.

Katika andiko la Policy Forum juu ya “Mfuko wa maendeleo ya jimbo” wamepata kusema kwamba  “Asilimia 2.5 ya bajeti ya matumuzi inayopendekezwa kutengwa kwa ajili ya mfuko wa majimbo ni kiasi kidogo sana cha kuweza kuleta maendeleo endelevu katika majimbo. Si zaidi ya kiasi cha Tshs milioni 600 kwa kila jimbo la uchaguzi lenye wastani wa watu laki
200-300. Ni wastani wa Tshs 2000 kwa kila mkazi wa jimbo. Hiki ni kiasi kidogo sana cha
kutuletea maendeleo endelevu.”

Wanajaribu kueleza pia kuwa “Kuna Hatari kubwa kwamba fedha za mfuko huu zikatumika vibaya kwa kukosa usimamizi na ufuatiliaji wa karibu wa wananchi kwani msimamizi wananchi waliomchagua kuwawakilisha naye ameingia kwenye utekelezaji. Upatikanaji wa taarifa za miradi utategemea sana utashi binafsi wa mbunge kuwa wazi na kuwajibika kwa wananchi.”
Kiujumla mfuko huu umekuwa na changamoto katika matumizi sahihi ya fedha zinazopatikana  ili kuleta maendeleo kwa wananchi hasa kufanikisha miradi.

Pia njia anayoitumia ndg mbunge ya kutanguliza pesa mbele ili aweze kueleweka na kukubalika kwa wananchi kwa upande wangu sidhani kama ni sahihi, sikatai kama kila mgombea lazima atumie fedha katika kampeni. Lakini kuna kiwango ambacho kimeelekezwa kwenye “AMRI YA GHARAMA ZA UCHAGUZI(KIWANGO CHA JUU CHA FEDHA 2015)”. Kwa jimbo la Kwimba takwimu zipo kama ifuatavyo;


S/N
JINA LA JIMBO
UKUBWA WA JIMBO (KWA KILOMITA ZA MRABA)
IDADI YA WATU KATIKA JIMBO
UBORA WA MIUNDOMBINU YA MAWASILIANO
KIWANGO CHA JUU CHA FEDHA SH.
163
KWIMBA
1,968.94
235,818
41.6
55,000,000/=

Kwahiyo bila shaka wagombea wote walikuwa wanalijua hili, na kama kuna aliyekiuka hii amri alipaswa kuchukuliwa hatua stahiki.

Nachoona kwa mbunge wangu ni kwamba, mh Mansoor ni mfanyabiashara na sio mwanasiasa. Kwa maana hiyo njia rahisi kwake kueleweka ni hiyo anayoitumia na sio kulisha propaganda nyingi wananchi. Katika hili kuna msemo anapenda kutumia kwamba..”Nyamu ni nyamu duhu” akimaanisha paka ni paka tu. Msingi wa msemo huu ni kwamba wananchi wasiangalie rangi ya paka bali waangalie paka anayeweza kukamata panya kwa mafanikio. Naweza kusema falsafa hii imempa mafanikio kwa kiasi kikubwa na kumjengea imani kwa wananchi.


USHAURI

Ningependa kushauri mambo machache kwa mbunge wangu mteule wa jimbo la Kwimba kwamba,
Ajenge utaratibu wa kufanya mikutano na wananchi wake kwa muda flani mfano kila miezi mitatu ambapo ataweza sikiliza kero ambazo zimepata jitokeza kwa muda huo, pia alete mrejesho wa kile alichichangia bungeni juu ya maendeleo ya jimbo letu.

Ashirikiane vizuri na madiwani wote katika kusimamia miradi na kuhakikisha inakamilika kwa wakati.. Aongeze msukumo katika kuisimamia serikali na watumishi wote kwa ujumla kutimiza majukumu yao kikamilifu

Ikumbukwe kuwa halmashauri ya Wilaya ya Kwimba ni moja ya halmashauri zinazopata hati chafu kila mara kulingana ripoti ya CAG inasemekana ni kwa miaka mitatu mfululizo sasa. Jitihada kubwa na za haraka zinahitajika katika hili ili kudhibiti matumizi ya halmashauri. Pia wadau na wachambuzi mbalimbali wameupongeza uamuzi wa Rais kuihamishia wizara yenye dhamana(TAMISEMI) kuwa chini ya ofisi yake. Bila shaka tunategemea mabadiliko makubwa ya kimfumo katika hilo.

Kuna mradi wa “KWIMBA TUITAKAYO” ambao bado haujapata mwitiko na ushirikiano ambao lengo lake ni kuandaa mwongozo utakaoweza kusaidia upatikanaji/utengenezaji wa ajira ndogo ndogo kupitia vikundi vya kijasiliamali ambavyo vitakuwa na mwongozo unaofuata taratibu na sheria katika ushiriki ili kuhakikisha walengwa wanashiriki kikamilifu. Mradi huu kwa sasa bado upo katika hatua za mwanzo chini ya NGUDU NYUMBANI BLOG, na ukishapata mwamko na ushiriki wa kutosha utapata kulifikisha wazo hili kwa viongozi wetu kwa hatua zaidi za utekelezaji ambapo ndg Mansoor kama kiongozi atahusika kulisimamia hili.

Akijibu swali la Mbunge Leticia Nyerere(2015) juu ya swali alilohoji
 “Mpango wa maendeleo wa miaka mitano unaoishia 2016. ulilenga kutoa huduma kwa miradi ya maendeleo ya vijana ili waweze kujiajiri na kupata mitaji kibiashara. je, serikali imetoa huduma gani kwa vijana wa wilaya ya Kwimba ili waweza kujiajiri?”
Naibu Waziri wa Ajira na Kazi alitoa majibu kama ifuatavyo;
A) Huduma ambazo serikali imetoa kwa vijana wa kwimba, ni pamoja na kuendesha mafunzo ya ujasilia mali, na ujuzi wa kuendesha mashine za kufyatua matofali, stadi za maisha na elimu ya biashara kwa baadhi ya vijana wa vijiji wa nyamilama, nyamatara na kakora
kutoa huduma ya mikopo yenye masharti nafuu kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana
kutoa nyenzo za kufanyia kazi, ambapo vikundi vya vijana kutoka nyamilama, nyamatara na kakora wamepatiwa mashine 4 za kufyatua matofali toka NATION HOUSING, na wameendelea na shughuli zao kama kawaida za ujasiliamali.
B) Jumla ya vikundi vya vijana 31 wamenufaika na huduma hizi za serikali ikiwa ni pamoja na kupatiwa mikopo ya kiasi cha shil mil 16 na laki 4, vifaa na mafunzo ya ujasiliamali mbalimbali kama nilivyoeleza hapo juu.

Hii ilikuwa ni hatua mojawapo katika kusaidia vijana kunufaika na mikopo yenye masharti nafuu pia kujiajiri katika Nyanja mbalimbali. Kupitia hilo program maalumu ya KWIMBA TUITAKAYO itajikita kushauri ongezeko la vijana wengi zaidi kujiajiri.

Kingine ni kuwa amkumbushe Makamu wa rais juu ya ahadi yake kwetu kujenga chuo cha mafunzo ya ufundi stadi(VETA) ambapo alibainisha kuwa ni ahadi ya serikali iliyopita hivyo kama wataipa kipaumbele kwa awamu ya 5. Pia ahadi lukuki za Rais JPM kwetu ikiwemo kuboresha bei za mazao na kuboresha mazingira ya mkulima ili anufaike na sekta hii.

Ushauri mwingine kwa mbunge, anatakiwa aunde kamati maalumu ya washauri jinsi ya uendeshaji wa jimbo. Nikimaanisha awe na wataalamu na wabobezi wa kada tofauti wa Kwimba ambao wanaijua wilaya vizuri ambao wataweza kumshauri katika mambo mengi juu ya maendeleo ya jimbo letu na wilaya kwa ujumla. Hii inafanywa na wabunge wengi mfano mzuri ni mbunge machachari wa jimbo la Arumeru Mashariki ndg Joshua Nasari

Jimbo la Kwimba bado lina changamoto lukuki(elimu,afya, miundombinu, n.k) ambazo kwa ushirikiano wa mbunge na viongozi wengine katika ngazi zote pamoja na ushirikiano mzuri wa wananchi wa kata zote za jimbo vijiji na vitongoji vyote tunaweza kuwa na safari nzuri kuelekea ‘KWIMBA TUITAKAYO’

HITIMISHO

Ningependa kutoa RAI yangu kwa wadau na wananchi wa jimbo zima kushiriki katika miradi ya maendeleo, pia kushirikiana na viongozi wetu wa ngazi zote kuhakikisha tunapiga hatua kimaendeleo.

Mfano mgogoro uliokuwepo kati ya Diwani wa Kata ya NGUDU ndg Malifedha na mwenyekiti wa kitongoji cha NGUDU MJINI ndg Casmiry Anthony bila shaka uliishia kwenye uchaguzi mkuu. Kwa sasa naimani wanahitaji kuungana na kuacha tofauti za kisiasa ili wasimamie vizuri maendeleo ya wananchi wa NGUDU na wilaya kwa ujumla.

Pia kwa wale wanaompinga mbunge kwa kile anachofanya, kwanza ni halali kufanya vile pia wasikomee kumpinga mitandaoni tu wanatakiwa wafanye zaidi ya hilo kama wanakuwa wanaona alichofanya mbunge si lolote kwao. Utasikia mtu anauliza “mmetumia kigezo gani kumteua mhindi tena?” na maswali mengine mengi ya kejeri halafu wao hawahusiki katika hatua zozote za kumpata kiongozi wanayehisi anafaa zaidi wanapaswa washiriki kwanza waache “kimuyemuye”. Dhana hii ni ya kibaguzi na ya kupuuzwa tu kama hatutabadili fikra zetu kwanza.

Pia ningependa kuwanasihi wale wote ambao hawakubaliani na uwakilishi wa ndg Mansoor waanze jitihada sasa wasisubiri uchaguzi ukaribie ndio waoneshe jitihada. Hii inajitokeza aghalabu kwa wagombea wengi. Nilipata kuona andiko la ndg Ntiga Otto(Cuf) akiashiria yupo tayari kugombea tena 2020. Ni wazo zuri sana ila anatakiwa aanze kusimika misingi imara sasa ili uchaguzi ukikaribia hapo baadae iwe rahisi kwake, ndg shilogela na makada wengine wamepoa kwa sasa pengine lengo wanalo ila wanasubiri miezi kadhaa kabla ya uchaguzi ndio waanze zile tunaita “amsha amsha”, au vijana wa mjini huita “tia maji tia maji”.

Ni imani yangu kuwa makala hii itamfikia mheshimiwa mbunge kwa njia yeyote  rahisi na atachukua kilicho bora na kuacha anachoona hakimgusi kisha maisha yataendelea. Nimtakie uwakilishi bora wa jimbo letu panapo majaliwa

Tafakari!
NGUDU NYUMBANI BLOG
nguduone@gmail.com




2 comments:

  1. Hongera kwa makala nzuri jadidi hasa katika uga wa historia na mwelekeo mpana wa wilaya yetu....nimejifunza mengi!!

    ReplyDelete

Previous Page Next Page Home