Monday, May 23, 2016

STORI YA MAISHA YA NG'WANAMALUNDI-2

Bottom of Form
Chanzo: Mwananchi
Akiwa anaendelea na ngoma yake wananchi wa Kijiji cha Sekke waliibiwa ng’ombe wengi sana na watu kutoka Kabila la Wamasai ambao walienda kuwahifadhi katika Pori la Mwanima karibu na Kijiji cha Bubiki.
Ng’wanamalundi na kikosi chake waliondoka Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza na kuelekea Sekke wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kwa lengo la kusaidia kuzikomboa ng’ombe zilizoibwa.
Hata hivyo kabla hawajafika uwanja wa vita, Ng’wanamalundi alifanya utabiri wake uliotokana na nguvu ambazo alizipata kutoka kwa Bibi Kizee wa porini.
Sitta anasema aliwaambia kuwa kabla ya vita, itatokea mvua kubwa sana na ikikatika watakuja ndege hai aina ya mwewe watakaokuwa wanazungukazunguka kwenye zile ng’ombe na hapo sasa wafuasi wake wakate miti mifupi mifupi (Lubugu).
Sitta anasema utabiri huo ulitimia, kwani mvua ilinyesha kubwa sana na baada ya kukatika wale mwewe walijitokeza wengi sana wakawa wanazunguka kwenye zile ng’ombe na ndipo yale mapigano ya Wamasai na wafuasi wake yalipoanza.
Aliwaeleza kuwa baada ya kuwa na fimbo ya Lubugu wale wenye upinde na mishale watakaa nyuma na kazi yao watakuwa wanazipiga zile ngao za Kimasai na zikidondoka chini ndipo wenye pinde na mishale waanze kushambulia.
Mwanamalundi alipigana hiyo vita ya Wamasai mpaka akazirejesha zile ng’ombe na aliwatokomeza Wamasai mpaka kwenye mpaka wa Mto Manonga unaotenganisha Tinde Shinyanga na Nzega mkoani Tabora.
Hapo ndipo ilibainika Wamasai hao walikuwa wametumwa kuiba ng’ombe Usukumani na Mtemi Tinginya wa Busongo Nzega, ambapo baada ya vita hiyo Ng’wanamalundi na kundi lake walirudi Sekke na kupewa jina la Kishosha Mang’ombe tafsiri ikiwa ni mrudisha ng’ombe.
Baada ya vita hiyo Ng’wanamalundi alirudi nyumbani kwao wilayani Kwimba kuoa, lakini bahati mbaya ilimkuta, kwani kila mke aliyejifungua, mtoto alikufa. Baba yake Bugomola akaenda Ntuzu kwa sasa Bariadi kufanyiwa tambiko kuhusu uzazi kwa mwanaye.
Akiwa huko Ntuzu, Bugomola alielezwa mwanaye Ng’wanamalundi hatapata mtoto kwa wake zake alionao. Hivyo aoe msichana atakayempata upande wa Mashariki ambaye atakuwa akiitwa Nkamba na atazaa watoto watatu; wa kwanza ataitwa Sitta, wa pili Ngassa na wa tatu Marieta.
Baada ya kurudi Bugomola, haikumchukua muda mwanaye Ng’wanamalundi akapata msichana akaoa na akaendelea na shughuli yake ya kuendesha kikundi cha ngoma.
Ng’wanamalundi kuwekwa kizuizini
Akiwa anaendelea na ngoma zake katika maeneo ya Kanda ya Ziwa, Sitta anasema siku moja yeye na kikundi chake walipokuwa wakiburudisha katika maeneo ya Bukumbi mkoani Mwanza, wafuasi wake walipumzika kwenye mti mkubwa ambapo pia kilikuwa Kituo cha Wajerumani, Ng’wanamalundi aliwaambia wafuasi wake waondoke waende kwenye ngoma, wafuasi wake waligoma wakadai wanapumzika kwenye kivuli hicho ili wavute sigara.
Baada ya kuwabembeleza vya kutosha akabaini hawataki kumsikiliza ndipo alipounyooshea kidole ule mti akisema “Ngh’walemelaga hanti gunugo aliyo gumaga,” akiwa na maana “Mmekatalia kwenye mti huo huku ukiwa umekauka.” Ghafla mti huo wote ulikauka.
Kuona hivyo wafuasi wake wakaondoka wote kwenye huo mti wakaenda kuendelea na ngoma yao ambayo walicheza katika eneo la Bukumbi na Busagara karibu na Mji wa Mwanza na walipomaliza walirejea Kwimba.
Akiwa Kwimba alicheza ngoma moja na Gindu Nkima, ngoma hiyo ilikuwa ngumu kwake ilichezwa sehemu za Mwanagwa. Baada ya kuwa amezidiwa Ng’wanamalundi, wapishi wake walimfuata na kumtaka awasaidie namna ya kupata kuni za kupikia.
Kutokana na uharaka aliokuwa nao Ng’wanamalundi alielekeza kidole chake kwenye miti ya minyaa iliyokuwa mbele yake huku akisema “Batemagi pye abenababa mkazugile,” akiwa na maana “Yakateni yote haya mkapikie.” Baada ya kauli hiyo minyaa yote ilikauka na kuwa kuni na wafuasi wake walikata wakaenda kupikia chakula.
Akiwa katika ngoma hiyo wakati huo barabara ya kutoka Shinyanga kwenda Mwanza ilikuwa inachongwa na manamba waliokuwa wakikamatwa na Wajerumani kwa ajili ya kazi hiyo, Gavana wa Kijerumani wa eneo la Mwanza alipita eneo hilo akiwa amepanda punda alikuta kazi imesimama, alipohoji kwanini kazi imesimama alielezwa wananchi wote wamekwenda kwenye ngoma ya Ng’wanamalundi.
Kitendo hicho kilimchukiza sana Mjerumani huyo, ambaye aliondoka akaenda Mwanza na baada ya siku mbili walikuja askari waliomkamata Ng’wanamalundi na kumfunga mnyororo na watuhumiwa wengine walipelekwa Mwanza na kuwekwa gerezani.
Kosa hilo kwa utawala wa Ujerumani lilihesabiwa kuwa ni uhaini wa kupinga utawala wao hivyo alitakiwa kupewa adhabu ya kunyongwa. Kabla hajapelekwa Mwanza, kwa kuwa ilikuwa ni safari ya kwenda kunyogwa, alipelekwa nyumbani kwa wazazi wake kuaga.
Alipofika nyumbani kwao alimpa mama yake shoka aliloliweka pembezoni mwa ukuta chumbani na maziwa, huku akitoa maelekezo.
“Mayu imbasa yeneye ulu yulina ng’wigulya mumhonatwalwa ulu yika hase mumhonashoka amabele genaya ulu guganda mumhonacha, ulu gita lububhi mumhonasata.” Akiwa na maana hii shoka ikipanda juu basi nitakuwa nimepelekwa ikishuka chini nitakuwa nimerudishwa.”
Sitta anasema Ng’wanamalundi aliendelea kumpa maelekezo mama yake kuwa haya maziwa yakiganda atakuwa amekufa na pindi yakipata utando atakuwa anaumwa, baada ya maelezo hayo Ng’wanamalundi alipelekwa Mwanza gerezani ambako alikutana na Mtemi Makongoro wa Mwanza.
Siku iliyofuata walitolewa wote ambapo Sitta alieleza kuwa walikutana pia na mganga aliyemtabiria kuzaa watoto watatu ambaye naye alikuwa amekamatwa kwa kosa la kupiga ramli iliyosababisha mauaji ya kishirikina.
Asubuhi kila mmoja alisomewa mashtaka yake ambapo Ng’wanamalundi alisomewa mashtaka matatu, shtaka la kwanza kuukausha mti uliokuwa ukitumiwa na maofisa wa utawala wa Wajerumani kama kituo cha kupumzikia huko Bukumbi Mwanza.
Shtaka la pili kuwatungia na kuwaimbia nyimbo mbaya Wajerumani na la tatu ni kukwamisha ujenzi wa Barabara ya Mwanza kwenda Shinyanga.

Ng’wanamalundi alidaiwa kuchezesha ngoma eneo la Mwanangwa hali iliyosababisha wafanyakazi wa manamba waliokuwa wakilima barabara hiyo kuacha na kwenda kuangalia ngoma yake hali iliyowachukiza Wajerumani…
Inaendelea...

No comments:

Post a Comment

Previous Page Next Page Home